Ukuhani wa Kifalme

Swahili
(1 Petro 2:1-12)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mungu anawaunganishaje watu wake leo? Je, kuwaunganisha huko kunafanana na kikundi kilichopangiliwa vizuri kilichoanza baada ya safari ya kutoka Misri? Ikiwa ni tofauti na hivyo, je, hiyo inamaanisha nini kiuhalisia kwa wafuasi wa sasa wa Yesu? Hiyo inaweza kuathirije teolojia yetu kwa namna nyinginezo? Juma lililopita tulimalizia kwa Petro kutuambia kuwa neno la Mungu ni la milele na kwamba tunazaliwa mara ya pili kwa ajili ya uzima wa milele. Hata hivyo, watu wengine wote waliosalia wanafifia kwa kasi kama nyasi na maua yanyaukavyo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kile alicho nacho Mungu mawazoni mwake kwa ajili yetu sisi tuliojengwa kwa ajili ya umilele na tunaoshiriki kupeleka neno la milele!

 

 1. Mapitio ya Mwisho Mwisho

 

  1. Soma 1 Petro 2:1. Maisha yako yangekuwaje endapo yasingekuwa na mambo yote haya?

 

   1. Je, ungeyafurahia maisha zaidi?

 

   1. Je, watu wengine wangefurahia kuwa nawe zaidi?

 

   1. Je, unafahamu jinsi unavyoweza “kujiepusha” na hii mitazamo isiyostahili?

 

  1. Soma 1 Petro 2:2-3. Kwa nini Petro anatulinganisha na “watoto wachanga?” Je, hii ina uhusiano wowote na ukweli kwamba “tunazaliwa mara ya pili?”

 

   1. Tunayapata wapi “maziwa ya kiroho?” (Inaleta mantiki kutambua kwamba Petro anazungumzia neno la Mungu kwa kuwa hivi punde tu (mwishoni kabisa mwa sura iliyotangulia) ametuambia kwamba neno la Mungu “hudumu hata milele.”)

 

   1. Hii inaashiria nini kuhusu uwezo wako wa “kujiepusha” na mitazamo hii? (Inaashiria kwamba hili si jambo unaloweza kulitenda kwa nguvu zako. Unatakiwa kunywa “maziwa ya kiroho” ili “kukua” kwenye huu mwelekeo. Kwa dhahiri hicho ndicho unachokifanya sasa hivi!)

 

   1. Jambo gani hasa linalokua? (Unatakiwa “kuukulia wokovu wako.” Ungetarajia mtu “aliyezaliwa mara ya pili” akue.)

 

 

    1. Hebu tuangalie kile jambo hili linachokimaanisha kuhusu neem Je, hii inamaanisha kuwa tayari umeshaokolewa? Maelekezo ya “kujiepusha” na mitazamo mibaya yanaendanaje na suala la neema? (Hili ni suala la muhimu. Petro hatuambii kwamba tunatakiwa kujiepusha na hii mitazamo ili tuokolewe, bali anatuambia kuwa hivi ndivyo ambavyo waliookolewa wanavyopaswa kukua na kuuelekea utakatifu mkuu. Endapo Petro angekuwa anazungumzia suala la sisi kujiepusha na mitazamo mibaya, basi kauli iliyopo katika 1 Petro 1:23 kwamba “tunazaliwa mara ya pili” kwa mbegu “isiyoharibika” isingekuwa na mantiki.)

