Nafsi ya Roho Mtakatifu

Swahili
(Yohana 14-15, Warumi 8)
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mara ngapi nimetumia neno “It” ninapomzungumzia Roho Mtakatifu? Mara nyingi sana! Huenda nawe pia umelitumia neno hilo. Huenda bado unalitumia! Je, neno “He” linaonekana kuwa sahihi kwa mtu anayelinganishwa na upepo? Mtu anayeweza kuwepo kila mahali kwa wakati mmoja? Mtu ambaye sio tu kwamba anakaa ndani yako, bali pia anakaa ndani ya Wakristo kila mahali? Ni vigumu kuizuia akili yako isizifikirie hizi dhana. Hata hivyo, nadhani ni rahisi kuelewa kwamba Roho Mtakatifu ni “He” ikiwa tutajikita kwenye nafsi yake, na si katika mfumo aliyopo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

1.      Mfariji [Msaidizi]

 

1.1.   Soma Yohana 16:2-5. Orodhesha mambo yote aliyoyasema Yesu yatakayowafanya wanafunzi wasikitike na kuhuzunika? (Hawataweza kuabudu “kanisani.” Watu watawaua wakidhani kwamba ni vyema kufanya hivyo. Yesu anawaacha.)

 

1.2.   Soma Yohana 16:6 na Matendo 1:6. Hatuwezi kutambua kiwango kamili cha upotevu walichokihisi wanafunzi isipokuwa tu kama tutakipima kiwango hicho dhidi ya tumaini lililopotea. Walitumaini jambo gani? (Kwamba Yesu atakuwa Mfalme wa Israeli, atawashinda Warumi, nao [wanafunzi] watakuwa watawala wakuu.)

 

1.2.1.      Sasa, hebu niambie jinsi orodha hii ya kupoteza kila kitu ilivyo pigo la kutisha kwao?

 

1.3.   Soma Yohana 16:6-7. Yumkini jambo gani linaweza kujazilizia upotevu tuliouorodhesha? (Kuwasili kwa Roho Mtakatifu.)

 

1.3.1.      Hivi karibuni tumekuwa tukiviangalia vifungu hivi katika kitabu cha Yohana kwa namna mbalimbali. Tunapopoteza mambo fulani na kuhuzunika, tunahitaji kufarijiwa. Tunaweza kumtumia mshauri. Hiyo inaashiria nini kuhusu nafsi ya Roho Mtakatifu kiasi cha Yesu kumuita kuwa “Msaidizi?” (Mtu pekee anayeelewa upotevu na huzuni anaweza kuwa mshauri mwenye mantiki.)

 

1.4.   Soma Yohana 14:16-18. Anachokisema Yesu hapa kinafanana sana na kauli yake katika Yohana 16. Hebu tujikite kwenye kifungu cha 18. Yesu anasema kuwa hatawaacha wanafunzi yatima. Hebu nielezee hiyo picha ya maneno. Mahitaji ya yatima ni yapi? (Yatima hawana wazazi, wanamhitaji mtu ambaye atawasaidia na kuwalinda.)

 

1.4.1.      Je, Roho Mtakatifu naye atatutendea vivyo hivyo? Ikiwa ndivyo, hiyo inazungumzia nini juu ya nafsi ya Roho Mtakatifu? (Ana uelewa wa kina unaoweza kuutarajia kutoka kwa mzazi. Ana uwezo wa kuelewa na kutoa msaada katika nyakazi za huzuni na zenye kuhitaji msaada.)

 

1.4.2.      Unadhani Yesu amechagua tu neno “yatima” kutoka hewani kama analojia nzuri? Au, je, kimsingi neno hilo linaakisi hali wanayokabiliana nayo wanafunzi? (Yesu alimzungumzia “Baba” yake. Dhana iliyopo ni kwamba Mungu ni mzazi wetu ambaye kamwe hafi, yupo siku zote. Yesu alitimiza wajibu huo kwa wanafunzi, na kisha Roho Mtakatifu alichukua wajibu huo kuanzia pale Yesu alipoishia. Inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayesimama kati yetu na Utatu Mtakatifu.)

1.5.   Soma Yohana 15:26-27. Wanafunzi wanashiriki jukumu na Roho Mtakatifu: kumshuhudia Yesu. Unadhani Roho Mtakatifu anatekelezaje jambo hilo?

