Somo la 12: Kifungoni Kaisaria

Swahili
(Matendo 24-26)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Watu wachache sana wanaitazamia kesi. Mara ya mwisho tulipojadili habari za Paulo, Liwali alimwambia, “nitasikiliza kesi yako washtaki wako watakapofika hapa.” Katika somo letu juma hili, washtaki wa Paulo wanawasili na tunaona mashtaka na jinsi Paulo anavyojitetea sio tu kwenye kesi moja bali kwenye kesi mbili! Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Mashtaka Mbele ya Feliki

 

  1.    Soma Matendo 24:1-4. Je, tumewaona viongozi wa Kiyahudi wakimwajiri mwanasheria ili kutoa mashtaka dhidi ya Paulo? (Sina kumbukumbu hiyo.)

 

   1.    Kwa nini safari hii wanamwajiri mwanasheria? (Wanataka waondokane kabisa na Paulo. Pia inaweza kuakisi kuwa huu ni mfumo rasmi.)

 

   1.    Mwanasheria Tertulo anaanzaje kesi yake dhidi ya Paulo? (Anaanza kwa kumsifia Liwali Feliki.)

 

    1.    Hii inatuambia nini kuhusu Feliki? (Hana lolote na yumkini si mwerevu sana. Feliki anapaswa kutambua kuwa hii haina uhusiano wowote na mashtaka dhidi ya Paulo.)

 

   1.    Umewahi kumsikia mwanasheria akijenga hoja? Ikiwa ndivyo, je, uliisikia ahadi kwa ufupi? (Hii ni ahadi inayotolewa mara kwa mara na kuvunjwa mara kwa mara.)

 

  1.    Soma Matendo 24:5-9. Mashtaka dhidi ya Paulo ni yapi? (Anasababisha matatizo na kuanzisha vurugu. Yeye ni kiongozi wa kanisa la Kikristo. Alijaribu kulinajisi hekalu.)

 

   1.    Je, mashtaka haya ni ya kweli? (Ni kweli kwamba mara kwa mara Wayahudi wanaanzisha vurugu wanaposikia ujumbe wa Paulo. Vivyo hivyo kwa wengine. Kimsingi, hili ni kosa la jinai kwa upande wa watu wanaoanzisha ghasia, na si kwa upande wa Paulo. Ni kweli kwamba Paulo ni kiongozi Kanisani. Shtaka la mwisho limebadilika, linganisha na Matendo 21:28-29.)

 

  1.    Soma Matendo 24:10. Je, Paulo pia anaanza kwa kutoa kauli isiyofaa? (Paulo anasema kuwa Feliki anafahamu kuwa viongozi wa Kiyahudi wana matatizo. Hamsifii Feliki, anamwambia Feliki aufikirie uzoefu wake mwenyewe kwa viongozi hawa.)

 

  1.    Soma Matendo 24:11-13. Je, hii inafikia kiwango cha kuwa shtaka la kufanya fujo aliloshtakiwa Paulo? (Shtaka ni kwamba Paulo anaanzisha fujo kila mahali. Paulo anakana kwamba hakuwa akiwashawishi watu kule Yerusalemu siku kumi na mbili zilizopita.)

 

   1.    Nani ana mzigo wa uthibitisho hapa? (Paulo anathibitisha kuwa viongozi wa Kiyahudi ndio wenye mzigo wa uthibitisho.)

 

  1.    Soma Matendo 24:14-16. Paulo anasemaje kuhusu shtaka la kwamba yeye ni kiongozi wa Kanisa? (Anakiri.)

 

   1.    Paulo anaendelea kuzungumzia teolojia. Kwa nini hilo ni muhimu? (Soma Matendo 23:29. Hii ni sehemu ya barua ya Klaudio Lisia kwenda kwa Liwali Feliki. Lisia anasema kuwa mashtaka dhidi ya Paulo yanahusiana na dini, sio mashtaka ya madai yanayostahili kifungo au adhabu kubwa zaidi ya kifungo. Paulo anakazia hitimisho hilo.)

