Yesu Katika Maandiko ya Petro

Swahili
(1 Petro 1:1; 2 Petro 1:1)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Miaka kadhaa iliyopita nilisoma kitabu chenye kutisha kilichoandikwa na Dan Brown kiitwacho “The Da Vinci Code.” Uandishi wake na mashaka yake havikuwa vibaya, kilichokuwa cha kutisha ni kwamba kitabu kilijenga hoja kuwa vitabu vya injili vilikuwa vimefanyiwa hila na Kanisa Katoliki ili kukandamiza maandiko yaliyosema kwamba Yesu alikuwa tu ni mtu mwema. Badala yake, kanisa lilisaidia katika kuchapisha vitabu hivyo vya injili vilivyosema kuwa Yesu alikuwa Mungu. Nilidhani kwamba jambo hili lilikuwa na madhara makubwa sana kwa sababu kwa mtu wa kawaida, asiyejua chochote kuhusu historia ya kale na anayefahamu Biblia kwa juu juu, hii ingekuwa vigumu kwake kukanusha hoja za mwandishi. Nyaraka za Petro tunazojifunza si sehemu ya vitabu vya injili. Bebu tuzame kwenye somo letu la barua za Petro ili tuone kile ambacho Petro (pamoja na wengineo) anakisema kuhusu asili ya Yesu!

 

 1. Msingi Wake ni Yesu

 

  1. Soma 1 Petro 1:1 na 2 Petro 1:1. Kuna jambo gani linalojirudiarudia kwa jinsi Petro anavyojitambulisha? (Anasema kuwa yeye ni “mtume wa Yesu Kristo.”)

 

   1. Unaposikia wazungumzaji wanatambulishwa, unadhani mtambulishaji anaamuaje kuwa aseme nini juu ya mzungumzaji?

 

   1. Unapojitambulisha mwenyewe kwa watu wengine, na unajielezea kwa ufupi, unachaguaje mambo ya kuyazungumzia? (Katika hali zote mbili, ama unasema mambo ambayo ni ya muhimu zaidi juu ya maisha yako, au angalao yaliyo ya muhimu zaidi kwa mujibu wa hadhira unayozungumza nayo.)

 

    1. Hii inazungumzia nini juu ya mtazamo wa Petro kwa Yesu? (Kwamba Yesu ndio kitu cha pekee ambacho amewahi kukutana nacho.)

 

     1. Je, hilo ni kweli kwako pia?

 

  1. Soma tena nusu ya pili ya 2 Petro 1:1. Yesu anaelezewaje? (“Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo.”

 

   1. Petro anatusaidiaje dhidi ya uongo uliomo kwenye kitabu cha Da Vinci Code? (Hii ni habari njema. Dan Brown, na wale wanaokubaliana na uongo huu, hawalifahamu Agano Jipya kwa kina. Madai kwamba Yesu ni Mungu hayapo tu kwenye vitabu vya injili, yapo kwenye Agano Jipya lote. Tunachokisoma kwenye nyaraka za Petro ni mfano wa jambo hili.)

 

  1. Soma 1 Petro 1:18-21. Hii inatuambia kuwa sababu ya Mungu kuanzisha mfumo wa utoaji kafara unaopatikana katika Agano la Kale ni ipi? (Mambo yote yalikuwa yanamwelekeza Yesu.)

 

   1. Ni kwa muda gani Mungu alikuwa na mpango wa kumtumia Yesu kutuokoa kutoka dhambini? (“Kabla haijawekwa misingi ya dunia!”)

 

 

   1. Inamaanisha nini kusema kuwa Mungu “alimpa utukufu” Yesu? (Soma Wakolosai 1:13-19. Yesu ana “mamlaka ya juu kabisa” kwa vitu vyote. Mungu aliumba “vitu vyote” na kwa uwezo wake “vitu vyote hushikana katika yeye.” “Utimilifu” wa Mungu hukaa ndani ya Yesu. Kwa dhahiri, Yesu hakuwa tu mtu mwema.)

