Somo la 12: Wameona Nini Nyumbani Mwako

English
(Isaya 38, 2 Wafalme 20, 2 Mambo ya Nyakati 32)
Year: 
2019
Quarter: 
2
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza. Lesson 12 What Have They Seen in Your House?

 

Utangulizi: Hezekia alikuwa mfalme mzuri! Aliyafuata mapenzi ya Mungu na kuigeuza nchi yake kuacha ibada ya sanamu. Alipokabiliana na kifo, alimgeukia Mungu ili kupata msaada wake. Kwa namna nyingi alikuwa mwaminifu kwa Mungu. Lakini, hakuwa na busara na majivuno yalikuwa yanamsumbua. Matatizo haya yalileta madhara makubwa kwa nchi yake na uzao wake. Vipi kuhusu wewe? Je, kutokuwa kwako na busara, majivuno yako, au kutokuwa kwako na utiifu vinahafifisha tamaa yako ya kuutangaza Ufalme wa Mungu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na Hezekia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Ahirisha

 

  1.    Soma Isaya 38:1-3. Mungu alidhamiria kwamba huu ndio mwisho wa Hezekia, lakini alimpa muda wa kutengeneza “mambo ya nyumba yake.” Ni kwa msingi gani Hezekia anamwomba Mungu abadili mawazo yake? (Ananukuu matendo yake mema. Ana uchungu mkubwa.)

 

  1.    Soma Isaya 38:4-5. Kwa nini Mungu anaongeza miaka kumi na mitano kwenye maisha ya Hezekia? (Maombi na machozi yake.)

 

   1.    Kwa nini Mungu habainishi matendo mema ya Hezekia?

 

  1.    Soma Isaya 38:6. Mungu anamwahidi Hezekia jambo gani jingine? (Kwamba watakuwa salama dhidi ya watu wa Ashuru. Unaweza kukumbuka kwamba Hezekia ana historia na watu wa Ashuru. Angalia Isaya 36.)

 

   1.    Kwa nini Mungu aliongezea hiyo ahadi? (Fikiria vile ambavyo ingekuwa kwa ile miaka ya ziada kumi na mitano ya utumwa!)

 

   1.    Soma 2 Wafalme 20:6 kwa maelezo yanayoendana na hayo. Hapa tunaona sababu gani iliyotolewa kuhusu kuulinda mji? (Mungu anaulinda mji kwa ajili yake na kwa ajili ya Daudi.)

 

    1.    Hii inatufundisha nini juu ya uhusiano mzuri na Mungu? (Kwamba itakuwa baraka kwa uzao wetu.)

 

   1.    Ninazingatia machapisho ya utafiti yanayosema kuwa ikiwa utafanya “X” basi utakuwa na miaka ya ziada mitano ya kuishi. Hadi kufikia hapa, ninafanya mambo mengi sana ya aina hii kiasi kwamba ninapaswa kuishi miaka 150! Kisa hiki kinatuambia nini kuhusu urefu wa maisha yetu na Mungu wetu? (Maisha yetu yako mikononi mwa Mungu.)

 

  1.    Soma Isaya 38:7. Kwa nini Hezekia ahitaji ishara? Kwani neno la Mungu halitoshi? (Soma maelezo yanayofanana na hayo katika 2 Wafalme 20:8. Hezekia aliomba ishara. Kwa dhahiri, neno la Mungu halikumtosha. Baadhi ya watoa maoni wanasema hii siyo ishara ya mashaka ya Hezekia, bali kwamba ilikuwa ni kawaida kuomba ishara.)

 

  1.    Soma 2 Wafalme 20:9-11. Je, unakubaliana kwamba ni rahisi kwa kivuli kwenda mbele kuliko kurudi nyuma? (Kwa jinsi ninavyoelewa sayansi, ishara ni jambo kubwa la kuonesha uwezo kuliko uponyaji. Mungu amebadilisha nafasi ya dunia au jua! Pia inawezekana kwamba Mungu amebadilisha utambuzi au amebadili mwanga kwenye eneo lile.)

 

   1.    Hii inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Mungu dhidi yetu? (Mungu sio tu kwamba aliyarefusha maisha ya Hezekia, bali alionesha asili yake ya uvumilivu kwa kutenda muujiza ili kusisitiza neno lake. Na kwa kuongezea, alimruhusu Hezekia achague undani wa muujiza.)

 

 1.   Majivuno

 

  1.    Soma 2 Mambo ya Nyakati 32:24-25. Hezekia aliitikiaje kitendo cha Mungu kurefusha maisha yake? (Tunaona maelezo mengine yanayotoa taarifa ya ziada kwamba kwa namna fulani Hezekia hakuitikia vizuri kile ambacho Mungu alimtendea.)

 

   1.    Unadhani Hezekia alioneshaje majivuno yake mbele ya muujiza? (Ubashiri wangu ni kwamba aliona kuwa alistahili kuongezewa kipindi cha uhai wake. Haikuwa haki kwamba anapaswa kufa sasa hivi. Mungu alimwongezea miaka ya kuishi. Isaya 38:9-17 inatoa ushahidi wa hii nadharia, ingawa ushahidi una mkanganyiko mkubwa.)

