Matokeo ya Utoaji wa Zaka

Swahili
(1 Wakorintho 9, Kumbukumbu la Torati 14, Mwanzo 28)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.                           

 

 

Utangulizi: Ingawa watu wengi leo wanajadili maana ya zaka, jambo ambalo kimantiki haliwezi kupingwa ni kwamba kwa uzito ule ule Mungu anafundisha kuwa wale wanaoitangaza injili yake wanastahili kutegemezwa na wanufaika wa injili hiyo. Ili kuelewa vizuri zaidi kile anachokimaanisha Mungu kwetu leo, hebu tuanze na fundisho la Paulo katika Agano Jipya na kisha tufuatilie fundisho hilo na kile alichokifundisha Musa katika Agano la Kale. Jambo gani laweza kuwa bora zaidi ya kuchimbua neno la Mungu ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Kuitangaza Injili

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:1-2. Paulo anaielezeaje kazi yake? (Yeye ni mtume.)

 

   1.    Yeye ni mtume kwa akina nani? (Anasema kuwa, kwa kiwango kidogo, yeye ni mtume kwa watu wanaowatumikia na kuwafundisha wengine.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:3-6. Utaelezeaje, kwa kutumia msamiati wa leo, utetezi wa Paulo kwenye mashtaka dhidi yake? (Kama hamnilipi, mnalalamikia nini sasa?)

 

   1.    Hakuna hata mteja wangu mmoja anayenilipa. Mfuko unagharamia kesi zote ninazozishughulikia mahakamani. Je, hiyo inamaanisha kuwa wateja wangu hawapaswi kuwa na matarajio ya kazi (weledi) ya kitaaluma kutoka kwangu?

 

   1.    Ni kwa jinsi gani Paulo na Barnaba hawakuwa na kile ambacho mitume wengine wote walikuwa nacho? (Mitume wengine walisafiri na wake zao, na walipewa chakula na vinywaji ili kuwategemeza.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:7. Utatoa jibu gani kwa maswali haya? (Hakuna afanyaye hivyo.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:8-10. Jambo gani linaunga mkono madai ya Paulo kwamba ana haki ya kupata malipo kutoka kwa watu wale anaowafundisha? (Hoja yake ni kwamba akili ya kawaida pamoja na Biblia vinaunga mkono dhana ya kwamba waihubirio injili wanastahili kutegemezwa (kusaidiwa) na wale wanaowahudumia kwa kuwapelekea injili.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:11. Baada ya kutafakari hoja ya Paulo, pamoja na hiki kifungu tulichokisoma sasa hivi, je, hii inakuambia nini kuhusu utoaji wa zaka? (Inatoa ujumbe wa jumla kwamba watenda kazi, wachungaji, na walimu wa injili wanastahili msaada wa mali kutoka kwa wale wanaowatumikia.)

 

   1.    Hoja ya Paulo ina vipengele vya kidadisi. Ananukuu Kumbukumbu la Torati 25:4. Hebu tusome kifungu hiki kutoka katika Agano la Kale. Je, kinazungumzia jambo lolote kuhusu kuitegemeza kazi ya Mungu?

 

   1.    Paulo hanukuu Malaki 3:10 kutoka katika Agano la Kale. Hebu tukisome kifungu hiki. Kwa nini Paulo ananukuu kifungu kutoka katika Agano la Kale kuhusu kumlisha ng’ombe na hanukuu kifungu chochote kutoka katika Agano la Kale kinachozungumzia zaka na kuwategemeza Walawi waliohudumu hekaluni?

 

   1.    Angalia tena 1 Wakorintho 9:9-10. Utajibuje swali la Paulo kuhusu endapo Mungu anajihusisha sana na ng’ombe? (Angalia muktadha wa Kumbukumbu la Torati 25:4. Hapana shaka yoyote kwamba Mungu anazungumzia ng’ombe. Lakini, nakubaliana na mantiki ya Paulo kwamba dhana hii inatumika katika kuwategemeza waihubirio injili.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:13-14 na Malaki 3:8-10. Unaelezeaje tofauti ya sauti kati ya hivi vifungu viwili?

