Somo la 1: Ushawishi wa Vitu

Swahili
(Luka 12)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Ushawishi wa Vitu

 

(Luka 12)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Inaweza kuonekana kama jambo lenye kuleta mgongano kutoka kujifunza somo linalohusu kuhesabiwa haki kwa imani katika kitabu cha Wagalatia na Warumi hadi kuingia kwenye somo linalohusu uwakili! Uwakili sio mada ninayoipendelea, lakini sikumbuki kuwahi kufundisha somo hili kwa kina. Hata hivyo, uwakili ni suala la muhimu na somo ambalo sote tunaweza kujifunza kuhusu mapenzi ya Mungu kwetu. Hebu tuchimbue Biblia yetu katika somo letu la kwanza kwenye huu mfululizo mpya wa masomo yanayohusu uwakili!

 

 1. Wafu, Tajiri, Kutokuwa na Wasiwasi (Woga)

 

  1. Soma Luka 12:13-14. Yesu anasema kuwa hakuna aliyemweka kuwa mwamuzi kwenye huu mgogoro wa urithi. Unadhani kwa nini mtu huyu aliomba msaada wa Yesu? (Yesu alikuwa mtu mwenye mamlaka. Kama kweli uliuelewa ujumbe wa Yesu, basi alikuwa Mungu.)

 

   1. Kimsingi Yesu anasema, “Sitaingilia kati.” Je, kuna maombi yako yoyote yale yanayoonekana kumwomba Yesu atende jambo linalofanana na hili?

 

  1. Soma Luka 12:15. Badala ya kujaribu kutatua mgogoro huu, Yesu anazungumzia uchoyo. Kwa nini uchoyo unahusika? (Kwa ujumla urithi unahusisha familia. Kwa dhahiri Yesu anadhani kuwa aina hii ya mgogoro kati ya wanafamilia inaakisi zaidi masuala ya kifedha kuliko uhusiano wa kifamilia.)

 

   1. Je, Yesu anamwita mtu huyu kuwa ni mchoyo? (Hapana. Yesu anasema tu kwamba “ajiangalie!” Huenda huu ni wito kwa mtu huyu kutafakari kama anatanguliza fedha mbele kuliko uhusiano wa kifamilia.)

 

   1. Yesu anatoa fundisho gani? (Suala la umiliki mali na uchoyo ni mambo tunayopaswa kuyaangalia kwa makini.)

 

  1. Soma Luka 12:16-18. Je, huu unaonekana kama uamuzi wa busara kibiashara?

 

   1. Kama wewe ni Mkristo, na unayafuata maelekezo ya Mungu maishani mwako, je, unapaswa kutarajia kuwa na mafanikio? (Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-4. Ukiyafuata maagizo ya Mungu, unaweza kuwa na matarajio ya kubarikiwa “mashambani,” kama ilivyo kwa mkulima huyu.)

 

  1. Soma Luka 12:19. Je, huu ni uamuzi wa busara kwa mkulima aliyefanikiwa? Kama umejipatia fedha za kutosha kiasi kwamba huhitaji tena kufanya kazi, je, ni sahihi kustaafu?

 

 

  1. Soma Luka 12:20. Kwa nini mkulima huyu ni mpumbavu? Hakuna mtu ajuaye siku ya kufa kwake. Mtu huyu alikuwa na matumaini ya kuishi kwa kipindi fulani kwa kutegemea akiba ya mazao yake, lakini sasa mtu mwingine atarithi fedha zake. Yumkini mtu aliyemwomba Yesu msaada kuhusu tatizo la urithi atarithi kutoka kwa mkulima huyu!

 

   1. Unapotafakari vipengele vyote katika kisa hiki, je, kuna kipengele chochote unachokiona kuwa si sahihi? Je, kuna maamuzi yoyote ya kidhambi unayoweza kuyabainisha?

 

  1. Soma Luka 12:21. Yesu anasema kuwa tatizo la kiroho kwa mkulima huyu ni lipi? (Hakuwa tajiri kwa Mungu. Alikuwa tu anajifikiria yeye mwenyewe.)

