Somo la 10: Wajibu wa Uwakili

Swahili
(Mwanzo 1, Wakolosai 1, Yohana 14, Ufunuo 14)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma hili nilisikiliza kipindi maarufu cha “TED talk” kuhusu mada ya ubepari. Mzungumzaji alisema kuwa ubebari haukua nadharia ya kisiasa au falsafa ya kiuchumi tu, bali ulikuwa ni “mfumo wa utendaji kazi.” Kama jinsi simu (au kompyuta) yako ilivyo na mfumo wa utendaji kazi, mzungumzaji alijenga hoja kwamba ubepari ulikuwa ni njia ambayo mafanikio ya kiuchumi maishani ulitenda kazi. Mfano wake ulikuwa ni kwamba mifumo miwili mikubwa kabisa kiuchumi duniani, Marekani na China, ina mifumo tofauti kabisa ya kisiasa, lakini ina mifumo ya uchumi wa kibepari. Somo letu juma hili linatafakari endapo uwakili ni “mfumo wa utendaji kazi” wa maisha ya Mkristo. Vyovyote itakavyokuwa juu ya mtazamo wako mahsusi wa kimafundisho, uwakili ndio asili ya Wakristo waliofanikiwa. Hebu tuzame kwenye Maandiko ili tuone kama unakubaliana na mambo haya!

 

 1.    Mfumo wa Utendaji Kazi wa Uumbaji

 

  1.    Soma Mwanzo 1:26. Kanuni ya Mungu ya asili ya utendaji kazi kwa wanadamu ni ipi? (Wakiumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, watakuwa watawala kwa vyote vitakavyoumbwa.)

 

  1.    Soma Mwanzo 1:27-28. Je, Mungu aliwaamuru wanadamu kutumia mamlaka yake kutawala? (Ndiyo. Mungu alituambia tuwatawale wanyama wote na kuitiisha nchi.)

 

  1.    Soma Mwanzo 1:29-30. Ikiwa ufunuo wa Mungu kwa wanadamu uliishia hapa, unadhani Mungu alikuwa anawaza jambo gani kwa ajili ya maisha yako? (Tuliumbwa ili tuwe watawala. Hiyo inamaanisha sisi ni mawakili wa dunia na wa mamlaka tuliyopewa kutoka kwa Mungu.)

 

  1.    Soma Wakolosai 1:16-18. Katika mamlaka haya ya uumbaji, Mungu anachukua nafasi gani? (Nafasi yake ni ya jumla. Sisi ni watawala chini ya mamlaka ya Mungu. “Vitu vyote viliumbwa kwa ajili yake.” Hayo ndio maelekezo yetu ya kiutendaji kwa ajili ya uwakili wetu.)

 

   1.    Kichwa cha habari “mzaliwa wa kwanza katika wafu” kinatuambia nini kuhusu huu wasifu wa Mungu? (Maelezo haya yanamwelezea Yesu. Yeye ni Muumbaji na ni mtawala ambaye kwake yeye tunatarajia kupata mamlaka yetu.)

 

  1.    Soma Wakolosai 1:19-23. Tatizo gani lilijitokeza katika utawala wetu ambalo Yesu amelitatua? (Tulitenda dhambi. Hiyo ilitutenga na Mungu na kutufanya kuwa maadui zake. Lakini, Yesu alitupatanisha na Mungu kwa maisha na kifo chake.)

 

   1.    Hiyo inaashiria nini kuhusu hali yetu ya sasa? (Mambo mawili. Kwanza, kwamba tumerejeshwa kwenye wajibu wetu ule ule wa “watawala wadogo.” Pili, tunaye Yesu wa kumshukuru kwa kuturudishia nafasi yetu.)

 

   1.    Kimantiki, hiyo inamweka Yesu kwenye nafasi gani maishani mwetu? (Yeye ndiye mhimili. Sio tu kwamba Yesu ni Muumba aliyetufanya kwa mfano wake na kutupatia wajibu wa utawala, bali pia aliturejeshea wajibu huo kwa gharama kubwa sana kwake. Hii inamfanya Yesu kuwa kiini cha yote tuyatendayo.)

 

   1.    Kuelewa wajibu wetu hapa duniani kuna umuhimu gani katika kukubali na kupokea maelezo ya Uumbaji katika kitabu cha Mwanzo?

 

 1.   Mfumo wa Utendaji Kazi wa Kiimani (Kimafundisho)

 

  1.    Soma Yohana 14:6. Kanuni ya jumla ya kwenda kwa Mungu ni ipi? (Lazima upitie kwa Yesu.)

 

   1.    Sisi ni watawala wadogo chini ya Yesu, na tunamwangalia Yesu kwa ajili ya nafasi yetu. Je, Yohana 14:6 inaongezea wazo gani pana kwenye wajibu wetu wa utawala? (Yesu ndiye chanzo chetu cha pekee cha wokovu. Sio tu kwamba alitupatia nafasi yetu (kutawala), bali pia alitupatia wokovu na uelewa wetu wa Mungu.)

 

   1.    Hoja ya jumla ni kwamba kuna “njia nyingi” za kufika kwa Mungu. Kutokana na dini nyingine ninazozifahamu, zote zina ukweli fulani. Zaburi 19:1 inatuambia kuwa mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu. Warumi 1:19-20 inasema kuwa sifa za Mungu zi dhahiri tangu uumbaji. Hii inaendanaje na Yesu kuwa “njia” pekee ya kwenda kwa Mungu? (Yesu aliumba mbingu! Yesu aliumba ulimwengu! Yesu aliwapatanisha wanadamu kwa Mungu! Vyovyote vile utafakarivyo jambo hili, kweli kabisa Yesu ni “njia na kweli na nuru” katika suala la kumwendea Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 14:6. Malaika huyu anabeba ujumbe gani? (Injili ya milele.

