Kukamatwa Yerusalemu

Swahili
(Matendo 21-23)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tuliishia pale ambapo Paulo alimfufua Eutiko alipokuwa anajiandaa kuondoka mji wa Troa. Kuanzia hapo Paulo aliendelea kidogo na kazi ya umisionari. Kisha katika Matendo 20:16 tunaona kwamba Paulo ana haraka ya kwenda Yerusalemu kwa wakati kwa ajili ya sikukuu ya Pentekoste. Anataarifu kwamba anahimizwa na Roho Mtakatifu kwenda huko (Matendo 20:22), lakini tuna ishara kinzani kuhusu jambo hilo. Somo letu juma hili linahusu uzoefu mgumu wa Paulo kule Yerusalemu. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Ishara kinzani

 

  1. Soma Matendo 21:2-4. Nani yuko nyuma ya onyo la kutokwenda Yerusalemu? (Roho Mtakatifu!)

 

  1. Soma Matendo 21:10-12. Nani yuko nyuma ya huu ujumbe mahsusi wa onyo? (Kwa mara nyingine, ni Roho Mtakatifu.)

 

  1. Hebu tusome kifungu nilichokirejea kwenye Utangulizi, Matendo 20:22. Tunaona ujumbe gani wa kuonesha wasiwasi? (Paulo anasema hajui kitakachomtokea. Hii itanifanya niwe na wasiwasi.)

 

  1. Paulo anasema kuwa Roho Mtakatifu “alimlazimisha” kwenda Yerusalemu – ingawa anaashiria kuwa panaweza pakawepo na matatizo. Kisha tunaona maonyo mawili yanayofuatana, yanayohusianishwa na Roho Mtakatifu, kwamba Paulo hapaswi kwenda Yerusalemu. Unauelezeaje huu ujumbe wa Roho Mtakatifu unaokinzana? (Soma Matendo 20:23. Sasa tunaona kuwa katika kila mji Roho Mtakatifu anamwonya Paulo kuwa yapo matatizo yanayomsubiri.)

 

  1. Soma Matendo 21:13-14 na Matendo 20:24. Paulo anajibuje kwenye huu mgogoro? Kwa nini anafanya kile ambacho Roho Mtakatifu alimwonya asikifanye? (Paulo anasema kuwa huu ni mgogoro wa kawaida maishani mwake. Kazi yake ni ya hatari. Lakini, ana lengo kubwa la kutangaza injili.)

 

   1. Soma Matendo 9:13-16. Je, Paulo alionywa? (Kati ya watu wote, Paulo anaelewa. Alikuwa mtesaji kwa sababu za kidini. Anaelewa mgogoro uliopo kati ya wema na uovu. Nadhani Roho Mtakatifu anamwonya kwa sababu hana sababu ya kuumizwa. Lakini, Paulo amejitoa kikamilifu kuutangaza Ufalme wa Mungu.)

 

 1. Yerusalemu

 

  1. Soma Matendo 21:17-19. Safari ya Paulo Yerusalemu inaanzaje?

 

 

  1. Soma Matendo 21:20-21. Je, viongozi wa kanisa wamefurahishwa kabisa na kazi ya Paulo? (Wanadhani kuwa ni vyema anavyofanya hiyo kazi nzuri kwa Mataifa, lakini taarifa za kazi yake zinasababisha matatizo Yerusalemu.)

 

  1. Soma Matendo 21:22. Ungejibuje swali hili kama wewe ndiye ungekuwa Paulo?

 

  1. Soma Matendo 21:23-24. Je, hili limewahi kukutokea? Mtu anakuomba maoni yako kuhusu kile unachopaswa kukifanya, na kabla hujajibu, anakuambia kile anachodhani kuwa unapaswa kukifanya?

