Maisha Katika Kanisa la Awali

Swahili
(Matendo 2:42-4:26)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Somo letu juma hili linahusu kanisa baada ya Pentekoste. Je, hiki ndicho kielelezo kwa ajili yetu leo? Kwa dhahiri kabisa ni tofauti na kanisa la leo. Tunaweza kujifunza nini? Kanisa la awali liliwataka wadhambi watubu. Hiyo inamaanisha nini? Tukiona maoni tofauti, na upande mmoja unakimbilia kwenye vitisho badala ya ushawishi, tunapaswa kuhitimisha nini? Hebu tuzame kwenye somo letu la Matendo na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Siku za Hofu

 

  1.    Soma Matendo 2:42-43. Jambo gani linakosekana kwenye hii ratiba ya kila siku? (Kufanya kazi! Wanakula, wanasali, wanafundishwa, wapo katika ushirika, na wanashuhudia miujiza. Ni kipindi kizuri, lakini hakionekani kuwa na mpango wa muda mrefu wa “kufanya kazi.”)

 

   1.    Unaweza kufikiria mfanano wowote leo? (Kwenye mojawapo wa kesi zangu zinazohusu uhuru wa dini, nilimtetea mke wa Myahudi mwenye msimamo mkali (asiyebadilika kirahisi). Nilitakiwa kuzungumza naye (mume) peke yake, na si kuzungumza na mkewe moja kwa moja. Kutokana na hali hii isiyo ya kawaida (kwangu), nilitambua kuwa mwanamke peke yake ndiye aliyekuwa akifanya kazi. Mwanaume alitumia muda wake kujifunza na kujadili Sheria ya Mungu.)

 

  1.    Soma Matendo 2:44-47. Suluhisho la tatizo la kifedha la kupata chakula na kutokufanya kazi lilikuwa lipi? (Waliuza vitu vyao hitaji lilipojitokeza.)

 

   1.    Sikumbuki kuona mfano huu mahali popote kwenye Biblia. Watu wengine wanasema kuwa hivi ndivyo ambavyo Wakristo wanapaswa kuishi leo. Una maoni gani? Hii ni programu ya kujitolea. Hata hivyo, serikali zinapochukua mali za watu wenye nazo na kuwapatia wale wasio navyo, hatimaye zinaishiwa “fedha za watu wengine” na hali inabadilika na kuwa mbaya zaidi. Pasipo na uwepo wa Mungu, huu si mpango wa muda mrefu.)

 

   1.    Ikiwa huu si mfano au mpango wa muda mrefu, kwa nini umeelezewa, kwa nini umeandikwa kwenye Biblia? (Pentekoste, hii “faragha” ya muda wa maombi, kujifunza, miujiza, ushirika na chakula, ni mambo ya pekee. Huenda asili yake ya upekee ndio sababu ya kuelezewa kwake?)

 

    1.    Je, umewahi kupitia uzoefu wa namna hiyo? (“Mkutano wa makambi” unanikumbusha jambo hili. Muda wa pekee katika mwaka kwa ajili ya mafundisho ya kiroho, ushirika na kula pamoja na marafiki. Nilizipenda sana nyakati hizo.)

 

 1.   Siku za Kuponya

 

  1.    Soma Matendo 3:1-4. Kwa nini mtu huyu hakuwaangalia Petro na Yohana moja kwa moja? (Bila shaka kuombaomba kulikuwa kunadhalilisha. Hakuangalia machoni mwa watu waliompatia fedha.)

 

   1.    Angalia Matendo 2:46. Ikiwa waumini wapya walikuwa na kila kitu kwa shirika, na walikuwa wakimpita huyu ombaomba mlemavu kila siku, kwa nini hawakumchukua kwenye kundi lao, na kushiriki naye chakula chao, kuwa na ushirika naye, na kujifunza pamoja naye?

 

  1.    Soma Matendo 3:5-8. Petro anapendelea suluhisho gani? (Wangeweza kumchukua hadi ndani. Huenda walifanya hivyo baadaye, lakini Petro anamponya kwa uwezo wa Mungu ili ombapmba aweze kujihudumia.)

