“Badiliko” la Sheria

Swahili
(Warumi 7 & 8, Ufunuo 14, Mwanzo 2)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Lengo la maisha ya Kikristo ni lipi? Je, si kumpa Mungu utukufu? Tunampaje Mungu utukufu katikati ya pambano kali kati ya wema na uovu? Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kuwa sehemu ya ujumbe wa nyakati za mwisho ni kwamba mji wa Babeli umeanguka. Ufunuo 14:8. Umeshindwa, lakini haujafa. Hiyo inamaanisha tunatakiwa kuwa makini na masuala yaliyopo kwenye hilo pambano na kutenda kile tunachoweza ili kumtangaza Mungu na ufalme wake. Hebu tuzame kwenye somo letu la juma hili ili tujifunze zaidi kuhusu jambo kuu katika msukumo wa kumpa Mungu utukufu!

 

 1.    Sheria Nzuri

 

  1.    Soma Warumi 7:14-16. Hapa tatizo ni lipi? (Kwamba tunahangaika na dhambi. Tunajikuta tunatenda mambo ambayo hatutaki kuyafanya.)

 

   1.    Hebu subiri kidogo! Unawezaje kusema kuwa “hutaki kutenda jambo fulani,” wakati unalitenda kwa hiari? (Nadhani hii inamaanisha kuwa kwa akili zetu tunajua kwamba hatupaswi kulitenda jambo hilo. Kiakili, tunataka kumtii Mungu.)

 

   1.    Kiwango kilichokubalika ni kipi, kile ambacho tunashindwa kukitimiza? (Sheria. Hili si shambulizi la sheria. Inaonesha kuwa tatizo lipo kwetu.)

 

  1.    Soma Warumi 7:17-20. Kwa nini tunashindwa kufikia kiwango ambacho Mungu ametuwekea? (Ni kwa sababu ya asili yetu ya dhambi. “Dhambi ikaayo ndani yangu.”)

 

   1.    Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kuwa Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu. Yohana 14:16-17, 23. Dhambi pia inawezaje kukaa ndani yetu? (Hii inaakisi mapambano katika mwenendo wetu wa Kikristo.)

 

  1.    Soma Warumi 7:21-25. Nani anayetuokoa kutoka kwenye haya mapambano? (Soma Warumi 8:1. Yesu! Hiki ndicho tulichojifunza majuma mawili yaliyopita, imani kwa Yesu ndio ufunguo wa wokovu. Njia ya kwenda mbinguni ni kupitia kwa Yesu peke yake.)

 

  1.    Hebu simama kidogo, na utafakari jinsi sheria inavyochukuliwa kwenye vifungu tulivyojifunza hivi punde. Je, sheria imelaaniwa? (Hapana. Warumi 7:22 “Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani.” Tatizo sio sheria, sisi ndio tatizo. Tatizo ni asili yetu ya dhambi. Habari njema sana ni kwamba Yesu aliitii sheria kwa niaba yetu. Kupitia kwake, tulilipa adhabu kwa ajili ya uvunjaji wetu wa sheria.)

 

 1.   Pambano kwa Ajili ya Mungu

 

  1.    Soma Ufunuo 14:6-7. Tuliangalia pia vifungu hivi majuma mawili yaliyopita, lakini kwa sababu tofauti. Ni mambo gani mawili tunayoambiwa kwenye vifungu hivi kuhusu Mungu wetu? (Kwamba yeye ni Muumbaji na kwamba analeta hukumu.)

 

   1.    Je, umewahi kusema kuwa, “Huna haki ya kunihukumu?” Kama hujawahi kusema, je, unakubaliana kwamba mtu anayetoa hukumu dhidi yako anapaswa kuwa na mamlaka ya kuhukumu? (Naam.)

 

    1.    Msingi wa mamlaka ya Mungu kutoa hii hukumu ni upi? (Msingi wake ni ukweli kwamba Mungu ni Muumbaji. Miaka mingi iliyopita, niliamua kujifunza Biblia ili kuona kipi alichokisema Mungu kwamba ndicho msingi wa madai yake ya kutaka tumtii. Sikumbuki idadi kamili, lakini angalao niliona zaidi ya mara 100 Mungu akitumia uumbaji wake kama msingi wa madai yake ya kuwa na mamlaka.)