 

   1. Kwa nini kisa hiki ni matokeo ya kimantiki ya mtu anayemwomba Yesu msaada kuhusu tatizo lake la urithi? (Mtu yule hakuwa akifikiria uhusiano wake na wanafamilia wengine (kipaumbele kwa Wakristo) na mkulima mstaafu hakuwa akifikiria kitu chochote zaidi ya kuhifadhi fedha zake.)

 

  1. Soma Luka 12:22-24. Endapo ningekuuliza kumlinganisha mkulima na mzee ambaye hakujitayarisha kustaafu zaidi ya kuwa kama kunguru, je, ungesema kuwa nani kati yao ni mpumbavu?

 

  1. Sina chembe ya shaka mawazoni mwangu kwamba Mungu anadhamiria tuvitafakari hivi visa vyote vitatu kwa pamoja. Hivyo, hebu tumalizie kile anachokisema Yesu kuhusu wasiwasi. Soma Luka 12:25-26. Je, mkulima alikuwa na wasiwasi juu ya kifo? (Yesu anaonekana kusema kwamba alikuwa na wasiwasi zaidi.)

 

   1. Jambo gani lilikuwa linampa mkulima wasiwasi?

 

  1. Soma Luka 12:27-31. Je, mkulima aliutafuta ufalme wa Mungu? (Huo ndio uliokuwa ukosoaji mahsusi wa Yesu kwa mkulima – hakuwa tajiri kwa Mungu.)

 

  1. Kwa mujibu wa kisa cha maua na ndege, Yesu anamaanisha nini? (Kutokuwa na wasiwasi. Mungu atayashughulikia mahitaji yetu. Wasiwasi hautibu tatizo lolote.)

 

  1. Hebu tuone kama tunaweza kuona jambo lenye mfanano au fundisho la aina moja katika hivi visa vitatu. Kwanza, fikiria jinsi utakavyounganisha kisa kinachohusu urithi na kisa cha mkulima. Kuna fundisho gani linalofanana kwenye hivyo visa viwili? (Wote wawili, yaani mtu mwenye kudai urithi na mkulima wangepaswa kuzingatia zaidi kuhusu kuyatangaza mapenzi ya Mungu. Wote wawili walijikita kwenye masuala ya kifedha maishani mwao.)

 

  1. Unaunganishaje kisa cha mkulima na kisa cha ndege na maua? (Mkulima angejali zaidi kuhusu kuhusu kutokuwa “tajiri” kwa Mungu. Kwa kuwa kisa cha ndege na maua kinahusu kutokuwa na wasiwasi juu ya masuala ya kifedha, watu hawa pia wana wasiwasi zaidi kuhusu fedha na kutomtumaini Mungu.)

 

 

   1. Je, itakuwa haki kukiangalia kisa cha mkulima na kisa cha ndege na maua na kuhitimisha kuwa hatupaswi kuweka akiba kwa ajili ya kustaafu?

 

   1. Kuna tofauti kati ya kuwa na busara na kuwa na wasiwasi? (Soma Mithali 6:6-11. Mungu si mwanzilishi wa uvivu au mipango hafifu. Tatizo la mkulima halikuwa kujipatia kipato na kuweka akiba, bali lilikuwa ni kufanya hivi bila kuwa “tajiri” kwa Mungu. Kumbuka kwamba Luka 12:16 inasema “shamba” lilizaa sana, na sio ustadi wa mkulima. Mkulima alikuwa anaangalia mustakabali wake katika ulimwengu huu pekee na sio mustakabali wake katika ulimwengu ujao.)

 

  1. Unaunganishaje kisa cha mkulima na kisa cha ndege na maua linapokuja suala la kumweka Mungu kwenye taswira pana? (Visa vyote viwili vina jambo moja la kufanana: wasiwasi unatokana na kutotafakari kile ambacho Mungu anakifanya kwa ajili yetu. Uchoyo wa mkulima ulitokana na kutotafakari kile ambacho Mungu anamtaka akitende. Wote wawili walishindwa kutafakari vya kutosha wajibu wa Mungu maishani.)

