Marekani na Babeli

Swahili
(Ufunuo 13 & 17, Danieli 7)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Una umahiri kiasi gani katika kupangilia mchezo-fumbo? Unaweza kuanza kwa kujaribu kulinganisha rangi na mpangilio wake, kisha unahakikisha kuwa umbo liko sahihi. Kupatia umbo sahihi si jambo rahisi mara zote. Somo letu juma hili linanikumbusha mchezo-fumbo. Tutalinganisha “vipande” fulani vya kihistoria ili tuone vipande vipi vinaonekana kuunda umbo vizuri zaidi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Mnyama wa Baharini

 

  1.    Soma Ufunuo 13:1. Mnyama huyu anatokea wapi? (Baharini.)

 

   1.    Fikiria kwamba umevua kitu hiki kwenye wavu wako!  Ikiwa umewahi kukivua, je, unaweza kusema kuwa umewahi kuona mojawapo ya vitu hivi hapo kabla? (Soma Danieli 7:7. Umeziona Pembe Kumi hapo kabla!)

 

  1.    Soma Danieli 7:2-3. Pembe Kumi za Danieli 7 zinatokea wapi? (Zinatokea baharini. Zinaweza kuwa Pembe Kumi zile zile.)

 

   1.    Maji ambako Pembe Kumi zinatokea yanawakilisha nini? (Soma Ufunuo 17:15. “Jamaa, makutano, mataifa na lugha.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 17:7. Je, hizi ni zile zile Pembe Kumi? (Zinaweza kuwa pembe ngapi? Zinaonekana ni zile zile.)

 

  1.    Soma Ufunuo 13:5-7. Tunafahamu nini kuhusu hizi Pembe Kumi? (Zina majivuno, zinamkufuru Mungu, na kufanya vita dhidi ya watakatifu. Hata hivyo, anao muda mfupi wa kuwa na mamlaka.)

 

  1.    Kama ilivyo kwetu, Danieli ana hamu kubwa ya kujifunza zaidi kuhusu Pembe Kumi. Hebu tufuatilie maswali ya Danieli na tuone kile tunachoweza kujifunza. Soma Danieli 7:19-22 na kisha Danieli 7:23-24. Je, Pembe Kumi ni kitu gani? (Wafalme kumi.)    

 

  1.    Yohana pia anashangazwa na Ndugu Pembe Kumi. Soma Ufunuo 17:8. Pembe Kumi zina muda kiasi gani? (Kwa kadri ambavyo watu ambao hawajaokolewa wanavyojihusisha, Ndugu Pembe Kumi ana nafasi mahala fulani katikati ya maisha yake.)

 

  1.    Soma Ufunuo 17:9-10. “Vichwa” vya Pembe Kumi ni kitu gani? (Ni “milima” na pia ni “wafalme.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 17:11-12. “Pembe” za Ndugu Pembe Kumi ni kitu gani? (Kwa mara nyingine tunaona kuwa ni wafalme ambao bado hawajapokea ufalme. Mmojawapo pia anaonekana kuwa ni mnyama. Wana uhasama na Mungu. Inaonekana kuwa kweli muda usio wa kawaida ni wa mmojawapo wa pembe.)

 

  1.    Soma Danieli 2:36-42. Unakumbuka kisa hiki kwenye Somo la 2 la mfululizo wa masomo haya? Tulihitimisha kuwa “ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma” ulikuwa ni ufalme gani? (Ufalme wa Rumi.)

 

  1.    Hebu tutumie mbinu za mchezo-fumbo wetu. Je, huu ufalme wa nne wa chuma wa Danieli 2 unaonekana kuwa ndio Pembe Kumi za Danieli 7, Ufunuo 17, na Ufunuo 13? (Binafsi nakubaliana. Rejea ya Ufunuo 17:9 ya “milima saba” inaihusianisha na jiji la Roma, ambao upo kwenye milima saba, na ni mji mkuu wa Ufalme wa Rumi.)

 

   1.    Je, Ufalme wa Rumi uliwatesa watakatifu? (Naam, hakika. Ulimuua Yesu. Ulimuua Paulo.)

 

  1.    Kuna baadhi ya taarifa kuhusu Pembe Kumi zinazoibua jambo. Soma Danieli 7:15-17. Hii inasema kuwa Pembe Kumi zilitokea “duniani” na si baharini. Tunalichukuliaje hili? (Sijui. Sehemu nyingine zote zinaendana.)

