Yesu na Kitabu cha Ufunuo

Swahili
(Ufunuo 1 & 19)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza jinsi Mungu alivyompatia Danieli maana ya maono yaliyotabiri mustakabali wa siku zijazo, hadi mwisho wa dunia! Kitabu cha Ufunuo, miongoni mwa mambo mengine, pia kinatuambia kuhusu wakati wa mwisho. Tunapokitafakari kitabu cha Ufunuo, tunaweza kupata taswira ya “madubwana/majinamizi” ya aina zote. Juma hili tunakiangalia kitabu cha Ufunuo kwa mwangaza wa kupendeza zaidi. Tunamwangalia Yesu katika kitabu cha Ufunuo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1.    Yesu na Makanisa

 

  1.    Soma Ufunuo 1:1. Ni nani aliye chanzo cha ujumbe wa kitabu cha Ufunuo? (Yesu.)

 

   1.    Kwa nini Yesu alitutumia ujumbe huu? (Ili tuweze kujua kitakachotokea katika siku zijazo. Hii inatukumbusha kuhusu somo letu la Danieli.)

 

   1.    Mjumbe ni nani? (Malaika alimpatia Yohana ujumbe.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:2. Tunawezaje kukielezea kitabu cha Ufunuo kwa ufupi? (Ni “Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo.”)

 

   1.    Tumeona wapi maneno haya hapo awali? (Soma Ufunuo 1:9. Yohana anasema kuwa yupo Patmo kwa sababu ya “Neno la Mungu na Ushuhuda wa Yesu.” Katika Ufunuo 12:17 tunasoma kwamba Shetani anafanya vita na wale “wazishikao amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu.” Maneno haya yanajitokeza kwenye maeneo mengine katika kitabu cha Ufunuo. Kitabu cha Ufunuo kinahusu injili ya Yesu Kristo. Injili ipo katikati ya pambano kati ya wema na uovu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:3. Tutapokea nini katika kujifunza kwetu kitabu cha Ufunuo? (Baraka.)

 

   1.    Hii ni mara ya pili katika vifungu vichache vya kwanza ambapo Yesu anazungumzia wakati kuwa “karibu” au “kile kitakachotokea upesi.” Soma Ufunuo 22:12. Haya yaliandikwa miaka elfu mbili iliyopita. Je, huu ni uongo? Ikiwa ni uongo, tunaweza kuyapuuzia? (Kuna mambo mawili. Tunaambiwa katika Zaburi 90:4 na 2 Petro 3:8 kwamba Mungu anao mtazamo tofauti kuhusu wakati. Kimsingi, muktadha wa 2 Petro 3:8 unajenga hoja kwamba hatupashwi kupoteza ujasiri wa ujio wa Yesu Mara ya Pili kutokana na kile kinachoonekana kwetu kama ucheleweshwaji. Pili, tukiliangalia jambo hili kama ufunuo wa juma lililopita (Nebukadreza na Danieli), tunatambua kwamba baadhi ya matukio yaliyofunuliwa kuhusu historia ya dunia yalishaanza.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:4-6. Nani anayezungumziwa hapa? (Ingawa inabainisha salaam kutoka maeneo mbalimbali ya mbinguni, Yesu anatajwa mara kadhaa. Yohana anaanza kwa kummiminia Yesu sifa.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:7-8. Hii inaonekana kuelezea tukio gani? (Ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

 

   1.    Hilo litakuwa tukio kubwa! Kwa nini kifungu kinasema kuwa “watu wote duniani wataomboleza kwa ajili yake?” (Utaona kwamba pia kifungu kinawazungumzia wale waliomtesa Yesu. Ninahitimisha kwamba “watu wa dunia” ni rejea ya wale walioikataa mbingu.)

 

   1.    Yesu atakujaje? (Kutoka mbinguni. Utaona kwamba “kila jicho litamwona.” Hapatakuwepo na shaka siku Yesu atakapokuja.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:9. Katika somo letu robo iliyopita, tulisoma vifungu kadhaa vilivyoahidi baraka za vitu na baraka nyinginezo ikiwa tutakuwa waaminifu kwa Mungu. Yohana ana hali gani? (“Anateseka” na mtazamo wake ni ule wa “kuvumilia kwa utaratibu.”)

 

   1.    Kwa nini yupo katika kisiwa cha Patmo? (Maoni ya watu mbalimbali yanasema kuwa Yohana alifukuzwa na kupelekwa kwenye hiki kisiwa kikame kisicho na faida yoyote na mmojawapo wa wafalme wa Rumi. Ilikuwa ni njia ya kumnyamazisha (ndivyo mamlaka ilivyodhani) bila kumwua.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:10-11. Yohana anavuviwa na Roho Mtakatifu katika siku ya Sabato. Roho Mtakatifu anawaza nini? (Kutomnyamazisha Yohana. Badala yake, ni kupeleka ujumbe kwa makanisa saba mahsusi.)

 

   1.    Unadhani haya yalikuwa makanisa halisi? (Ndiyo, inaonekana yalikuwepo makanisa halisi saba. Ukisoma kitabu cha Ufunuo sura za 2-3, utaona ujumbe kwa kila kanisa.)