 

   1.    Angalia tena Matendo 3:6. Kweli Petro hakuwa na fedha yoyote? Kwa dhahiri lazima alikuwa na fedha ikiwa Matendo 2:45 inaeleweka kama jinsi ilivyoandikwa. Tunafundishwa nini hapa? (Hii inatufanya tuangalie jambo hili kwa undani zaidi. Kuangalia kwa juu juu vifungu tulivyovisoma kunahitimisha kwamba watu “matajiri” wanapaswa tu kutoa mali zao na kuwapa wahitaji. Ingawa Biblia inazungumzia sana suala la fadhila (misaada), kamwe haiungi mkono utoaji usio wa mpango, au kile ambacho leo tunakiita “matendo mema yasiyo na mpangilio.” Biblia inahamasisha kufanya kazi (Mambo ya Walawi 19:9-10), stahili (1 Timotheo 5:9-10), na huruma (Mithali 28:27 & Kutoka 22:25-27).)

 

  1.    Soma Matendo 3:9-12. Nia gani ya ziada inaashiriwa kwa uponywaji wa mtu huyu? (Tuliona jambo lile lile kwa Yesu – miujiza ndio iliyokuwa msingi wa kupata usikivu wa watu na kisha kuwafundisha injili.)

 

  1.    Pitia kwa haraka haraka hubiri la Petro akimzungumzia Yesu katika Matendo 3:13-18. Soma Matendo 3:19-21. Petro anatoa wito gani? (Anawataka watubu.)

 

   1.    Watubu nini? (Hubiri tulilolipitia lilihusiana na wao kumkataa Yesu kama Masihi. Wito wa kutubu ni wito wa kumkiri Yesu.)

 

   1.    Kwa muda mrefu nimekuwa na uelewa wenye mashaka kuhusu maana ya “kutubu.” Nilipokuwa mdogo, niliaminishwa kuwa lazima nikumbuke na kutubu kila dhambi. Ikiwa, kwa namna fulani hivi, nilisahau dhambi, basi nisingeokolewa kwa kuwa palikuwepo na dhambi ambayo sikuitubu. Leo, binafsi naona kitendo hiki kama namna nyingine ya kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo. Mara hii matendo yanafuatilia na kutubu kila dhambi. Kama sitapatia kwa kukosea, basi siokolewi. Je, wazo la kukumbuka na kutubu kila dhambi linaendana na wito wa Petro wa toba? (Petro anaiomba hadhira yake imkiri Yesu na itubu kutokana na kitendo chao cha kumkataa.)

 

  1.    Soma Waebrania 6:1. Hii inaielezeaje toba? (Inaiita toba kuwa ni “mafundisho ya kwanza ya Kristo.”

 

  1.    Soma Waebrania 6:4-6. Tunaweza kutubu mara ngapi? (Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anasema “haiwezekani” baada ya “kuanguka.” Hii inaonekana kama jambo tunalolifanya mara moja.)

 

   1.    Ngoja nikuulize swali binafsi. Je, unajikuta unatubu dhambi ile ile mara kwa mara? (Nafahamu ninafanya hivyo, na hiyo inanifanya nichukulie kile nilichofundishwa nikiwa mdogo kuhusu kutubu dhambi kuwa ni makosa. Toba ni badiliko la mawazo, wazo la kumkiri Yesu kama Mwokozi wako.)

 

  1.    Soma Matendo 3:19, Matendo 5:31, na Luka 24:47. Je, toba na msamaha wa dhambi ni vitu viwili tofauti? (Matokeo ya toba ni kwamba dhambi zetu “zinafutwa.” Wakati huo huo, vinaonekana kuwa vitu viwili tofauti.)

 

  1.    Soma Matendo 26:20. Hapa matendo yanahusishwaje na toba? (Ikiwa umebadili mawazo yako, umebadili mtazamo wako, basi unapaswa kuenenda tofauti.)

 

  1.    Soma Luka 11:2-4. Mara hii Yesu anasema kuwa tunapaswa kuomba mara ngapi? (“Msalipo.” Hiyo inaashiria kuwa hii ni sala ya kila mara. Tunaomba mara nyingi.)