 

  1.    Soma Matendo 24:17-21. Hapa tunaona utetezi wa shtaka la kuanzisha vurugu duniani kote? Utetezi wa Paulo ni upi? (Wale waliotoa mashtaka ya awali hawapo hapa. Hakuna ushahidi kamili kuhusu shtaka hili. Paulo hakufanya jambo lolote baya alipokuwa hekaluni Yerusalemu, hivyo hakuna chochote kwenye mwenendo wake wa sasa kinachoweza kuashiria kutenda jambo baya kwenye maeneo mengine.)

 

   1.    Baraza lilimkuta Paulo na hatia kwenye shtaka gani? (Soma Matendo 23:9-10. Baraza halikufikia uamuzi kwa sababu vurugu ilijitokeza mahali pale.)

 

  1.    Soma Matendo 24:22-23. Kwa nini Feliki anamsubiria Lisia? Je, Lisia ataongezea jambo lolote? Tayari ameshaandika barua akielezea kuwa Paulo hana hatia.

 

   1.    Tunapaswa kuielewaje kauli ya kwamba Feliki anajua habari nyingi kuhusu Ukristo?

 

  1.    Soma Matendo 24:24-25. Je, kuna tatizo lolote la kisheria hapa? (Hakimu Feliki anasikiliza upande mmoja tu wa Paulo kwenye hii kesi. Katika mahakama ya sheria nchini Marekani, pande zote mbili zinatakiwa kuwepo.)

 

   1.    Kwa nini hakimu anakuwa na wasi wasi? Je, hii inatufundisha jambo kuhusu jinsi tunavyotakiwa kushuhudia? (Hii inaonesha kuwa Feliki si mtu mwema. Hataki kusikia habari za kujizuia au “hukumu itakayokuja.”)

 

    1.    Paulo ni mtetezi wa neema? Hii inazungumzia nini kuhusu neema? (Neema haituweki huru kuishi vyovyote tutakavyo. Mungu anayawazia maisha sahihi kwa ajili yetu.)

 

  1.    Soma Mtendo 24:26. Kwa nini Feliki anadhani kuwa Paulo anaweza kumpa rushwa? (Soma tena Matendo 24:17. Paulo anawapelekea fedha maskini, huenda anaweza kumpelekea Feliki sehemu ya fedha. Kimsingi huu ni uthibitisho zaidi kwamba Feliki ni mtu mbaya.)

 

  1.    Soma Matendo 24:27. Kigezo cha muhimu kabisa kwenye haya mashtaka ni kipi? (Si kuutafuta ukweli, bali kuzingatia masuala ya kisiasa.)

 

   1.    Kwa nini Mungu anaruhusu hili? Kumbuka kwamba huyu ni Mungu yule yule aliyemtoa Petro kutoka gerezani. Angalia Matendo 12:6-10. (Tunafahamu kwamba Mungu ana uwezo wa kumweka Paulo huru. Hivyo, Mungu ana sababu zake za kumwacha Paulo kizuizini.)

 

 1.   Mashtaka Mbele ya Festo

 

  1.    Soma Matendo 25:1-3. Jambo gani linaweza kumhamasisha Festo akubaliane na suala hili? (Alikuwa mgeni kwenye kazi hii. Sehemu ya muhimu ya kazi yake ilikuwa ni kuendeleza amani na Wayahudi.)

 

  1.    Soma Matendo 25:4-5. Ni kwa msingi gani Festo anaamua kukataa pendekezo la viongozi wa Kiyahudi? (Inaonekana kuwa suluhisho mwafaka kwa kila mtu isipokuwa kwa viongozi wa Kiyahudi.)

 

   1.    Festo anaonesha ujuvi gani kuhusiana na mashtaka ya Paulo? (Anadhania Paulo hana hatia.)

 

  1.    Soma Matendo 25:6. Utaona kwamba ndani ya majuma mawili tangu aanze kazi, Festo anasikiliza mashtaka dhidi ya Paulo. Hiyo inaashiria nini? (Mashtaka ya Paulo ni ya muhimu. Fikiria kazi nyingine nyingi ambazo Festo anapaswa kuzifanya kwenye kazi yake mpya.)