 

   1.    Bila shaka yalikuwepo makanisa zaidi ya saba katika kipindi hicho, unadhani kwa nini Roho Mtakatifu alichagua makanisa saba? Unadhani namba “saba” pia ina ishara yoyote? (Saba ni namba kamilifu. Ninaamini, pamoja na watu wengine, kwamba haya makanisa saba yanawakilisha tabia za kiroho za Kanisa la Kikristo katika nyakati zote. Kwa mantiki hiyo, maono haya yanayoelezea mustakabali wa Kanisa la Kikristo ni sawa na yale yaliyotafsiriwa na Danieli, ambayo yalielezea mataifa ya siku zijazo.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:12-15. Je, huyu ni Roho Mtakatifu? (Hapana. Tunapewa taarifa zaidi. Huyu ni mtu ambaye Yohana anamwona – na mwonekano alio nao!)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:16-18. Huyu ni nani? (Yesu! Rejea ya awali (kifungu cha 13) inayosema “mfano wa mwanadamu” na rejea ya hapa inayosema “nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele” inaashiria kuwa huyu ni Yesu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 1:19-20. Nani aliye nyuma ya maneno aliyopewa Yohana? (Yesu! Utaona kwamba Yesu anazungumzia “yale yatakayokuwa baada ya hayo.” Sasa hapana shaka kwamba Yohana anatupatia taswira ya siku zijazo, kama tulivyoona kwa Danieli.)

 

 1.   Ushindi wa Yesu

 

  1.    Soma Ufunuo 19:11-15. Unadhani maneno haya yanamwelezea nani? (Utakumbuka kwamba katika Ufunuo 1:16 tulikubaliana kuwa mtu aliyeshikilia upanga utokao katika kinywa chake ni Yesu. Katika juma la kwanza la mfululizo wa masomo haya, tulisoma mwanzo wa Ufunuo 12 na tuliona katika Ufunuo 12:5 rejea inayomzungumzia Yesu kutawala mataifa yote kwa “fimbo ya chuma.”)

 

   1.    Nadhani inashangaza na haipendezi kwa kitendo cha upanga kutokea kinywani mwako. Kwa nini usiushikilie mkononi mwako?

 

   1.    Soma Mwanzo 1:1-3 na Yohana 1:1-3. Yesu anadhihirishaje uwezo wake? (Kwa kuzungumza. Nadhani hii ndio maana ya upanga. Hiyo ndio sababu Yesu, “ambaye ni Neno,” hana haja ya kubeba upanga mkononi mwake. Utaona kwamba kwenye vifungu tulivyovisoma hivi punde (Ufunuo 19:13) kwa mara nyingine Yesu anaitwa “Neno la Mungu.”)

 

  1.    Angalia tena Ufunuo 19:14. Mbingu zina majeshi mangapi? (Zaidi ya moja! Tafsiri ya NIV inatafsiri neno hili kwa uwingi: “majeshi ya mbinguni.”)

 

   1.    Je, majeshi haya yanaundwa na watu kutoka katika dunia nyinginezo?

 

   1.    Endapo kamwe hawajawahi kutenda dhambi, je, “wako tayari” kwenda vitani?

 

  1.    Soma Ufunuo 19:16. Je, hii inathibitisha kwamba Mpanda farasi (Ufunuo 19:11) ni Yesu? (Naam, hakika.)

 

  1.    Soma Ufunuo 19:17-18. Malaika huyu ana uhakika kiasi gani kuhusu matokeo ya pambano lililoibuka?

 

   1.    Hii inaakisi mtazamo wa namna gani? Ulinganishe na mtazamo ambao Yesu aliuonesha kwa wadhambi wakati wa ujio wake wa kwanza? (Haya ni mazungumzo magumu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 19:19-21. Je, Yesu anahitaji majeshi? (Watu wote isipokuwa viongozi wanauawa kwa upanga utokao kinywani mwa Yesu. Ikiwa niko sahihi kuhusu jambo hili, Yesu anawaangamiza kwa kuzungumza. Majeshi hayana haja ya kupambana.)

 

   1.    Angalia kauli ya muhimu sana kwenye hivi vifungu. Nani anayeungua katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti? (Mnyama na nabii wa uongo.)

 

    1.    Nini kinawatokea wengine waliosalia? (Wanauawa na kuliwa na ndege.)

 

    1.    Hii inazungumzia nini kuhusu dhana ya jahanamu iwakayo milele kwa wale waliopotea? (Kifungu hiki kinatofautisha kati ya viongozi wa juu kabisa na waovu wengine waliosalia. Kwa kuwa hii ni rejea moja tu, haipashwi kutatua jambo hili, lakini unatakiwa kutilia maanani tofauti iliyotolewa hapa huku ukitafakari jambo kubwa zaidi.)

 

  1.    Soma Ufunuo 22:12-16. Nani anayehitimisha kitabu cha Ufunuo? (Yesu!)

 

   1.    Waovu na wenye haki wanaelezewaje? Kwa nini hii ni muhimu? (Waovu wanaelezewa kwa matendo yao. Wenye haki wanaelezewa kwa uamuzi wao wa kuikubali haki kwa njia ya imani – “wale wafuao mavazi yao.” Linganisha na Ufunuo 7:14. Hakuna neno lisemwalo kuhusu dhambi za wale waliovikwa haki ya Yesu.)

 

  1.    Rafiki, Yesu ndiye mwanzilishi na mwanzo na mwisho wa Ufunuo. Ikiwa unataka kuokolewa, ikiwa hutaki neno lisisemwe juu yako kuhusu dhambi zako, kwa nini basi usikiri kwamba Yesu ni Bwana, sasa hivi? Kwa nini, sasa hivi, usiyadai maisha yake makamilifu, kifo chake kwa ajili ya dhambi zako, na uwezo wake dhidi ya kifo kama vazi lako la haki?

 

 1. Juma lijalo: Wokovu na Wakati wa Mwisho.