Mamlaka ya Paulo na Injili

Swahili
(Wagalatia 1)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Unapotaka kumshawishi mtu akubaliane na hoja yako, unafanyaje? Je, unamwambia kuwa unafanya kazi serikalini? Je, unawaambia kuwa una elimu kubwa? Je, unawaambia kwamba wewe ni mwerevu? Je, unawaambia kuwa una mtazamo wa pekee juu ta tatizo lililopo? Je, unamwambia kuhusu uzoefu wako? Paulo anakubaliana na jambo hili hili. Wakristo katika kanisa la Galatia wanatoka nje ya msitari katika uelewa wao wa injili. Paulo anatakiwa kuwashawishi ili kuwarejesha kwenye msitari. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone jinsi Paulo anavyotekeleza jambo hili! Tunapokuwa kwenye hali hiyo, tuwe makini zaidi katika kile anachokizungumzia Paulo kuhusu wokovu wetu.

 

 1. Mamlaka ya Barua

 

  1. Soma Wagalatia 1:1-2. Utamaduni wa uandishi wa barua katika kipindi cha Paulo ni kuanza na jina la mwandishi na kisha kuandika jina la mhusika anayepelekewa hiyo barua. Unaichukuliaje njia aliyoitumia Paulo kujitambulisha?

 

  1. Soma 1 Wathesalonike 1:1. Hapa utangulizi wa Paulo unatofautianaje?

 

  1. Soma Luka 6:12-16 na Mathayo 10:1-2. Hivi karibuni nimesoma wasifu wa mtu anayeshikilia nafasi ya ushauri serikalini, wasifu huo unaofanana na wangu. Hata hivyo, mtu huyo ameielezea nafasi anayoishikialia kwa namna inayoifanya nafasi hiyo ionekane kuwa ni ya muhimu sana. Mwanzoni nilidhani kuwa kitendo hiki ni “kusifia wasifu kupita kiasi,” kisha nikajiuliza, “Je, nami niiandike nafasi hiyo vivyo hivyo kwenye wasifu wangu?” Wewe una maoni gani? Je, Paulo anapaswa kujiita “mtume” wakati yeye si mmojawapo wa mitume kumi na wawili?

 

  1. Soma tena Wagalatia 1:1. Hoja ya Paulo ni ipi inayounga mkono yeye kujiita mtume? (Anasema kuwa alitumwa na Yesu na Mungu Baba. Kwa namna hii anafanana na mitume kumi na wawili halisi wa awali.)

 

   1. Unadhani kwa nini Paulo anayataja mamlaka yake kwa ngazi ya juu kabisa kadri inavyowezekana? (Anawaambia wasomaji wake kwamba anayo mamlaka ya hali ya juu kuweza kuandika yale tutakayoyajifunza. Huu ndio mwanzo wa hoja yake anapotoa sababu ya kwa nini wanapaswa kumwamini.)

 

 1. Neema na Amani

 

  1. Soma Wagalatia 1:3-5. Soma tena Wagalatia 1:1. Paulo anasisitiza nini anapomwelezea Yesu? (Katika kifungu cha 1 anabainisha kifo cha Yesu. Katika kifungu cha 4 anabainisha mateso (“alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu”). Maisha makamilifu ya Yesu, kifo chake kwa ajili yetu, na ufufuo wake na kurejea kwake mbinguni ni msingi wa kuhesabiwa kwetu haki kwa imani, kipengele cha muhimu kabisa cha neema. Paulo analizungumzia jambo hili katika utangulizi wake. Kwa mara nyingine, hii ni sehemu ya hoja ya Paulo kwa kanisa la Galatia.)

 

 

  1. Soma Wagalatia 1:6-7. Kuna tatizo gani katika kanisa la Galatia? (“Wanaigeukia injili tofauti.”)

 

   1. Je, sasa unaona sababu ya Paulo kubainisha ngazi yake ya juu kabisa ya mamlaka mwanzoni mwa barua?

 

  1. Hebu turukie mbele kidogo ili tuelewe vizuri zaidi jambo linalohusika kwenye mjadala wa “injili.” Soma Wagalatia 2:15-16. Paulo anamaanisha nini anapoandika juu ya “injili?” (Kuhesabiwa haki kwa imani pekee tofauti na kuhesabiwa haki kwa matendo.)

 

  1. Soma Wagalatia 1:8-9. Paulo anawaelezeaje wale wanaojenga hoja kupinga injili ya kuhesabiwa haki kwa imani? (Wanapotosha (kifungu cha 7) injili, na Paulo anasema (mara mbili) kuwa wanapaswa “kulaaniwa milele.”)

 

   1. Haya ni maneno mazito sana! Je, tunapaswa kuwalaani wale wanaojenga hoja kupinga neema kwa kutumia hayo maneno mazito?

 

   1. Asubuhi ya leo nilikuwa ninatafakari juu ya kaulimbiu ya “salama kwa ajili ya kuokoa.” Hii inaakisi fundisho ambalo kimsingi linasema kuwa ili kwenda mbinguni unatakiwa uwe “salama” – kwa maana ya kwamba hutaanzisha dhambi katika ukamilifu wa mbinguni. Kuna wakati nilidhani kuwa hali hii inaleta mantiki nzuri, na nikajiuliza kama nilikuwa “salama kwa ajili ya kuokoa.” Baada ya kutafakari zaidi, nilitambua tu kwamba hii ni injili ya matendo. Ili kuokolewa, ninatakiwa kujifanya “salama.” Ninapomsikia mtu akirudia kusema kaulimbiu hiyo, je, niwaite kuwa ni “wapotoshaji” wanaopaswa “kulaaniwa milele?”