 

 1. Mpango Mpya

 

  1. Soma 1 Petro 2:4. Ni nani huyu aliye “Jiwe lililo Hai?” (Lazima hii itakuwa inamrejea Yesu.)

 

   1. Hebu tupitie tena mjadala tuliokuwa nao katika masomo mawili yaliyopita. Soma Mathayo 16:16-19. Kipindi kile sikutaka kuingia kwenye mjadala wa alichokimaanisha Yesu kwa kusema “mwamba” ambao juu yake kanisa linajengwa. Wengine wanadhani kuwa ni Petro na wengine wanadhani kuwa ni tamko la Petro kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye Hai. Tumejifunza nini kutoka katika 1 Petro 2:4 juu uelewa wa Petro kuhusu mwamba? (Petro anasema kuwa mwamba ni Yesu! Huu ni ushuhuda mkuu kwamba Petro anaamini kuwa ujumbe wa Yesu kwake katika Mathayo ni kwamba Yesu ndiye Mwamba ambao kanisa linajengwa juu yake.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:5. Kifungu hiki kinasema kuwa kitu gani kinajengwa juu ya Mwamba? (Mawe yaliyo hai yanajengwa kwenye “nyumba ya Roho ili yawe ukuhani mkuu.”)

 

   1. Haya mawe yaliyo hai ni akina nani? (Ni sisi. Ni watu wanaoamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu aliye Hai.)

 

   1. Makuhani walifanya nini chini ya mfumo wa sheria ya Musa? (Walikuwa wawakilishi maalumu wa Mungu. Walilitunza hekalu, walitoa kafara, kwa njia mbalimbali walikuwa kiungo kati ya Mungu na wanadamu.)

 

   1. Hii inatuambia nini kuhusu jinsi ambavyo kanisa linapaswa kujiendesha leo? (Kwa dhahiri, tunajiongoza kwa namna tofauti kabisa na jinsi kanisa lilivyokuwa linaendeshwa chini ya Musa. Sisi sote ni sehemu ya “ukuhani mtakatifu.”)

 

   1. Hii inazungumzia nini kuhusu jambo ambalo unapaswa kuwa unalifanya kama kuhani aliye “jiwe lililo hai?” (Hebu turuke vifungu kadhaa na tusome 1 Petro 2:9. Hii inathibitisha kuwa sasa kila mshiriki ni kuhani. Majukumu maalumu waliyopewa watu (wanaume) wachache kutokana na uhusiano wao wa kifamilia katika Agano la Kale sasa majukumu hayo yanaelekezwa (wanapewa) kwa Wakristo wote kutokana na uchaguzi wetu wa kuwa jiwe lililo hai linalojengwa juu ya Yesu.)

 

    1. Jukumu letu ni lipi hasa? (Kumsifu Mungu. Ujumbe maalumu ni jinsi tulivyoitwa kutoka gizani na kuingia katika “nuru ya ajabu.”)

 

  1. Hebu turejee nyuma na tumalizie mjadala wetu wa 1 Petro 2:5. Dhabihu gani za kiroho tunazozitoa?

 

   1. Inamaanisha nini kusema kwamba tunatoa dhabihu hizi za kiroho “kwa njia ya Yesu?” (Kumbuka kwamba kafara ya wanyama katika mfumo wa zamani wa ukuhani ilikuwa ni kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Hivyo, dhabihu yetu inajumuisha maelezo ya kile ambacho Yesu ametutendea kupitia maisha, kifo na ufufuo wake, na pia inaturejesha kwenye suala la “kujiepusha” na mitazamo mibaya kwa njia ya uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

 

   1. Je, hii ni kafara? (Unao uchaguzi wa kufuata mambo (asili) yako ya kibinadamu au kufuata ushawishi wa Roho Mtakatifu. Uamuzi uliopo ni kuutangaza Ufalme wa Mungu.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:6. Kwa nini “fedheha” inatajwa? (Yesu aliuawa kama mhalifu. Watu (hadhira) waliokuwa wanamsikiliza Petro walikimbia kwa sababu ya mateso. Mungu anatuambia kuwa tunapomfuata yeye mambo yataishia kuwa mazuri.)

 

 1. Athari za Mwamba

 

  1. Soma 1 Petro 2:7-8. Mwamba unawafanya watu wawe na miitikio tofauti. Kwa nini? (Unahusiana na imani kwa Yesu. Ikiwa tunamwamini, basi yeye ni wa thamani. Kama hatumwamini, hatutakuwa na utii, tutajikwaa na kuangauka.)

