Pambano Kuu

Indonesian
(Ayubu 1)
Year: 
2016
Quarter: 
4
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kitabu maarufu cha Kikristo kinaanza kwa kusema, “Si kwa ajili yako.” Ayubu anatufundisha kuwa kauli hii haielezei kikamilifu hali halisi. Sio tu kwamba maisha hayatuhusu, bali ni kuwa tayari na uwezo wa kuyaacha yale tunayoyatamani ili kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Jambo la kufurahisha kuhusu Ayubu, na “kuacha matamanio yetu,” ni kwamba Ayubu alianza na kuhitimisha kama mtu tajiri aliyepata kuwepo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 1. Kujifunza Habari za Ayubu

  1. Soma Ayubu 1:1. Tunajifunza nini kuhusu mwenendo wa Ayubu kwa Mungu? (Alikuwa mkamilifu na mwelekevu!)

  2. Soma Ayubu 1:2-3. Tunajifunza nini kuhusu familia ya Ayubu na utajiri wake? Alikuwa mtu tajiri kuliko watu wote katika upande wa Mashariki. Watoto kumi! Wana saba na mabinti watatu. Alimiliki maelfu ya wanyama.)

   1. Angalia jambo fulani kuhusu tarakimu. Idadi ya watoto ni kumi. Idadi ya wanyama inahusiana na kumi (kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, nk.). Unadhani jambo hili linamaanisha kitu chochote? (Kumi ni namba kamili. Ayubu ni mtu mkamilifu: kiroho na ki-mali.)
  3. Soma Ayubu 1:4-5. Je, Ayubu alikuwa mtu mwenye kuipenda na kuijali familia yake? (Alijali sana hali ya kiroho ya familia yake.)

 2. Pambano

  1. Soma Ayubu 1:6. Tafsiri ya Biblia ya NIV inatafriri neno la Kiebrania “wana wa Mungu” kama “malaika.” Unadhani Kiebrania kinamaanisha nini? Kwa umahsusi kabisa, je, wewe ni mwana au binti wa Mungu? (Ndiyo!)

   1. Je, tafsiri ya NIV iko sahihi kutafsiri “wana wa Mungu” kama “malaika?”

   2. Kwa nini Shetani anajumuishwa? (Tunajiita “watoto wa Mungu” kwa sababu sisi ni matokeo ya uumbaji wake. Hii ni kweli kwa malaika pia. Hivyo, inaleta mantiki kuwaita “wana wa Mungu.” Kwa kuwa Shetani ni malaika aliyeanguka na kutupwa (Ufunuo 12:7-9), inaleta mantiki kumjumuisha kama “mwana wa Mungu.”)

   3. Tunaweza kuelewa sababu ya Shetani kuitwa “mwana wa Mungu,” lakini kwa nini anajumuishwa kwenye huu mkusanyiko? (Soma Yohana 12:31-32. Tulipomtii Shetani, alikuwa mtawala wa ulimwengu huu. Hivyo, Shetani anakuja kwenye huu mkusanyiko kama mwakilishi wa dunia.)

   4. Unadhani lengo la mkusanyiko huu ni lipi? (Walikuja “kujihudhurisha mbele za Bwana.” Inaonekana kama ni mkutano wa kibiashara ambapo malaika wanatoa taarifa kwa Mungu kwamba maendeleo yao ni kutenda mambo makuu. Ni kama ilivyo kwenye “mkutano wa wafanyakazi” kazini!)

  1. Soma Ayubu 1:7. Unadhani Mungu alifahamu Shetani alitokea wapi? (Naam, Mungu alifahamu.)

   1. Kwa nini basi Mungu aliuliza?

   2. Je, huwa unawauliza watoto wako kile walichokuwa wanakifanya wakati unafahamu kuwa walikuwa wakifanya jambo baya?

   3. Je, Shetani ananukuu mambo yote mabaya aliyokuwa akiyafanya? (Hapana. Badala yake, anasema kuwa alikuwa “akizunguka-zunguka” huku na huko duniani.)

