Somo la 8: Kutoka Kuwa Watumwa Hadi Kuwa Warithi

Swahili
(Wagalatia 3:26-4:20)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Unakumbuka kipindi ulipokuwa likizo na kuona mlima mzuri au korongo lenye mandhari nzuri ya kupendeza macho? Je, uliweza kuuzunguka mlima huo au korongo hilo ili uweze kuviona kutokea mahali tofauti tofauti? Hivyo ndivyo somo letu linavyoonekana kwa sasa. Tumekuwa tukijiuliza swali hili: “Ikiwa tuliokolewa kwa kumtumaini Mungu tangu mwanzo kabisa, kwa nini Mungu alitupatia Amri Kumi baadaye?” Tumeliangalia swali hili mara kadhaa sasa, na tunaliangalia kwa mara nyingine tena katika somo hili. Kwa dhahiri Paulo anatutaka tuliangalie swali hili katika nyanja mbalimbali, hivyo hebu tuzame kwenye somo letu ili tuliangalie katika mfumo tofauti!

 

 1. Wana na Binti

 

  1. Soma Wagalatia 3:23-26. Je, hadhi yako imeboresheka? (Tumekua kutoka kuwa “watumwa” hadi kuwa “wana!”)

 

   1. Ni kwa jinsi gani tumefanyika kuwa wana? (“Kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.”)

 

  1. Soma Wagalatia 3:27. Ubatizo ni wa muhimu kwa kiasi gani? (Ni wa muhimu kupita kiasi! Tunapozamishwa majini katika ubatizo, “tunajivika” maisha, kifo na ufufuo wa Yesu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:28. Katika kipindi ambacho Paulo aliandika kitabu cha Wagalatia, palikuwepo na tofauti kubwa sana ya kijamii kati ya Wayahudi, Wayunani, watumwa, wanawake na wanaume. Umuhimu wa tofauti hizi ni upi unapookolewa? (Vinapotea. Sote tunakuwa wamoja katika Yesu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:29. Je, huu ni muktadha tofauti na ule tulioujadili majuma mawili yaliyopita? Kisha tulijadili kwamba tulirithi kutoka kwa Ibrahimu mkataba aliouingia kati yake na Mungu. Mkataba huo ulisema kwamba Ibrahimu anapaswa kumwamini (kumtumaini) Mungu, na Mungu ataangalia haki ya Ibrahimu. Hii inazungumzia nini juu ya namna tunavyorithi ahadi iliyotolewa kwa Ibrahimu? (Inasema kwamba tunarithi ikiwa sisi “ni wa Kristo.” Kuwa wa Kristo inamaanisha kwamba tunaamini kile alichokifanya kwa niaba (ajili) yetu. Hii inathibitisha tena ahadi ile ile, urithi ule ule.)

 

 1. Watumwa na Warithi

 

  1. Soma Wagalatia 4:1-2. Paulo anawezaje kusema kuwa mtoto “hana tofauti na mtumwa?” Mtoto (mwana) ana matumaini na mustakabali wa siku zijazo. Mtumwa hana. Tunawezaje kuelewa kile anachokisema Paulo kwa namna inayoleta mantiki? (Paulo anaandika kama mwanasheria. Kwa mtazamo wa kisheria, mtoto mdogo ana ukomo ule ule kama wa mtumwa.)

 

 

  1. Soma Wagalatia 4:3. “Kanuni za msingi za dunia” ni zipi? (Adamu na Eva walionywa kuwa kanuni ya msingi ni kwamba wadhambi wanakufa kifo cha milele. (Linganisha Mwanzo 2:15-17 na Mwanzo 3:1-5). Kwa ujumla Amri Kumi zinaakisi kanuni za msingi za dunia. Usiibe, usiue, na kanuni nyingine za wazi kabisa. Huhitaji Amri Kumi kujua kwamba vitendo hivyo si vizuri.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:4-5. Tunapomzungumzia mtoto, kukua kutoka utotoni hadi utu uzima hutokea mapema kabisa maishani. Mabadiliko haya ya kutoka utumwani hadi kuwa mtu mzima hutokea wakati gani katika muktadha wa uhusiano wetu na Mungu? (Mabadiliko haya yalitokea Yesu alipokuja duniani kuishi, kufa na kufufuliwa kwa niaba (ajili) yetu.)

