Uongozi wa Utumishi

Swahili
(1 Petro 5:1-10)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mara ya kwanza nilipohama kutoka nyumbani, nilijiunga na kanisa lililoonekana kuwa kamilifu. Lilikuwa zuri sana! Niliwapenda washiriki. Nilimpenda mchungaji. Hapakuwepo na migawanyiko kanisani. Mwaka uliofuata, nilioa na mke wangu alianza kufundisha shule iliyokuwa inahusiana na kanisa hili. Mara nilipoanza kuona taswira ya “ndani” ya kanisa, niligundua kwamba mambo yote hayakuwa shwari, hapakuwepo na utulivu kamili wala umoja. Petro amekuwa akishauri juu ya mahusiano ya aina mbalimbali, na juma hili tunajifunza maelekezo yake kwenye uhusiano kati ya kanisa na viongozi wake. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Wazee

 

  1. Soma 1 Petro 5:1. Petro anapowaandikia “wazee,” je, anawazungumzia wazee wanaoshikilia nyadhifa za kanisa, au wale wenye umri mkubwa? (Soma 1 Petro 5:5. Mara zote nimekuwa nikichukulia kwamba Petro anazungumzia ofisi ndani ya kanisa, lakini kuchunguza kwa kina zaidi inaonekana Petro anawazungumzia wazee.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:2. Petro anawaambia wazee wafanye nini? (Kuwa “wachungaji wa kundi la Mungu.” Kwa dhahiri hii ni rejea juu ya kuwa na ofisi au nafasi kanisani.)

 

   1. Fikiria jambo hili. Je, kuna mantiki kuwahusianisha washiriki wazee na wale wanaoshikilia nafasi za uongozi kanisani? Soma tena 1 Petro 5:1 ili tuone kama unaona dalili zozote kuhusu jambo hili. (Petro anasema kuwa wazee walikuwa mashahidi katika mateso ya Yesu. Wazo lililopo ni kwamba wazee wanaelewa mambo mengi zaidi, wana uzoefu zaidi, na kwa hiyo inaleta mantiki kuwafanya kuwa viongozi – wachungaji.)

 

   1. Maoni ya watu mbalimbali niliyoyasoma yanaeleza kwamba neno “mzee” lilimaanisha mtu mzee, lakini pia walidhani kuwa katika kanisa la awali mara nyingi lilikuwa linazungumzia watu walioshika nyadhifa za juu kanisani. Kwa nini? Kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya umri na kushikilia nyadhifa katika ofisi hizi. Robertson’s New Testament Word Pictures inasema kuwa maandishi ya awali yalitumia neno lililotafsiriwa kama “wazee,” kwa ajili ya wazee wa mjini – “alderman.” Unadhani kuwa panapaswa kuwepo kwa uhusiano wa namna hiyo katika kanisa la zama za leo?

 

  1. Angalia tena 1 Petro 5:2. Kwa nini Petro anaandika “si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari?” (Hii inanishawishi kuwa kimsingi kabisa Petro anazungumzia suala la umri, sio ofisi. Inaleta mantiki alipoandika kuwa wazee wanapaswa kuhudumu kama “washauri,” si kwa sababu ni lazima, bali kwa sababu wanataka kufanya hivyo.)

 

 

   1. Kwa ujumla, watu wanakuwa na busara wanapoendelea kuwa watu wazima. Tatizo ni kwamba nimewaona na kuwashuhudia “wapumbavu” wasiobadilika kwa kadri ya mabadiliko ya umri wao. Je, umri ndio kigezo cha msingi cha kukizingatia? (Hebu tuendelee kusoma kwa sababu nadhani Petro anajibu swali hili.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:2-3. Tumejadili kwamba wazee wameshuhudia historia muhimu na imewapasa kuwa na busara. Je, Petro anabainisha vigezo gani vingine kwa watu kabla hawajafuzu kushikilia ofisi ya “ushauri?” (Wanatakiwa kuwa na hamu ya kuhudumu. Hawatakiwi kuingia kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kujinufaisha kifedha. Hawatakiwi kuwa “mabwana” kwa kundi la kondoo. Wanatakiwa kuwa mfano mzuri.)

