Kutoka Katika Upepo wa Kisulisuli

Swahili
(Ayubu 38 - 42)
Year: 
2016
Quarter: 
4
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tunazifahamu hoja, je, ni kweli? Marafiki wa Ayubu wanajenga hoja kwenye kanuni ya kawaida: kwamba kutokutii husababisha matatizo na utii huleta mibaraka. Lazima Ayubu atakuwa hakuwa mtiifu kwa sababu anakabiliwa na matatizo mengi. Ayubu anapinga kwa kutoa madai kuwa yeye ni mwenye haki na kwamba hastahili mateso anayoyapitia. Haki haikutendeka kwake na anamtaka Mungu ampe nafasi ya kumsikiliza ili aweze kuelezea mashtaka dhidi yake. Tukiwa kama hadhira inayofahamu ukweli, tunaweza kusema kwamba pande zote mbili zinasema ukweli. Marafiki wako sahihi juu ya kanuni za kawaida, na Ayubu yuko sahihi juu ya haki yake. Juma hili, Mungu anaingilia kati. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tusikilize kile anachokisema Mungu!

 

1)      Mashtaka ya Mungu

 

a)      Soma Ayubu 38:1-3. Kuna habari gani njema kwenye ujumbe huu kutoka kwa Mungu? (Inaonekana kama vile Ayubu anaelekea kuupata usikivu ambao amekuwa akiuomba.)

 

i)       Mungu anasema kuwa Ayubu anatia “giza” mashauri ya Mungu kwa “maneno yasiyo na maarifa.” Nilidhani tulihitimisha kwamba Ayubu alikuwa sahihi juu ya yeye kuwa mwenye haki. Kwa kuwa Mungu anapaswa kuwa sahihi, je, Mungu anazungumzia jambo gani? (Ayubu hana uelewa wa habari kamili.)

 

ii)     Ayubu anatiaje mazungumzo “giza”? (Anabainisha kwa lugha nyepesi, na kufunika kwa njia ya giza. Ayubu anabainisha kutokuelewa kwake, hivyo mawazo yake yanatatanisha (yanatia giza) kweli zilizopo.)

 

iii)   Mungu anajibu “katika upepo wa kisulisuli.” Unadhani Ayubu alikuwa katika hali gani? (Utakumbuka kwamba upepo uliwaua watoto wa Ayubu. Ayubu 1:18-19.)

 

b)      Soma Ayubu 38:4-7 na Ayubu 39:19-20. Majibu kwa maswali ya Mungu ni yapi? (Hapana. Ayubu hakuiumba dunia au mnyama yoyote.)

 

i)       Nimechomoa baadhi ya maswali kutoka sura ya 38 na 39. Maswali yote ya Mungu yaliyosalia yapo kwenye mwelekeo wa aina moja. Kama ungekuwa mwanasheria wa Ayubu, na kwamba mashtaka haya yalikuwa halisi, je, ungesema nini? (Ningepinga kwa mujibu wa uhusiano. Alichokiomba Ayubu ni kwamba mashtaka dhidi yake yawekwe hadharani ili aweze kuyajibu. Maswali haya yanakabiliana na umahiri wa Ayubu maishani.)

 

 

c)      Soma Ayubu 40:1-2. kama ungekuwa mwanasheria wa Mungu, ungejibuje kwenye pingamizi la uhusiano? Swali hili linaashiria nini juu ya jibu la Mungu? (Madai ya Ayubu ya kutaka kusikilizwa yana nadharia isiyo ya kweli. Nadharia hiyo ni kwamba Mungu anawajibika kisheria kumjibu Ayubu. Maswali ya Mungu yanaitia changamoto nadharia hii. Ayubu ni nani hadi amuulize Mungu maswali? Mwanadamu ana uzoefu na umahiri wa namna gani kiasi cha kumpa Mungu changamoto? “Je, mwenye hoja atashindana na Mwenyezi Mungu?”

 

2)      Jibu la Ayubu kwa Maswali ya Mungu ya Kiuchunguzi

 

a)      Soma Ayubu 40:3-5. Unalichukuliaje jibu la Ayubu? Amekuwa akidai kwamba mashtaka dhidi yake yabainishwe. Jambo hili linaendanaje na nafasi ya Ayubu ya awali? (Ayubu ameyaondoa madai yake ya kutaka kusikilizwa. Ametambua kwamba hastahili kudai yote hayo kutoka kwa Mungu.)