 

   1.    Kwa nini kusamehewa kwa dhambi zetu kunahusianishwa na sisi kuwasamehe watu wengine? (Hiki ndicho kinachonifanya nidhani, kwa mara nyingine, kwamba toba na ungamo la dhambi ni suala la kimtazamo zaidi, badala kutafuta kuangalia kila dhambi. Je, ninawasamehe wale wanaotenda dhambi dhidi yangu? Ikiwa nina huo mtazamo, basi Yesu anatumia mtazamo huo huo dhidi yangu.)

 

   1.    Tanbihi kwa msomaji: ninajumuisha maswali haya kuhusu toba na ungamo ili kuchochea fikra yako kwenye mada hii, bado sijapata suluhisho la suala hili mawazoni mwangu.

 

 1. Serikali Yajibu Mapigo

 

  1.    Soma Matendo 4:1-4. Ujumbe gani unazihangaisha mamlaka za Kiyahudi? (“Katika Yesu tunao ufufuo wa wafu.”)

 

   1.    Unadhani hii inamaanisha nini? (Sidhani kama ufufuo wa wafu ulikuwa suala lenye mjadala moto moto. Badala yake, ufufuo wa Yesu kutoka katika wafu ndio ilikuwa suala lenye ubishani.)

 

  1.    Soma Matendo 4:5-6. Kwa nini suala la ufufuo wa Yesu linalihangaisha kundi hili? (Wao ndio viongozi walioshinikiza Yesu kusulubiwa. Ikiwa Yesu amefufuka, na ninadhani walilijua hili, basi tatizo lao limekuwa baya zaidi, halijapungua.

 

  1.    Soma Matendo 4:7. Petro na Yohana wanaulizwa swali gani mahsusi? (Mlimponya ombaomba mlemavu kwa nguvu gani?)

 

  1.    Soma Matendo 4:8-10. Je, hili ndilo jibu ambalo viongozi wa Kiyahudi walikuwa wanalitafuta? (Ni kinyume chake kabisa. Hoja ya Petro, iliyovuviwa na Roho Mtakatifu, ni kwamba ufufuo wa Yesu unathibitishwa na uponyaji wa kimiujiza wa ombaomba mlemavu!)

 

  1.    Soma Matendo 4:11-12. Kuna madai gani yemetolewa kwa Yesu? (Tafakari jambo hili. Kauli hii inamaanisha kuwa mfumo wote wa ibada ya Kiyahudi hauna thamani yoyote linapokuja suala la wokovu. Hii ndio changamoto kuu kwa viongozi wa Kiyahudi.)

 

  1.    Soma Matendo 4:13-14. Viongozi wa Kiyahudi wana utetezi gani kwenye hii changamoto ya kijasiri? (Wanaweza kusema nini? Uthibitisho ulikuwa mbele yao!)

 

  1.    Soma Matendo 4:15-18. Hii inakuambia nini kuhusu malengo ya kiroho ya uongozi wa Kiyahudi? (Sasa wameamua kuachana na ukweli. Vitisho vinachukua nafasi ya uthibitisho na hoja, kwa kuwa vitisho ndio silaha pekee waliyosaliwa nayo.)

 

  1.    Soma Matendo 4:21-26. Msingi wa kwanza uliowafanya wamsifu Mungu kwenye maombi yao ni upi? (Kwamba Mungu ndiye Muumbaji! Kuukiri uumbaji ni kiini cha kuukiri uwezo wa Mungu. Ikiwa Mungu anaweza kusema na uumbaji ukatokea, anaweza kushughulikia vitu vyote vidogo tunavyovihitaji maishani.)

 

  1.    Rafiki, je, utayachunguza maisha yako? Unaweza kuona kama kuna maeneo ambayo mawazo yako yanayokinzana na uthibitisho unaokuzunguka? Tafadhali mwombe Roho Mtakatifu ili ayapangilie mawazo yako yaendane na uwezo wa Mungu uliofunuliwa.

 

 1.   Juma lijali: Viongozi wa Kwanza wa Kanisa.