 

    1.    Je, tuna mtazamo huu – kwamba tunastahili mambo mazuri yanayotutokea?

 

  1.    Soma Isaya 39:1. Je, haifurahishi pale unapokuwa mgonjwa kukumbukwa na marafiki walio katika nafasi za juu?

 

  1.    Soma Isaya 21:1-2. Kitabu cha “The Bible Knowledge Commentary” kinasema kuwa huyu “mvamizi/mharibu” ni Marduk, mtu yule yule aliyeandika barua kwa Hezekia. Aliivamia Ashuru, akaiteka Babeli, na akavikwa kuwa “Mfalme wa Babeli.” Sasa, je, unadhani hii ni barua ya kirafiki tu, kwamba, nina furahi umepona? (Unakumbuka hapo awali kwamba Hezekia alikuwa na historia na watu wa Ashuru? Alikuwa ametishiwa na kutukanwa nao, na kwa miujiza Mungu aliiokoa Yuda. Mwandishi wa barua alikuwa ni mtu aliyewashambulia watu wa Ashuru. Inaleta mantiki kwamba alimwendea Hezekia ili kumpata mshirika dhidi ya watu wa Ashuru.)

 

  1.    Soma Isaya 39:2. Kwa nini Hezekia anawaonesha wawakilishi wa Marduk utajiri wake na silaha zake?

 

  1.    Soma 2 Mambo ya Nyakati 32:31. Mungu anasema ujumbe kutoka kwa wawakilishi wa Marduk ni jaribu. Jaribu la nini? (Utakumbuka kwamba Hezekia ana tatizo la majivuno.)

 

   1.    Chukulia kwamba tuko sahihi kuwa jambo linalozungumziwa ni majivuno, ni kwa jinsi gani hili ni jaribu kwa tatizo la Hezekia la majivuno? (Jibu la dhahiri ni kwamba inaonesha kuwa Hezekia ni tajiri. Jibu lisilo dhahiri sana ni kwamba inaonesha kuwa Hezekia ni mshirika anayestahili katika kusaidia kuwashinda watu wa Ashuru.)

 

  1.    Soma Isaya 10:5 na Isaya 10:10-13. Kwa nini Ashuru inarejewa kama “fimbo ya hasira ya [Mungu]?” (Mungu analitumia taifa hilo la kipagani kuwaadhibu wasio watiifu.)

 

   1.    Nani aliye miongoni mwa wasio watiifu? (Isaya alitabiri kwamba watu wa Ashuru watawaadhibu watu wa Mungu kwa ajili ya uabudu wao wa sanamu.)

 

  1.    Unaweza kuchambuaje kile anachokifanya Hezekia? Hii inahusianaje na jaribu la majivuno ya Hezekia? Kumbuka kwamba yeye ni mfalme mzuri na aliangamiza sanamu za miungu ya uongo. (Badala ya kumwacha Mungu atende jambo hili, badala ya kutegemea ahadi ya Mungu ili kuwa salama dhidi ya watu wa Ashuru katika kipindi cha uhai wake, Hezekia anajaribu kuchukulia kushindwa kwa watu wa Ashuru mikononi mwake.)

 

 1. Mtazamo wa Kusikitisha

 

  1.    Soma Isaya 39:3-6. Majivuno ya Hezekia na mpango wake tarajali wa vita unaendaje kinyume na matarajio – yaani, unalipuka mapema kabla ya muda? (Marduk ataishambulia Yuda. Hatafuti kufanya ushirika na Hezekia. Mungu anaahidi kuwa Yuda itakuwa salama dhidi ya Ashuru, bali sasa Hezekia ameileta Babeli mlangoni mwao.)

 

  1.    Soma Isaya 39:7-8. Hezekia anawezaje kulichukulia hili kuwa neno jema? (Pale tu utakapolichukulia hili kwa namna ya ubinafsi uliopindukia ndipo jambo hili linapoweza kuchukuliwa kuwa “jema.” Uzao wake, familia yake, watachukuliwa mateka. Watahasiwa. Hii inanifanya nimchukulie Hezekia kuwa mtu wa hadhi ya chini.)

 

  1.    Hebu turejee nyuma na tupitie baadhi ya mafanikio ya Hezekia. Soma 2 Wafalme 20:20, 2 Mambo ya Nyakati 31:21 na 2 Mambo ya Nyakati 32:30. Maisha ya Hezekia yalikuwa ni yale ya kumtangaza Mungu wa kweli na ibada yake. Aliiboresha Yerusalemu kwa namna ambayo yalisalia kuwa mafanikio ya wakati wote. Hii inaendanaje na maoni ya “neno jema” kuhusu mustakabali wa kutisha kwa Yerusalemu na familia yake? (Nadhani hii ni kinyume na kila kitu ambacho Hezekia alijaribu kukifanya katika kipindi cha uhai wake.)

 

   1.    Nini kilicho kiini cha mateso ya Hezekia kugeuka kwa kila kitu alichokifanyia kazi katika kipindi chote maishani mwake, yakiwemo matendo mengi makuu ya kidini? (Majivuno. Upendeleo wa mambo binafsi.)

 

   1.    Soma tena 2 Mambo ya Nyakati 31:21. Nani aliyemfanya Hezekia kuwa tajiri? (Mungu.)

 

   1.    Tunatenganishaje kuufurahia usitawi wa maisha mazuri dhidi ya majivuno katika usitawi wetu? (Soma tena 2 Mambo ya Nyakati 32:25. Biblia inatuambia kuwa anguko la Hezekia lilitokana na kutoitikia wema wa Mungu. Nadhani hii inamaanisha kuwa hakuonesha shukrani kwa Mungu kwa kumsitawisha na kuyaokoa maisha yake.)

 

  1.    Rafiki, watu wengine wanaona nini katika maisha yako? Wanaona nini nyumbani mwako? Je, wanaona majivuno? Ubinafsi? Au, je, wanaona shukrani kwa Mungu kwa wema wake? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi ili akupatie mtazamo sahihi? Mtazamo ambao utawavuta watu wengine kwa Mungu?

 

 1.   Juma lijalo: Kugeuza Mioyo Wakati wa Mwisho.