 

  1.    Rafiki, hitimisho tulilolifikia hadi kufikia hapa linakubalika na wanafunzi wa Biblia. Tunapoelekea katika sehemu inayofuata, suala la Pembe Ndogo lilikubalika kwa usawa mmoja miongoni mwa wasomi wa miaka 150 iliyopita.)

 

 1.   Pembe Ndogo

 

  1.    Angalia tena Danieli 7:7-8. Tumeona rejea za hii pembe “ndogo” kama sehemu ya Pembe Kumi. Hiyo inatuambia nini kuhusu Pembe Ndogo? (Asili yake ni kutoka katika Ufalme wa Rumi.)

 

   1.    Hii Pembe Ndogo inafananishwa na nani? (Mtu.)

 

    1.    Hiyo inaweza kumaanisha nini? (Inaashiria kuwa umuhimu wa ufalme umejengwa juu ya mtu.)

 

   1.    Pembe Ndogo inachukua nafasi ya nani? (Inang’oa pembe tatu (wafalme). Maoni ya Jamieson, Fausset na Brown yanawaelezea wafalme watatu na kuonesha, kama suala la kihistoria, jinsi falme zao zilivyogeuzwa na kurejeshwa kwenye Upapa – nguvu ya kidini iliyoibuka kutoka kwenye Ufalme wa Rumi.)

 

  1.    Angalia tena Danieli 7:24-26. Mtazamo huu wa Pembe Ndogo unafunua jambo gani? (Kwamba inampinga Mungu, inawakandamiza watakatifu, na inajaribu kubadili “majira na sheria.”)

 

   1.    Umegundua muda uliotolewa? Ni upi huo? (Mwaka mmoja, miaka miwili na nusu mwaka. Hii ni sawa na siku 1,260, au kama tunahitimisha kuwa hizi siku ni miaka ya kiishara/kinabii (angalia Ezekieli 4:6), basi itakuwa miaka 1,260.)

 

   1.    Soma Ufunuo 13:5-7. Tunaona kipindi gani hapa? (Kipindi kile kile kama cha Danieli 7. Miezi arobaini na miwili mara 30 ni sawa na 1,260!)

 

  1.    Tuhitimishe nini kuhusu kipande hiki cha mchezo-fumbo? Maoni ya Jamieson, Fausset na Brown, kama nilivyoyabainisha hapo juu, yanasema kuwa Upapa ndio Pembe Ndogo – ambayo ndio iliyokuwa imani ya kawaida miongoni mwa Waprotestanti miaka 150 iliyopita. Una maoni gani? (Moyo wangu na kichwa changu vinakinzana. Ninachukia kuwashambulia Wakristo wenzangu. Katika kesi zangu mahakamani kuhusu uhuru wa kuabudu nimewawakilisha Wakatoliki wazuri kipekee na waaminifu ambao sasa ni marafiki wangu. Mashambulizi yanayofanywa na vyombo vya burudani kwa Kanisa Katoliki yananikasirisha. Hata hivyo, kubadilisha madaraka na uwezo kihistoria kutoka Ufalme wa Rumi kwenda Vatican inaonekana, kwenye huu mchezo-fumbo, kuendana na unabii wa Danieli na Ufunuo. Mfalme Hadrian wa Rumi, mwaka 135 BK, alikuwa mhimili kwenye kubadili siku ya ibada kutoka Jumamosi kwenda Jumapili. Kwa mujibu wa tovuti: www.catholic.com Katekisimu inasema “Kanisa linasherehekea siku ya Kufufuka kwa Kristo katika ‘siku ya nane,’ Jumapili, ambayo kwa usahihi inaitwa Siku ya Bwana.” Ufalme wa Rumi na Kanisa Katoliki zina historia mbaya ya kuwaua Wakristo. Siwezi kupuuzia hilo.)

 

   1.    Kipindi hiki cha siku/miaka 1,260 kinakubaliana na kuendana na kipindi cha mwaka 38 BK hadi mwaka 1798 BK. Mwaka 1798 BK ndio mwaka ambao Papa alichukuliwa mateka. Hii inaashiria nini kuhusu mchezo-fumbo wetu wa historia?

