Mahusiano ya Kijamii

Swahili
(1 Petro 2:13 – 1 Petro 3:17)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tunapaswa kuhusianaje na serikali? Tunapaswa kuhusianaje na mwajiri wetu? Tunapaswa kuhusianaje na wenzi wetu? Haya ni maswali yanayolenga uhalisia ambayo kwa kiasi fulani yanatofautiana kutokana na aina ya serikali, mwajiri na mwenzi wako. Licha ya hayo, Petro anatupatia ushauri makini katika maeneo yote matatu. Maelekezo yake yanakinzana na baadhi ya hoja na fikra zilizopo katika kipindi hiki, kwa hiyo jiandae kwa changamoto hiyo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Serikali

 

  1. Soma 1 Petro 2:13-14. Petro anaelezea tofauti kati ya wafalme na magavana. Kamwe sijawahi kuishi chini ya utawala wa mfalme wa kidunia, bali nimefanya kazi na magavana. Petro anamaanisha nini anapoandika kuwahusu wafalme na magavana wao? (Anatuambia kumtii mfalme, kama mamlaka kuu, na wale waliokabidhiwa madaraka ya kushika mamlaka ya mfalme.)

 

   1. Sababu ya msingi ya kutii mamlaka ya serikali ni ipi? (“Kwa ajili ya Bwana.” Hii inahusiana na hadhi ya Mungu.)

 

    1. Sababu nyingine ya kawaida ya kutufanya tutii mamlaka ya serikali ni ipi? (Inaweza “kuwaadhibu [kuwalipiza kisasi] watenda mabaya … kuwasifu watenda mem”)

 

  1. Soma 1 Petro 2:15. Petro anachukulia kwamba tunapoitii mamlaka ya serikali “tunatenda vyema.” Je, hiyo ni kweli? Vipi kuhusu serikali ya Kirumi katika kipindi cha Petro? Vipi kuhusu mamlaka iliyowaambia wanafunzi wasihubiri na ikafanya kila iwezalo ili kumsulubisha Yesu?

 

   1. Petro anasema kuwa lengo la utii ni lipi? (“Kuziba vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu.”)

 

    1. Ikiwa watu hawa ni wajinga (mbumbumbu) na wapumbavu, kwa nini jambo hili lituhangaishe akili? (Hii inaturejesha kwenye hadhi ya Mungu.)

 

  1. Ninapata shida kidogo kwa kile anachokisema Petro. Wajinga na wapumbavu watakosea katika kutenda mambo fulani. Je, Petro anasema kuwa tusitende mambo mema pale mambo hayo yanapokuwa kinyume na sheria, kwa sababu ya watu wajinga na wapumbavu?

 

   1. Hebu tuliangalie jambo hili kwa undani zaidi kwa Marekani. Hapa “mfalme” ni nani? Je, ni Rais au ni wewe? (Mamlaka, kwa mujibu wa Katiba ya Marekani, yapo mikononi mwa watu. Watu ndio wanaoamua nani awe rais wao na magavana wao. Je, tofauti hiyo inamaanisha kuwa “kutii kila mamlaka” kuna maana tofauti hapa?

 

 

   1. Hebu tuzungumzie kuhusu mamlaka na “kutenda mema.” Nchini Marekani utoaji mimba na ndoa za jinsia moja ni jambo la halali kisheria. Kutoa uhai wa mtu mwingine kwa manufaa yako ndicho ninachokiita “kuenenda kinyume na injili.” Ndoa za jinsia moja sio tu kwamba kwa mahsusi kabisa zimekatazwa katika Biblia (Mambo ya Walawi 20:13, Warumi 1:26-28), bali pia ni kinyume na mpango wa uumbaji juu ya ndoa. Je, tuseme kwamba sisi ndio “mamlaka” na tunapaswa kupigania jambo lililo halali, au tuwe watiifu kwa uamuzi wa serikali?