 

   1. Kila mtu anayesoma somo hili alizaliwa baada ya muda ambao Yesu alikuja duniani. Unadhani Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa sisi (Wagalatia 4:5) tuna “haki kamili za wana?” Je, “haki” hizo ni zipi hasa? (Muktadha unaonesha kuwa tuna haki ya kuwa huru kutoka kwa “walezi na wadhamini.” Hatufanani tena na watumwa.)

 

    1. Je, hii inajumuisha kuwa huru dhidi ya Amri Kumi? (Ndiyo! Pamoja na sheria nyingine zote zilizotolewa na Mungu ili kuwaongoza wanadamu.)

 

   1. Ngoja nikuulize swali la uhalisia kivitendo. Kwa nini wazazi waliwakodisha walezi na wadhamini? Kwa nini uliwafundisha watoto wako kwamba watende mambo fulani na wasitende mambo mengine?

 

    1. Je, unaweza kutarajia kwamba wanao watakapokuwa watu wazima, wataacha mambo yote uliyowafundisha? (Ni kinyume chake tu. Wazazi wanawakodisha “walezi na wadhamini” kuwafundisha na kuwaelekeza watoto wao kwa lengo lile lile la kuwashawishi watoto juu ya namna bora ya kuishi watakapokuwa watu wazim)

 

  1. Soma Wagalatia 4:6. Sisi tulio “watu wazima” na ambao tu watoto wa Mungu ambao tuko huru tunaishi chini ya ushawishi wa nani? (Unaweza kuchoshwa na haya maneno yangu, lakini Paulo anasisitiza kwa kurudiarudia kila mara: tunaye Roho Mtakatifu mioyoni mwetu. Roho Mtakatifu anatuongoza kwenye uhusiano wa Baba na mwana (binti) na Mungu.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:7. Muktadha wa sisi kuwa “warithi” ni upi? Tumekuwa tukijadili nini juu ya urithi wetu? (Tunarithi ahadi ya kwamba ikiwa tunamtumaini Mungu, tutapewa thawabu ya kuwa na haki.)

 

   1. Je, kifungu hiki kinaashiria kuwa tumerithi urithi mwingine zaidi ya huo? (Ndiyo! Tumekuwa sehemu ya familia ya Mungu. Sisi ni wana na binti wa Mungu.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:8. Ulipokuwa ukijadili maswali kadhaa ya mwishoni, yumkini ulisema, “sote tunaishi baada ya kipindi cha Yesu kuwepo hapa duniani, hivyo basi kwa nini hata tunajadili dhana ya sisi kuwa “watumwa” badala ya “wana (watoto)?” Je, kipindi cha utumwa bado kinaendelea hata sasa kwa baadhi ya watu? (Ndiyo. Kwa wale “wasiomjua Mungu,” bado ni watumwa!)

 

   1. Je, mtu anaweza kuzijua Amri Kumi na asimjue Mungu? (Wafikirie wapagani unaowafahamu. Je, wanawaua watu wengine? Je, wanatambua kwamba ni makosa kuiba? Dhana hizi zinaeleweka sana.)

 

 

   1. Wafikirie watu wanaojichukulia kwamba wao ni “watu wema,” lakini wanaikataa na kuipinga “dini.” Je, ni watumwa? (Ndiyo! Wao si watoto wa Mungu kwa kuwa wameikataa zawadi ya Yesu ya wokovu na fursa ya kuwa wana au binti zake.)

 

   1. Nani au kitu gani “si miungu” katika Wagalatia 4:8?

 

  1. Soma Wagalatia 4:9-11. Baadhi ya watu wanasema kuwa dini ambayo Wagalatia “wanairudia” ni fumbo. Je, tuna vidokezo vyovyote? (“Siku na miezi na nyakati za pekee” kwa hakika vinaonekana kufanana na sikukuu za Agano la Kale pamoja na mifumo yake ya kanuni za kiuchumi. Unapotafakari Wagalatia 2:11-15 jibu linaonekana kuwa dhahiri – Paulo anazungumzia juu ya wao kuirudia dini ya Kiyahudi, ambayo inasisitiza juu ya matendo ya sheria.)

