Je, Ayubu Yuamcha Mungu Bure?

Swahili
(Ayubu 2)
Year: 
2016
Quarter: 
4
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma lililopita tulimsikitikia na kumhurumia Ayubu kwa kuwa aliwapoteza watoto pamoja na utajiri wake. Utakumbuka kwamba ingawa Mungu aliruhusu majanga haya yatokee, alimzuia Shetani asimdhuru Ayubu mwenyewe. Ayubu 1:12 (“usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe”). Mungu alishinda katika hatua ya kwanza. Utabiri wa Shetani haukuwa sahihi: Ayubu alipoteseka kwa kupoteza vitu vyote vilivyotokea hakumkufuru Mungu, badala yake alimrudishia Mungu sifa (Ayubu 1:21). Je, wewe ni mtu unayeweza kuthibitisha kuwa Shetani hayuko sahihi? Hebu tuzame kwenye kisa cha Ayubu ili tuone jinsi pambano hilo linavyoendelea!

 

1)      Kikao cha Pili cha Watumishi (Wafanyakazi)

 

a)      Soma Ayubu 2:1-2. Kwa mara nyingine tena tunaona suala la “mkutano wa pili wa watumishi” wa mbinguni ambapo Mungu anapokea taarifa kutoka kwa viongozi wa ulimwengu na sayari zake. Taarifa sahihi ya Shetani ni ipi? (Alitakiwa kukiri kwamba alifanya makosa katika sakata la Ayubu.)

 

b)      Soma Ayubu 2:3. Mungu anatambua kuwa kuna jambo Shetani hakulijumuisha kwenye taarifa yake, hivyo anamtaja Ayubu. Je, jambo hili linatuhabarisha kitu gani kumhusu Mungu? (Yuko makini kwa yale yanayowatokea wafuasi wake.)

 

i)        Je, Mungu pia anamsuta Shetani?

 

ii)      Soma Mithali 24:17-18. Unalinganishaje mafungu haya na kile ambacho Mungu anamwambia Shetani? Inaonekana kama vile anamcheka kwa kumbeza au kumsuta, sawa? (Ikiwa kweli hiki ni kikao cha watumishi, basi haya si maongezi binafsi kati ya Mungu na shetani. Tunapolielewa jambo hili, tunaona kwamba Mungu anatangaza upande wake kwenye hili pambano kati ya wema na uovu.)

 

(1)   Angalia jinsi Ayubu alivyo mpambanaji mkuu kwa Mungu!  Je, ungependa kuwa mpambanaji wa Mungu?

 

iii)    Mungu anabainisha nini juu ya mtazamo wake pale tunapoteseka kwenye mikono ya uovu? (Mungu anaonekana kutofurahia kile kilichomtokea Ayubu.)

 

c)      Soma Ayubu 2:4-5. Unaweza kuelezeaje mantiki ya hoja ya Shetani? Ninaielewa kauli ya “kuyatoa yote aliyonayo [mtu] kwa ajili ya uhai wako,” lakini je, hilo linahusianaje na kumkufuru Mungu? (Tunu ya Ayubu maishani mwake ni uhusiano wake na Mungu. Ikiwa Mungu anaonekana kukata tamaa na hivyo kushindwa kumlinda Ayubu, ikiwa Mungu anamwadhibu Ayubu kimakosa, basi Shetani anadhani kuwa Ayubu ataachana na rasilimali yake ya muhimu kuliko zote, yaani, uhusiano wake na Mungu.)

 

d)     Soma Ayubu 2:6. Je, tungekuwa wapi Mungu asingekuwepo? (Shetani angemwua Ayubu, na angependa kukuua.)

 

2)      Shambulizi Dhidi ya Ayubu Mwenyewe

 


a)      Soma Ayubu 2:7-8. Jambo gani katika taswira hii linakufanya ujisikie vibaya? (Hakuna anayemsaidia Ayubu kupata matibabu. Anaomboleza, anakaa kwenye majivu, na kujikuna.)

 

i)        Je, ni sahihi kwa Ayubu kuhisi kwamba Mungu anamwadhibu?

