Danieli na Wakati wa Mwisho

Swahili
(Danieli 1-3)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, huwa una kawaida ya kuzingatia mambo madogo-madogo maishani? Je, haya “mambo madogo-madogo” yanakufanya ubadili mtazamo wako kwa Mungu? Endapo nchi yako imevamiwa na kushindwa kivita, endapo ungechukuliwa mateka na wavamizi, je, ungeyaita mambo hayo kuwa ni “madogo-madogo?” Yumkini la hasha! Katika somo letu siku ya leo tunajifunza kuwa Mungu ana mkono wake katika maisha yetu, na katika historia ya mwanadamu! Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1.    Maafa

 

  1.    Soma Danieli 1:1-2. Fikiria kwamba ulikuwa unaishi Yerusalemu wakati tukio hili linatokea, na ulikuwa mfuasi mwaminifu wa Mungu. Je, ungefikiria nini? (Katika matukio yote, Mungu mkuu wa Mbinguni ameshindwa. Watu wake wameshindwa, na vyombo vya Mungu vilivyokuwa katika nyumba ya Mungu vimeporwa na kuwekwa nyumba ya mungu wa kipagani!)

 

  1.    Soma Danieli 1:3-6. Sasa fikiria kwamba wewe ndiye Danieli, je, mustakabali wako umekuwa mbaya zaidi kwa kiasi gani? (Sio tu kwamba Mungu wako na nchi yako wameshindwa, bali sasa wewe ni mtumwa. Inaweza isiwe kazi mbaya kwa mtumwa, lakini hauko huru tena.)

 

 1.   Majaribu

 

  1.    Soma Danieli 1:8. Kwa mara nyingine, jiweke kwenye nafasi ya Danieli. Je, ungeshawishika kwamba endapo Mungu angekutaka ufuate kanuni zake za ulaji chakula, basi angewashinda watu wa Babeli? Au, walau asikufanye uchukuliwe mateka?

 

  1.    Soma Danieli 1:11-16. Ungejisikiaje sasa endapo ungekuwa Danieli? (Ningefurahia kwenye huu ushindi mdogo, na kuichukulia kama ishara kwamba Mungu bado yu pamoja nami endapo ningesalia kuwa mwaminifu.)

 

  1.    Soma Danieli 1:17-20. Hii inatufundisha nini juu ya upendeleo wa Mungu pale ambapo dunia inayotuzunguka inapokuwa inaporomoka? (Hatuna muda wa kuingia kwa kina kuhusu sababu za kuanguka kwa Yerusalemu, lakini kulitokana na watu kutokuwa waaminifu. Hii inaonesha kuwa dunia yetu inapoonekana kuporomoka, Mungu anawaangalia (anawatafuta) wale walio waaminifu na kuwatunuku.)

 

  1.    Soma Danieli 2:1-4. Je, jibu hili linaonekana kuwa lenye mantiki kwenye ombi la mfalme?

 

  1.    Soma Danieli 2:5-6. Je, mfalme huyu ana wazimu, au kuna jambo jingine linaloendelea hapa? (Kwa dhahiri Nebukadreza alikuwa na sababu ya kuwashuku watu wake wenye “hekima.” Angeweza kuwa na uhakika kwamba walikuwa wanasema ukweli endapo wangemkumbusha matukio ya kwenye ndoto yake.)

 

  1.    Soma Danieli 2:10-13. Je, utasema kwamba maisha ya Danieli ni ya “amani?” Je, Danieli au marafiki zake wametenda jambo lolote baya?

 

   1.    Ikiwa unafahamu jinsi kisa hiki kinavyoishia, je, Mungu anao mpango katika kipindi hiki cha shida? (Mungu alipeleka ndoto! Ninapenda ungamo la “watu wenye hekima” kwamba “miungu” pekee ndio inayoweza kutimiza ombi la mfalme.)

 

  1.    Soma Danieli 2:14-16. Je, ungeonesha hekima na busara? Au, je, ungekuwa unapiga kelele jinsi jambo hili lisivyo la haki na uvunjaji wa sheria wa hivi karibuni kabisa uliofanywa kwa watu wako na watu wa Babeli? (Tunatakiwa kujifunza jambo kutoka kwa Danieli kuhusu akili ya hisia.)

 

  1.    Soma Danieli 2:17-19. Ni jambo gani la kwanza analolifanya Danieli? (Anapendekeza kwa marafiki zake wakutane kwa ajili ya maombi! Wanamgeukia Mungu.)

 

  1.    Soma Danieli 2:20-23. Ni jambo gani la pili analolifanya Danieli? (Anamsifu Mungu pale ombi lake linapojibiwa. Zingatia kifungu cha 21. Inaonesha kuwa Danieli anaamini mabadiliko ya nguvu ya kisiasa yaliyodhuru maisha yake kwa kiwango kikubwa yaliwekwa na Mungu.)

 

  1.    Soma Danieli 2:24. Je, ungefanya kile alichokifanya Danieli hapa?

 

  1.    Soma Danieli 2:25-28. Je, ungeanza kujibu kwa namna iyo hiyo? (Maneno ya kwanza kutoka kinywani mwangu yangekuwa “Ndiyo!” Nisingetaka kuhatarisha uhai wangu kwa kurudia jambo lile lile lililowasababishia wenye hekima kuwa kwenye amri ya kifo.)

 

   1.    Hivyo basi, kwa nini Danieli alianza kutoa jibu lake kwa namna alivyoanza? (Tukiachilia mbali mimi kutokuwa kocha wa Danieli, tunaona kwamba anampa Mungu utukufu. Hajichukulii utukufu huu – hata kama unamsababishia hatari.)