 

    1.    Hugh Ross ameandika vitabu kadhaa kuhusu sayansi ya Uumbaji. Ufahamu wa Ross juu ya sayansi ni mkubwa sana kuliko wangu, lakini anachokimaanisha ni kwamba kazi ya Mungu ya kisayansi inashangaza na iko sahihi. Akili yangu inastaajabu kwamba Mungu mwenye akili nyingi na uwezo mkubwa kiasi hicho awe ananijali kila siku!)

 

    1.    Hebu tuangalie mantiki kwenye Ufunuo 14:6-7. Unatarajia kwamba jambo gani linaendelea kati ya wanadamu ukingoni mwa miaka inayoelekea katika nyakati za mwisho? (Mamlaka ya Mungu kama Muumbaji.)

 

  1.    Soma Mwanzo 2:1-3. Kwa nini Mungu aliibariki siku ya saba na kuitakasa? (Kwa sababu alimaliza Uumbaji. Kwa umahsusi sabato inahusianishwa na uumbaji.)

 

  1.    Soma Kutoka 20:8-11. Hapo awali tulikuwa tunajadili mtazamo wa Paulo kwamba sheria inafurahisha. Kiini cha sheria ni Amri Kumi, na katikati ya Amri Kumi kuna hii amri. Nini sababu ya kuwepo kwa hii amri? (Kumsherehekea, kumkumbuka Mungu kama Muumbaji wetu!)

 

   1.    Je, huwa unafurahia siku za sikukuu (siku za mapumziko) na likizo? Kumbuka kwamba Paulo anasema kuwa sheria inafurahisha. Je, hii siku ya mapumziko kila juma inakufurahisha?

 

  1.    Soma Ufunuo 14:8. Endapo ungekuwa Shetani, na ukawa unawahamasisha wanadamu wasiwe waaminifu kwa Mungu, ungelenga jambo gani kwanza? (Uumbaji. Ningejaribu kuvunjavunja imani kwamba Mungu ni Muumbaji.  Hiyo inayashambulia mamlaka ya Mungu juu yetu. Uibukaji ni shambulizi linalodhuru sana kwa sababu una madai kwamba bahati ingeweza kutenda kazi ya Mungu yenye kushangaza iliyo makini na sahihi kabisa. Pia ningeshambulia kumbukizi ya tendo la Mungu la uumbaji, Sabato ya siku ya saba.)

 

   1.    Shetani anafanyaje na mpango wake wa dhahiri wa pambano?

 

 1. Biblia na Sabato

 

  1.    Sababu ya kuitunza Sabato ni ya kututia sana, tukizingatia pambano kati ya wema na uovu. Hebu tuangalie vifungu vingine ili tuone kama Mungu alielekeza mabadiliko yoyote kwenye kumbukizi ya Uumbaji wake. Soma Luka 4:14-16. Yesu alikuwa na desturi gani kuhusu ibada ya kila juma? (Kuabudu siku ya Sabato.)

 

  1.    Soma Luka 23:55-56. Desturi ya wafuasi wa Yesu ni ipi? (Walipumzika siku ya Sabato.)

 

  1.    Soma Luka 23:50-54. Yesu aliteswa siku gani? “Siku ya Maandalio.” Hii inatuambia kuwa Yesu alikufa siku ya Ijumaa.)

 

  1.    Soma Luka 24:1-7. Yesu alifufuliwa lini kutoka katika wafu? (Siku ya Jumapili. Rejea ya “siku ya kwanza ya juma” na “siku ya tatu” inatuambia kuwa Yesu alikuwa kaburini siku ya Sabato.)