 

   1. Soma Wafilipi 2:9-11. Hii inaelezeaje jinsi Yesu alivyotukuzwa? (Yesu anainuliwa katika nafasi ya juu kabisa. “Yesu Kristo ni Bwana.”)

 

 1. Uaminifu Katika Mateso

 

  1. Soma 1 Petro 2:21-22. Uongo mwingine kwenye kitabu cha Da Vinci Code ni kwamba Yesu alifanya ngono na Mariamu na walikuwa na familia. Kama unataka kusema uongo juu ya Yesu, je, huo ni uongo maridhawa kutokana na watu unaowafahamu? (Linaonekana kama jambo wanalolifanya wanadamu.)

 

   1. Je, yale anayoyaandika Petro kwenye vifungu hivi yanawezekana kuwa ni ya uongo? Hususani, ikiwa ulitaka kumsawishi mtu kwamba Yesu alikuwa Mungu, je, huu ndio uongo ambao ungeuchagua? (Mungu atesekaye si aina ya uongo ambao ningeutumia. Endapo ningekuwa ninataka kumtengeneza mungu, ningemchagua/ningemtengeneza mungu mwenye ushindi.)

 

   1. Fikiria jambo hili. Kama ungetaka kuwahadaa watu wamfuate mungu wa uongo, je, ungewalaghai (ungewashawishi) kwa kusema “mliitwa” ili mpitie mateso? (Hapana! Hii inaelekea kuthibitisha ukweli wa kile anachokiandika Petro kuhusu Yesu.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:23-24. Petro anapoandika “mwili wake juu ya mti,” je, anarejelea jambo gani? (Kusulubiwa kwa Yesu.)

 

   1. Je, hiyo ndio njia bora ya kuwalaghai wafuasi? (Mambo yote haya yanazungumza nasi juu ya uaminifu. Hivi sivyo ambavyo utatunga kisa kuhusu mungu wa uongo.)

 

 1. Masihi – Agano Jipya

 

  1. Soma 1 Petro 1:3-4. Petro anatoa madai gani yasiyo na kifani yanayomtofautisha Yesu na mtu wa kawaida tu? (Kwamba alifufuka kutoka katika wafu, na kwamba kifo chake kinakuandalia thawabu mbinguni.)

 

  1. Soma 1 Petro 3:21-22. Nani yupo mbinguni, katika “mkono wa kuume wa Mungu,” na “malaika, na enzi na mamlaka vimetiishwa chini yake?” (Yesu. Hii ni kauli nyingine ya dhahiri, nje ya vitabu vya injili, kwamba Yesu ana mamlaka mbinguni.)

 

  1. Soma Ufunuo 20:6. Hii inazungumzia nini juu ya mustakabali wa Yesu? (Hii inaunga mkono kauli inayosema kwamba Yesu ana mamlaka mbinguni.)

 

  1. Soma Yohana 11:25-27. Hii ni kauli ya injili inayosema, kwa mujibu wa Dan Brown, kwamba injili ilifanyiwa hila na Kanisa Katoliki. Inakaribiana kwa kiasi gani na kifungu tulichokisoma hivi punde kwenye Ufunuo? Kinakaribiana kwa kiasi gani na kile anachokiandika Petro juu ya Yesu kwenye nyaraka zake?

 

 1. Masihi – Agano la Kale

 

  1. Soma Zaburi 2:2-4 na uilinganishe na Matendo 4:25-27. Kitabu cha Matendo kinatafsirije unabii huu uliopo kwenye kitabu cha Zaburi? (Kinasema kuwa ni unabii kumhusu Yesu.)

 

 

  1. Soma Danieli 9:25-26. Sitaingia kwenye ukokotoaji hapa, lakini hapa tunayo rejea nyingine ya “Aliyetiwa Mafuta” akija katika kipindi mahsusi. Kipindi hicho kinaingiliana na kipindi ambacho Yesu aliishi duniani. Je, Kanisa Katoliki lilikuwepo katika kipindi cha ufalme wa Babeli (Danieli 9:1-2) ili kuufanyia hila unabii wa Danieli? (La hasha!)