 

   1.    Angalia tena 1 Wakorintho 9:13. Paulo anarejea jambo gani? (Anazungumzia mfumo wa utoaji zaka wa kuwategemeza Walawi.)

 

   1.    Ikiwa Paulo anafanya rejea mahsusi ya mfumo wa utoaji zaka, hiyo inazungumzia nini kuhusu hoja yake?

 

   1.    Angalia tena 1 Wakorintho 9:14. Je, “vivyo hivyo” inazungumzia jambo gani? (Mfumo wa utoaji zaka.)

 

    1.    Paulo anaposema kuwa “Bwana ameamuru,” je, anaashiria kwamba kuwategemeza waihubirio injili si suala la lazima? (Hapana.)

 

   1.    Unafikia hitimisho gani kutokana na namna ya pekee ambayo Paulo anajenga hoja yake kuhusu jinsi ambavyo sisi (ambao tunapelekewa huduma ya injili) tunapaswa kuwategemeza wale wanaotuletea huduma ya injili? (Kwanza, bila utata wowote Paulo anasema kuwa ni amri ya Mungu kwamba waihubirio injili wanapaswa kutegemezwa kutokana na kazi yao ya injili. Pili, inakaribia kuwa dhahiri kabisa kwamba ingawa Paulo ananukuu mfumo wa hekalu wa utoaji zaka, hajengi hoja kwamba mfumo huo bado upo. Ikiwa anajenga hoja kwamba mfumo huo upo, basi angenukuu Malaki 3 na si kifungu kinachozungumzia kumlisha ng’ombe. Hitimisho lenye mantiki ni kwamba Paulo anaamini kuwa jambo lenye maana inayofanana na mfumo wa utoaji zaka ni sahihi kwa Wakristo.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 9:15-18. Mfumo huu wa kutegemeza anaouzungumzia Paulo, je, unaonekana kuwa ni jambo la lazima? (Hadai msaada, ingawa anauita kuwa ni “haki.” Badala yake, anabainisha baraka za kuwasaidia watu wengine kama suala la kujitolea. Utakumbuka kwamba hapo awali (kifungu cha 14) aliandika kuwa Mungu “aliamuru” uwepo mfumo kwamba waihubirio injili wanapaswa kupata riziki kwa hiyo injili.)

 

   1.    Soma Matendo 18:3. Paulo anafanya kazi gani? (Fundi wa kushona hema.)

 

   1.    Je, ni wazo jema kutumia muda kushona mahema, wakati Paulo (ikiwa aliomba na kukubali msaada) angeweza kutumia muda wake kuhubiri na kufundisha injili?

 

 1.   Mfumo wa Zaka

 

  1.    Tumejifunza kwamba Paulo anatumia mfumo wa utoaji zaka wa Agano la Kale kama msingi wa hoja yake kwamba lazima tuwategemeze kifedha wale wanaoitangaza injili. Hebu tuchunguze zaidi mfumo wa utoaji zaka wa Agano la Kale ili tuweze kuuelewa vizuri zaidi. Soma Hesabu 18:21, 24-28. Lengo la zaka hii ni lipi? (Walawi hawakupewa ardhi na Mungu, bali walipewa wajibu wa kutumika “katika Hema ya Kukutania.” Zaka ilikuwa mbadala wa Mungu wa ardhi. Badala ya kupata chakula kutoka katika ardhi, Walawi watakipata kutoka kwa makabila mengine waliopewa ardhi na walionufaika kutokana na kazi ya kidini ya Walawi.)

 

   1.    Utagundua kwamba Walawi pia walitoa zaka. Unadhani kwa nini Mungu aliwataka watoe zaka? Walikuwa wapokeaji wa zaka! (Iliwafundisha Walawi suala la baraka na wajibu wa kutoa.)

