Somo la 13: Matokeo ya Uwakili

Swahili
(Mathayo 7, Mithali 3, 1 Petro 2, Wafilipi 4)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
13

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tunapaswa basi kuishije? Baada ya kujifunza masomo yote haya juu ya uwakili, kwa kuwa sasa tumefikia kwenye somo letu la mwisho, je, umebadili mitazamo yako na matendo yako? Tumejifunza kwamba Mungu ni mkarimu kwetu zaidi ya jinsi anavyohitaji. Tumejifunza kwamba kuwa mkarimu, kama alivyo Mungu wetu, ndio njia nzuri ya kuwa na maisha bora. Tumejifunza kwamba ukarimu sio tu kuhusu fedha, bali pia unahusu muda wetu, talanta zetu, na usikivu na kujali kwetu. Tumejifunza kwamba mawakili lazima wawe watu wa kutumia akili. Tumejifunza kwamba mawakili wanamtumaini Mungu. Hebu tumalizie mfululizo wa masomo haya kwa kujifunza baadhi ya vifungu vya Biblia vinavyotusaidia kuelewa vizuri jinsi maisha ya wakili wa Mungu yanavyofanana!

 

 1. Kumkiri Mungu

 

  1. Soma Mathayo 7:21. Hii inaashiria kuwa wakili sahihi atafanya nini? (“Mapenzi ya Baba yangu.” Kwa dhahiri kuliita tu jina la Yesu haitoshi.)

 

  1. Soma Mathayo 7:22. Endapo ungeulizwa “Kwa nini uende mbinguni?” “Jambo gani linathibitisha kwamba ulikuwa wakili sahihi wa Mungu?” Je, ungetoa jibu kama linalopatikana kwenye hiki kifungu?

 

   1. Endapo ungeweza kutoa jibu zuri sana kama hilo (mimi nisingeweza) je, ungedhani kwamba ulikuwa wakili wa Mungu uliyetukuka?

 

  1. Soma Mathayo 7:23. Hebu subiri kidogo! Je, kuyatenda mambo yote haya hakuhusishi uwezo wa Roho Mtakatifu? Hakuna mwanadamu wa kawaida awezaye kuwa nabii wa kweli, kuzishinda pepo, au kutenda miujiza! Haya ndio mambo aliyoyatenda Yesu!

 

   1. Kibaya zaidi, ni kwa jinsi gani wale watendao matendo haya makuu wanaweza kuitwa “watenda maovu?”

 

  1. Hebu turuke sura hii na tusome Mathayo 8:5-8. Je, huu ndio mtazamo utakaoutarajia kutoka kwa akida wa jeshi la Kirumi?

 

  1. Soma Mathayo 8:9-12. Akida huyu wa jeshi la Kirumi angejibuje swali la endapo anapaswa kwenda mbinguni? (Kwa dhahiri, asingedai kupata manufaa ya matendo yake. Angedai upendeleo wa uwezo wa Mungu.)

 

   1. Je, sasa unaona kasoro kwenye majibu yaliyopo kwenye Mathayo 7:22? (Watu hawa wanadai matendo yao wenyewe kama msingi wa wokovu. Matendo haya yanawezekana tu kutendeka kwa njia ya uwezo wa Roho Mtakatifu. Mungu ndiye aliyetenda mambo haya, na si watu.)

 

 

   1. Tuchukulie kwamba watu wanaoelezewa kwenye Mathayo 7:22 hawasemi uongo. Kweli miujiza hii ilitendeka. Kwa nini wao ni watenda maovu? (Kwa dhahiri, kuondoa pepo, kutenda miujiza, na kutenda kazi za kinabii si matendo maovu. Hiyo inamaanisha kwamba uovu ni kudai kuwa mambo haya yametendeka kwa uwezo binafsi. Ni kudai kwamba wanastahili kutunikiwa kutokana na mtu aliyeokolewa.)