 

   1. Unauchukuliaje ushauri wa Yakobo na wazee?

 

   1. Je, mashtaka ni ya kweli – kwamba Paulo anasema kuwa Wayahudi wasiwatahiri watoto wao au wasifuate “desturi” za Kiyahudi? (Soma Wagalatia 5:6 na Wagalatia 5:1 Je, tuseme kwamba msimamo wa kweli wa Paulo ni “tohara kamili?” Wale wenye ari ya torati wanapaswa kukata kiungo chao chote? Unaweza kujenga hoja kwamba Paulo hawaambii Wayahudi kuepuka tohara, lakini kwa dhahiri anapiga vita wazo kwamba lazima Mataifa watahiriwe. Na kwa kuongezea, anasema kuwa tohara haileti tofauti yoyote.)

 

  1. Soma Matendo 21:25. Kwa nini Yakobo na wazee wanaongezea dondoo hii? (Wanataka Paulo ajue kwamba hawaghairi mtazamo wao wa mahitaji ya Mataifa.)

 

   1. Habari njema ni kwamba Paulo na viongozi wa kanisa kule Yerusalemu wanakubaliana na tofauti inayotakiwa kuwepo kati ya Wakristo wa Kiyahudi na wa Kimataifa. Unawachukuliaje washiriki wa kanisa moja kuwa na viwango tofauti kabisa?

 

    1. Unawezaje kuwa na umoja wa kanisa wakati viwango tofauti vinatumika kwa watu tofauti? (Inaonekana kuwa umoja unakuwepo uongozi unapokubaliana jambo.)

 

  1. Soma Matendo 21:26. Ikiwa viongozi wa kanisa hawakupendekeza jambo hili, je, Paulo mwenyewe angedhani kuwa hili ni jambo zuri? (Soma 1 Wakorintho 9:19-23. Hatujui kinachoendelea mawazoni mwa Paulo kwa sasa, lakini hili ndilo haswa jambo ambalo Paulo anataarifu kuwa atalitenda. Yuko radhi kubadilika kwenye suala hili ili kusaidia kuwapata na kuwahifadhi waongofu wapya.)

 

 1. Kukamatwa

 

  1. Soma Matendo 21:27-29. Mashtaka makuu ni yapi? (Si kulinajisi hekalu, jambo linaloonekana kuwa ni mashtaka “ya ziada.” Bali, ni kufanya mafundisho kinyume na watu wetu na torati yetu.)

 

   1. Washtaki wanaishi wapi? (Mahali ambapo Paulo amekuwa akiishi. Paulo alikuwa akitangaza injili kwa Mataifa kule Asia, na ikiwa mashtaka si ya kweli, kwangu mashtaka hayo yanaonekana kabisa kuwa ni ya kweli.)

 

 

    1. Ikiwa Paulo hakupitia utaratibu wa kutakaswa kama ilivyopendekezwa, unadhani kweli angekamatwa? (Nina uhakika kuwa angekamatwa kutokana na mashtaka makuu dhidi yake.)

 

  1. Soma Matendo 21:30-32 na Matendo 21:35-36. Unadhani hivi ndiyo ambavyo kwa kawaida Wayahudi walikuwa wakienenda? Je, wao ni kundi tu la watu wasio na adabu wanaochukia haki ya uhuru wa kujieleza? (Nadhani haya ni mashetani. Wafuasi wa Yesu wanaweza kutarajia aina hii ya mwitiko hata miongoni mwa watu “waliosafishwa” ushawishi wa kishetani unapokuwa mkubwa.)

 

   1. Kuna nyakati za giza katika historia ambapo Wakristo waliwatesa na kuwaua Wayahudi. Je, unadhani kisa hiki kinahusiana na mateso hayo? (Inaonekana kuwa na mantiki kwamba Shetani anapenda kutumia kazi yake mwenyewe kuchochea chuki. Matusi na maneno mabaya anayoyashawishi anayatumia kuchochea matusi kutoka upande mwingine.)

