Sifa za Wakili

Swahili
(Mathayo 6 & 24, Waebrania 11, Zaburi 12)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Chukulia kwamba unataka kumwajiri wakili kwa sababu unazo mali za kutosha. Utaangalia sifa gani kwa mtu unayemwamini kuangalia fedha zako au mali zako nyingine? Unaweza kupuuzia sifa zipi? Utataka mtu awe mwerevu, au angalao mwenye busara, sawa? Mwaminifu? Mwaminifu, kwa maana ya moyo wako kuridhika naye? Mwenye uwezo/uhodari/ustadi? Ikiwa unadhani sifa hizi ni za muhimu, au hata huenda ni za lazima kuwa nazo, je, vigezo vya Mungu vitakuwa tofauti? Vinaweza kuwa tofauti, sawa? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi juu ya kuwa wakili wa Mungu!

 

 1.    Busara

 

  1.    Soma Luka 16:8. Utakumbuka kwamba katika somo la 3 kwenye mfulilizo wa masomo haya tulijifunza kisa hiki. (Ikiwa hukumbuki, soma kisa chote cha meneja asiye mwaminifu, Luka 16:1-12.) Yesu alionekana kuashiria kwamba tabia ya muhimu kuliko yote ni ipi – angalao katika mfano huu? (Kuwa “mwerevu.” Yesu anazungumzia mkusanyiko wa umahiri (akili) na akili ya kawaida.)

 

   1.    Je, meneja huyu asiye mwaminifu alikuwa “wakili?” (Ndiyo!)

 

  1.    Soma Mathayo 24:45-46. Yesu anamwelezea wakili wa namna gani? (Wakili mwenye akili na mwaminifu.)

 

   1.    Matendo gani yanatokana na busara hii? (Utendaji wa uaminifu.)

 

    1.    Je, baadhi ya sifa muhimu zina, kama matokeo yake ya sili, sifa nyingine muhimu? (Katika muktadha huu, kwa dhahiri huu unaonekana kuwa ndio ukweli wenyewe. Kuwa na busara (akili) ni matokeo ya kuwa mwaminifu. Hebu tuzungumzie juu ya kuwa mwaminifu katika sehemu inayofuata.)

 

 1.   Uaminifu

 

  1.    Soma Waebrania 11:1. Niambie juu ya kitu kimoja usichokuwa nacho, lakini una uhakika utakuwa nacho katika siku zijazo? (Kama wewe ni kijana mdogo, tafuta jibu tofauti na kuwa na mvi na makunyanzi.)

 

   1.    Taja kitu kingine ambacho umehakikishiwa kuwa nacho katika siku zijazo, lakini huoni ushahidi wowote wa kuna nacho kwa sasa?

 

   1.    Kama unaweza kuwa na majibu ya maswali haya mawili, basi unayo “imani” katika majibu yako.

 

  1.    Soma Waebrania 11:2-3. Je, unayo imani kwamba Mungu ndiye Muumbaji wa ulimwengu? (Nadhani! Wengi hawaamini.)

 

  1.    Soma Waebrania 11:8. Jambo gani lilikuwa la pekee sana juu ya uamuzi wa Ibrahimu kwenda mahali alipomwambia Mungu?

 

   1.    Ikiwa nitakwambia kwamba ninakutaka usiende safari, lakini uhamie mahala fulani moja kwa moja, je, ungependa kupafahamu mahali hapo? (Wapi.)

 

   1.    Ikiwa hukujua mahali ulipokuwa unahamia, je, ungekubali kuhama?

 

  1.    Unapotafakari majibu uliyoyatoa hivi punde, je, yanakufundisha nini juu ya asili ya imani?

 

   1.    Sasa, chukulia kwamba aina hii ya imani ni “sifa” ya wakili. Unadhani kwa nini ni sifa ya mojawapo ya mawakili wa Mungu?

 

    1.    Je, lingekuwa jambo la msaada ikiwa wakili wako alikuwa mojawapo ya watu werevu sana hapa duniani, lakini hakuwa mwaminifu kwako? Hakukwamini katika nyakati ngumu?

 

 1. Maono

 

  1.    Soma Mathayo 6:19-21. Utakumbuka kwamba tulijifunza kauli hii kwenye Luka 12 katika muktadha wa mkulima mwenye mafanikio aliyepata mavuno makubwa, akajenga maghala ya kuhifadhi mazao yake, na kisha akafariki usiku huo huo. (Luka 12:16-21.) Kisha vifungu vinavyofuata katika kitabu hicho cha Luka vinatuambia tumtumaini Mungu, sio fedha, na kutengeneza mali mbinguni kwa sababu hapo ndipo tutakapoishi katika siku zijazo. Je, unayakumbuka haya?

 

  1.    Hebu pia tuchimbue muktadha wa kisa hiki kwa mujibu wa kitabu cha Mathayo. Soma Mathayo 6:22-23. Je, macho yetu yanahusikaje na kutunza hazina zetu mbinguni badala ya kuzitunza duniani?