 

   1. Tunayo rejea nyingine ya majaaliwa yetu. Hii inamaanisha nini hapa? (Hoja yangu ni kwamba ikiwa hatumwamini Yesu hatima yetu ni kujikwaa na kuanguka. Tunafanya uchaguzi, na mambo mengine yote yatafuata yenyewe. Lakini, hebu tuendelee kuchimbua zaidi ili kujua kama tunao uchaguzi katika wokovu wetu.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:9-10. Kama hatima yetu ingekuwa inajulikana kwa namna moja au nyingine, tunawezaje kubadilika kutoka “kutokuwa watu” hadi kuwa “watu wa Mungu?”

 

  1. Soma Warumi 10:10-13. Kifungu hiki kinazungumzia nini kuhusu majaaliwa yetu? (Kwamba wale (“mtu yeyote”) wanaomwita Yesu wataokolewa. Kumkiri kwako Yesu ndiko kunakoleta tofauti.)

 

  1. Soma Warumi 10:16-18 na Warumi 10:21. Israeli na Waisraeli walikuwa wateule wa Mungu. Lakini, hii inaonesha kuwa ingawa Mungu aliwapangia wokovu, si wote walioitikia wito wake. Sasa majaaliwa yetu sisi (Mataifa) ni wokovu na lazima tufanye uchaguzi wa kujibu wito wa Mungu wa kujenga juu ya “Jiwe lililo Hai.” Nadhani hii inaonesha kuwa Mungu anawapangia watu wote wokovu, na chaguzi zetu ndizo zinazobainisha matokeo ya jambo hili.)

 

 1. Maisha Makamilifu

 

  1. Soma 1 Petro 2:11-12. Je, Petro anatuambia mambo yasiyowezekana – mambo tusiyoweza kudhibiti tamaa zetu? (Hii inaonekana kama kauli ya “kujiepusha” (kuweka mbali) iliyopo katika 1 Petro 2:1.)

 

   1. Unapokiangalia kifungu cha 12, Petro anazungumzia matendo, si tamaa. Kwa nini anazungumzia matendo (“mwe na mwenendo mzuri”) baada ya kuandika juu ya tamaa? (Dhambi inaanzia akilini. Matamanio ya dhambi yako “vitani” dhidi ya mambo ambayo Mungu anayataka kwa ajili yetu. Ikiwa hatuitamani dhambi, hatutaenenda katika matamanio ya dhambi.)

 

   1. Wapagani watasema nini juu yetu? (Watatoa mashtaka ya uongo dhidi yetu. Hili ni jambo ambalo hatuwezi kulidhibiti.)

 

    1. Tunaweza kudhibiti nini? (Tunaweza kudhibiti kama mashtaka ni ya kweli au ya uongo. Wapagani watajua kuwa mashtaka yao ni ya uongo Yesu atakapowataka wayatete. Hata hivyo, ikiwa mashtaka ni ya kweli, tutaleta madhara kwa Mungu na si utukufu.)

 

 

   1. Paulo anajenga hoja gani hapa? (Anasema kwanza yaangalie matamanio yako. Epuka matamanio yatakayokutumbukiza kwenye matatizo maishani mwako. Kisha anatuambia kuwa ikiwa tutaingia kwenye matatizo, basi matatizo hayo yatakuwa mikononi mwa “wapagani” ambao wanatamani kusema uongo juu yetu. Lakini ikiwa mashtaka ni ya kweli, basi yanamdhuru Mungu.)

 

   1. Hili linahusianaje na Mwamba? Hili linahusianaje na mpango mpya ambapo wewe ni kuhani? (Sasa wewe ni kuhani wa Mungu, mwakilishi wake. Sifa njema ya Mungu inajengwa kwa kile unachokifanya.)

 

  1. Rafiki, je, utaichukulia hadhi yako ya ukuhani kwa umakini na uangalifu mkubwa? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie kumpa Mungu utukufu katika mambo yako yote uyatendayo?

 

Juma lijalo: Mahusiano ya Kijamii.