Kuokoka Kutoka Katika Njia za Dunia

Swahili
(Wakolosai 3)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, umeyasikia madai kwamba matajiri ni waroho? Je, unayachukulia madai hayo kuwa ni ya kweli? Kama matajiri tayari ni matajiri, kwa nini wawe na tamaa zaidi? Au, je, hii ni rejea ya wakati matajiri hawakuwa matajiri? Ikiwa ni rejea ya kipindi ambacho matajiri walikuwa maskini, je, haitakuwa sahihi zaidi kusema kwamba maskini ndio waroho? Fikiria kipindi maishani mwako ulipokuwa na fedha kidogo sana. Je, malengo yako yote yalikuwa kwenye fedha? Nafahamu kwamba mimi pamoja na mke wangu tulizingatia zaidi kutafuta fedha tulipooana na tulikuwa maskini sana. Somo letu juma hili linazungumzia juu ya kuwa tofauti na ulimwengu, na kuepuka kujikita katika kuzingatia fedha. Nadhani hili ni somo ambalo kila mmoja wetu analihitaji, bila kujali kama unajihisi wewe ni tajiri au maskini. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze juu ya uzingativu!

 

 1. Uzingativu Sahihi

 

  1. Soma Wakolosai 3:1. Ni watu gani hao “waliofufuliwa pamoja na Kristo?” (Hii inaonekana kuwa ni rejea ya ubatizo. Ikiwa ulimpokea Yesu kama Mungu aliyefanyika kuwa mwanadamu, aliyeishi maisha makamilifu, akafa kwa ajili ya dhambi zetu, na kufufuliwa katika uzima wa milele ili kuchukua tena nafasi yake mbinguni, basi ujumbe huu ni kwa ajili yako! Huu ni ujumbe kwa watu ambao tayari wameokolewa.)

 

   1. Inamaanisha nini “kuyatafuta yaliyo juu?”

 

  1. Soma Wakolosai 3:2. Sasa tunaambiwa kuyaweka “mawazo” yetu kuyafikiria yaliyo juu. Je, tunaambiwa kutenda mambo mawili tofauti? (Ninayachukulia mawazo yangu kuwa kama kiti cha mantiki, na moyo wangu kama kiti cha hisia. Yumkini tunaambiwa kuziweka mantiki zetu na hisia zetu “kwa mambo yaliyo juu.”)

 

   1. Hebu niambie, unadhani mawazo gani mahsusi au hisia zipi zinazohusika hapa?

 

  1. Soma Wakolosai 3:3-4. Mustakabali wetu ni upi? (Kwamba tutafunuliwa pamoja na Yesu katika utukufu kwa kuwa sasa “tumefichwa pamoja” naye.)

 

   1. Kwa nini wokovu wetu uongoze uzingativu wetu maishani? (Tunapaswa kuzingatia yaliyo juu, na si mambo ya duniani kwa sababu tumeyafia mambo ya duniani.)

 

   1. Unaufikiria mustakabali wako kwa kiwango gani? (Natumai tunaufikiria mustakabali wetu zaidi kuliko mambo yaliyopita. Mungu anatufundisha kuwa mustakabali wa wale waliookolewa u naye mbinguni. Hivyo, tunapaswa kuuzingatia mustakabali huu!)

 

 

   1. Hii inazungumzia nini kuhusu uwakili? (Utakumbuka kwamba tulipojifunza Luka 12:16-21, kisa cha mkulima tajiri aliyefariki, tatizo lake ni kwamba alijiandaa kwa ajili ya mustakabali wake hapa duniani na si mustakabali wake wa mbinguni.)

 

   1. Je, hili suala la mustakabali lipo kwa ajili ya Wakristo pekee? (Fikiria tamaduni zote za kipagani ambazo katika taratibu (matambiko) zao za vifo, wanajaribu kuhamisha silaha, utajiri na vitu vingine kwa ajili ya matumizi ya marehemu kwa siku zijazo.)

 

  1. Soma Wakolosai 3:5. Sasa tunaingia kwenye vitu mahsusi kabisa. Tunapaswa “kuvifisha” vitu gani?

 

   1. Je, pendekezo la kwamba tuvifishe vitu hivi lina uhusiano wowote na ukweli kwamba tulikufa pamoja na Yesu na hivyo tunautarajia uzima wa milele? (Nadhani hicho ndio haswa kinachozungumziwa hapa. Tunapaswa kuachana na mambo haya.)

 

   1. Unadhani kifungu hiki kinaonekana kuzungumzia mambo mawili: dhambi za zinaa na tamaa mbaya? Au, unazichukulia “kuepuka adhabu” na “tamaa za uovu” kuwa pana zaidi kuliko dhambi za zinaa?

 

    1. Kwa kuwa mfululizo wa masomo yetu unahusu uwakili, tatizo mahsusi la “uroho” ni lipi? (Wakolosai inasema kuwa ni “ibada ya sanamu.”)

 

     1. Ni kwa jinsi gani uroho ni ibada ya sanamu? (Tatizo kuu la tamaa ni kwamba tunazitegemea fedha zetu badala ya kumtegemea Mungu. Mungu alituokoa kwa neema, na kwa hiyo tunapaswa kuishi kwa neema yake!)