 

   1. Je, hiyo ndio “si miungu” ya Wagalatia 4:8?

 

  1. Jikite kwenye Wagalatia 4:10 na rejea yake ya “siku.” Ninaabudu siku ya Jumamosi kwa mujibu wa Mwaanzo 2:2-3, na Kutoka 20:8-11, pamoja na ukweli kwamba Yesu alipumzika kaburini siku ya Jumamosi baada ya kifo chake msalabani. Je, Paulo ananiambia kuwa ninakosea? Je, neema haiko pamoja nami? (Ukiangalia maoni mbalimbali ya kale, watoa maoni wanajenga hoja kwamba kifungu hiki hakihusiani na siku ya pumziko ya kila juma. (Wanajenga hoja kutetea kwenda kanisani siku ya Jumapili.) Nadhani maoni ya Robertson yanafafanua vizuri zaidi: “Paulo hapingani na ushikaji wa kanuni hizi za dini kwa kuwa yeye mwenyewe kama Myahudi alizishika. Alipingana na Mataifa kuzichukulia kama njia ya wokovu.” Kuabudu siku ya Sabato hakukuokoi. Kumtumaini Mungu kunakuokoa.)

 

   1. Ikiwa unaamini, kama ambavyo ninaamini, kwamba pumziko la siku moja katika kila juma na kuabudu ni mpango wa Mungu, je, utapumzika siku gani na kuabudu ikiwa unamtumaini Mungu? (Kutoka 20:11 inatuambia kwamba Sabato inatukumbusha kuwa Mungu ni Muumba wetu. Pumziko la Yesu la Sabato baada ya kuteswa kwake hutukumbusha kwamba Mungu ni Mkombozi wetu. Kwa nini nijichagulie siku yangu mwenyewe (siku tofauti) ikiwa ninamtumaini Mungu?)

 

  1. Soma Wagalatia 4:12-16. Unajisikiaje mtu anapokukosoa kwa lengo la kukusahihisha? Mtu asipokubaliana na mitazamo yako ya kiteolojia? (Hatupendi. Lakini, Paulo anawaambia Wagalatia waizingatie historia yao pamoja naye. Awali alipowafundisha juu ya tumaini na neema walijawa na furaha.)

 

 1. Ari

 

  1. Soma Wagalatia 4:17-18. Je, unaamini katika uinjilisti? Je, unaamini juu ya kuwa “na cheche” katika kueneza injili? Paulo anatupatia onyo gani juu ya kuwa watu wa injili na kuwa na “cheche?” (Anasema kuwa ni sawa ilimradi tu unatekeleza “lengo jema.”)

 

   1. Lengo gani baya linahusishwa hapa? (Kuitangaza sheria badala ya kumtumaini Mungu.)

 

   1. Je, mmewahi kuwa na mjadala kanisani kwako juu ya njia bora ya kueneza injili katika mji wenu? Ikiwa ndivyo, washiriki walipendekeza nini? (Ninakumbuka mapendekezo kadhaa. Pendekezo mojawapo ni kuzungumzia unabii na madubwana yaliyomo katika kitabu cha Ufunuo. Pendekezo jingine lilikuwa ni kuzungumzia juu ya Sabato. Jingine ni kuboresha stadi za mapishi na afya. Jingine ni kuwa na semina zitakazowasaidia watu wa maeneo ya mji kwa namna fulani. Kwa dhahiri baadhi ya mapendekezo hayo yanalenga tu kuwaleta watu katika lango la kanisa.)

 

 

    1. Ikiwa kwa umahsusi unalenga “kumtumaini Mungu” kama sehemu ya kampeni yako ya kusambaza injili, je, utafanya nini?

 

  1. Soma Wagalatia 4:19-20. Kwa nini Paulo “anaigeuza sauti yake” ikiwa alikuwa pamoja na Wagalatia? (Inawezekana anatumia sauti kali ili kuvuta usikivu wao. Ikiwa alikuwepo, asingetakiwa kufanya hivyo.)

 

  1. Rafiki, je, kuiangalia sheria na neema kwa muktadha wa “utumwa” na “wana” inakusaidia kuuelewa umuhimu wa kumtumaini Mungu vizuri zaidi? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akusaidie umtumaini Mungu zaidi?

 

 1. Juma lijalo: Ombi la Paulo la Kichungaji.