 

(1)   Soma Mathayo 27:46. Ikiwa umesema kuwa, “ndiyo, Ayubu anapaswa kuhisi kuwa Mungu anamwadhibu au amemwacha,” basi ongezea hilo kwenye matatizo yote yaliyomkabili Ayubu. Je, utajibuje?

 

b)      Soma Ayubu 2:9. Nani anayepaswa kukutia moyo na kukuinua pale unapokuwa mgonjwa au kukata tamaa? (Mwenzi wako!)

 

i)        Hebu tuyaangalie maneno ya mkewe kwa makini.  Je, anguko lake ni kushindwa kumtia moyo Ayubu kwa usahihi au ni zaidi ya hapo? (Anamwambia Ayubu kuwa afe. Kuna jambo lisilo sahihi kabisa hapa. Ama ana uhusiano mbaya na Ayubu, au ana uhasama na Mungu. Au huenda vyote viwili. Huenda ana hasira kali sana kuhusu kupoteza hadhi yake kama mke wa mtu tajiri kutoka upande wa Mashariki.)

 

ii)      Kwa nini Shetani hakumwua mke wa Ayubu wakati alipokuwa anawaua watoto wa Ayubu?

 

iii)    Hebu tuangalie mantiki ya pendekezo la mke wa Ayubu. Anamkaripia Ayubu kwa kung’ang’ania “utimilifu” wake. Kwa nini utimilifu wa Ayubu ni sehemu ya tatizo?

 

(1)   Niliangalia uelewa wa Strong juu ya neno la Kiebrania, linaashiria kuwa “utimilifu” humaanisha “kutokuwa na hatia.” Je, hiyo inakusaidia kuelezea kauli ya mkewe? (Mke wa Ayubu anaweza kuwa anasema kuwa Ayubu haelewi kuwa Mungu amemwangusha. Haelewi mambo ya uhalisia ya dunia hii, mahali ambapo miungu si marafiki wako.)

 

c)      Soma tena Ayubu Job 2:3 na Ayubu 2:9. Je, umegundua kwamba tunaona neno lile lile “utimilifu?” Kwa mujibu wa Strong, mzizi wake ni ule ule kwa Kiebrania. (Mungu hatumii neno hilo kwa maana ya “kutokuwa na hatia,” badala yake Mungu analitumia kumaanisha haki au kujitoa kwa bidii kwa Mungu.)

 

i)        Ikiwa mke wa Ayubu analitumia neno hili, “utimilifu,” kwa namna ile ile ambayo Mungu analitumia, je, mke wa Ayubu anaashiria nini? (Anamwambia ageuke na kumwacha Mungu. Hiyo inatusaidia tuelewe ushauri wake wa “umkufuru Mungu” (Ayubu 2:9). Kati ya hizi maana mbili, mke wa Ayubu anapendekeza kuwa Ayubu aachane na utii wake kwa Mungu.)

 

(1)   Hata kama Mungu amemwacha Ayubu, au si rafiki yake, unaelezeaje pendekezo lake la kumkufuru Mungu? (Ana hasira, chuki, na mwenye kutaka kulipiza kisasi (asiyesamehe).)

 

d)     Soma Ayubu 2:10. Unadhani Shetani anaichukuliaje kauli ya Ayubu? (Kwa mara nyingine tena Shetani amekosea! Ayubu anaendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu. Yeye ni shujaa wa kweli wa Mungu!)

 


i)        Hebu tuangalie kwa undani zaidi alichokisema Ayubu. Kwa kuwa tumejadili ushauri wa mkewe, jibu la Ayubu linaweza kutusaidia kuelewa vizuri zaidi kile ambacho mkewe alikipendekeza. Ayubu anasema nini juu ya ushauri wake? (Anasema kuwa ni “upumbavu,” tunaweza kuelewa alimaanisha “bila kuwa na mantiki.”)

 

ii)      Tafsiri ya Biblia ya NIV ina rejeo/tanbihi inayosema kuwa kwa Kiebrania “upumbavu” maana yake ni “kutokuwa na maadili.” Je, hiyo inaelezea vizuri zaidi ushauri wa mkewe? (Mke wa Ayubu amejiingiza kwenye shambulio la Shetani. Hamkatai Mungu tu, bali pia anamshambulia. Hili linaweza kuonekana kuwa ni jambo jema, lakini si sahihi kimaadili.)

