Unabii na Maandiko

Swahili
(2 Petro 1:16-20)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Majuma mawili yaliyopita tulijadili sababu za sisi kuwa na imani na ujasiri wa kusema kuwa Yesu ni Mungu. Juma hili Petro anarejea kwenye mada hii. Kwa nini? Je, inaonekana ajabu kwako kwamba Petro anatumia muda mwingi sana kuthibitisha imani yake kwa Yesu? Inaweza kuonekana ajabu maelfu ya miaka baadaye, lakini katika kipindi kile, hiki ndicho kilichokuwa kiini cha uongofu – kujenga hoja kwamba Yesu, mtu aliyeishi duniani na ambaye alisulubiwa na mamlaka za kipindi hicho, pia alikuwa Mungu kamili. Bado hili ni suala kubwa katika kuwaleta wasioamini kuishika imani. Hebu tuchambue hoja za Petro ili kuimarisha imani yetu leo na tujifunze jinsi tunavyoweza kumtangaza Yesu vizuri zaidi kwa watu wengine!

 

 1. Sauti

 

  1. Soma 2 Petro 1:16. Unakumbuka mjadala wetu wa Da Vinci Code? Tulijadili ili kufahamu kama vitabu vya injili vilikuwa ni habari za “kutunga” kuhusu uungu wa Yesu. Pia tulijifunza kuwa Petro alikuwa mtetezi mkuu juu ya uungu wa Yesu. Hivyo, tunaweza kuuliza suala hilo hilo kumhusu Petro, je, alibuni habari hizi? Petro anaandika nini juu ya habari za kutunga kumhusu Yesu? (Anakana kwamba alipotoshwa kwa habari za kutungwa kwa ustadi. Kwa dhahiri, Petro anakiri kuwa suala hili lipo, lakini anadhani kuwa watu wataamini kuwa alipotoshwa, na sio kwamba anawapotosha watu wengine.)

 

   1. Hilo linazungumzia nini juu ya anachokiwazia Petro kuhusu kuwapotosha watu wengine? (Hajafikiria kwamba watu watadhani kuwa anabuni suala hili. Ama kwa hakika, hakuna mtu aliyependekeza jambo hilo kwake.)

 

   1. Petro anakanushaje dhana ya kwamba alikuwa amepotoshwa na habari zilizobuniwa kwa umahiri? (Anasema kuwa hapati taarifa hii ikiwa imezeeka. Hapana, alikuwa shuhuda kwenye ukuu na utukufu wa Yesu.)

 

  1. Soma 2 Petro 1:17 na Mathayo 17:4-5. Petro anasema kuwa nani aliyeidhinisha uungu wa Yesu? (Mungu Baba. Petro aliyasikia maneno hayo!)

 

   1. Angalia muda ambao maneno hayo yalitamkwa katika Mathayo 17:5. Mungu aliingilia kati Petro alipomwita Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu. Petro anakumbuka kile kitendo cha kuingiliwa kati!

 

   1. Hebu tusome muktadha. Soma Mathayo 17:1-6. Kama ungekuwa Petro, na ukawa unahoji kujua uungu wa Yesu, je, ungesema tu kwamba, nilisikia “sauti hii…. kutoka mbinguni?” (Hapana! Ningesimulia kisa chote cha kusisimua. Kingemtangaza Yesu na kingenitangaza!)

 

    1. Tunajifunza nini kutokana na ukweli kwamba Petro anajizuia kuzungumzia hiki kisa chote? (Kwa dhahiri, Petro hatii chumvi wala kuongeza maneno yake katika kumthibitisha Yesu.)

 

 

  1. Soma 2 Petro 1:18. Je, Petro anao watu wengine watakaothibitisha kisa chake? (Anasema “Na sauti hiyo sisi tuliisikia.” Tulijifunza katika Mathayo 17 kwamba Yakobo na Yohana pia walikuwepo mahali pale.)

 

  1. Chukulia kwamba wewe ni mwanasheria uliyekuwa unaandaa uthibitisho wa Petro. Je, ungechukulia mambo gani kuwa ni ya muhimu katika huo uthibitisho? (Petro alisikia na kuuona ukuu wa Yesu. Aliisikia sauti ya Mungu iliyodai kuwa Yesu alikuwa Mwanaye. Mungu aliidhinisha yale aliyokuwa akiyafanya Yesu. Petro anao mashahidi wanaoweza kuthibitisha. Namna Petro anavyoelezea kisa hiki inaonekana kuwa ni ukweli mtupu. Anaepuka kutia chumvi na kuzungumzia jambo hili kwa undani kitendo kinachoweza kugadimu hadhi yake.)

 

 1. Unabii

 

  1. Soma 2 Petro 1:19. Petro anazungumzia uthibitisho gani mwingine kuhusu uungu wa Yesu? (Manabii wa Agano la Kale.)

 

  1. Hebu tuangalie baadhi ya masuala haya. Soma Zaburi 22:1 na Zaburi 22:16-18. Je, unayafahamu maneno haya? (Soma Mathayo 27:37-46 na Luka 24:36-39. Ilikuwa ukweli kwamba mtu aliyesulubiwa alipigiliwa misumari mikononi na miguuni pale msalabani. Yesu aliwaambia wafuasi wake kuangalia mikono na miguu yake kwa sababu ilikuwa na alama za makovu yaliyotokana na kusulubiwa kwake.)