 

   1.    Kwa ujumla unadhani ni kwa nini Mungu aliweka mfumo wa utoaji zaka? (Ni jambo la mantiki kabisa kivitendo, na lilifundisha kuhusu baraka zitokanazo na utoaji.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 14:22-23. Nani anayekula zaka hapa? (Wale walioitoa!)

 

   1.    Lengo la Mungu ni lipi kwa kuwataka watu wale zaka zao wenyewe? (Watajifunza kumcha Mungu.)

 

   1.    Vipi kuhusu Walawi? Je, wameachwa?

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 14:24-27. Zaka hii inaonekana kutumika kugharamia sherehe mbele za Mungu. Je, huo ndio uelewa wako?

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 14:28-29. Hapa zaka inatumikaje? (Kuwasaidia wahitaji pamoja na Walawi.)

 

   1.    Je, maelekezo juu ya kufanya sherehe na kuwasaidia wahitaji kutokana na zaka unaonekana kukinzana na amri ya kuwapatia Walawi zaka yote? (Ndiyo, vifungu hivi vinaonekana kukinzana. Watoa maoni wengi wanatatua ukinzani huu wa dhahiri kwa kusema kuwa zaka itolewayo kwa Walawi ni “Zaka ya Kwanza.” “Zaka kwa ajili shughuli ya Mungu” ni “Zaka ya Pili.” Inaonekana kwamba Zaka ya Pili ilitolewa kila mwaka kutokana na masalia ya Zaka ya Kwanza. Hata hivyo, katika mwaka wa tatu jambo tofauti lilifanyika. Zaka ya “kuwasaidia masikini,” inayoonekana kuwa zaka yote, ilitolewa ili kuwasaidia Walawi na masikini. Kumbukumbu za kihistoria zinaunga mkono tafsiri hii.)

 

   1.    Unajifunza nini kutokana na jambo hili kwetu leo?

 

    1.    Kwamba wale wanaotoa asilimia 10 leo wanatoa kidogo sana, na hivyo wanamwibia Mungu (Malaki 3:10)?

 

    1.    Kwamba Mungu anajali sana kuhusu kuitegemeza kazi yake, anajali sana kuhusu sisi kuwa na muda wa furaha kifamilia mbele za Mungu, na, anawajali sana masikini?

 

  1.    Soma Mwanzo 28:20-22. Je, hii inaashiria kwamba Yakobo alikuzwa kwa kuaminishwa kuwa utoaji wa zaka ilikuwa jambo la lazima? (Inaashiria kwamba hapo awali hakuwahi kutoa zaka, na sasa alikuwa anaitoa sasa hivi endapo tu kama Mungu atamwangalia na kumbariki.)

 

  1.    Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na maandiko ya Paulo na hivi vifungu kutoka katika Agano la Kale vinavyozungumzia utoaji zaka? (Kuna mada ya jumla kwamba wale wanaoitangaza injili wanapaswa kutegemezwa na wale wanaobarikiwa kutokana na utangazwaji wa injili hiyo. Dhana ya utoaji zaka ilijulikana katika Agano la Kale na Agano Jipya. Mfumo rasmi kabisa za utoaji zaka ulihusishwa na kulitegemeza hekalu/mfumo wa kafara na urithi wa Walawi. Asilimia kumi ndio kipimo cha utoaji, na tunajifunza kuwa kiwango hicho kiliongezeka zaidi katika mfumo uliorasimishwa.)

 

  1.    Rafiki, je, unaitegemeza kazi ya Mungu, kazi ambayo kutokana nayo unanufaika? Kwa nini usidhamirie sasa hivi kwamba utazikaribisha baraka za Mungu zisizo na kikomo maishani mwako angalao kwa kurejesha zaka kutokana na mapato yako?

 

 1. Juma lijalo: Sadaka za Shukurani.