 

   1. Nimekuwa “Mzee” kwenye makanisa mbalimbali nilipokuwa na ushirika katika sehemu kubwa na maisha yangu ya utu uzima. Hakuna mtu aliyewahi kunilipa fedha yoyote. Je, tatizo hili lipo kanisani kwako?

 

    1. Ikiwa fedha si tatizo, je, kuna tatizo linaloenda sambamba lisilohusisha fedha? Je, kuna Wazee wanaonufaika wao binafsi kutokana na kushikilia nafasi ya uongozi?

 

  1. Angalia tena 1 Petro 5:3. Je, “kujifanya mabwana” juu ya watu wengine kuna manufaa binafsi? (Petro anaelezea aina ya tabia ambayo inapaswa kumuengua mtu asiyestahili nafasi ya ushauri. Hutakiwi kufanya kazi kwa sababu ya manufaa binafsi, bila kujali kama ni manufaa ya kifedha, au suala la majisifu, au mamlaka. Petro anaruhusu Wazee kulipwa kutokana na kufanya kazi hiyo, na kufurahia sifa ya kawaida na mamlaka yanayotokana na kazi hiyo. Hata hivyo, anaandika kwamba unapaswa kuifanya kazi hiyo ili kuwanufaisha watu wengine, si kwa sababu una “ulafi” wa kulisha majisifu yako au kuonyesha madaraka (mamlaka).

 

   1. Kama umewahi kuwa Mzee, je, ulipata kujiridhisha kutokana na madaraka hayo? (Kuwasaidia watu wengine hukupatia furaha kubwa wanapoitikia vizuri katika hali chanya. Huo ni mmojawapo wa mbaraka wa nafasi hiyo.)

 

   1. Kwa miaka mingi nimeona mwelekeo unaoonekana kuwa wa kawaida sana, lakini ni suala linalohitaji kuangaliwa kwa kina. Washiriki wa kanisa ambao shughuli/kazi zao haziwapi nafasi za uongozi, wanaishia kuona kuwa kanisa linatimiza hitaji hilo. Tatizo kwa viongozi hawa ni kwamba kupoteza nafasi ya uongozi kanisani inaonekana kama kufukuzwa kazi – na matokeo yake ni magumu sana kwa mtu huyo na kwa kanisa. Je, hili ni tatizo lisilozuilika?

 

   1. Kwa muda sasa nimekuwa nikiangalia mitizamo yangu mwenyewe. Je, nilikuwa nikifundisha, kuhubiri na kuongoza kwa sababu nilipenda kuwa mbele, au kwa sababu nilikuwa najaribu kumpa Mungu utukufu? Nani aliyekuwa msingi kwangu wa kumpa utukufu? Ikiwa wewe ni kiongozi, je, umelifikiria jambo hili? (Dkt. William Shea, mmojawapo wa wanateolojia wakubwa katika madhehebu yangu, alikuwa mshiriki wa kanisa langu mahalia. Yeye ni mfano wa kuigwa wa watu wanyenyekevu. Siku moja nilimuuliza, “Bill, unapokuwa unafundisha na kuhubiri, je, kwa kiasi fulani unafanya hivyo kwa sababu unapenda kuwa mbele?” Akasema, “Hakika, hiyo ni sababu mojawapo.” Ukweli kwamba mtu huyu mnenyekevu anafurahia hiyo sehemu mojawapo ya kazi ilituliza mawazo yangu. Lengo ni kuutangaza Ufalme wa Mungu. Lakini, kufurahia heshima inayotokana na shughuli hiyo uifanyayo si dhambi. Yohana 12:26.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:4. Thawabu kuu ya kuwa mshauri ni ipi? (Mbingu! “Taji ya utukufu.” Ikiwa sababu yako ya kuwa kiongozi ni utukufu wa hapa, basi tayari umeshapewa kikamilifu hapa.)

