Kazi ya Roho Mtakatifu

Swahili
(Yohana 16)
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Inamaanisha nini kumsikiliza Roho Mtakatifu? Ninaposoma Biblia ili kuandika masomo haya, ninapata utambuzi mpya ambao sikuwa nimeuwaza hapo awali. Nadhani huyo ni Roho Mtakatifu. Bila shaka hali hiyo pia inakutokea unapokuwa unajifunza Biblia. Lakini, nadhani kuna dhana kubwa zaidi katika suala la kumsikiliza Roho Mtakatifu. Watu ambao kweli wamejifungamanisha na Roho Mtakatifu wanaongozwa kuchukua hatua au kuepuka matendo fulani. Mke wangu alianza kupata ushawishi wa kumchangia fedha mwanafunzi fulani mahsusi. Alimfahamu mwanafunzi huyu, japo hakumfahamu kiundani. Mke wangu aliendelea kupata ushawishi huo hadi alipoamua kuandika hundi na kuituma. Alipokuwa anaandika hundi, alikuwa na ushawishi wa kiasi cha fedha ambacho alitaka kukituma. Baada ya kuituma hundi hiyo, mwanafunzi huyu alimpigia simu na kumwambia kuwa kiasi cha fedha alichomtumia ndicho kiwango halisi alichokihitaji katika hitaji lake, na kilimfikia katika siku ya mwisho kabisa ya uhitaji wa fedha hizo. Hebu tuzame kwenye Biblia zetu ili tujifunze zaidi juu ya kujifungamanisha na Roho Mtakatifu!

 

 1. Maelekezo Juu ya Dhambi

 

  1. Soma Yohana 16:5-6. Wanafunzi walijisikiaje baada ya Yesu kuwaambia kuwa alikuwa anawaacha? (Walihuzunika sana kiasi kwamba hawakuweza kufikiri vizuri. Walishindwa kuuliza swali la dhahiri kabisa, “Unakwenda wapi?”)

 

  1. Soma Yohana 16:7. Yule ambaye Yesu anamwita “Msaidizi” ni Roho Mtakatifu. Kati ya majina yote ambayo Yesu angeweza kuyatumia kumwita Roho Mtakatifu, kwa nini anamuita Msaidizi? (Linaendana kikamilifu na kile ambacho Yesu anataka kutuelezea. Roho Mtakatifu atachukua jukumu la Yesu kwa wanafunzi – jukumu la kuwafundisha kumjua Mungu vizuri zaidi na jinsi wanavyopaswa kuishi.)

 

   1. Je, ahadi hii pia iko wazi kwa ajili yetu?

 

  1. Soma Yohana 16:8. Roho Mtakatifu anatusaidia katika mambo gani matatu? (Hatia (itokanayo na dhambi), haki na hukumu. Utaona kwamba kwenye jibu kwa swali langu lililotangulia Yesu anasema Roho Mtakatifu “atauhakikisha ulimwengu.” Hiyo inamaanisha kuwa nasi tumejumuishwa!)

 

   1. Kwa kuangalia jambo hili, je, mambo haya yanaonekana kuwa ya bashasha – hatia, haki na hukumu?

 

  1. Soma Yohana 16:9. Hebu kwanza tujikite kwenye kuhakikishwa dhambi. Ni kwa namna gani mahsusi Roho Mtakatifu anatuhakikisha kwa dhambi? (Hii inahusiana na wanadamu kutomwamini Yesu.)

 

   1. Kumwamini Yesu kuna umuhimu gani kwenye hatia juu ya dhambi? Kuna msingi gani wenye mantiki kusema hivyo? Viongozi wa Kiyahudi waliomkataa Yesu waliamini katika dhambi. Kwa nini imani kwa Yesu ni muhimu linapokuja suala la hatia?

 

   1. Soma Ufunuo 12:10-11. Nani anayetushtaki kwa dhambi zetu? (Shetani ndiye anayetushtaki kwa dhambi zetu.)

 

 

   1. Soma 1 Yohana 5:10-12. Imani ipi kwa Yesu iliyo ya muhimu sana katika uelewa wetu wa dhambi? (Ni kwa njia ya maisha na kifo cha Yesu ndio tunashinda mashtaka ya Shetani. Hivyo, kama humwamini Yesu, umepotea. Roho Mtakatifu anatugusa kwa kutuhabarisha kwamba Yesu ndiye suluhisho la dhambi na hatia yetu. Sasa, hiyo ni habari njema!)

 

 1. Maelekezo Juu ya Haki

 

  1. Soma Yohana 16:10. Biblia inaposema kuwa Roho Mtakatifu atauhakikisha ulimwengu kwa haki “kwa sababu [Yesu] anaenda kwa Baba,” unadhani hiyo inamaanisha nini? (Yesu anaondoka. Wanafunzi wanahitaji maelekezo ya jinsi ya kuishi maisha yao kwa namna inayompendeza Mungu. Roho Mtakatifu anatimiza wajibu huo.)

 

   1. Kwenye utangulizi, nilibainisha suala la Roho Mtakatifu kumwongoza mke wangu kumsaidia mtu. Je, huo utakuwa uongozi juu ya haki?

 

  1. Soma Waebrania 4:14-16. Je, Roho Mtakatifu anajaza nafasi ya Yesu kutokana na ushauri unaohusu kuishi maisha makamilifu? (Hapana. Sehemu ya uhakikishwaji wa haki ni kwamba Yesu ni Kuhani wetu Mkuu ambaye anatuombea kwa Mungu Baba. Yesu ni mwombezi mkamilifu kwa sababu anayaelewa matatizo ya dhambi yanayotukabili. Habari njema zaidi!)