 

  1.    Soma Matendo 25:7-11. Ni upendeleo kiasi gani kwa Wayahudi kuhamishia mashtaka Yerusalemu ikiwa bado Festo ataendelea kuwa hakimu?

 

   1.    Utakumbuka katika Matendo 25:3 tulijifunza kuwa Wayahudi walitaka kumwua Paulo wakati akihamishwa. Unadhani kuwa Festo alilielewa hili? (Ninatilia shaka, isipokuwa kama alitaarifiwa kuhusu ile njama ya awali dhidi ya Paulo kule Yerusalemu.)

 

   1.    Kwa nini Festo anaomba ukubali wa Paulo ili mashtaka yake yahamishiwe Yerusalemu? (Kama Paulo atakubali, basi uamuzi utakuwa rahisi.)

 

    1.    Kwa nini Paulo hakubali? (Katika Matendo 25:11 anazungumzia kuhusu kukabidhiwa kwa Wayahudi. Paulo anajua watakuwa na nguvu zaidi kwake kule Yerusalemu.)

 

   1.    Unadhani hadi kufikia hapa mashtaka yanamwendeaje Paulo? (Vizuri sana.)

 

    1.    Kama mashtaka yanaendelea vizuri, kwa nini Paulo anakata rufaa kwa Kaisari?

 

  1.    Soma Matendo 25:12. Je, huu ni uamuzi rahisi kwa Festo?

 

  1.    Soma Matendo 25:16-21. Sasa tunaona mawazo binafsi ya hakimu! Kwa nini Festo alikuwa radhi kuruhusu Paulo ahamishiwe Yerusalemu ikiwa Paulo aliridhia?

 

   1.    Festo angetoa uamuzi gani kwenye mashtaka endapo Paulo asingekata rufaa? (Paulo angeshinda.)

 

  1.    Soma Matendo 25:23-27. (Tatizo kubwa la Festo ni lipi? (Hawezi hata kutoa kauli yenye mantiki ya mashtaka dhidi ya Paulo.)

 

  1.    Katika Matendo 26:1-21 Paulo anaelezea kisa cha kuongolewa kwake na kazi ya injili aliyopewa na Mungu kama utetezi wake kwenye mashtaka dhidi yake. Utaona kwamba kwenye haya mashtaka yanayosikilizwa hapa Paulo hana washtaki. Soma Matendo 26:22-24. Nini kimemfanya Festo afikirie kuwa Paulo ana wazimu? (Habari ya Yesu kuwa wa kwanza kufufuliwa katika wafu.)

 

   1.    Je, kuna maneno ya sifa kwenye shambulizi la Festo? (Paulo ni msomi mkubwa.)

 

  1.    Soma Matendo 26:25-28. Je, Mfalme Agripa anadhani kuwa Paulo ana wazimu? (Anadhani kinyume chake kabisa. Anasema tu kuwa bado hajashawishika.)

 

  1.    Soma Matendo 26:29-32. Je, Paulo alikosea kukata rufaa kwa Kaisari?

 

   1.    Soma Matendo 28:17-19. Unayachukuliaje maelezo ya Paulo kuhusu rufaa yake?

 

   1.    Hebu tupitie jambo ambalo tayari tumeshalisoma. Soma Matendo 23:11. Unadhani maneno haya ya Yesu yalimhamasisha Paulo?

 

  1.    Rafiki, mashtaka haya pamoja na kusikilizwa kwake yanaonesha kuwa Paulo hana hatia ya mashtaka yoyote ya jinai, lakini bado anaendelea kushikiliwa chini ya ulinzi mkali. Je, vitendo visivyo vya haki vimekutokea maishani mwako? Je, vilitokana na utiifu wako kwa Mungu? Je, utadhamiria kwamba, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, utasalia kuwa mwaminifu kwa Mungu hata kama vitendo visivyo vya haki vinakutokea?

 

 1. Juma lijalo: Safari Kwenda Roma.