Somo la 2: Urithi Usioharibika

Swahili
(1 Petro 1)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma hili tunaanza somo letu la Barua ya kwanza ya Petro. Wale wanaosoma injili iliyoandikwa na Petro wanampenda Petro. Yeye ni mkakamavu, jasiri, na anajua inavyomaanisha kumwangusha Mungu. Katika somo letu juma hili, Petro anatupatia mtazamo wa jumla wa maisha ya Kikristo. Hebu tuzame kwenye Biblia ili tuone hekima aliyonayo Petro kwa ajili yetu na kile anachotutumainisha!

 

 1. Watu Mbalimbali

 

  1. Soma 1 Petro 1:1. Barua za kale zinaanza na jina la mwandishi kisha hadhira ambayo barua hiyo inawalenga. Je, bado tunafanya hivyo leo? (Barua nyingi za kiofisi zina nembo ya ofisi pamoja na anwani. Barua pepe nyingi zinaonesha jina la mwandishi katika upande wa juu. Jibu ni “ndiyo,” mara nyingi nasi tunafanya vivyo hivyo.)

 

   1. Utaona kwamba Petro anaonesha wasifu wake kwa kusema “mtume wa Yesu Kristo.” Unawezaje kumwelezea Petro? (Kwa mujibu wa somo la juma lililopita, unaweza kusema “mvuvi,” “mtu ambaye wakati mwingine anavuviwa na Mungu na wakati mwingine anavuviwa na Shetani.”)

 

    1. Je, unajitahidi kuwa na uso wa furaha kanisani? Kwa mujibu wa Petro, je, hicho ni kitendo kizuri? (Ndiyo. Petro anaandika wasifu wake bora kabisa kwa waumini wenzake. Hii inaleta mantiki kwa kuwa anaandika kama mtu mwenye mamlaka aliyevuviwa na Roho Mtakatifu.)

 

  1. Angalia tena 1 Petro 1:1. Wale anaowaandikia wana wasifu gani? (Ni wateule wa Mungu.)

 

   1. Hiyo inamaanisha nini? Mungu anawachagua washindi na washindwa? (Tutajadili jambo hili kwa kina hapa chini.)

 

   1. Utaona kwamba Petro pia anawaita kuwa “wakaao katika hali ya ugeni.” Hii inamaanisha nini? (Inamaanisha kwamba huu ulimwengu sio nyumbani kwao.)

 

   1. Inamaanisha nini kwamba hadhira ipokeayo ujumbe wa barua yake “imetawanyika” katika maeneo haya ya ulimwengu? (Inaonekana kama kuna jambo lililowafanya watawanyike. Huenda ilikuwa ni mateso katika Yerusalemu. Hii inaendana na wazo la “mgeni.”)

 

  1. Soma 1 Petro 1:2. Tunaona sababu tatu zilizowafanya watu hawa “wateuliwe.” Je, ungependa “kuteuliwa” na Mungu? Ikiwa ndivyo, basi hebu tuchambue sababu zote tatu:

 

   1. Je, “kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua [kuwachagua]” inamaanisha nini? Je, hatima ya watu wengine ni kuokolewa na hatima ya wengine ni kupotea?

 

 

   1. Katika mfululizo wa masomo yetu yaliyopita tulijifunza Matendo 15. Kanisa la awali lilijadili walichotakiwa kuwa nacho waongofu wapya wa Mataifa. Hebu tupitie tena mjadala huo kwa kusoma Matendo 15:14-19. Utaona kwamba kifungu cha 18 kinasema “ajulishaye hayo tangu milele.” Hii inatuambia nini juu ya kumjua Mungu na kuujua wokovu “tokea awali?” (Mugu alijua kile alichotaka kukifanya mapema sana – kwamba injili inapaswa kwenda kwa Mataifa. Haizungumzii chochote kuhusu mtu mmoja mmoja.)