1.5.1.      Unawezaje (unamshuhudiaje) kumshuhudia Yesu?

1.5.2.      Jiulize, “Jambo gani linaweza kumshawishi mtu kumfuata Yesu?” (Ujumbe wa awali unaweza kuwa ni kwamba Yesu atakupatia tumaini la kuishi maisha bora katika siku zijazo. Ikiwa hiyo ndio njia anayoitumia Roho Mtakatifu, tunaona kwamba anawafariji na kuwapa tumaini wale walio na wasiwasi juu ya siku zijazo.)

2.      Mwongozo wa Maisha

2.1.   Soma Warumi 8:1-3. Tunawekwaje huru dhidi ya mauti ya milele? (Kwa kupokea na kukiri kile alichotufanyia Yesu msalabani. Yesu alitenda kile ambacho sheria isingeweza kukitenda, anatuweka huru dhidi ya dhambi na mauti.)

2.1.1.      Angalia tena sehemu ya mwisho ya Warumi 8:3. Yesu ana mtazamo gani dhidi ya dhambi? (“Aliihukumu dhambi katika mwili ulio wa dhambi.” Yesu haidhinishi dhambi. Alikuja kuishinda dhambi.)

2.2.   Soma Warumi 8:4. Yesu anataka nini kutoka kwetu kinachomhusisha Roho Mtakatifu? (Tunaona mambo mawili yanayokinzana: asili ya dhambi na kuishi kwa mujibu wa uongozi wa Roho Mtakatifu. Tumeambiwa tuishi “kwa kufuata mambo ya Roho.”)

2.2.1.      Je, tunapaswa kuishi ndani ya Roho Mtakatifu ili “maagizo ya torati”? yatimizwe kikamilifu?

2.2.2.      Hii inaashiria nini kuhusu nafsi ya Roho Mtakatifu?

2.3.   Soma Warumi 8:5. Wajibu wetu ni upi katika kuishi maisha makamilifu? (Ama tuyaweke mawazo yetu “kwenye mambo ambayo Roho anayatamani” au kwenye “mambo ambayo asili [ya dhambi] inayatamani.” Tunatakiwa kuyaweka mawazo yetu kwenye matamanio ya Roho Mtakatifu.)

2.3.1.      Je, umefikiria juu ya wajibu wa kuchagua kwamba uyaweke mawazo yako juu ya nini?

2.3.1.1.            Je, huu ndio uchaguzi mmoja unaoufanya asubuhi? (Kwa uzoefu wangu, ni uchaguzi endelevu. Ninaendelea kuuchukua [kuufanya] huu uamuzi.)

2.4.   Soma Warumi 8:6-8. Huu ni uchaguzi wa muhimu kiasi gani? (Hatuwezi kumpendeza Mungu ikiwa mawazo yetu yanadhibitiwa na asili yetu ya dhambi.)

2.4.1.      Je, tunapaswa kuishi kwa kufuata mambo ya Roho ili kuifurahia neema? Je, hicho ndicho kinachomaanishwa kwenye hivi vifungu?

 

2.5.   Soma Yohana 5:24-25 na Warumi 10:13. Hizi rejea mbili zinaniambia kuwa nikimwita Mungu, ikiwa ninaamini kwamba Mungu alimtuma Yesu, nitaokolewa. Unahusianishaje jambo hilo na kauli zilizopo katika Warumi 8 kwamba ninatakiwa kuyaweka mawazo yangu juu ya mambo ambayo Roho Mtakatifu anayatamania ili kumpendeza Mungu?

 

2.5.1.      Utaona kuwa Yohana 5:24 inaonekana kurejea uamuzi mmoja – kwamba mtu anayesikia na kuamini “amekivuka kifo na kuingia kwenye uzima.” Unaelezeaje jambo hilo? (Ufafanuzi wangu ni kwamba Warumi 8:5-7 inaelezea aina ya maamuzi ambayo Mungu anayatamani kutoka kwetu. Mungu anatutaka tumwite kila wakati. Hii ndio maana ya kuyaweka mawazo yetu juu ya mambo ambayo Roho Mtakatifu anatamani tuyafanye. Inaonekana kuleta mantiki kwamba ikiwa kweli unamwamini Yesu, basi umefanya uamuzi kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, na hutaishi maisha ya “uadui juu ya Mungu.”)

 

2.6.   Soma Warumi 8:9. Tafakari jambo hili kidogo. Kifungu hiki kinazungumzia nini juu ya nafsi ya Roho Mtakatifu na wajibu wake maishani mwako?