 

    1. Unadhani kwa nini Paulo alitumia hayo maneno mazito?

 

    1. Soma 1 Petro 3:15. Je, maneno mazito ya Paulo yanaendana na kuonyesha “upole na hofu” kwa wale wasiokubaliana? (Ninazidi kwenda mbele na kurudi nyuma katika jambo hili. Tulipojadili nyaraka za Petro, nilifundisha kwamba lengo ni kuwa na utii. Hata hivyo, wote wawili, Paulo na Yesu (Mathayo 22:33) walitumia lugha nzito sana ambayo siichukulii kama ni ya utii endapo wangekuwa wananizungumzia mimi!)

 

 1. Mamlaka ya Paulo

 

  1. Soma Wagalatia 1:10-12. Paulo anaandika kwamba hachukulii nafasi yake ya injili kuwa maarufu, na haichukulii kwa sababu mtu fulani kamfundisha kufanya hivyo, au kwa sababu ameyafanya haya yeye mwenyewe. Sababu ya Paulo kuchukua nafasi yake ni ipi? (Mtazamo wa Paulo unatokana na ufunuo wa Yesu. Kwa mara nyingine tunaona sababu ya Paulo kusema kuwa yeye ni mtume. Kudai kwamba huo ni ufunuo wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu, ndio mamlaka ya mwisho.)

 

  1. Soma Wagalatia 1:13-14. Je, Paulo anatuambia kuwa tunatakiwa kumwamini kwa sababu amefanikiwa kwa kiwango cha juu? Yeye ameendelea miongoni mwa wenzake? (Hapana. Ni ukweli anaposema kwamba alikuwa anafanya vizuri zaidi ya wengine. Lakini, anachokimaanisha ni kwamba hakuwa na sababu za hapa duniani kubadili mitazamo yake. Alikuwa mtu wa mafanikio, sio mtu aliyeshindwa, katika maisha yake ya utu uzima.)

 

  1. Soma Wagalatia 1:15-16. Nani aliyebadili mawazo ya Paulo? (Mungu aliingilia kati ili kuyabadili maisha yake. Mara zote huu ulikuwa mpango wa Mungu (“aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu”) kwa ajili ya maisha ya Paulo.)

 

 

  1. Soma Wagalatia 1:16-17. Je, haya ni majigambo? Kwa nini asipate msaada kutoka kwa viongozi wa kanisa? Kwa nini asipate msaada kutoka kwa wale waliomsikia Yesu akihubiri?

 

  1. Soma Wagalatia 1:18. Paulo anatuambia (kifungu cha 17) kwamba alikwenda “mara moja” Arabuni na Dameski ambapo (kifungu cha 18) alikaa kwa muda wa miaka mitatu. Unadhani Paulo alikuwa anafanya nini katika hicho kipindi cha miaka mitatu? (Paulo hasemi moja kwa moja, lakini inaonekana kwamba Paulo aliutumia muda huo kufundishwa na Mungu, akitafakari maisha yake ya zamani, na kufikia hatua ya kuielewa injili. Ujumbe wa msingi wa Paulo ni kwamba ujumbe wake ulitoka kwa Mungu na si kutoka kwa wanadamu.)

 

  1. Soma Wagalatia 1:19-20. Kwa nini Paulo anasisitiza kwamba hakutumia muda na mitume, zaidi ya Petro? Wao ni viongozi wa kanisa! (Ingawa ni viongozi, wao si chanzo kizuri cha mafundisho ya kiroho kama ilivyo kwa Yesu mwenyewe.)

 

  1. Uelewa wako wa injili ungekuwa na tofauti gani endapo ungekuwa hujasoma na kuvikubali vitabu vya Agano jipya vilivyoandikwa na Paulo?

 

  1. Soma Mathayo 25:31-36. Linganisha na Mathayo 25:41-43. Ungeuelewaje wokovu endapo ungekuwa na ufahamu wa huu mjadala pekee kuweza kufanya maamuzi?

 

   1. Hii inaendanaje na Wagalatia 2:15-16?

 

   1. Paulo anasema kuwa alipokea uelewa wa injili kutokana na ufunuo wa Yesu Kristo (Wagalatia 1:11-12). Hii inamaanisha kwamba Yesu yule yule aliyeelezea mfano wa mbuzi na kondoo, pia alimpatia Paulo Wagalatia 2:15-16. Ikiwa unayaamini madai ya Paulo ya kuwa na mamlaka (mimi ninaamini), basi kwa dhahiri, huu mgongano wa wazi unahitaji kujifunza zaidi! Kwa hakika hiki ndicho tutakachokwenda kukifanya katika masomo yaliyosalia kwenye mfululizo wa masomo haya.)

 

  1. Soma Wagalatia 1:21-24. Paulo ana sifa gani katika makanisa ya Uyahudi? (Hawezi kubadili maisha yake ya zamani. Lakini, Wakristo wanamtukuza Mungu kwa sababu ya mabadiliko katika maisha ya Paulo.)

 

  1. Rafiki, je, umeshawishika na kuridhika na mamlaka ya Paulo? Je, umeshawishika kwamba injili yake inatoka kwa Yesu moja kwa moja? Ikiwa ndivyo, basi hebu tujifunze kwa makini kile anachotufundisha Paulo tunapojikita zaidi kwenye somo letu la waraka kwa kwa Wagalatia!

 

 1. Juma lijalo: Umoja wa Injili.