 

 1. Mnyama wa Duniani

 

  1.    Soma Ufunuo 13:11. Utaona kuwa mnyama huyu anaonekana kuifuata Pembe Ndogo. Hivyo, inapaswa “kutoka katika nchi” katika kipindi cha mwisho cha Pembe Ndogo – 1798. Marekani ilianzishwa lini? (Tarehe 4 Julai, 1776.)

 

   1.    Australia ilianzishwa lini? (Tarehe 1 Januari, 1901. Hata hivyo, koloni lake la kwanza la kuadhibia lilianzishwa mwezi Januari, 1788.)

 

   1.    Canada ilianzishwa lini? (Tarehe 1 Julai, 1867.)

 

   1.    New Zealand ilianzishwa lini? (Tarehe 7 Mei, 1856.)

 

   1.    Petro Mkuu alianzisha Ufalme wa Urusi lini? (Mwaka 1721.)

 

   1.    Mapinduzi ya Ufaransa yalitokea lini? (Mwaka 1789-1799.)

 

  1.    Kama mwaka 1798 ni wa muhimu kubainisha alama ya Mnyama wa Duniani, zipo nchi kadhaa zilizo na tarehe muhimu katika kipindi kinachokaribiana na mwaka huo. Hebu tuzichunguze zaidi ili tuone kama zinaendana na mchezo-fumbo wetu. Ufunuo 13:11 inasema kuwa mnyama huyu alipanda juu “kutoka katika nchi.” Baadhi ya watu wanaashiria kuwa kitendo hiki kinamaanisha maeneo yasiyo na watu wengi sana. Watahiniwa wetu gani wanaendana na kigezo hicho? (Marekani, Canada, Australia, New Zealand, na, huenda Ufalme wa Urusi.)

 

   1.    Utakumbuka Danieli 7:17 inasema kuwa Ufalme wa Rumi uliinuka “kutokea duniani.” Ikiwa neno “dunia” inazungumzia eneo la kijiografia, na si idadi ya watu, basi kauli hiyo itakuwa inaimaanisha Ufaransa. Ufalme wa Urusi na Ufalme wa Rumi pia zinapishana.)

 

  1.    Soma Ufunuo 13:11-12. Je, yeyote kati ya watahiniwa wetu ameifanya dunia iziabudu Pembe Kumi au Pembe Ndogo? (Uelewa wangu wa historia si mkamilifu, lakini ninadhani jibu ni “hapana.” Kihistoria Marekani, Canada, Australia na New Zealand zimeruhusu uhuru wa dini. Watu wa Marekani (ambao wengi wao ni Waprotestanti) wamekuwa na ubaguzi dhidi ya Kanisa Katoliki. Mapinduzi ya Ufaransa yalikuwa na chuki kwa dini. Ufalme wa Urusi ulikuwa na Kanisa Katoliki la Ki-Orthodox (lenye imani kamili) kama dini ya taifa. Hata hivyo, mwaka 1054 BK liligawanyika na kuachana na Kanisa Katoliki kuhusiana na mamlaka ya Papa. Hakuna mtahiniwa wetu hata mmoja anayeendana na maelezo haya – angalao hadi hapa tulipofikia.)

 

  1.    Soma Ufunuo 13:13. Je, kuna mtahiniwa yeyote kati ya watahiniwa wetu ambaye amefanya “moto ushuke kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu?” (Kama ulitazama uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq, uliona jambo hili. Je, televisheni inahusisha “mbele ya wanadamu?”)

 

  1.    Soma Ufunuo 13:14-15. Je, hili limetokea? (Hapana.)

 

   1.    Tunapaswa kufanya nini kuhusu hiki kipande cha mchezo-fumbo? (Tunatakiwa kuwa macho ili tuone kuwa mamlaka (nguvu) ipi inaendana vizuri na maelezo ya Mnyama wa Duniani.)

 

  1.    Rafiki, ulimwengu wa kidini haukutarajia Yesu aje kwa jinsi alivyokuja, hata kama palikuwepo na unabii mwingi kuhusu kuja kwake. Hii inatuonya tuwe makini na tuendelee kujifunza Biblia na kulinganisha matukio ya sasa. Je, utadhamiria kuwa makini zaidi?

 

 1.   Juma lijalo: Mhuri wa Mungu au Alama ya Mnyama?