 

   1. Tunapaswa kuvifishaje vitu hivi? Unadhani Biblia inapendekeza njia ipi halisi? (Hii inaturejesha kwenye Wakolosai 3:1-2 inayotuambia kuiweka mioyo yetu na mawazo yetu kwa “yaliyo juu,” badala ya kuiweka kwenye mambo tunayojaribu kuyafisha.)

 

    1. Je, unaweza kuyadhibiti mawazo yako au moyo wako? (Hapa ndipo haswa tunapohitaji msaada wa Roho Mtakatifu.)

 

 1. Ghadhabu Inayokuja

 

  1. Soma Wakolosai 3:6. Kwa nini mambo haya ya “kidunia” ndio yanayosababisha ghadhabu ya Mungu? (Yanakinzana na Ufalme wa Mungu, “mambo yaliyo juu.” Sisi tumeokolewa! Kwa nini tuendelee na hayo mambo yatakayowafanya waovu waangamizwe na Mungu?)

 

  1. Soma Wakolosai 3:7-8. Jana, nilikuwa na mazungumzo ya kina na mwanagenzi ambaye alitaka kuniongoa ili niwe Mkatoliki. Katika mjadala wetu juu ya mafundisho ya Kanisa Katoliki yanayonizuia kuwa mshiriki wa kanisa hilo, mojawapo ya fundisho tulilojadili ilikuwa ni mtazamo wangu wa kawaida kuhusu neema. Mwanagenzi mwenzangu alinukuu Biblia ikisema kwamba mashetani pia wanamwamini Yesu (Yakobo 2:19). Je, unadhani kwamba orodha ya vitu tunavyopaswa kuachana navyo maishani mwetu ni suala la wokovu? (Rafiki yangu wa Kikatoliki hakunipa dondoo ya Biblia au nukuu kamili. Yakobo anasema mashetani wanaamini “na kutetemeka.” Kwa dhahiri, mashetani hawamwamini Yesu kama Mwokozi wao. Orodha iliyopo kwenye Wakolosai ni orodha ya “mambo kwa ajili ya utekelezaji” kwa wale ambao tayari wameokolewa – kuyafanya matendo yao yaendane na uhusiano wao mpya na Yesu.)

 

 

  1. Soma Wakolosai 3:9-10. Hapo awali tulijadili hitaji la uwezo wa Roho Mtakatifu ili kuyafanya mawazo yetu na matendo yetu yaendane na maisha yetu mapya. Vifungu hivi vinabainisha zana ipi inayotusaidia kubadilika na kuwa na sura ya Muumba wetu? (Maarifa. Kujifunza Biblia ni muhimu kwa mabadiliko haya kufanyika maishani mwetu.)

 

   1. Unadhani kwa nini kifungu hiki kinabainisha kwa mahsusi uongo wetu kama tatizo linalotakiwa kukomeshwa? (Fikiria rejea inayohusu maarifa. Kwa mahsusi uongo unahafifisha uwezo wetu wa kuwa na uelewa sahihi wa mambo.)

 

  1. Soma Wakolosai 3:11. Jambo gani jingine linapaswa kubadilika maishani mwetu? (Tunatakiwa kuachana na ubaguzi/chuki bila sababu.)

 

   1. Kwa dhahiri kifungu hiki kinazungumzia ubaguzi wa rangi. Kifungu hiki kinazungumzia aina gani nyingine za ubaguzi? Aina gani ya ubaguzi inajumuishwa kwenye “mtumwa au mwungwana?” (Ubaguzi wa kiuchumi. Ubaguzi wa madaraja ya watu. Hii ipo katika pande zote mbili. Hatupaswi kuwa na ubaguzi dhidi ya maskini. Hatupaswi kuwa na ubaguzi dhidi ya matajiri.)

 

  1. Soma Wakolosai 3:12. Unaweza kuwa unajiuliza endapo tumepoteza mwelekeo wa mada ya uwakili. Je, maadili haya yana uhusiano wowote na uwakili? (Yanaonekana kuwa msingi wa hisia kwa ajili ya uwakili – huruma, wema, na unyenyekevu.)

 

  1. Soma Wakolosai 3:13. Je, kuna uhusiano kati ya msamaha na uwakili? (Una uwezekano mdogo wa kumsaidia mtu aliyefanya makosa. Siashirii kwamba kamwe upendo “mgumu” si jibu sahihi, bali ninafahamu kuwa Mungu ananisamehe kwa kurudia-rudia dhambi zile zile.)

 

  1. Soma Wakolosai 3:14. Mtazamo mkuu unaoifanya hii mitazamo mingine ifanye kazi pamoja ni upi? (Upendo.)

 

 1. Roho Mtakatifu

 

  1. Soma Yohana 14:16-17. Sehemu gani ni ya msingi kabisa katika kuishi maisha mapya na kuachana na maisha ya kale? (Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu.)

 

  1. Soma Yohana 16:7-13. Ni kitu gani kilicho ufunguo wa badiliko la mawazo yetu na mioyo yetu katika kuakisi aina ya tabia na matendo ambayo tumekuwa tukijifunza katika somo hili? (Roho Mtakatifu. Hatuwezi kubadili mioyo yetu au mawazo (akili) yetu. Lakini, Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu anaweza.)

 

  1. Rafiki, je, utaubadili uzingativu wa mustakabali wako na maisha yako mapya na Yesu? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akae ndani yako na kuyafanya mabadiliko haya yawezekane? Kwa nini usimwombe Mungu akutendee vivyo sasa hivi?

 

Juma lijalo: Mawakili Baada ya Edeni.