Pentekoste

Swahili
(Matendo 2)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Ninaposoma ukosoaji kutoka ndani ya Kanisa ambalo mimi ni mshiriki wake, mara nyingi ukosoaji huo unahusiana na tofauti za kiteolojia, au viwango stahiki kitabia. Hii inanikumbusha gari langu. Endapo halikuwa na taa, au bamba la gari lilikuwa na mbonyeo, nilidhani kuwa linatakiwa kufanyiwa matengenezo. Lakini, endapo injini haikuwa ikifanya kazi, hicho ndicho nilikizingatia kwanza. Ndani ya kanisa, uwepo (au kutokuwepo) wa Roho Mtakatifu ndio unaopaswa kuwa jambo letu la kwanza kulizingatia. Bila kuhafifisha umuhimu wa mambo mengine, tunatakiwa kuwa na uzingativu sahihi. Somo letu la leo linatusaidia kwenye uzingativu wetu. Hebu tuchimbue Biblia yetu na tujifunze zaidi kuhusu Roho Mtakatifu!

 

 1.    Mahali Pamoja

 

  1.    Soma Matendo 2:1 na Matendo 1:11-14. Unadhani hapo “mahali pamoja” walipokuwa wamekusanyika ni wapi? (Hatuwezi kuwa na uhakika. Hata hivyo, ninaviweka vifungu hivi pamoja ili uweze kuona uhusiano wa karibu kati ya kupaa kwa Yesu mbinguni, kukusanyika kwenye chumba cha orofani kwa ajili ya kuomba na kukusanyika siku ya Pentekoste. Inawezekana bado walikuwemo ndani ya chumba kile kile kwenye ile nyumba “walipokuwa wakikaa.”)

 

  1.    Soma Matendo 2:2-4. Mambo gani matatu tofauti yalitokea baada ya kuwasili kwa Roho Mtakatifu? (Upepo wa nguvu wenye kasi na sauti kubwa. Ndimi za moto. Kusema kwa lugha nyingine. Hebu tuyaangalie mambo haya kila moja kivyake.)

 

 1.   Roho Mtakatifu na Upepo

 

  1.    Upepo wa nguvu wenye kelele kubwa unasaidia jambo gani? (Soma Matendo 2:6. Ilisaidia kupata usikivu. Ilikuwa moja ya sababu iliyofanya makutano kukusanyika.)

 

  1.    Kwa nini Roho Mtakatifu alitokea katika mfumo wa upepo? Kelele za upepo ndilo jambo la kwanza lililobainishwa!

 

  1.    Soma Ezekieli 37:9-10 na Ezekieli 37:14. Hapa Roho Mtakatifu anatimiza wajibu gani? (Anawapatia uhai!)

 

  1.    Soma Yohana 3:5-8. Hapa Roho Mtakatifu anajihusisha na kazi gani? (Anatia uhai kwenye maisha mapya ndani ya Yesu. Utaona kwamba Yesu anamlinganisha Roho Mtakatifu na upepo.)

 

  1.    Soma Yohana 20:19-23. Je, kuna uhusiano wowote kati ya kumpokea Roho Mtakatifu na msamaha?

 

   1.    Vipi kuhusu uhusiano kati ya Roho Mtakatifu na kuwa na amani?

 

   1.    Vipi kuhusu uhusiano kati ya Roho Mtakatifu na kushuhudia? (Sehemu ya maisha mapya, ubatizo wa maji na Roho Mtakatifu, ni msamaha wa dhambi na kuyaacha mambo ya kale, maisha mafu.)

 

  1.    Rafiki, unaona kwamba Roho Mtakatifu analeta uhai, maisha mapya, kama vile pumzi tunayoivuta inavyoendeleza uhai wetu? Je, unaye Roho Mtakatifu ndani yako? Ikiwa jibu ni hapana, basi umekufa kiroho! Umeacha kupumua!

 

 1. Moto

 

  1.    Soma Isaya 4:4. “Moto” wa Roho Mtakatifu unatenda nini hapa? (Unasafisha.)

 

  1.    Soma Mathayo 3:11-12. Hapa moto wa Roho Mtakatifu unatenda jambo gani? (Hii haisemi kwa mahsusi kwamba moto wa Roho Mtakatifu ndio unaoteketeza “makapi,” bali pendekezo ni kwamba Roho Mtakatifu ni sehemu ya huu mchakato wa utenganishaji.)

 

  1.    Unapotafakari kipengele cha Roho Mtakatifu cha “moto,” unaelezeaje lengo la uwezo huu? (Sehemu ya uwezo huo inatenda kazi mawazoni mwangu kugusa dhambi zangu na kunifanya niziache. Watu wengine wanaukubali maelekezo ya Roho Mtakatifu na wengine hawayakubali. Matokeo yake ni utenganishaji wa ngano na makapi.)

 

  1.    Soma 1 Wathesalonike 5:19-22. Nini kinatokea ikiwa utazima moto wa Roho Mtakatifu maishani mwako? (Hutayasikia maelekezo yake, hutaweza kuelezea kinachotoka kwa Mungu na kisichotoka kwa Mungu, hutaweza kutenganisha wema na ubaya na hivyo kuuepuka uovu.)

 

 1.   Ndimi

 

  1.    Soma tena Matendo 2:4. Unaielewaje kauli ya “kama Roho alivyowajalia?” (Hii ni karama inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Uwezo wote huu unatoka kwa Roho Mtakatifu, lakini hii inaashiria kuwa Roho Mtakatifu aliwezesha baadhi ya lugha.)