 

iii)    Kwa kuwa hapo awali tulijadili mfanano uliopo dhidi ya ule wa kwenye jaribu la Eva lililopo katika Mwanzo 3, unadhani Shetani angefaulu endapo angemjaribu Adamu kwanza? (Soma Mwanzo 3:12. Adamu sio Ayubu.)

 

e)      Hebu tuangalie mantiki iliyopo kwenye sehemu ya mwisho ya kauli ya Ayubu katika Ayubu 2:10. Je, matatizo ya Ayubu yalitoka kwa Mungu? (Kwa dhahiri Mungu hakuwa mwanzilishi wa matatizo hayo. Halikuwa wazo la Mungu. Hata hivyo, Mungu aliruhusu yatokee. Ayubu 2:3 inatuonesha kuwa Mungu hafurahishwi na mateso ambayo Ayubu anayapitia.)

 

i)        Je, hii inatufundisha nini kuhusu kuteseka kwetu?

 

ii)      Mara kwa mara huwa ninawasikia watu wakisema kuwa wanapata mateso kwa sababu “Mungu anawajaribu.” Je, hitimisho hilo lina mantiki kutokana na kile tulichokwishajifunza hadi sasa? (Hapana. Utakumbuka Kumbukumbu la Torati 28 inatuambia kuwa tunapata kile tunachostahili – tii nawe utabarikiwa, usiwe mtii nawe utapata mateso. Kimsingi, hivi ndivyo ambavyo Ayubu anaielewa dunia. Kisa cha Ayubu kinatupatia uelewa mpana wa pambano kati ya Mungu na Shetani na jinsi linavyotuathiri.)

 

iii)    Kwa kuwa tulianza kwa kujadili mwisho wa kisa, tunajua kwamba kimsingi Mungu alimwambia Ayubu, “Mimi ni Mungu na wewe si Mungu, kaa chini na unyamaze kimya.” Kwa nini Mungu hakutumia jibu hilo hilo kwa Shetani? “Mimi ni Mungu na wewe si Mungu. Nakwambia kuwa Ayubu hatanikufuru kwa hiyo kaa kimya na usimdhuru!” (Kwa kuwa mambo haya yanatokea kwenye kikao cha watumishi, wajumbe kutoka kwenye ulimwengu wote uliosalia wako makini kusikiliza huu mjadala.)

 

f)       Soma Ayubu 2:11. Marafiki wa Ayubu walipatana kwa pamoja kuwa na lengo gani? (Kumlilia na kumtuliza moyo.)

 

g)      Soma Ayubu 2:12-13. Unaizungumziaje hii njia ya kuwahurumia na kuwafariji watu wanaoteseka?

 

i)        Hatutajadili kwa kina juu ya mazungumzo baina ya Ayubu na mafariki wake kwa sasa. Lakini, ili kufahamu mambo waliyoyasema marafiki wake baadaye, soma Ayubu 4:5-9. Hii inafananaje na njia ya kwanza aliyoitumia huyu rafiki? (Baadaye marafiki wanajaribu kuelezea sababu za mateso ya Ayubu – na wanadhani kuwa kosa ni la Ayubu kwa sababu wanafahamu nadharia ya “tii nawe utabarikiwa, usiwe mtii nawe utalaaniwa.” Ilikuwa vyema zaidi kulia pamoja na Ayubu na kukaa naye kimya.)

 

ii)      Huwa unasema nini pale unapojaribu kumfariji mtu aliye kwenye mateso?

 


h)      Rafiki, tumejifunza nini kivitendo tunapowatembelea watu wanaoteseka? Wakati mwingine ule uwepo wetu tu na kuwahurumia ni jambo bora zaidi. Kufafanua/kuelezea sababu za mateso ni jambo la hatari. Jambo baya zaidi ni kudhoofisha imani kwa Mungu. Je, utatumia mafunzo uliyoyapata kutoka kwa Ayubu wakati mwingine utakapojaribu kuwafariji watu?

 

3)Juma lijalo: Mungu na Mateso ya Wanadamu.