 

   1. Soma Mathayo 6:8. Hii inazungumzia nini kuhusu Mungu kuwa na ufahamu wa mambo tokea awali? (Mungu anajua kile unachokihitaji kabla hujamwomba. Ukweli kwamba anafahamu haimaanishi kwamba tutamwomba. Tunao uchaguzi katika jambo hili.)

 

   1. Soma Warumi 11:2. Mungu alimjua nani “tokea awali?” (Israeli! Licha ya hayo, tunafahamu kutoka kwenye Biblia kwamba sio wote wanaokolewa.)

 

   1. Soma Warumi 8:28-30. Vifungu hivi vinazungumzia juu ya hatima. Jambo gani linaanzisha hii “hatima?” (Wale wanaompenda Mungu. Soma sura yote ya Warumi 8 na utapata picha ya kwamba kitendo cha kuokolewa ni uchaguzi wako. Kama bado hujashawishika, soma kitabu cha Warumi sura ya 9 ambapo Paulo anasema kuwa Mungu aliichagua Israeli, lakini ni wachache tu ndio waliomfuata. Matokeo yake ni kwamba Mungu aliwaita wale ambao “si watu wangu” kuwa wana wa Mungu aliye hai. Warumi 9:26.)

 

  1. Hebu turejee kwenye sababu ya pili ya walengwa wa ujumbe wa barua kuwa “wateule wa Mungu.” Soma tena 1 Petro 1:2. Roho Mtakatifu ana wajibu gani kwenye maisha ya watu ambao ni wateule wa Mungu? (Soma Warumi 8:5-8. Roho Mtakatifu ndio kiini cha maisha ya mtu anayetaka kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Anatuongoza kuwa watiifu na kupandikiza ndani yetu mitazamo inayoakisi haki na utakaso.)

 

  1. Soma tena nusu ya mwisho ya 1 Petro 1:2. Sababu ya tatu ya wao kuwa “wateule wa Mungu” ni ipi? (“Kunyunyiziwa damu yake.”)

 

   1. Hiyo inamaanisha nini? (Hii inatukumbusha huduma ya patakatifu. Dhambi iliondolewa [ilihamishwa] kwa njia ya damu. Hii inaturejesha kwenye wokovu wetu kwa njia ya imani kupitia kafara ya Yesu.)

 

  1. Kwa nini kuteuliwa kwetu kunatupatia “neema na amani” kwa wingi? (Tunajua kuwa sisi ni wateule wa Mungu. Tunajua tunaokolewa kwa neema. Unapomruhusu Roho Mtakatifu ayaongoze maisha yako unakuwa na amani.)

 

 1. Tumaini letu

 

  1. Soma 1 Petro 1:3. Je, umezaliwa upya? (Ndiyo, ikiwa wewe ndiye uliyemchagua Yesu. Ufufuo wake ni “uzao wetu mpya.”)

 

  1. Soma 1 Petro 1:4. Nini kinatokea kwenye kitu chako jipya? (Kinazeeka, kinafubaa, na hatimaye kinatupwa.)

 

   1. Hii inafananishwaje na urithi wako wa mbinguni? (Kamwe hauzeeki!)

 

  1. Soma 1 Petro 1:5. Nini kinatutokea wakati hayo yakiendelea? (Tunalindwa na Mungu kwa njia ya imani.)

 

 

   1. Mara kwa mara huwa ninasikia kwamba hatupaswi kuizingatia sana mbingu. Je, unakubaliana na kauli hii? (Kila mtu anatazamia thawabu au zawadi. Mungu asingetoa ahadi hii kama asingetaka tuitazamie.)

 

  1. Soma 1 Petro 1:6. Kwa nini majaribu ya hapa duniani (kumbuka kwamba hawa ni watu waliokuwa “wametawanyika”), yanaifanya mbingu kuwa ya muhimu zaidi? (Tunataka magumu yakome. Lingekuwa jambo la kukatisha tamaa kiasi gani endapo tusingekuwa na tumaini la kuwa na wakati na mahali bora.)