 

   1. Ni ipi basi iliyo “kazi” ya kwanza ya wakili wa kweli wa Mungu? (Kuelewa kwamba mambo yote yanayotimizwa ili kuutangaza Ufalme wa Mungu yanatendeka kwa neema na uwezo wa Mungu – na sio wakili.)

 

 1. Kumtumaini Mungu

 

  1. Soma Mithali 3:5-6. Mambo gani mawili yapaswayo kuelezea maisha ya wakili anayeelewa fundisho tulilojifunza katika sehemu iliyotangulia? (Kumtumaini Mungu. Kumkiri Mungu.)

 

   1. Inamaanisha nini kusema kuwa Mungu “atanyosha” mapito yetu? (Maisha yetu hayatakuwa magumu.)

 

  1. Soma Mithali 3:7. Unadhani kwa nini kuwa na “hekima machoni pako” kunatofautishwa na kumcha Mungu na “kujiepusha na uovu?” (Hii inaashiria kwamba ikiwa tunaitegemea hekima yetu wenyewe, hatutaweza kuuepuka uovu au kustahi hekima ya Mungu.)

 

  1. Soma Mithali 3:8. Je, hii inaleta mantiki kwako? Kumtumaini Mungu, kuheshimu hekima yake na maelekezo yake, kunakufanya uwe na afya na kuimarisha mifupa yako? Tunadhani kuwa kula vizuri na kufanya mazoezi hutupatia afya njema na kuimarisha mifupa! (Tukiheshimu hekima ya Mungu, tunaona kwamba maisha ya kumtegemea Mungu hutufanya kuwa na afya bora.)

 

 1. Kumpa Mungu Utukufu

 

  1. Soma 1 Petro 2:11. Kwa nini Petro anatuita kuwa “wapitaji na wasafiri?” (Hii inaashiria mtazamo wa upande wetu – kwamba kweli hapa si nyumbani kwetu.)

 

   1. Kuna tatizo gani na “tamaa za mwili (dhambi)?” (Zinashambulia roho zetu. Je, hii inaweza kuwa inahusiana na suala tulilolijadili muda mfupi uliopita, kwamba tumaini na utii hutupatia afya bora? Ikiwa roho zetu zinajisikia kuwa chini ya shambulizi kutokana na tamaa zetu mbaya, afya yetu inatetereka?)

 

  1. Soma 1 Petro 2:12. Je, wapagani watatushitaki kwa kutenda mambo mabaya? (Ndiyo!)

 

   1. Je, watajua kwamba wanadanganya? (Ndiyo.)

 

   1. Je, tunao wajibu kuhakikisha kuwa wanasema uongo? (Ndiyo. Petro anatuambia kuwa kuishi maisha kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu sio tu kunaboresha maisha yetu, bali pia humpa Mungu utukufu.)

 

    1. Angalia muda unaozungumziwa: “Katika siku ya kujiliw” Je, tutawashuhudia wapagani wakimpa Mungu utukufu muda wowote hivi karibuni?

 

  1. Soma 1 Petro 2:15. Hii inazungumzia nini kuhusu mazungumzo ya kipumbavu na kuishi maisha kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu? (Hii inatuambia kuwa kuishi maisha sahihi kutawashawishi watu wengi kuwa mashambulizi ya wapagani kwetu ni ya uongo, ya kipumbavu na ya kijinga. Hilo linaweza kutendeka sasa hivi, halina haja ya kusubiri ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

 

 1. Maisha ya Amani

 

 

  1. Soma Wafilipi 4:4-5. Tunaona dhana mbili zinazohusiana: kufurahi na upole. Kwa kawaida, huwa sizifikirii kama zinahusiana. Zina mantiki gani kwako? (Mimi huwa si mpole ninapokuwa ninajenga hoja mahakamani. (Na hata pale ninapokuwa nje ya mahakama mara nyingi hoja zangu huwa si za upole.) Bila shaka hii ni kutokana na ukweli kwamba ninajaribu kubadili jambo. Unapofurahi, huwa unaridhika na hali yako. Kwangu mimi hii inahusianisha dhana mbili – kuridhika na hali yako na matokeo ya upole wa matendo.)