    1. Unadhani nia ya Shetani ni nini katika kumkumbusha Mungu juu ya milki yake?
  1. Soma Ayubu 1:8. Je, ungependa Mungu aseme hivi juu yako? (Shamirisho (sifa) zuri ajabu! Maoni ya Mungu kumhusu Ayubu ni chanya sana. “Hapana mmoja aliye kama yeye duniani!”)

   1. Kwa nini Mungu anasema jambo kama hilo kwa Shetani? Kauli hii inaendanaje na mazungumzo yao? (Angalia mambo mawili. Shetani anasema kuwa anaimiliki dunia. Mungu anajibu kuwa hana umiliki/mamlaka kamili kwa sababu Mungu anao wafuasi wake, na mmoja wao ni Ayubu. Pili, Mungu anaashiria kuwa Shetani alipokuwa “anazunguka-zunguka” huku na huko duniani, ama alikuwa anafanya jambo baya lenye hila kwa kuwaangalia “watiifu wake,” au huenda Shetani aligundua kwamba kulikuwa na “watu” ambao walikuwa hawamfuati.
  1. Soma Ayubu 1:9-11. Je, Mungu amempendelea Ayubu kwa kubainisha haki yake kuu?

   1. Lengo la maisha yetu ni lipi? (Kumpa Mungu utukufu. Kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Katika huu muktadha, Ayubu ni mpiganaji wa Mungu. Yeye ndiye anayelithibitisha jina la Mungu.)
  1. Hebu tujikite katika Ayubu 1:9. Shetani anasema nini kwenye hili jibu? (Kwanza, anaitia changamoto tabia ya Mungu. Ayubu hamtii Mungu kwa kuwa njia ya Mungu ni bora. Badala yake, Ayubu anakuwa mtiifu kwa sababu Mungu anampatia vitu. Pili, hii ni changamoto kwenye tabia ya Ayubu. Ayubu anatii si kwa kuwa ana upendo, bali kwa sababu yeye ni mlafi. Mungu alimpa Ayubu rushwa.)

  2. Soma Ayubu 1:12. Hii inatufikisha kwenye kiini cha somo la juma lililopita. Ayubu anataka kufahamu kwa nini mambo yote haya ya kutisha yalimtokea. Juma lililopita tulijifunza kwamba Mungu anamwambia Ayubu kuwa, “Mimi ni Mungu na wewe si Mungu, kaa chini na unyamaze kimya.” Je, Ayubu, hata angepewa miaka milioni moja, angeweza kubashiri sababu halisi ya mateso yake?

   1. Je, changamoto hii pamoja na jibu la Mungu vinatufundisha nini kuhusu tabia ya Mungu?

   2. Je, changamoto hii pamoja na jibu la Mungu vinatufundisha nini kuhusu asili ya kazi yetu kwa Mungu?

   3. Je, changamoto hii pamoja na jibu la Mungu vinatufundisha nini kuhusu pambano kuu kati ya wema na uovu? (Inatufundisha kwamba tupo katikati ya pambano. Kazi/wajibu yetu ni kuuendeleza Ufalme wa Mungu kwa namna tunavyoishi. Mungu anathibitisha baadhi ya changamoto kwenye tabia yake kupitia kwetu.)

  1. Endapo Samsoni angekuwa hai, je, Mungu angemwelekeza kwa Shetani? (Nadhani jibu ni dhahiri kabisa kwamba “hapana.” Pamoja na hayo, Samsoni yupo kwenye orodha ya Watu Mashuhuru wa Imani katika kitabu cha Waebrania 11 (Waebrania 11:32-33). Hii inatufundisha jambo la muhimu sana kuhusu imani na matendo. Samsoni, kutokana na imani yake, atakuwepo mbinguni. Lakini, alimwangusha Mungu katika idara ya matendo. Mojawapo ya sababu ambayo Mungu anatutaka tuishi maisha ya haki ni kulithibitisha jina lake na tabia yake.)
 1. Shambulizi la Shetani

  1. Soma Ayubu 1:13-15. Endapo ungekuwa Ayubu, je, hii ni mojawapo ya hatari ya maisha ya kibishara – kwamba Waseba wanaweza kuiba mali zako?