 

 1. Maelekezo Juu ya Hukumu

 

  1. Soma Yohana 16:11. Unapofikiria juu ya Roho Mtakatifu kukuhakikisha kwenye “hukumu,” je, hilo ni jambo jema au baya? Je, hilo ni onyo kwamba hukumu inakuja na unahitaji kufanya matengenezo? (Huo sio ujumbe mkuu. Ujumbe mkuu ni kwamba “mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.” Yesu amepata ushindi! Ameifanya haki kwa imani iwezekane.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:8-9. Tunajua nini kuhusu huyu simba aungurumaye? (Ameshindwa!)

 

   1. Je, hiyo inamaanisha kuwa Shetani si wa hatari tena? (Anaweza kutumeza tusiposimama imara katika imani. Lakini, habari njema ni kwamba huyu simba hatari ni simba aliyekwisha shindwa.)

 

   1. Kifungu hiki kinatufundisha nini kuhusu chanzo cha mateso maishani mwetu?

 

 1. Maelekezo Juu ya Ukweli

 

  1. Soma Yohana 16:12-13. Ni kwa namna gani nyingine Roho Mtakatifu anaweza kutuongoza? (Atafundisha ukweli ulio mgumu sana kwa wanafunzi kuuelewa kwa sasa.)

 

 

   1. Kuna ujumbe mzito sana ambao haujatajwa katika hizi ahadi juu ya namna ambayo Roho Mtakatifu atatusaidia. Ujumbe gani haujabainishwa katika wajibu wetu wa kuzungumza na watu wengine kuhusu hatia, dhambi, haki, hukumu, na kweli? (Tunatakiwa kuwa makini juu ya wakati na namna tunavyochukua uamuzi wa kuwashauri/kuwasaidia watu matatizo yanayowakabili maishani mwao. Ushauri/usaidizi wa msingi tayari umeshafanywa na Roho Mtakatifu. Tulipoangalia kwa ukaribu zaidi usaidizi wa Roho, ulikuwa chanya, badala ya kuwa “mshitaki wa ndugu zetu.” Wajibu huo unatekelezwa na Shetani.)

 

  1. Soma Warumi 5:5. Ikiwa tunatafuta uongozi na msaada wa Roho Mtakatifu katika kuwaleta watu wengine kwenye imani, hii inaashiria nini juu ya kuwa mshitaki? (Roho Mtakatifu anamimina upendo mioyoni mwetu, hamimini huzuni na fedheha. Njia yetu inatakiwa kujaa upendo.)

 

  1. Soma Mathayo 5:7. Katika suala la usaidizi/ushauri, je, rehema ni mojawapo ya vigezo vyako vya muhimu?

 

 1. Maelekezo Juu ya Mambo Yajayo

 

  1. Soma tena Yohana 16:13. Je, Roho Mtakatifu atatupatia ushauri gani mwingine? (Atatuambia pia mambo yajayo yatakayotukia.)

 

  1. Soma 2 Wakorintho 5:5. Roho Mtakatifu ana wajibu gani mwingine kwenye mambo yetu yajayo? (Roho Mtakatifu sio tu kwamba anatufunulia mambo yetu yajayo, bali pia yeye ni uthibitisho, mdhamana, wa mambo yetu yajayo yaliyoahidiwa na Mungu.)

 

  1. Soma Waefeso 1:13-14. Hiki ni kifungu kingine kinachokusu Roho Mtakatifu kuwa “amana,” uthibitisho, mdhamana, kuhusu mambo yetu yajayo pamoja na Mungu. Ninachokutaka ukiangalie ni lugha inayohusu “muhuri.” Wakristo “wanatiwaje muhuri,” wanatiwaje “alama” kama “milki ya Mungu?” (Roho Mtakatifu!)

 

   1. Soma Ufunuo 14:9-10. Tunapaswa kuzingatia alama gani mbadala?

 

   1. Hii inatufundisha nini juu ya umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu aliye hai maishani mwetu? (Hii ndio alama ambayo tunataka kuwa nayo. Ni alama ambayo lazima tuwe nayo. Kuwa na “alama” ya Roho Mtakatifu “kunahakikisha urithi wetu.” Waefeso 1:14. Mungu apewe sifa!)

 

  1. Soma Warumi 8:16-17. Roho Mtakatifu anatuambia nini juu ya mambo yetu yajayo? (Kwamba sisi ni warithi pamoja na Kristo. Tunao mustakabali wetu wa mambo yajayo pamoja naye! Hata hivyo, kama warithi pamoja na Yesu pia tunashiriki katika mateso yake.)

 

  1. Soma Warumi 8:13-15. Roho Mtakatifu anafanya nini ili kutusaidia katika mateso? (Anatupatia njia ya kuepuka hofu. Sio tu kwamba tunakuwa na ujasiri wa kuwa na uwezo wa kumwita Mungu Baba yetu, bali pia Roho Mtakatifu anayaongoza mawazo yetu na matendo yetu ili tuweze kuepuka kuyasababisha matatizo hayo maishani mwetu, matatizo yanayotusababishia hofu.)

 

  1. Rafiki, Roho Mtakatifu anayo mambo mengi sana ya kutufundisha. Ana hamu ya kuyaongoza maisha yako. Kwa nini usimwombe akuongoze na kukushauri? Kwa nini usimwombe ayafungue masikio yako ili uweze kusikia maelekezo yake? Kwa nini usimfanye mshirika maishani mwako katika mambo yote uyatendayo? Kwa nini usiamue kufanya hivyo sasa hivi?

 

 1. Juma lijalo: “Lisha Kondoo Wangu: 1 na 2 Petro.” Tutaanza somo jipya kutoka kwenye hivi vitabu viwili vya Biblia vya kupendeza.