 

2.7.   Soma Warumi 8:10-11. Hebu tuangalie jambo hili. Kifungu kinaposema kuwa, “mwili umekufa kwa sababu ya dhambi,” unadhani hiyo inamaanisha nini? (Sisi ni wadhambi. Adhabu ya dhambi ni mauti.)

 

2.7.1.      Kwa nini Yesu alikufa? (Alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Tunaona mwelekeo huu kwenye hivi vifungu kati ya dhambi zetu ziletazo mauti na dhambi zetu ambazo Yesu alizifia.)

 

2.7.1.1.            Tiba moja ya dhambi hizi zisababishazo mauti ni ipi? (Uwezo wa Roho Mtakatifu. Anatupatia uzima kama alivyompa Yesu uzima.)

 

2.8.   Soma Warumi 8:12-13. Kutokana na kile tulichokijadili muda mfupi uliopita, tunao wajibu gani? (Paulo ametuambia kuwa Roho Mtakatifu anatupatia uzima, hata kama tulikuwa tumekufa dhambini. Je, utajisikia kuwajibika kwa mtu aliyeyaokoa maisha yako? Naam, hakika! Wajibu huo ni “kuyafisha matendo ya mwili.”)

 

2.8.1.      Je, matendo yetu yanahusika? (Ndiyo. Yohana 5:24 inatuambia kuwa imani inatuvusha kutoka kwenye kifo na kutupeleka kwenye uzima wa milele. Warumi inatuambia kuwa kuachana na matendo mabaya ni “wajibu.” Unaokolewa na unawajibika.)

 

2.8.1.1.            Tunawezaje kuachana na matendo mabaya? (“Kwa njia ya Roho Mtakatifu.”)

 

2.9.   Soma Warumi 8:14-16. Unapotenda dhambi, je, inasababisha hofu ndani yako? Hofu kwamba utakamatwa? Hofu kwamba mazingira halisi yatakudhuru? (Hii inatuambia kuwa maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu yanatuweka huru dhidi ya hofu. Maisha hayo yanatupatia uhuru wa kufurahia kama wana na binti wa Mungu.)

 

2.9.1.      Hebu turejee nyuma kidogo na tutafakari jambo hili. Tunaishi katikati ya pambano kati ya wema na uovu. Mungu ametuokoa na kutupatia maelekezo ya namna ya kuishi maisha bora sasa hivi. Je, matendo yetu yanajalisha? Je, kazi zetu zinajalisha? (Chukulia kwamba ulikuwa vitani – kwenye vita halisi. Je, inajalisha ikiwa ulifuata maelekezo ya kamanda wako? Je, inajalisha ikiwa ulianza kuwafyatulia raisasi maaskari wenzako? Je, inajalisha ikiwa ulianza tu kutembea na kuvuka msitari kuelekea kwa maadui? Kimsingi mambo haya yanahusika. Wazo la kwamba unadai kuwa na Yesu mara moja, na kisha baadaye kutomzingatia, haileti matiki kabisa.)

 

2.10.                    Soma tena Warumi 8:16. Je, roho yako ina nafsi? (Roho yako ndio nafsi yako.)

2.10.1.  Ukweli kwamba Roho Mtakatifu “hushuhudia pamoja na roho zetu” hutufundisha jambo gani juu ya nafsi ya Roho Mtakatifu? (Kwa dhahiri Roho Mtakatifu sio fungu la upepo. Yeye ni mwombezi hai kati ya Utatu Mtakatifu na mawazo yako.)

2.11.                    Soma Warumi 8:26-27. Roho Mtakatifu anaweza kutusaidia kwa njia gani nyingine? (Kwa maombi yetu. Hii inatuambia kuwa Roho Mtakatifu “anatuombea kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu.” Roho Mtakatifu atazisaidia juhudi zetu dhaifu kuomba.)

2.11.1.  Ninapofikiria suala la kuombewa, ninafikiria kile anachotufanyia Yesu mbinguni (Waebrabia 8-9), na ninawafikiria wanasheria mahakamani. Hii inahitaji ustadi wa kiwango gani? Hii inazungumzia nini juu ya Roho Mtakatifu kuwa na nafsi?

2.12.                    Rafiki, unamhitaji Roho Mtakatifu ndani yako kwa udi na uvumba. Unamhitaji akufariji, ayaongoze matendo yako, na akuongoze na kukuombea unapomwendea Mungu katika maombi [sala]. Je, utamwomba Roho Mtakatifu, sasa hivi, akae ndani yako?

Juma lijalo: Ubatizo na Ujazo wa Roho Mtakatifu.