 

 1. Hazina Yako

 

  1. Soma Luka 12:32-34. Maneno haya yanahusianaje na visa vitatu tulivyojifunza hivi punde? (Nadhani ni maneno ya Yesu kuhusu visa vitatu tulivyojifunza kwa ufupi.)

 

   1. Je, Yesu anatuambia tuuze mali zetu zote? (Hapana. Hasemi kuwa uzeni mali zenu “zote.”)

 

   1. Tunatakiwa kuuza kiasi gani cha mali zetu na kuwapatia masikini? (Yesu hajabainisha.)

 

   1. Ikiwa Yesu hajabainisha, basi tufanye nini sasa? Tunapaswa kuelewaje jambo hili? (Utaona kwamba Luka 12:32 inatuambia kuwa tusiogope. Hiki ndicho kilichomaanishwa kwenye kisa cha ndege na maua. Luka 12:33 inatuambia kuwa tunaweza kuhamisha fedha kwenye akaunti zetu za mbinguni kwa kuwapatia masikini. Hiki ndicho kilichomaanishwa kwenye kisa cha mkulima – alikuwa anajitayarisha kustaafu hapa duniani, ingawa kimsingi alikuwa anaelekea (tunatumaini) mbinguni. Alishindwa kuweka fedha zake mahali sahihi.)

 

   1. Zingatia Luka 12:3 Hii inamaanisha nini? (Kwangu mimi inaonekana kwamba visa vyote vitatu vinahusu mazingatio yetu maishani. Mioyo yetu, kwa kauli ya Yesu, ndio kiti cha uwepo wetu. Kile tunachokitenda kwa mali zetu kinaakisi jinsi tulivyo.)

 

    1. Ugawaji wako wa mali unakuzungumziaje?

 

  1. Soma Luka 12:35-37. Katika visa vilivyopita Yesu anaonekana kuzungumzia fedha na utajiri. Yesu anazungumzia mali gani kwenye hiki kisa cha nne? (Tukifanyacho katika kipindi chetu.)

 

   1. Je, unadhani kwamba Yesu alipokuwa anazungumzia urithi, matokeo ya ukulima, na kisa cha maua na ndege, kwamba hitimisho lake pia lilihusisha jinsi tunavyotumia muda wetu? (Watu wanasema kwamba “muda ni pesa.” Kama hili ni kweli, na nadhani ni kweli, basi matumizi ya muda wetu pia yanaakisi mazingatio yetu maishani, kipaumbele cha kweli cha mioyo yetu.)

 

 

  1. Soma tena Luka 12:31 na Luka 12:37. Somo letu linahusu mali. Je, umasikini ndilo lengo letu? (Sidhani. Vifungu vyote hivi viwili vinasema kuwa Mungu atatupatia vitu ambayo wapenda mali wanavitafuta.)

 

   1. Ikiwa unakubaliana na hitimisho hili, jambo gani tunalopaswa kulizingatia kwenye hivi visa vyetu vinne katika Luka 12? (Mungu anataka mioyo yetu na mawazo yetu yajikite kwake na kuutangaza ufalme wake.)

 

   1. Utakumbuka kwenye utangulizi nilipendekeza kwamba ni “mgongano” kutoka kwenye masomo yetu juu ya neema hadi kuingia kwenye somo la uwakili. Je, hiyo ni kweli? (Hapana! Neema ni kujikita kwenye uhusiano wetu na Mungu badala ya matendo yetu. Inaonekana kwamba uwakili ni vile vile – kuyaweka mazingatio yetu kwa Mungu!)

 

  1. Rafiki, je, utayaelekeza mawazo yako katika kuutangaza Ufalme wa Mungu? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu leo akusaidie kwenye huo mtazamo wako?

 

 1. Juma lijalo: “Ninaona, Ninahitaji, Ninachukua.”