 

  1.    Soma Matendo 2:5-8. Hapa karama ya lugha ni ipi? (Karama ya kuwafanya watu wengine kuelewa kwa lugha yao.)

 

   1.    Je, hii inaendana na upepo na moto? (Sehemu ya maisha mapya ndani ya Yesu ni kuyaelewa mapenzi yake kwa ajili yako. Huwezi kuelewa hadi usikie kwanza.)

 

  1.    Matendo 19:4-6. Nini kiliwatokea hawa Wakristo wapya Roho Mtakatifu alipowaingia? (Walinena kwa lugha na kufanya unabii.)

 

   1.    Je, ni dhahiri kwamba walihitaji kuwasiliana na wale wanaowazunguka? (Ni vigumu kuona kwamba huo ndio ukweli wa mambo hapa. Inaonekana tunaambiwa kuwa ndimi za kumthibitisha Roho Mtakatifu ziliwakalia. Walipewa uwezo wa pekee.)

 

  1.    Soma Marko 16:14-18. Je, kuna namna ya kuthibitisha kwamba tunamwamini Yesu? (Yesu anasema kuwa vifuatavyo ndivyo “ishara” ya mtu anayeamini: kutoa pepo, kusema kwa lugha mpya, kushika nyoka, kunywa sumu, kuwaponya wagonjwa.)

 

   1.    “Ishara” ngapi kati ya hizi “zinakuzunguka?”

 

   1.    Hebu tuchambue jambo hili kwa undani zaidi. Yesu anawaambia wanafunzi wake wafanye nini? (Waende ulimwenguni na kuhubiri.)

 

    1.    Endapo ungetakiwa kuweka mpango wa safari ya uinjilisti ulimwenguni, ungezingatia jambo gani? (Upinzani kutoka kwa Shetani na malaika wake walioanguka. Kuzungumza lugha ya watu wa eneo utakalokwenda. Hatari ya wanyama wakali. Hatari ya chakula kibaya au maji yasiyo salama. Kutoweza kuwashawishi watu ujumbe wangu. Unaona jinsi ambavyo kimsingi “ishara” hizi ni njia za kuyashinda matatizo yanayoibuka kwenye uinjilisti?

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 14:1-4. Hadi hapa tulipofikia, rejea za karama ya kunena kwa lugha ama zinazungumzia kwa dhahiri lugha za kigeni au haziko wazi. Je, hii karama ya Roho ya kusema kwa lugha ni lugha ya kigeni? (Kwa mahsusi kifungu kinasema kuwa si lugha ya kigeni. “Hakuna anayeelewa.”)

 

   1.    Vifungu hivi vinajenga hoja kwamba kueleweka ni jambo la muhimu zaidi kwa sababu linawasaidia watu wengine. Kwa nini Roho Mtakatifu atoe karama ya kusema kwa lugha isiyoweza kueleweka na mtu yeyote? Manufaa ya kunena mafumbo ni yapi? (Ukisoma vifungu hivi kwa makini, vinatufundisha kuwa tafsiri moja ya karama ya kusema kwa lugha ni kuwasiliana na Mungu kunako “muadilisha” Mkristo.)

 

    1.    Je, hii inaleta mantiki yoyote? (Fikiria ukweli kwamba kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ni ya ndani – kuyaelekeza mawazo yetu kwenye njia sahihi.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 14:27-28. Hii inatufundisha nini kuhusu kusema kwa lugha ya mafumbo? (Haipaswi kutokea kanisani isipokuwa tu kama kuna mtu wa kutafsiri.)

 

 1.    Siku Zijazo Sasa Hivi

 

  1.    Soma Matendo 2:14-18. Je, tunaishi katika “siku za mwisho?” (Petro anasema kuwa Pentekoste ilikuwa sehemu ya siku za mwisho, hivyo kwa dhahiri tupo katika siku za mwisho.)

 

  1.    Hebu tujikite kwenye Matendo 2:17-18. Karama ya unabii, karama ya maono na karama ya ndoto vimeenea kwa kiasi gani? (Vifungu hivi vinasema kuwa “watu wote.” Roho Mtakatifu atatenda kazi kupitia kwa kila mtu, bila kujali jinsi au umri.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 13:1-3. Je, wafuasi wa Mungu wanatakiwa kuwajaribu wale wanaodai kuwa na karama ya unabii? (Ndiyo.)

 

   1.    Jaribu ni lipi? (Kama wanakuelekeza kwa Mungu au mbali na Mungu.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 13:5. Jambo gani linatakiwa kutokea ikiwa nabii atashindwa jaribio? (Kifo.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 18:22. Tunaambiwa kufanya nini ikiwa nabii anatoa ujumbe usiotimia? (Hatuna haja ya kumwogopa nabii huyo, kwa kuwa nabii amenena kwa kiburi na ufidhuli.)

 

  1.    Kwenye Agano la Kale, katika hali ya kawaida manabii walikuwa wachache. Yoeli anatuambia kuwa manabii wa siku za mwisho watakuwa wengi. Tunapaswa kuwa na mwitiko gani kwa manabii wa kisasa? (Tunapaswa kuwajaribu. Ikiwa wanakosea katika mambo yao, basi sina haja ya kuwa na ujasiri kwenye mambo wanayoyasema. Lakini, kwa karama iliyotapakaa, sidhani kama adhabu ile ile kali ya kifo ni sahihi. Hata hivyo, leo sisi si dola na hatuna mamlaka kama hayo.

 

  1.    Rafiki, je, Roho Mtakatifu yu hai ndani yako? Je, unamruhusu Roho atende kazi yake kwa ukamilifu: kutupatia maisha mapya, kutusafisha dhambi zetu, kutusaidia kuwapa watu wengine mtazamo sahihi wa Yesu? Ikiwa jibu ni hapana, kwa nini usiombe jambo hilo sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Maisha Katika Kanisa la Awali.