Somo la 12: Tabia za Wakili

Swahili
(Waefeso 5, 1 Wakorintho 10, Mathayo 5)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikihudhuria kwenye kikundi cha kujifunza Biblia kila juma. Makundi hayo hubadilika kwa kadri miaka inavyobadilika. Wakati mwingine ninakuwa kiongozi, na wakati mwingine mimi huwa si kiongozi. (Huna ninapendelea pale ninapokuwa si kiongozi.) Hivi karibuni, nilimwambia rafiki ambaye kikundi chetu cha sasa kilikuwa kinakutana nyumbani kwake kwamba inawezekana wakaja watu watatu wageni usiku ule. Kilichotokea ni kwamba hakuna hata mmoja kati yao aliyejitokeza. Kwa nini? Tofauti na washiriki wa sasa wa kikundi, mahudhurio hayajawa tabia ya wengi. Je, umegundua kwamba unaweza kujifunza tabia mpya zinazoweza kuboresha maisha yako? Hivi karibuni nimeanzisha tabia ya kwenda kwenye ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo (gym). Je, ungependa kuanzisha tabia gani? Biblia inatuambia tuchukue tabia zipi? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Tabia ya Upendo

 

  1. Soma Waefeso 5:1-2. Ungeulizwa kama unampenda Mungu na kuwapenda wafanyakazi wenzako, ungesemaje? (Kwa miaka mingi nimekuwa nikihangaika kwamba sikuwa nampenda Mungu, na kwa hakika nilifahamu kuwa sikuwa nikiwapenda watu wengi niliowafahamu – isipokuwa tu wanafamilia.)

 

   1. Jinsi unavyouelezea upendo ni jambo la muhimu hapa. Unauelezeaje upendo? (Ninaufikiria upendo kama kitendo cha hisia kali, mara nyingi hisia za kimapenzi. Ingawa leo nina hisia za upendo kwa Mungu, sidhani kama hisia zinaweza kuanza kuelezea kile kinachomaanishwa na Biblia inapotuambia “tuenende katika upendo.”)

 

  1. Soma tena Waefeso 5:2. Upendo umeelezewaje? (Umeelezewa kama kujitoa sadaka/dhabihu.)

 

   1. Unapozungumza na mtu, niambie unapendelea jambo gani zaidi:

 

    1. Kutaka kumjua zaidi mtu huyo; au,

 

    1. Kuelezea jambo linalokuhusu kuhusiana na mada inayojadiliwa na kukuweka kwenye nafasi nzuri? Mkuu wangu wa zamani wa Shule ya Sheria, Jeffrey Brauch, ana tabia ya pekee. Kila nilipomsikiliza akizungumza na mwanafunzi, mara zote alikuwa akisikiliza kwa makini na kuuliza maswali. Anafanya vivyo hivyo anapozungumza nami. Kitendo hicho kilinifundisha tabia ya thamani ya upendo – kupendelea kuzingatia mazungumzo kwa watu wengine badala ya kujipendelea mwenyewe.)

 

  1. Soma Waefeso 5:3-4. Je, hii inamaanisha kwamba kutamani kimapenzi na kuonekana kuwa na fedha ni makosa? Kuna tatizo gani na mzaha wa mara moja moja wa “kiutu uzima?”

 

 

   1. Mbadala gani unapendekezwa kwenye mazungumzo ya namna hii? (Shukrani! Kumshukuru Mungu.)

 

  1. Soma Waefeso 5:5. Kwa nini mazungumzo haya yasiyo na hatia ni tatizo? (Tatizo ni kwamba yanaakisi moyo wa uasherati, uchafu na kupenda fedha. Kwa ujumla tunachokizungumza kinaakisi kile tunachokifikiria. Mazungumzo yetu ni dirisha linaloifungua mioyo yetu.)

 

   1. Biblia inasema kuwa mzizi wa tatizo ni upi? (“Mtu huyo ni mwasherati.”)

 

    1. Ni kwa jinsi gani hiyo ni kweli? Simfahamu mtu hata mmoja anayetengeneza sanamu na kisha kuisujudu na kuiabudu. (Kuwa mwaminifu. Je, mazungumzo yote haya sio ya ubinafsi kwa namna fulani? Mzaha wa kishenzi kwa ujumla unafanyika kwa gharama ya mtu mwingine – na kukufanya uonekane mwerevu, sawa? Je, utakiri kwamba tamaa ya kimapenzi inaimarisha uhusiano wako (au majisifu yako) kwa gharama ya mwenzi wa mtu? Kuzungumzia utajiri wako huwaelezea watu wengine kwamba wewe ni bora kuliko wao. Mambo yote haya yanakufikisha wapi? Inaamsha taswira yako! Unajiabudu mwenyewe.)

 

    1. Unaweza kuona mtiririko wa mantiki katika mambo yote haya? (Mada ni kubadili tabia ya upendo kwa ajili yako na kuuelekeza kwa watu wengine. Moyo wa shukrani unayaelekeza mawazo yako kwa wema wa watu wengine.)

 

    1. Unaweza kufanya nini ili kuvunja hiyo tabia na kuibadilisha na mazungumzo yasiyo na ubinafsi? (Tunatakiwa kuwa makini na tatizo, na kumwomba Roho Mtakatifu abadili mioyo yetu.)

 

  1. Soma 1 Wakorintho 10:1-4. Unapimaje usuli (historia ya awali) wa watu hawa? (Walikuwa na manufaa mengi ya kiroho.)

 

   1. Je, wanafanana nasi?

 

  1. Soma 1 Wakorintho 10:5. Tatizo ni lipi? (Licha ya haya manufaa ya kiroho, hawakumpendeza Mungu na walikufa.)

 

  1. Soma 1 Wakorintho 10:6. Kwa nini Paulo ananukuu historia hii? (Anataka tujifunze kuhusu kuiweka mioyo yetu kwenye mambo maovu.)