 

  1. Soma 1 Petro 2:16. Utaona kwamba Petro anaandika katika 1 Petro 2:15 kuhusu “kutenda mema” na hapa anaandika kuhusu “uhuru” wetu “kusitiri ubaya [uovu].”

 

   1. Anamaanisha “uhuru” gani? (Kufuata sheria ya nchi.)

 

   1. Maelekezo haya mawili, kutenda mema na si uovu, yanatuambia nini kwa kuzingatia sheria zinazoendeleza uovu?

 

   1. Petro anatuambia “tuishi kama watumwa wa Mungu.” Je, hii inaashiria mpango mwingine – kutopingana na sheria ovu, badala yake kuchukua maamuzi binafsi yanayouendeleza wema? (Baadhi ya Wakristo watatafsiri jambo hili kumaanisha kuwa wanapaswa kupuuzia uovu wowote unaoweza kuruhusiwa na serikali, na kuzingatia maisha yao pekee. Kwa upande mwingine, ikiwa unaweza kubadili historia kutokana na ushawishi wako, je, unao wajibu wa kufanya hivyo?)

 

  1. Soma 1 Petro 2:17. Je, unaheshimu mitazamo ya kisiasa na ya kiroho ambayo unadhani kuwa haiko sahihi? (Tunatakiwa kuonesha heshima bila kujali kama tunadhani kuwa upande mwingine ni mpumbavu na umepotoka.)

 

   1. Ngoja nimuulize Petro, nawe unaweza kumjibia. Je, unaonesha “utii” kwa kurejea “mazungumzo ya kijinga ya watu wapumbavu” (1 Petro 2:15)?

 

 1. Mwajiri

 

  1. Soma 1 Petro 2:18. Kwa kuwa nina shaka, na sidhani kama yeyote anayesoma somo hili ni mtumwa halisi, unawezaje kulitumia somo hili kivitendo kwa mwajiri wako?

 

   1. Je, unakisaidia chama cha wafanyakazi? Je, vyama hivyo vinasimamia heshima za waajiri?

 

  1. Soma 1 Petro 2:19. Je, umewahi kutotendewa haki kazini kwako? Kwa nini Petro anasema kuwa ni “sifa” kuvumilia mateso yatokanayo na vitendo visivyo vya haki? (Hii inahusiana na “kumjua Mungu.”)

 

   1. Unadhani hilo linamaanisha nini: umjue Mungu pale unapoyavumilia mateso? (Yesu aliteseka kwa ajili yetu, na Yeye ni Bwana wetu.)

 

   1. Kuna tofauti gani ya msingi kati yako na mtumwa? (Unaweza kubadili kazi yako.)

 

 

    1. Je, hivyo ndivyo tunavyopaswa kufanya tunapokuwa na waajiri wasiotenda haki? (Ndiyo! Petro anawaandikia watu wasioweza kufanya mabadiliko hay Unaweza. Lakini, hadi pale utakapofanya mabadiliko hayo, unapaswa kufuata ushauri wa Petro kwa watumwa.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:20-23. Petro anatuambia kuwa hatustahili sifa kwa kupigwa pale tunapostahili kupigwa. Hata hivyo, pale ambapo hatustahili kipigo hicho tunakuwa tunafuata nyayo za Yesu. Je, tumaini letu la haki lipo wapi? (Lipo kwa Mungu. Tunajiaminisha kwa Yeye ahukumuye kwa haki.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:24-25. Yesu alikuwa na sababu ya yeye kuteseka. Sababu ya wewe kuteseka ni ipi? (Inapaswa kuwa ile ile kama ya Yesu – kwamba itampa Mungu utukufu.)

 

  1. Kabla hatujahitimisha katika haya maeneo mawili, angalia tofauti kati ya kuwa chini ya mamlaka ya Rumi au kuwa chini ya mamlaka ya mtu fulani anayekumiliki, na kuwa raia katika demokrasia na kumfanyia kazi mwajiri unayemchagua wewe mwenyewe. Kanuni zipi anazozielezea Petro zinatumika kwetu leo?