 

  1. Soma Zekaria 12:10, Isaya 53:5, na Isaya 53:10. Vifungu hivi vinatabiri nini kilichomtokea Yesu msalabani? (Nimenukuu unabii mchache tu unaoelezea maisha ya Yesu.)

 

  1. Angalia tena 2 Petro 1:19, lakini mara hii hebu tujikite kwenye nusu ya pili ya kifungu hicho. Petro anatumia analojia gani katika uelewa wetu wa jinsi unabii ulivyotabiri maisha ya Yesu? (Anailinganisha na kuchomoza kwa jua majira ya asubuhi.)

 

   1. Ni kwa jinsi gani ulinganifu huo unafaa sana? (Watu walipojifunza unabii, na kuulinganisha na matukio yanayohusu maisha ya Yesu, uelewa wao uliendelea kukua na kukua. Hatimaye, waliweza “kuona” jinsi Yesu alivyotimiza unabii wa Agano la Kale na jinsi alivyotimiza mfumo wa kafara wa Agano la Kale.)

 

  1. Soma 2 Petro 1:20-21. Petro anajihusisha kwenye hoja inayosema kwamba Yesu ni Masihi. Anakabiliana na hoja gani hapa? (Dhana ya kwamba unabii wa Agano la Kale ulikuwa tu ni mawazo ya wanadamu. Petro anatuambia kuwa Roho Mtakatifu aliuweka unabii huu akilini (mawazoni) mwa manabii.)

 

   1. Kwa nini jambo hili ni la muhimu? (Inaonesha kwamba ujio wa Yesu ulikuwa ni mpango wa Mungu. Mamia ya miaka kabla Yesu hajaja duniani kama mwanadamu, Mungu aliwavuvia manabii kuandika juu ya ujio wa Yesu na kifo chake.)

 

   1. Angalia jinsi unabii wa Agano la Kale ulivyoandikwa. Je, hii inaashiria kuwa Roho Mtakatifu ndiye aliyetoa mwongozo (kwa njia ya imla) wa maneno ya manabii? (Petro anaandika juu ya “mapenzi ya mwanadamu.” Anaonekana kutuambia kuwa Roho Mtakatifu alitenda kazi kutokana na “mapenzi” ya nabii. Kisha waliandika (“walizungumza”) kwa kadri Roho Mtakatifu “alivyoendana” na mapenzi yao.)

 

 

  1. Soma 2 Timotheo 3:14-15. Huyu ni Paulo akimwandikia Timotheo (2 Timotheo 1:1-2). Ni kwa msingi upi Paulo anasema kuwa Timotheo anapaswa kusalia katika imani? (Uaminifu/uadilifu wa watu waliomfundisha, maamuzi ya injili aliyoyafanya, na kile anachokisoma kwenye Biblia.)

 

   1. Je, unaona mambo yanayofanana kwenye hoja za kumwamini Mungu zilizotolewa na Petro na Paulo?

 

  1. Soma 2 Timotheo 3:16-17. “Pumzi ya Mungu” ni neno lisilo la kawaida sana. Unadhani linamaanisha nini? (Maoni ya Barnes yanatafsiri wazo hili kama “kupulizia, au kuipulizia roho.”)

 

   1. Soma Mwanzo 2:7. Je, hii inakusaidia kuelewa vizuri zaidi maelezo ya kwamba Maandiko yana“pumzi ya Mungu?” (Mimi inanisaidia. Mungu alimhuisha Adamu kwa pumzi yake. Akawa hai kwa pumzi ya Mungu. Maandiko yamehuishwa na Roho wa Mungu. Sidhani kama Mungu alitoa mwongozo kwa njia ya imla na waandishi wakaandika maneno aliyoyasema Mungu katika kuandika Biblia. Badala yake, nadhani waandishi wa Biblia walivuviwa na Roho Mtakatifu. Mawazo ya Mungu yalikuwa hai alipowapulizia waandishi vifungu vya maandiko.)

 

   1. Sasa, hebu turejee nyuma kidogo na tusome tena 2 Petro 1:21. Hii inathibitishaje hoja ya Petro kwamba unabii ndio sababu ya kuamini kwamba Yesu ni Mungu? (Unabii huo ulitokana na uwezo wa Mungu. Kama Mungu alivyompatia Adamu uhai, vivyo hivyo Mungu anaupa uzima unabii unaomzungumzia Yesu.)

 

  1. Rafiki, je, umeridhika kuhusu habari za Yesu? Je, unaamini kuwa alitumwa kutoka kwa Mungu, akafanyika mwanadamu, akaishi na kufa ili kutuondolea dhambi zetu, na sasa amerejea kwa Baba yake mbinguni kuwa Mtawala wa vitu vyote?

 

 1. Juma lijalo: Walimu wa Uongo.