 

i)       Je, hili ni fundisho kwa ajili yetu leo? Tunapojaribiwa kusema kwamba Mungu hatendi haki, je, tunapaswa tu kuweka mikono yetu kwenye vinywa vyetu na kukaa kimya?

 

(1)   Maelezo ya kitabu cha Mwanzo juu ya Uumbaji na Anguko yanaonesha kuwa Mungu aliwapatia wanadamu uhuru wa kuchagua. Tunaweza kumkataa Mungu. Je, uhuru wetu wa kuchagua tuliopewa na Mungu unaendana na wazo la kwamba Mungu anapoonekana kutuangusha, tunapaswa kufunika vinywa vyetu na kukaa kimya?

 

b)      Soma Ayubu 40:8. Je, umewahi kusikia jambo hili? (Soma Ayubu 8:1-3, Ayubu 34:5 na Ayubu 34:12. Ikiwa marafiki wanasikiliza maswali ya Mungu ya kiuchunguzi, yumkini wanapiga kelele na kushangilia “Endelea Mungu, mwambie! Hiki ndicho ambacho kwa hakika tumekuwa tukimwambia Ayubu.”)

 

c)      Soma Ayubu 40:11-14. Nataka nijikite kwenye fungu la 14. Tunapotenda dhambi, je, tunamkosea nani? (Katika Zaburi 51:3-4 Daudi anasema “Nimekutenda dhambi Wewe peke yako.” Tunaweza kuwadhuru watu wengine kutokana na dhambi zetu, lakini dhambi i dhidi ya Mungu peke yake.)

 

i)       Mungu anaposema katika Ayubu 40:11-14 kwamba anaweza kumpondaponda mtu mwovu mwenye kiburi, inaleta mantiki kwamba anafanya hivi kutokana na dhambi yetu dhidi Yake. Kuna fundisho gani katika Ayubu 40:14? (Kuhesabiwa haki kwa njia ya imani. Kama ilivyokuwa kwa Ayubu, hatuwezi kukabiliana na Mungu. Kamwe “mkono wetu wa kuume” hauwezi kutuokoa. Tumaini letu pekee lipo kwenye kile ambacho Yesu ametutendea.

 

d)      Soma Ayubu 41:11. Mungu anasema nini juu ya mtazamo kwamba Mungu anawajibika kwa namna fulani hivi kwa wanadamu?

 

i)       Hadi sasa hoja ya Mungu imekuwa ikihusu uwezo na mamlaka. Kwa dhahiri, Mungu anavyo vyote viwili. Je, uwezo unapaswa kutoa majibu kwa vitendo visivyo vya haki?

 

3)      Hitimisho la Ayubu

 

a)      Soma Ayubu 42:1-3. Ubashiri wangu ni kwamba takribani kila mtu alijibu swali lililotangulia la “Ndiyo, uwezo unapaswa kuwajibika kwa vitendo visivyo vya haki.” Je, sasa Ayubu anatoa jibu gani? (Kama ambavyo kwa ujumla ni kweli kwamba matendo sahihi huleta mibaraka na matendo mabaya huleta matatizo, vivyo hivyo kwa ujumla ni kweli kwamba uwezo na mamlaka vinapaswa kuwa vya haki. Hata hivyo, katika hii hali mahsusi, Ayubu anasema “sikufahamu.” Tunawezaje kumwita Mungu aje atoe maelezo wakati hatujui kweli zote?

 

b)      Soma Ayubu 42:4-6. Nini kinamfanya Ayubu aseme, “najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu?” (Ayubu anakutana na Mungu wa Ulimwengu.)

 

 

i)       Je, Mungu ana haja ya kujibu viwango vyetu? (Hapana. Mungu anasema kuwa aliumba kila kitu. Hafananishwi na mwanadamu mwenye uwezo mkuu na mamlaka. Kiuhalisia aliumba na anamiliki kila kitu. Hawajibiki kwa wanadamu. Hahitaji kujielezea.)

 

ii)     Ikiwa unakubaliana kwamba Mungu hahitaji kujielezea kwetu, je, unatoa maelezo gani juu ya Ayubu 1 & 2? Kwa nini Mungu anatufunulia kisa chote? (Kwa sababu Mungu anatupenda. Kwa kuwa anatupenda, anataka turidhike na maamuzi yake, kivyovyote vile hawajibiki kwetu, lakini kutokana na upendo wake anatupatia maelezo.)