 

  1.    Soma Ufunuo 14:7. Tunatakiwa kumwabudu nani? (Hivi punde tu tumejadili kwamba Yesu ni Muumba, hivyo huu ni wito wa kumwabudu Yesu.)

 

   1.    Angalia tena rejea ya maelezo ya uumbaji ya kitabu cha Mwanzo. Msingi wa madai ya Yesu ya kuabudu ni upi? (Kwamba yeye ni Muumbaji. Kuikubali dhana ya uibukaji kunaharibu hoja moja ya muhimu sana ya kumwabudu Mungu. Wakristo wanaoikubali dhana ya uibukaji hawaelewi mkakati wa Shetani kwenye hii nadharia ya uongo.)

 

   1.    Kama watawala wadogo juu ya nchi, wajibu wetu wa uwakili ni upi kuhusu ujumbe huu? (Malaika anatuambia kwamba “saa ya hukumu yake imekuja.” Hiyo inamaanisha kuwa ikiwa tunataka kuuhifadhi uumbaji, tunatakiwa kupeleka haraka ujumbe wa kumcha na kumtukuza Mungu Muumbaji wetu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 14:8. Kwa nini ufunuo huu ni wa muhimu? (“Babeli,” inayotusukuma ili kututenganisha na Yesu kwa kuabudu miungu wengine, umeshindwa. “Umeanguka.”)

 

   1.    Hiyo inamaanisha nini kuhusu utawala wako? (Uko salama! Unaendelea kuwa mtawala na wakili ilimradi tu uko upande wa Mungu.)

 

    1.    Je, hilo ni jambo unalopaswa kushiriki na watu wengine?

 

  1.    Soma Ufunuo 14:9-10. Ikiwa Babeli umeshindwa, je, bado wanadamu wanaungana na upande ulioshindwa? (Ujumbe tunaotakiwa kuutangaza ni kwamba Yesu ameshinda! Ama kwa hakika watu hawalitambui jambo hili na wanaendelea kujiunga na upande ulioshindwa.)

 

   1.    Wanadamu wanakabiliana na uchaguzi gani? (Kumwabudu Yesu, na kuingia kwenye uelekeo wa njia pekee ya kwenda kwa Mungu. Au, mwabudu mnyama.)

 

   1.    Matokeo ya mwisho kwa wale wanaomkataa Yesu na kuchagua kumwabudu mnyama ni yapi? (Utapokea ghadhabu kamili ya Mungu na utachomwa moto.)

 

  1.    Soma Ufunuo 14:11. Je, hizi kauli mbili zinahusiana? Je, waovu hawana pumziko “mchana wala usiku” kwa sababu wanateswa kwa moto wa “salfa iwakayo?”

 

   1.    Moto unapowaka vizuri, je, unatoa moshi? (Kwa uzoefu wangu mdogo, moshi ni mkubwa pale ninapojaribu kuwasha moto au pale ninapouzima.)

 

   1.    Soma Mwanzo 3:2-5. Nyoka alisema uongo gani kuhusu dhambi na kifo? (Alisema kuwa dhambi haiishii kwenye kifo.)

 

   1.    Ikiwa kauli ya Shetani kuhusu dhambi isiyoishia kifoni ni uongo, ni kwa jinsi gani basi waovu wanaweza kuwa na maisha ya milele ya mateso yanayotokana na salfa inayowaka? (Nadhani kitabu cha Mwanzo kinazuia dhana mbili zinazohusishwa katika Ufunuo 14:11. Moshi unatoka milele kwa sababu moto umezimika – unaendelea tu kufuka. Katika kipindi cha uhai maishani, wale wanaomwabudu mnyama na kumkataa Yesu hawana pumziko. Wanateswa.)

 

   1.    Unakumbuka majuma mawili yaliyopita tulijifunza 1 Wakorintho 9:7-9 ambapo Paulo alitumia akili ya kawaida na kifungu cha Agano la Kale kinachohusu ng’ombe kujenga hoja kwamba Wakristo wanapaswa kuwategemeza waihubirio injili? Je, tunapaswa kutumia akili ya kawaida kuelewa kauli za Mungu kuhusu mustakabali wa waovu? (Ndiyo, endapo maana mbili mbadala zinawezekana kuwepo.)

 

    1.    Ikiwa unakubali kwamba “ndiyo” ndilo jibu sahihi, fikiria kosa la kutisha sana lililokujia mawazoni mwako. Kwa maoni yako, je, itakuwa adhabu ya haki kumchoma mkosaji huyo kwa moto wa salfa milele?

 

  1.    Soma Ufunuo 14:12. Tunahitaji kuwa na mtazamo wa namna gani katika siku za mwisho? (Subira! “Kusubiri kwa ustahimilivu.”

 

   1.    Matendo na mitazamo ya namna gani inapaswa kuakisiwa kwenye uwakili wetu? (Kwanza kabisa, tunasalia kuwa waaminifu kwa Yesu. Sisi ni watawala chini yake, na ni mawakili wa injili yake na uumbaji wake. Pili, tunamtii Mungu. Tunaelewa kwamba Mungu alitupatia amri zake ili kuyaboresha maisha yetu.)

 

  1.    Rafiki, je, unakubali kwamba kuuelewa uhusiano wetu na Yesu, kuelewa kwamba yeye ni Muumbaji na Mkombozi wetu, na kwamba alitupatia mamlaka ya kutawala, huuelekeza uwakili wetu kwake? Ikiwa unakubaliana na kauli hizi, kwa nini usiamue leo kukubali wajibu wako kama mtawala, na kumtumikia na kumwabudu Yesu?

 

 1. Juma lijalo: Deni: Uamuzi wa Kila Siku.