 

  1.    Soma Mathayo 6:24. Kauli ya Yesu kuhusu mabwana wawili inahusianaje na macho yetu?

 

   1.    Cha muhimu zaidi, kauli hiyo inahusianaje na kuwa wakili? (Mada ya jumla ni kuwa na maono ya kuutangaza Ufalme wa Mungu. Ikiwa lengo lako ni Mungu, badala ya fedha, ikiwa maono yako maishani ni kumpa Mungu utukufu, basi muda wako, fedha zako na mali zako nyingine zinafuata maono yako.)

 

   1.    Je, maono ni tofauti na kuwa mwaminifu? (Nadhani ni upande tofauti wa kuwa mwaminifu. Upande wa uaminifu unasema kuwa unamwamini Mungu na unaiamini mipango yake kwa ajili ya maisha yako. Upande wa maono unasema kuwa unao mpango maishani unaoendana na imani zako.)

 

 1.   Unyofu (Uaminifu)

 

  1.    Soma Zaburi 12:1-2. Jambo gani la kutisha limetokea duniani, kwa mujibu wa mtunzi wa Zaburi? (Kila mtu anasema uongo.)

 

  1.    Soma Zaburi 12:3-4. Tatizo la wakili anayejivuna ni lipi? (Anadhani kuwa yeye ndiye chanzo cha mafanikio yake, na si tajiri na mwelekeo wa bwana wake.)

 

   1.    Kuna uhusiano gani kati ya kujivuna na uaminifu? (Ujivuni wa kweli ni uongo. Unamfanya wakili kutokuaminika.)

 

  1.    Soma Yohana 8:44. Je, umekutana na watu ambao “lugha yao ya asili” ni kusema uongo?

 

   1.    Je, utamwajiri wakili anayezungumza lugha hiyo kwa ufasaha?

 

  1.    Soma 1 Timotheo 4:1-4. Je, watu walioelezewa hapa wana dhamiri? (Imefanywa kuwa “sugu,” hivyo ninaamini jibu ni kwamba hawana dhamiri inayofanya kazi vizuri.)

 

   1.    Mtu anapokwambia kwamba Mungu anakutaka kuchukua hatua za ziada kuwa mwaminifu zaidi, je, unachukulia kwamba mtu huyo ni mcha Mungu na mwaminifu?

 

   1.    Mtu anapokwambia kwamba Mungu hataki ufanye jambo unalolifanya sasa hivi, jambo unalodhani kuwa linahitajika, je, unachukulia kwamba mtu huyo humcha Mungu kidogo na huenda si mwaminifu wa dhati?

 

    1.    Utagundua kwamba watu ambao ni wanafiki, waongo, na wasio na dhamiri, wanawasihi watu watende zaidi kwa ajili ya Mungu. Wanawasihi watu waache kutenda mambo wanayoyafurahia. Unalichukuliaje wazo kwamba Wakristo “wenye kutiisha (strict)” kweli wanaweza kuwa waovu?

 

    1.    Hii inahusianaje na sifa za wakili? (Unamtaka wakili akupatie ushauri sahihi. Hapa, ushauri unatokana na pepo wabaya.)

 

 1.    Utii

 

  1.    Soma 1 Samweli 15:22. Unalinganishaje utii na “dhabihu” katika zama za leo? (Kutii ni bora kuliko kusema “samahani.”)

 

   1.    Je, utii ni jambo unalodhani ni la muhimu kwa wakili? (Unataka maelekezo yako yafuatwe.)

 

    1.    Kwa nini? (Kwa sababu mali zako ndizo ziko hatarini.)

 

     1.   Je, vigezo hivyo hivyo vinatumika kwenye uwakili wetu kwa Mungu? (Bila shaka anataka maelekezo yake yafuatwe, lakini anatupatia maelekezo kwa manufaa yetu.)

 

  1.    Soma 1 Samweli 15:23. Hebu tujadili asili ya kutokuwa na utiifu. Kifungu hiki kinasema kuwa chanzo cha kutokutii ni kipi? (Ukaidi na uasi.)

 

   1.    Je, ungependa wakili mkaidi na muasi akufanyie kazi? (Hapana. Fikiria jinsi jambo hili linavyohusika katika utendaji wako wa kazi.)

 

   1.    Sababu gani nyingine zinaweza kumfanya mtu asiwe mtiifu? (Udhaifu. Mkanganyiko wa akili.)

 

    1.    Je, ungependa kuwa na wakili aliyekuwa mdhaifu na mkanganyiko wa akili?

 

  1.    Soma 1 Samweli 15:24-25. Sauli anamlaumu nani kwa kutokuwa kwake mtiifu? (Watu.)

 

   1.    Unadhani kuna tatizo gani kwenye kisingizio cha Sauli? (Hakubali kuwajibika.)

 

  1.    Unapozitafakari “sifa za wakili” ambazo tumezijadili, sifa ngapi kati ya hizo zinahusu uwajibikaji? (Sifa zote. Tunatakiwa kuwajibika kwa sifa zote hizi. Hii haihusu wokovu, bali inahusu huduma yetu kwa Mungu. Inahusu jinsi tutakavyoishi maisha yetu.)

 

  1.    Rafiki, je, utatafakari kila mojawapo ya hizi sifa za wakili, na kuzilinganisha na maisha yako? Ukiona kwamba hukaribiani nazo, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akusaidie kuboresha mwenendo wako na Mungu?

 

 1.   Juma lijalo: Uaminifu kwa Mungu.