 

   1. Je, kuna uhusiano kati ya tabia zetu na kuiweka mioyo yetu? (Ndiyo. Hivi punde tu tumejadili kuhusu kuwa makini na suala la mioyo yetu, na kisha kumwomba Roho Mtakatifu kubadili mioyo yetu.)

 

  1. Soma 1 Wakorintho 10:7-11. Manung’uniko yana jambo gani lenye kufanana na uasherati na kuabudu sanamu? (Ni jambo lile lile ambalo tumekuwa tukilijadili. Manung’uniko yanaibuka kutokana na kujizingatia wewe mwenyewe.)

 

 1. Tabia ya Kutumaini

 

 

  1. Soma Mathayo 6:28. Utajibuje? (Mara nyingi wasiwasi hutokana na jinsi unavyojitokeza mbele za watu. Hakuna mtu ambaye anataka kuaibika.)

 

  1. Soma Mathayo 6:29-30. Yesu anatuhamasisha tuchukue tabia gani? (Tabia ya kumtumaini Mungu na kutokuwa na wasiwasi.)

 

  1. Soma Mathayo 6:31-33. Kipaumbele cha kwanza cha wapagani ni kipi? (Kutafuta nguo, chakula, vinywaji na vitu.)

 

   1. Kipaumbele chetu cha kwanza kinapaswa kuwa kipi? (Kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake. Mungu anatupatia “vitu” vyote hivi ambavyo wapagani wanavitafuta kama bonasi!)

 

   1. Hebu tuliangalie jambo hili kwa vigezo vya kitabia. Ni kitu gani cha kwanza unachokifikiria asubuhi? Je, ni kile unachohitaji kukifanya kwa ajili ya kazi? Kile unachotakiwa kukifanya ili ujifurahishe mwenyewe? Fedha?

 

    1. Maisha yako yangekuwa na tofauti gani endapo mawazo yako ya kwanza kabisa asubuhi yangehusu jinsi ya kuboresha mwendendo wako na Mungu? Kile ambacho ungekifanya ili kuutangaza Ufalme wa Mungu?

 

  1. Soma Yakobo 4:13-14. Unalinganishaje jambo hili na wapagani ambao tumesoma habari zao hivi punde ambao wana wasiwasi wakati wote kuhusu kupata vitu? (Hii ni tofauti kwa kiasi fulani. Hawa ni watu wenye mipango ya siku zijazo.)

 

   1. Je, kuna ubayo wowote katika kuwa na mipango? (Kupanga bila uwepo wa Mungu kwenye mipango ndio tatizo. Mipango yetu binafsi ina tatizo kubwa kwamba sisi, tofauti na Mungu, hatuwezi kubashiri mustakabali wa siku zijazo.)

 

  1. Soma Yakobo 4:15. Jambo gani linapaswa kuwa katikati ya mipango yetu yote? (Mapenzi ya Mungu! Hatupaswi tu kutoendeleza tabia ya kuwa na wasiwasi, bali pia tunapaswa kuendeleza tabia ya kumweka Mungu katikati ya mipango yetu.)

 

 1. Tabia za Akili (Mawazo)

 

  1. Soma Wafilipi 4:6. Je, hii inaonekana kuelezea mjadala wetu kwa ufupi hadi hapa tulipofikia?

 

  1. Soma Wafilipi 4:7. Ni yapi matokeo ya kuzifanya tabia hizi zitende kazi? (Amani ya Mungu. Amani ilindayo mioyo yetu na mawazo yetu. Amani ambayo watu wengine hawaielewi.)

 

  1. Soma Wafilipi 4:8. Tafakari kuzijaribu tabia zako za kiakili dhidi ya kile ambacho tumekuwa tukijifunza. Unapofikiria kuihusu jana, je, mawazo yako yalichukua vitu vilivyokuwa sahihi, visafi, vizuri, na vyenye kupendeza? (Wengi wetu tunahitaji tabia za kiakili zilizo bora. Ninawakumbuka marafiki waliokuwa wakizungumzia kuhusu sinema walizozitazama au walizotaka kuzitazama. Mawazo yangu ya papo hapo yalikuwa ni kwamba marafiki hao walikuwa wanachosha – na baadaye nilijisikia hatia kwa sababu sinema hizi zilikuwa zenye maadili, safi na za kupendeza.)

 

 

   1. Unadhani inamaanisha nini kuyaelekeza mawazo yako kwenye mambo yaliyo ya “kweli?” Vipi kuhusu yaliyo ya “kupendeza?” Yenye “sifa njema?” (Kiasi gani cha fikra zako kipo kwenye mambo yako ya siku zote? Kiasi gani cha fikra zako kinatumika kwenye mambo yasiyo ya maana – au, ikiwa yana maana, yanaweza kukuingiza kwenye matatizo? Hii inaashiria kwamba tunaendeleza tabia ya kufikiria fikra “kuu.” Fikra kuhusu jinsi unavyoweza kutumia neno la Mungu kwenye kazi yako, kwenye mahusiano ya familia yako, siasa, uchumi, kanisa lako, na maisha yako.)

 

  1. Rafiki, je, tabia zako zinahitaji marekebisho? Ikiwa ndivyo, mkaribishe Roho Mtakatifu, sasa hivi, ili ayaongoze mawazo yako na maneno yako kwenye tabia bora zaidi!

 

 1. Juma lijalo: Matokeo ya Uwakili.