 

   1. Angalia sentesi ya mwisho: “Bwana yu karibu.” Hiyo inahusianaje na kuwa mpole? (Tofautisha kile nilichokisema hivi punde (kuhusu kujenga hoja) kwa watu katika Mathayo 7:22. Ninatumbukia kwenye mtego ule ule – kufikiria kwamba juhudi zangu “zisizo za upole” zitaleta mabadiliko. Ukweli ni kwamba Mungu wetu, ambaye yu “karibu,” ndiye atiaye nguvu ya mabadiliko.)

 

  1. Soma Wafilipi 4:6-7. Je, ungependa kufikia hatua kama hii maishani mwako? (Hii inaashiria taswira ya kupendeza ya maisha yenye amani.)

 

   1. Je, itakuwa dhahiri kwa watu wote wanaokuzunguka kwamba utajisikia hali hii ya amani? (Kauli iliyopo ni “amani…ipitayo akili zote.” Hiyo inatuambia kuwa mtazamo wetu wa amani hauna maana kwa ulimwengu. Lakini, unaleta mantiki sahihi kabisa kwa wale wanaomtumaini Mungu wao aliye karibu.)

 

    1. Nilipouliza hapo awali kuhusu “kufikia hatua” ambayo utakuwa na amani, nilikuwa ninafikiria maendeleo ya hali ya kawaida ya maisha sahihi. Hili linaonekana kuwa jambo tofauti, jambo tunaloweza kuwa nalo bila kujali kinachoendelea maishani mwetu. Je, hivyo ndivyo unavyoelewa kifungu hiki kuhusu “amani” ipitayo uelewa wa kipagani? (Kumtumaini Mungu huleta amani sasa hivi.)

 

  1. Soma Wafilipi 4:8. Je, umetafakari kwamba kiasi gani cha muda wako unapotea kufikiria mambo ambayo, kwa dhati kabisa, si ya msingi?

 

   1. Wakati mwingine mawazo yangu yanashangaza. Nilikuwa kwenye ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo (gym) wakati mtu mwenye kutisha alipoingia. Alionekana kuwa mtu wa hatari, na ninadhani alitaka aonekane hivyo. Nilipokuwa nikifanya mazoezi, nilikuwa ninatafakari jinsi anavyoweza kunishambulia na jinsi ninavyoweza kujitetea kwa kujilinda. Siku kadhaa baadaye pale ndani ya “gym,” alipoona kuwa tunanyanyua uzito unaolingana, alizungumza nami. Tulikuwa marafiki sana – na akatoa maoni jinsi isivyo kawaida kwamba tumekuwa marafiki. Je, mzee (Bruce Cameron) anayeandika masomo ya Biblia angepaswa kuwa anafikiria nini badala ya kufikiria juu ya kujilinda? (Ningekuwa ninaifuata Biblia, ningekuwa ninafikiria jinsi ambavyo ningeweza kumpelekea injili mtu huyu! Ingawa nilianza kwa kufikiria jambo tofauti kabisa kiakili, niliishia kumkaribisha kwenye kikundi changu cha kujifunza Biblia.)

 

  1. Soma Wafilipi 4:9. Tunapaswa kufanya nini kwa masomo yote tuliyojifunza kuhusu uwakili? (Kuyatenda kivitendo! Matokeo ni kwamba “Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.”)

 

 

  1. Rafiki, je, ungependa kuwa na amani? Je, ungependa kufurahia maisha bora? Kwa nini usiazimie sasa hivi, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kuishi maisha ya wakili wa Mungu?

 

 1. Juma lijalo: Tunaanza mfulilizo wa masomo unaoitwa “Kujiandaa kwa Ajili ya Wakati wa Mwisho.”