 

4)      Marafiki

 

a)      Soma tena Ayubu 42:6. Unadhani marafiki wa Ayubu wanafikiria nini katika hatua hii? (Bila shaka wanajisikia furaha maneno yao kuthibitishwa kutokana na kile alichokisema Mungu. Inaonekana walikuwa sahihi, na sasa Ayubu ametubu.)

 

b)      Soma Ayubu 42:7-8. Mambo yamebadilika! Sasa, nani yuko sahihi? (Mungu anasema kuwa marafiki “hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.” Hivyo, Ayubu yupo karibu zaidi na ukweli kuliko marafiki.)

 

i)       Hii inawezaje kuwa kweli kwa sababu Ayubu alishatubu (Ayubu 42:6)? Kibaya zaidi ni kwamba, katika somo letu Mungu alianza kwa kusema kuwa Ayubu alikuwa “anatia giza” mashauri ya Mungu kwa “maneno yasiyo na maarifa” (Ayubu 38:2). Unaelezeaje jambo hili? (Mambo mawili. Kwanza, Ayubu yuko kwenye tishio na hii inawafanya watu waseme mambo ambayo katika hali ya kawaida wasingeyasema. Marafiki hawako chini ya tishio na hawana huruma kiasi hicho. Pili, Ayubu yuko sahihi kwamba yeye ni mtu mwenye haki ambaye hastahili mambo yaliyomtokea. Ingawa marafiki wanasema ukweli wa jumla, kanuni ya jumla huwa haihusiki nyakati zote. Hawamwakilishi Mungu wanapochukulia kwamba mambo magumu yanayotokea maishani kila mara yanaakisi kutokuwa na utiifu kwa Mungu.)

 

c)      Soma Waebrania 11:35-38. Ukisoma muktadha wa hivi vifungu, utaona kwamba baadhi ya mashujaa wa imani waliteseka na kupitia mambo ya kutisha. Ni kwa jinsi gani wanafanana na Ayubu? Hii inapaswa kuathirije mtazamo wetu juu ya kanuni ya jumla?

 

d)      Soma tena Ayubu 42:7. Mungu anazungumza na marafiki wangapi? (Elifazi na marafiki wake wawili, Bildadi na Sofari.)

 

i)       Marafiki wangapi walikuwa wanahojiana (wanabishana) na Ayubu? (Soma Ayubu 2:11 na Ayubu 32:1-4. Pamoja na marafiki watatu wa awali, tulitumia somo zima kujadili hoja ya Elihu iliyojaa hasira dhidi ya Ayubu.)

 

e)      Kwa nini Mungu hamhukumu Elihu au kumtaka amsihi Ayubu amwombee? (Tulipojifunza kauli za Elihu juma lililopita, tuliona kwamba baadhi ya kauli zilikuwa sawa (zilifanana) na zile zilizotolewa na marafiki watatu wazee. Lakini, kauli nyingine zilikuwa tofauti. Kwa mfano, katika Ayubu 32:8-9 na Ayubu 32:18-19 Elihu anadai kwamba Roho Mtakatifu ananena kupitia kwake. Hapo awali hatukusoma hoja zote za Elihu, lakini katika Ayubu 36:22-23 Elihu anajenga hoja kwamba wanadamu hawana nafasi ya kumshtaki Mungu kwamba ametenda mambo mabaya. Ukipitia kwa haraka haraka Ayubu 36:26-37:24, utaona kwamba Elihu anatoa kauli ile ile ya “Mungu ni Mungu na wewe si Mungu,” kauli ambayo Mungu anaitoa katika sura inayofuata. Mambo ya muhimu kuzingatia ni kwamba Elihu anatarajia mambo ambayo Mungu atayasema, na nadhani hiyo ndio sababu hahukumiwi.)

 

 

f)       Rafiki, nadhani fundisho kwetu ni kwamba tusifanye haraka kuwahukumu watu wengine pale tunapotumia mantiki ya kibinadamu, badala ya kuichunguza dhambi halisi. Elihu anatufundisha kwamba njia bora ya kuithibitisha tabia ya Mungu ni kujielekeza kwenye utukufu Wake, badala ya kujielekeza kwenye dhambi za wanadamu. Je, utatafakari upya jinsi unavyokabiliana na dhambi ya dhahiri kwenye maisha ya watu wengine?

 

Juma lijalo: Mkombozi wa Ayubu.