 

 1. Mwenzi

 

  1. Soma 1 Petro 3:1-2 na 1 Petro 3:5-6. Je, Petro anazungumzia ushauri huu kwa wanawake walioolewa na wapagani pekee? (Hapana. Ibrahimu hakuwa mpagani, pamoja na hayo bado Sara anaelezea kile ambacho Petro anakifafanua.)

 

   1. Unadhani inamaanisha nini kuwa “watiifu?”

 

  1. Hebu turuke mafungu kadhaa hadi 1 Petro 3:8. Petro anatoa ushauri gani kwa waumini wote? (Kuishi kwa kupatana, kuhurumiana, wasikitivu na wanyenyekevu.)

 

   1. Ikiwa ninataka kuwa mtu wa mapatano, mwenye huruma na mnyenyekevu kwa Wakristo wenzangu kwa ujumla, mimi (mume) ninapaswa kuwa na mtazamo gani dhidi ya mke wangu? (Kwa dhahiri, angalao kuwa na mtazamo uliobainishwa hapo juu!)

 

   1. Fikiria wanandoa ambapo mume ni mtu wa mapatano, mwenye huruma na mnyenyekevu kwa mkewe na mke ni mtii kwa mumewe. Je, hiyo inaleta mantiki katika ulimwengu wa sasa?

 

   1. Soma Waefeso 5:3 Paulo anaelezea kwamba mume anapaswa kuwa na mtazamo gani kwa mkewe? (Anapaswa kumpenda kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe.)

 

    1. Utaona kuwa Paulo anawaambia wake “wawatii” waume wao. Ujumbe huo ni wa muhimu kiasi gani kwenye ndoa?

 

  1. Soma 1 Petro 3:7. Petro anazungumzia nini kuhusu waume kuwaheshimu wake wao? (Anasema kuwa heshima inastahili. Hivyo, katika ndoa ya Kikristo, mume na mke wanapaswa kuheshimiana.)

 

   1. Jambo gani litamtokea mume ambaye anamtendea mkewe visivyo? (Mawasiliano yake na Mungu yanakuwa na “kizuizi.”)

 

  1. Mjadala unaweza kuonekana wa ajabu katika nyakati za sasa na unaweza kuwaghadhabisha watetezi wa haki na usawa kwa wanawake. Kiwango cha talaka ni cha hali ya juu nchini Marekani, na asilimia ya wenza wanaoishi pamoja bila ndoa ni kubwa. Hiyo inaashiria nini kuhusu ustahili wa mawazo ya nyakati za sasa juu ya ndoa? (Kwa dhahiri mawazo hayo hayafanyi kazi vizuri sana. Ni vigumu sana kuukataa ushauri wa Petro na Paulo wakati ushauri wa sasa unatutumbukiza kwenye matokeo mabaya.)

 

 

  1. Tuliruka 1 Petro 3:3-4. Soma hivyo vifungu. Je, hii inawaasa wanawake wasigharamikie nywele zao, wavae mavazi mabaya na kuepuka mapambo ya vito? (Hapana. Badala yake, kifungu kinasema kuwa urembo wako wa kweli unapaswa kutokana na utu wako wa ndani, sio kile unachokivaa.)

 

   1. Je, huu ni ushauri mzuri pale unapokuwa unamtafuta mwenzi? Unaangalia tabia zisizobadilika kutokana na kubadilika kwa nyakati?

 

  1. Rafiki, je, unaona mpangilio kwenye ushauri wa Petro? Mpangiliowelekeo huo ni juu ya kuwa na mtazamo wa heshima na utii dhidi ya mamlaka. Waasi wanajiingiza kwenye matatizo. Je, utachunguza upya mitazamo yako leo?

 

 1. Juma lijalo: Kuishi kwa Ajili ya Mungu.