 

 

 1. Vijana

 

  1. Soma 1 Petro 5:5. Unadhani kwa nini ilikuwa muhimu kwa Petro kuandika maneno haya? (Si mara zote vijana wanatambua kwamba uzoefu ni wa muhimu.)

 

   1. Kwa ujumla Petro anataka tuwe na mtazamo gani? (Kwamba sote, wadogo kwa wakubwa, tutendeane kwa unyenyekevu.)

 

   1. Manufaa ya unyenyekevu wa pamoja ni yapi? (Kama una majivuno, Mungu atapingana na wewe. Kama wewe ni mnyenyekevu, Mungu atakupatia neema.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:6. “Wakati muafaka” ambao Mungu atatuinua ni upi? (Vijana wadogo watakuwa wazee! Angalao, hilo ndilo lengo. Hii pia inaunga mkono jambo tulilojifunza hapo awali, kwamba Mungu anatamani kutupatia heshima.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:7. Wasiwasi unahusiana vipi na kuwa mnyenyekevu, na kukubali maelekezo kutoka kwa wazee? (Jiulize kwamba, ni kwa kiasi gani wasiwasi wako na hofu yako vinahusiana na sura ya kushindwa? Kupoteza jambo linalokufanya uonekane wa muhimu? Unyenyekevu ni ngao dhidi ya wasiwasi.)

 

 1. Shetani vs Mungu

 

  1. Soma 1 Petro 5:8. Je, unao wajibu katika “kutoraruliwa/kutoteketezwa” na Shetani? (Ndiyo. Uwe na “kiasi na kukesha.”)

 

   1. Unadhani inamaanisha nini kivitendo “kuteketezwa” na Shetani?

 

  1. Soma 1 Petro 5:9. Kupambana na Shetani hakuonekani kuwa wazo jema. Angalia kile alichomfanyia Ayubu. Unadhani Petro anamaanisha nini hasa anapotuambia “tumpinge” Shetani? (Jambo la msingi ni kauli ya maneno “mkiwa thabiti katika imani.” Tunaweka tumaini letu kwa Mungu. Tuna imani kwa Mungu. Pambano ni kati ya Mungu na Shetani, hatusimami peke yetu dhidi ya Shetani.)

 

   1. Kwa nini ni muhimu kujua kwamba Wakristo wengine wanateseka? (Unapata faraja kwamba hauko peke yako.)

 

   1. Kwa nini Petro anabainisha “mateso” katika muktadha wa kumpinga Shetani na kumfanya asiturarue? (Muktadha huu ni wa muhimu sana tena sana. Pambano linahusiana na majaribu na mateso. Shetani anatuletea magumu maishani, na, kusimama imara katika imani yetu kwa Mungu ndilo jibu kwa shambulizi hili.)

 

   1. Je, mjadala wetu mpana juu ya unyenyekevu unatumika hapa? (Ikiwa tuna majisifu, tuna uwezekano mdogo wa kumgeukia Mungu kwa ajili ya msaada wake.)

 

  1. Soma 1 Petro 5:10. Kwa upande mmoja yupo Shetani ambaye angependa “kutuangamiza,” je, tunaye nani katika upande mwingine? (Mungu!)

 

   1. Mtazamo wa Mungu kwetu ni upi? (Neema! Yeye ni “Mungu wa neema yote.”)

 

 

   1. Mpango wa Mungu kwetu ni upi? (Kutujenga upya kutoka kwenye majeraha na uharibifu unaosababishwa na Shetani, na kutufanya kuwa “imara, thabiti na wenye msimamo.”)

 

  1. Rafiki, je, unatamani kuwa “thabiti, imara na mwenye msimamo?” Kuelewa uhusiano sahihi kati yako na serikali yako, mwajiri wako, mwenzi wako, mateso yako, washiriki wenzako wa kanisa, na pambano kati ya Shetani na Mungu, itakuweka kwenye mwelekeo wa kuwa Mkristo mwenye kumwamini Mungu. Kwa nini usimwombe Mungu leo akusaidie, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kusalia kwenye njia ya mahusiano sahihi?

 

 1. Juma lijalo: Yesu Katika Maandiko ya Petro.