 

 1. Nyakati za Mwisho

 

  1.    Soma Danieli 2:29-30. Jiweke kwenye nafasi ya Nebukadreza. Kwa kawaida wenye “hekima” wa duniani wangedhihirishaje “hekima” yao kwa mfalme? Njia hiyo inalinganishwaje na njia aliyoitumia Danieli? (Danieli hajikwezi (hajiinui). Hajigambi. Anatilia mkazo umuhimu wa mfalme na Mungu wa mbinguni.)

 

  1.    Soma Danieli 2:31-35. Endapo ungekuwa umeota ndoto hii, na pasiwepo na mtafsiri, ungefikiria jambo gani kama kipengele cha muhimu sana? (Mwamba! Uliangamiza sanamu na kuikuza na kuijaza dunia yote.)

 

  1.    Soma Danieli 2:36-38. Je, jambo hili lilionekana jema kwa Nebukadreza?

 

   1.    Nani aliyempa Nebukadreza uwezo wake? (Mungu wa Mbinguni. Danieli anamweka Mungu wa kwanza.)

 

  1.    Soma Danieli 2:39-43. Ndoto hii inawakilisha nini? (Matukio ya historia. Inadhihirisha falme za dunia zitakazofuatia.)

 

  1.    Soma Danieli 2:44-45. Hatimaye nani anayeshinda? (“Mungu wa mbinguni” ataweka ufalme usioweza kuharibika.)

 

   1.    Mungu anakuwaje mshindi? (Ufalme wake “utazivunja-vunja zile falme zote na kuzikomesha.”)

 

   1.    Unadhani kwa nini Mungu alichagua mwamba kuwakilisha ufalme wake, wakati falme nyingine zilikuwa za metali, baadhi ya metali hizo ni za thamani?

 

  1.    Hebu tutulie kidogo na tutafakari jambo hili. Jambo gani limekuwa likiendelea maishani mwa Danieli? (Machafuko ya aina nyingi. Mungu wake anaonekana kuwa ameshindwa. Kama mfuasi wa Mungu, yeye ni mtumwa, na si bwana. Dunia haiendi kama inavyopaswa kwenda.)

 

   1.    Ndoto hii inamwambia nini Danieli? (Kwamba yeye ni raia wa Ufalme wa Mwamba unaoshinda kupita akili ya kawaida (kimwujiza). Huu ni utiaji moyo mkubwa sana kwamba Mungu anashughulika nyakati zote.)

 

   1.    Hii inakuambia nini kwenye “mambo madogo-madogo” yanayojitokeza maishani mwako? (Hata kama mambo yako “madogo-madogo” ni mambo makubwa, si makubwa kama kujua kwamba Mungu wako atakuwa mshindi. Ufalme wa Mwamba, ambao wewe ni raia wake, kamwe hautaangamizwa au kuachwa kwa watu wengine.)

 

  1.    Soma Danieli 2:46-47. Mfalme huyu mjivuni, ambaye alikaribia kabisa kuwaua Danieli na marafiki zake, ana mwitiko gani? (Anampa Mungu utukufu na kumpa heshima Danieli.)

 

   1.    Hii inatuambia nini kuhusu uhalali/uthabiti wa tafsiri? (Kwa wazi kabisa, Danieli ameielezea ndoto kwa usahihi. Mfalme Nebukadreza ameshawishika na kukubaliana na Danieli.)

 

  1.    Soma Danieli 2:48-49. Uaminifu kwa Mungu umebadilishaje maisha ya Danieli?

 

   1.    Je, kuwa raia wa Ufalme wa Mwamba kunagawa gawio?

 

   1.    Katika tukio hili lote, je, Danieli alifanya jambo lolote la kujitangaza? (Jifunze somo hili. Danieli alimwacha Mungu amtangaze.)

 

 1.   Wanadamu Wasioaminika (Wasiotegemewa)

 

  1.    Soma Danieli 3:1-3. Nebukadreza ameibadilishaje sanamu kwenye ndoto yake?

 

   1.    Danieli 2:49 inatuambia kuwa Danieli alikuwa katika “lango la mfalme” Nebukadreza. Unadhani alibainisha mchepuko huu kutoka kwenye ndoto?

 

  1.    Soma Danieli 3:4-6. Je, hii inaendana na ndoto? Je, unadhani mpango huu ulijadiliwa kwa pamoja na Danieli?

 

  1.    Soma Danieli 3:9-12. Tayari Nebukadreza alikuwa anapaswa kufahamu jambo hili kwa kiasi gani?

 

  1.    Soma Danieli 3:13-15. Je, Nebukadreza amesahau kabisa kile alichokisema hapo awali kuhusu Mungu wa Danieli? Unaelezeaje jambo hili?

 

  1.    Soma Danieli 3:16-18. Kwa nini wanasema kuwa hawana haja ya kujitetea? (Hii inathibitisha kwamba Nebukadreza anaijua imani yao na anamjua Mungu wao.)

 

  1.    Soma Danieli 3:19-25. Tafakari jambo hili, watu wanne wamemshinda Nebukadreza, wakati taifa lao lote halikuweza kumshinda. Jambo gani lilileta utofauti?

 

  1.    Soma Danieli 3:28-30. Hii inatufundisha nini kuhusu kukabiliana na dunia? (Mungu ni mwaminifu, wanadamu si waaminifu.)

 

  1.    Rafiki, tunaye Mungu aujuaye mwanzo tokea mwisho. Sio tu kwamba anatuambia kitakachotokea katika siku zijazo, bali pia ni mwaminifu sasa hivi ikiwa tu waaminifu kwake. Je, utadhamiria, sasa hivi, kuwa mwaminifu kwa Mungu – hata kama mambo hayaendi kama ulivyotarajia?

 

 1.    Juma lijalo: Yesu na Kitabu cha Ufunuo.