 

   1.    Kwa nini Yesu alipumzika kaburini siku ya Jumamosi? Ikiwa Mwanao ameshinda tuzo ya “Super Bowl” ya ulimwengu," ikiwa Mwanao ameteswa vibaya sana na kuuawa, je, usingependa kumleta nyumbani na kumkumbatia? (Naam, hakika! Yesu anafanya jambo lile lile ambalo yeye na wafuasi wake wamekuwa wakilifanya – kupumzika siku ya Sabato.)

 

   1.    Kupumzika siku ya Sabato kunaleta mantiki gani hapa? (Unapokumbuka kwamba pumziko la Sabato ni ukumbusho wa uwezo wa Yesu kama Muumbaji wetu, basi inaleta mantiki kamili kwamba baada ya Yesu kushinda pambano dhidi ya uovu, alipotushindia na kuturejesha kwake, atapumzika tena siku ya Sabato ili kuukumbuka ushindi wake wa kishindo.)

 

  1.    Soma Matendo 16:13-14. Hii inatuonesha nini kuhusu kazi za Paulo baada ya kifo na ufufuo wa Yesu? (Biblia inaizungumzia hii siku kama Sabato (na si kwa jina la kidunia kama vile Jumamosi au siku ya saba ya juma) na inatuambia kuwa Paulo pamoja na wanawake walikusanyika ili kuomba.)

 

   1.    Kuna umuhimu gani kwenye ukweli kwamba huu sio mkusanyiko ndani ya sinagogi? (Vifungu vinavyowaonesha wanafunzi wakiongea ndani ya sinagogi siku ya Sabato vinaweza tu kuakisi kwamba walihamasishwa na wasikilizaji, na si kutoa kauli juu ya siku ya ibada.)

 

  1.    Soma Yohana 20:17-19. Je, hii inaonesha kuwa wanafunzi wanaabudu siku ya Jumapili? (Hapana. Kumbuka kwamba Yesu alifufuka siku ya Jumapili, hivyo Yesu anajionyesha kwa wanafunzi wake siku hiyo hiyo.)

 

  1.    Soma Matendo 20:6-7. Watu walikutana siku gani ili kula pamoja na kufanya mkutano? (Utakumbuka utambuzi wa siku wa Kiyahudi ulianza kuanzia kuzama kwa jua hadi kuzama kwa jua. Rejea ya Paulo kuzungumza baada ya giza kuingia inaweza kumaanisha kuwa watu walikuwa pamoja siku ya Sabato, na walianza kula kisha Paulo alianza kuzungumza baada ya giza kuingia – hivyo, rejea ya siku ya kwanza ya juma.)

 

   1.    Muda ambapo kisa hiki kinaelezewa hauko wazi. Kwa hakika, maelezo ya kwamba mkutano (kikao) ulifanyika siku ya Jumapili hayazungumzii chochote kuhusu mabadiliko ya sheria. Ikiwa Mungu alidhamiria kubadili siku ya pumziko, unadhani kuwa angekuwa wazi kuhusu mabadiliko?

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 16:1-2. Hii inazungumzia nini kuhusu kuabudu katika siku ya kwanza ya juma? (Haizungumzii chochote kuhusu ibada, badala yake inazungumzia kuhusu kuweka pamoja michango yenu. Paulo anawaambia wafanye hivi ili asiwakute wakifanya hivyo atakapokuwa anakuja. Hiyo inaashiria shughuli isiyoendana na Sabato, badala ya uthibitisho wa ibada ya Jumapili.)

 

  1.    Soma Isaya 66:22-23. Ni katika kipindi gani tunaabudu siku ya Sabato hapa? (Katika nchi itakayofanywa upya! Hii inaashiria ibada ya siku ya Sabato inayoendelea.)

 

  1.    Rafiki, ikiwa unaelewa kiini cha ugomvi kati ya Mungu na Shetani, ikiwa unaelewa kwamba lengo la Shetani ni kufuta uelewa wetu kwamba Mungu ni Muumbaji wetu, basi unatambua umuhimu wa kuitunza Sabato. Ikiwa bado hauabudu katika siku ya Sabato kama siku maalumu ya pumziko, je, utafanya uamuzi huo sasa hivi?

 

 1.   Juma Lijalo: Mathayo 24 na 25.