 

  1. Soma Zaburi 16:8-11 na uilinganishe na Matendo 13:35-38. Kitabu cha Matendo kina uelewa gani wa vifungu vya kitabu cha Zaburi 16? (Bado ni unabii mwingine kuhusu Yesu.)

 

  1. Soma Danieli 7:13-14 na uilinganishe na Mathayo 9:6. Yesu alitabiriwa kutwaa mamlaka gani? (Mamlaka yote. Katika Mathayo 9 Yesu anawaelezea watu kwamba anayo mamlaka ya kusamehe dhambi.)

 

  1. Soma Mika 5:2 na uilinganishe na Mathayo 2:1-6. Agano la Kale lilisema kuwa Yesu atazaliwa wapi?

 

  1. Hebu tuchimbue uongo wa Dan Brown kwa kina zaidi. Ikiwa Brown yuko sahihi kwamba Yesu hakufa, na badala yake alioa na kuzaa watoto wengi, tuhitimisheje kuhusu huu unabii wa Agano la Kale? (Mtu fulani, aliyezaliwa katika kipindi kimoja na Yesu, alipaswa kuwa Masihi. Mtu huyo yupo wapi?)

 

   1. Maelezo ya Brown ni yapi kuhusu unabii wa Agano la Kale juu ya “Mtiwa Mafuta” aliyefanya mambo yale yale aliyoyafanya Yesu? (Hoja ya Brown, kama ambavyo nimeielewa, sio kwamba Kanisa Katoliki liliandika vitabu vya injili, badala yake ni kwamba liliwakandamiza wale waliokuwa wanasema kuwa Yesu alikuwa mwanadamu tu. Ikiwa jambo hili ni kweli, basi inamaanisha kuwa maelezo ya Yesu ambayo Kanisa liliyaunga mkono yaliandika kumbukumbu ya matendo ya Yesu yaliyoendana na unabii kwa kulingana (kufanana). Yaani, kama wasemavyo, daraja lililo mbali sana kuweza kulivuka. Masihi wa uongo anawezaje kufanya mambo yale yale kama yalivyotabiriwa kwenye Agano la Kale? Hii ingewezekana tu endapo injili za sasa zingekuwa ni za kutunga – zikiwa zimebuniwa na watu waliokuwa na uelewa sahihi wa unabii wa Agano la Kale. Kwa nini mtu anayemtafuta masihi wa kweli kwa dhati abuni masihi wa uongo?)

 

 1. Roho Yako

 

  1. Soma Yohana 16:7-10. Je, itakuwa vigumu kwa wapagani kughushi aina hii ya maelekezo na ubashiri?

 

  1. Soma Warumi 8:5-9. Hii inatuambia nini juu ya uzoefu wa muumini asiyetegemea usahihi wa maandiko ya injili? (Inatuambia kuwa Roho Mtakatifu anauhakikisha uelewa wetu wa Yesu. Inathibitisha kauli ya Yesu (katika vitabu vya injili) kwamba Roho Mtakatifu atakuja na kufanya kazi pamoja nasi. Huu ni uthibitisho unaojitegemea unaothibitisha kuwa Yesu ni Mungu, hakuwa tu mwanadamu aliyeishi na kufa kama mtu yeyote yule.)

 

 

  1. Rafiki, je, utaweka tumaini lako kwa Yesu kama Masihi na Mkombozi wako? Dan Brown si wa kwanza kuhoji kwamba Yesu hakuwa Masihi. Lakini, uthibitisho wa Yesu kama Masihi unatoka katika Agano la Kale, na unaungwa mkono na vitabu vyote vya Agano Jipya (tofauti na vitabu vya injili), na unaendana na maelezo ya maisha ya Yesu. Kwa kuongezea, kama umekuwa mfuasi wa Yesu, basi utakuwa umehisi mwongozo wa Roho Mtakatifu maishani mwako.

 

 1. Juma lijalo: Kuwa Vile Utakavyo Kuwa.