 

  1. Soma Matendo 21:39-40. Katika Matendo 22:1-21 Paulo anawaelezea watu kisa cha kuongolewa kwake wakati wakimsikiliza kwa utulivu. Kwa kuwa tumejifunza habari za kuongolewa kwa Paulo, hatutayazingatia maswali kuhusu kisa hicho. Soma Matendo 22:21-22. Kwa nini kazi ya Paulo inawafanya kundi la watu litake kumwua? (Fikiria kwamba unaondolewa kutoka kwenye nafasi yako ya kiongozi wa kampuni na nafasi (kazi) yako inachukuliwa na mtu mwingine. Paulo anawaambia kuwa wao si tena watu wa pekee wa Mungu. Sasa Mataifa wanafurahia upendeleo wa uhusiano na Mungu. Kisa cha Paulo kinakemea kile wanachokifanya sasa hivi.)

 

  1. Soma Matendo 22:24-25. Tunajifunza nini kuhusu Paulo kudai haki zake kisheria? (Kwa mara nyingine, tunamwona Paulo akisisitiza juu ya haki zake kama raia wa Kirumi.)

 

  1. Soma Matendo 22:29-30. Nafasi ya kisheria ya Paulo imebadilikaje? (Mpango wa awali ulikuwa ni kumpiga Paulo sababu ikiwa ni umati wa watu kutaka kumwua. Sasa, viongozi wa Kiyahudi wanatakiwa kuthibitisha mashataka yoyote waliyonayo dhidi ya Paulo. Wakati huo huo Paulo anaachiliwa kutoka mahabusu.)

 

 1. Kesi

 

  1. Soma Matendo 23:1-3. Majuma kadhaa yaliyopita tulijadili maelekezo ya Yesu kuhusu kugeuza shavu jingine (Mathato 5:39), na ukweli kwamba baadaye Yesu alidai haki zake kisheria dhidi ya yeye kupigwa kofi (Yohana 18:22-23). Hapa Paulo anafanya nini? (Anapinga kwa nguvu kuhusu kupigwa kwake.)

 

  1. Soma Matendo 23:6. Je, hii ni kweli? (Ndiyo. Ikiwa Yesu alikufa tu, basi asingetimiza desturi zote za Kiyahudi zilizosababisha ghasia. Vitendo hivyo havihusiki tena.)

 

   1. Je, huu pia ni utetezi wa kilaghai? (Soma Matendo 23:7-10. Ndiyo! Paulo anajinasibisha na upande mmoja, Mafarisayo, na anasema kesi yake inatokana na kuamini kama wanavyoamini.)

 

 

  1. Soma Matendo 23:11. Je, unadhani Yesu alimtokea Paulo? Au, je, huyu ni Roho Mtakatifu? (Kifungu kinasema “Bwana” na kwenye Biblia yangu maneno haya yameandikwa kwa rangi nyekundu, ikimaanisha kwamba watafsiri walidhani kuwa hayo yalikuwa maneno ya Yesu.)

 

   1. Tumebishana kama Paulo anafuata maelekezo ya Roho Mtakatifu. Maneno ya Yesu yenye kutia moyo yanatufundisha nini? (Yesu hatuachi. Paulo amedhamiria kutangaza injili bila kujali chochote. Yesu anakuja yeye mwenyewe kumtia moyo katika kipindi hiki cha kesi yake.)

 

  1. Hebu tuangalie kwa ufupi somo letu lililosalia kwa kusoma barua rasmi kwa Liwali Feliki. Soma Matendo 23:26-30. Kwa nini bado Paulo yuko mahabusu? (Kwa sehemu fulani ni ili kumlinda. Kwa sehemu nyingine, ni kupata hukumu kutoka kwa afisa wa mamlaka ya juu.)

 

  1. Rafiki, somo hili linakufundisha nini kuhusu kumfuata Mungu? Linatufundisha kwamba tunaweza kupitia nyakati ngumu, lakini Mungu yu pamoja nasi katika kila hatua. Pia linatufundisha kuwa kudai na kutetea haki zetu halali ni jambo sahihi. Je, utamwomba Roho Mtakatifu kukufanya uwe mwaminifu katika nyakati ngumu?

 

 1. Juma lijalo: Kifungoni Kaisaria.