  2. Soma Ayubu 1:16. Sasa unafikiria nini, ikiwa wewe ni Ayubu? (Hili si jambo ambalo katika hali ya kawaida unapaswa kulikubali. Jambo hili linaonekana kuingiliwa kati na Mungu. Kwa dhahiri mtumishi anadhani kuwa jambo hili limetoka kwa Mungu kwa sababu ameuita “Moto wa Mungu!”)

   1. Kwa nini Shetani hakuwatumia Waseba tena? (Alitaka Ayubu afikie hitimisho la dhahiri kuwa Mungu alikuwa anamwadhibu.)
  1. Soma Ayubu 1:17. Tunapokumbuka nukuu ya utajiri wa Ayubu (Ayubu 1:3), je, hii inamaanisha nini kwa Ayubu? (Kundi lake lote la wanyama limetoweka. Utajiri wake umetoweka kwa huu muda mfupi tu.)

   1. Je, jambo hili linauzungumziaje utajiri wako?

   2. Je, tunapaswa kumwogopa Shetani? (Shetani ni mtu wa kuogofya, lakini utaona kwamba hakuwa na uwezo juu ya Ayubu isipokuwa pale Mungu alipomkubalia (ayubu 1:12).)

  1. Soma Ayubu 1:18-19. Endapo ungekuwa Ayubu, je, ungejali habari ya vifo vya watoto wako peke yake wakati habari hizi za kutisha zilipokufikia? (Soma tena Ayubu 1:4-5. Karamu hizi ndizo sababu zilizomfanya Ayubu ajali na kufikiria kuwa watoto wake walitenda dhambi. Ayubu anaweza kuwa anafikiria kwamba huenda watoto wake walifariki huku wakiwa wanatenda dhambi, na bado alikuwa hajatoa sadaka kwa ajili yao!)

   1. Jiweke kwenye nafasi ya Ayubu. Ungejisikiaje?
  1. Soma Ayubu 1:20-21. Je, ungejisikia hivi?

  2. Soma Ayubu 1:22. Juma lililopita tulijifunza kuwa Ayubu alitaka kumshtaki Mungu. Kwa nini? Kwa sababu alitaka kumwonesha Mungu kuwa alikuwa mtiifu na hakustahili mambo yaliyokuwa yakimtokea. Je, huko ni “kumshtaki Mungu kwa kutenda jambo baya?” Je, baadaye Ayubu alibadili mtazamo wake? (Sidhani. Angalao situmaini hivyo. Mtazamo wangu juu ya kisa hiki ni kwamba Mungu anatutaka tumwendee pale tunapodhani kuwa hatukutendewa haki (tumetendewa isivyostahili). Anatutaka tumwendee tukiwa na malalamiko yetu. Jambo baya kabisa ni pale tunapogeuka na kumwacha Mungu kwa sababu hatumtumaini tena.)

  3. Ayubu alipoteza karibu kila kitu. Je, unakubaliana na mambo yaliyomtokea Ayubu? Je, unadhani hii ni hasara aliyostahili kuteseka nayo? Au, je, haya yalitokea ili tu kuwa nguzo ya fahari ya Mungu? (Nadhani haya ni marudio ya jaribu la Eva (Mwanzo 3:1-6). Eva alimtumaini Shetani na hakumtumaini Mungu. Ayubu anamtumaini Mungu sana kiasi kwamba ana uhakika kuwa ikiwa atasikilizwa kwa haki, Mungu atamthibitisha. Samsoni, pamoja na dosari na upungufu katika tabia yake, pia alimtumaini Mungu.)

  4. Rafiki, je, mambo ya kutisha yameshawahi kukutokea maishani? Ikiwa yameshawahi kukutokea, je, utamtumaini Mungu bila kujali matukio hayo?

 1. Juma lijalo: “Je, Ayubu Yuamcha Mungu Bure?”