 

 1. Mateso

 

  1. Soma 1 Petro 1:7. Mateso yana upande gani wenye manufaa? (Imani yetu inajaribiwa kuwa ni halisi!)

 

   1. Unafikiria nini unaposoma neno “mateso?” (Ninafikiria maumivu ya mwili.)

 

   1. Unakumbuka kipindi imani yako ilipoimarishwa? Je, ilihusisha maumivu ya mwili? (Kwangu hilo halijawahi kutokea. Kinachoimarisha imani yangu zaidi ni pale Mungu anaposhughulikia mashinikizo na matatizo maishani mwangu. Ninasema kuwa “Ametenda. Kwa nini nilikuwa na wasiwasi mkubwa kiasi hicho?”)

 

  1. Angalia tena 1 Petro 1:7. Kwa nini tunahitaji imani yetu ithibitishwe kuwa ni halisi? (Humpa Yesu “sifa, utukufu na heshima.”)

 

  1. Soma 1 Petro 1:8. Jambo gani lingine linatokana na mateso? (Kuongezeka kwa imani yetu kwa Yesu, ambayo inatupatia “furaha isiyoneneka na yenye utukufu.”)

 

   1. Je, umewahi kupitia uzoefu huu?

 

  1. Soma 1 Petro 1:9. Je, tunaokolewa kwa njia ya mateso? (Sidhani kama hicho ndicho kinachosemwa. Mateso yanaimarisha imani yetu. Imani yetu kwa Yesu ndio inayotuokoa. Kwa kuona jinsi Yesu anavyotutendea, tunaongeza tumaini letu na upendo wetu kwake.)

 

 1. Wokovu

 

  1. Soma 1 Petro 1:10-11. Manabii gani wanarejewa na Petro? (Manabii wa Agano la Kale.)

 

   1. Unadhani Petro ana ujumbe gani wa msingi kwa kuandika kuhusu huu utafutaji wa kina? (Ujio wa Yesu ulieleweka na manabii wa Agano la Kale, lakini walitaka kujifunza zaidi.)

 

   1. Manabii walikuwa na “Roho wa Kristo ndani yao.” Huyo Roho ni kitu gani? (Ni Roho Mtakatifu. Unaona jinsi Petro anavyounganisha Agano la Kale na Agano Jipya? Agano Jipya (ambalo alikuwa analiandika wakati huo) haimaanishi kuachana na Agano la Kale.)

 

  1. Soma 1 Petro 1:12. Habari mbaya kwa manabii wa Agano la Kale ni ipi? (Yesu alikuwa anakuja katika kipindi chao. Walikuwa wanaandika ili kutupatia tumaini na mwelekeo.)

 

 

   1. Tunapaswa kuhitimisha nini kutoka kwenye kauli inayosema kuwa, si hata malaika walilielewa jambo hili?

 

  1. Soma 1 Petro 1:13-16. Petro anawezaje kusema “Yesu Kristo atakapofunuliwa?” Tayari Yesu alishakuja na kurejea mbinguni! (Yesu anakuja tena!)

 

  1. Soma 1 Petro 1:17-21. Ikiwa “imani yangu na tumaini langu vipo kwa Mungu” kwa nini Petro ananiambia kuwa Mungu Baba “anamhukumu kila mtu pasipo upendeleo?”

 

  1. Soma 1 Petro 1:22-23. Je, jambo hili ni baya zaidi – Petro ananiambia kwamba “nijitakase?” Hilo linaendanaje na ishara ya Yesu kuwa Mwana-kondoo aichukuaye [aiondoaye] dhambi yetu? (Petro anakubaliana na suala la wokovu kwa njia ya imani pekee. Lakini, pia anatusihi tuuelekee utakatifu – tuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Kwa kufanya hivyo sio tu kwamba tunakuwa bora zaidi, bali pia inatufanya tumwakilishe Mungu vizuri zaidi hapa duniani.)

 

  1. Rafiki, kutembea na Yesu ni jambo la kufa na kupona. Je, utamwomba Roho Mtakatifu aendelee kukuongoza katika njia ielekeayo kwenye kuuelekea utakatifu?

 

 1. Juma lijalo: Ukuhani wa Kifalme.