Somo la 3: Mtazamo wa Yesu na Mitume Kwa Biblia

(Mathayo 4, 12 & 22)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Nimezoea sana kulifikiria Agano la Kale na Agano Jipya kama Biblia moja, kiasi kwamba ninafikia hatua ya kujikumbusha kwamba rejea/nukuu yoyote ya “Maandiko” katika Agano Jipya ni rejea ya Agano la Kale. Jinsi Yesu na mitume wake walivyolielewa Agano la Kale inayo mafundisho ya muhimu kwetu leo katika jinsi tunavyoitafsiri Biblia. Kwa mfano, katika mfululizo wetu wa masomo uliopita kuhusu Danieli tulisumbuka sana juu ya rejea ya “chukizo la uharibifu.” Angalia Danieli 11:31 na Danieli 8:13. Wanamaoni kadhaa wanajenga hoja kwamba vifungu vyote hivi viwili vinamrejelea Antiokia Epifanesi. Hivyo sivyo Yesu alivyomwelewa Danieli. Katika Mathayo 24:15 Yesu anasema kuwa “chukizo la uharibifu” litatokea katika siku zijazo. Hiyo inamwondosha Antiokasi, aliyeishi kabla Yesu hajazaliwa duniani. Yesu alitafsiri vifungu vingapi vingine? Hebu tuzame kwenye somo letu na tuangalie baadhi ya njia ambazo Yesu alilielewa Agano la Kale!

 

 1.     Pambano la Yesu Nyikani

 

  1.     Soma Mathayo 4:1-3. Unalichukuliaje jaribu hili? Je, limejengwa juu ya njaa? Je, linahusu majivuno? Linahusu nini?

 

  1.     Soma Mathayo 4:4. Yesu anajenga hoja gani? Yesu anaonekana kukubaliana na ukweli kwamba mkate ni wa muhimu (“hataishi kwa mkate tu”). kwa kuwa mkate ni wa muhimu, kwa nini asiutengeneze?

 

   1.     Je, mwili wako unaweza kuishi kwa maneno?

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 8:2-3. Tunaona kwamba hiki ndicho kifungu ambacho Yesu alimnukulia Shetani. Unaielewaje Kumbukumbu la Torati 8:2-3? (Mana ilitoka mbinguni. Mungu aliitengeneza (bila shaka) kwa kutamka tu. Aliitengeneza kwa maneno yake.)

 

   1.     Hilo lina mjibuje Shetani? Je, hicho sicho haswa ambacho Shetani anampendekezea Yesu akifanye – kwamba atengeneze chakula kwa nguvu za kimungu? (Hapana. Yesu anasema kwamba wanadamu hawakuwa na haja ya kujilisha, Mungu aliwalisha na Mungu Baba angemlisha Yesu wakati alipokuwa akiishi kama mwanadamu.)

 

  1.     Soma Mathayo 4:6. Unalichukuliaje jaribu hili? Je, anatilia shaka uungu wa Yesu? Je, anatilia shaka tumaini la Yesu kwa Mungu? Je, anamtaka Yesu awe na kiburi na kujiamini mno?

 

  1.     Soma Mathayo 4:7. Yesu alilielewaje jaribu hili?

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 6:16. Tunaona kwamba Yesu ananukuu kifungu hiki, lakini je, hii inatupatia utambuzi wowote wa hoja yake?

 

  1.     Soma Kutoka 17:1-2 na Kutoka 17:6-7. Sasa tunaweza kuona kile kinachozungumziwa kwenye Kumbukumbu la Torati 6:16. Je, hii ndio aina ya kumjaribu Mungu inayowasilishwa na Mathayo 4:6? (Jaribu la pale Masa lilihusu endapo Mungu alikuwa pamoja nao. Shetani alitilia shaka kama Yesu alikuwa “Mwana wa Mungu,” hivyo alikuwa anatilia shaka kama Mungu alikuwa na Yesu. Yesu alilielewa jaribu kwa namna hiyo na alilijibu kwa kifungu kilichojibu changamoto ya Shetani.)

 

  1.     Soma Mathayo 4:8-9. Unadhani Shetani anamaanisha nini anaposema, “Haya yote nitakupa?” (Yesu alikuja kuukomboa ulimwengu na kuuchukua tena kutoka kwa Shetani. Shetani anatoa zawadi isiyo na maumivu (bila msalaba) ya kuuchukua ulimwengu.)

 

   1.     Yesu alilielewaje jaribu hili?

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 6:13. Hiki ndicho kifungu ambacho inaonekana Yesu anakinukuu. Hii inatuambia nini kuhusu jinsi Mungu alivyokielewa kifungu hiki? (Hatuwezi kuchukulia njia rahisi kwa kuhatarisha utiifu wetu kwa Mungu.)

 

 1.   Yesu, Upendo, na Torati

 

  1.     Soma Mathayo 22:34-36. Kama ungeulizwa swali hili, na ukawa na Agano la Kale pekee la kulifikiria, ungejibuje?

 

  1.     Soma Mathayo 22:37-38. Je, hivi ndivyo ambavyo ungesema?

                                                 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 6:5-6 na Kumbukumbu la Torati 6:3. Kwa nini Yesu alichagua Kumbukumbu la Torati 6:5 dhidi ya Kumbukumbu la Torati 6:3 kwa jibu lake?

 

   1.     Kwa nini Yesu alinukuu Biblia badala ya kutoa jibu lake mwenyewe? (Hii inaonesha kwamba Yesu aliichukulia Biblia kama mamlaka.)

 

  1.     Hebu tuendelee na jibu la Yesu. Soma Mathayo 22:39. Je, jibu lako lingekuwa sawa na hili kutokana na uelewa wako wa Agano la Kale? Vipi kuhusu fundisho la “jicho kwa jicho” (Kutoka 21:24)?

 

  1.     Soma Mambo ya Walawi 19:18. Tunaona kwamba Yesu ananukuu sehemu ya kifungu hiki. Je, hii inakinzana na torati ya “jicho kwa jicho?”

 

   1.     Unadhani kwamba kuitafuta haki ni tofauti na kutafuta kulipiza kisasi au kuwa na kinyongo?

 

  1.     Hebu tusome Mambo ya Walawi 19:15-17 ili kuuelewa muktadha vizuri zaidi. Je, hii inakupa uelewa tofauti wa kauli ya Yesu kwenye kauli ya “mpende jirani yako kama nafsi yako?”

 

   1.     Unadhani Yesu aliielewa Mambo ya Walawi 19:18 kama ulivyoielewa?

 

  1.     Hebu tusome Mathayo 5:38-39. Nilipoangalia muktadha wa Mambo ya Walawi 19:18, nilidhani inamaanisha kwamba “jicho kwa jicho” inamaanisha haki, na hiyo inaendana na kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Haki ni tofauti na kisasi au kuwa na kinyongo. Hapa Yesu anafundisha nini? (Nadhani anasema kwamba hatuna haja ya kulazimisha haki zetu.)

 

   1.     Je, hii ni amri kwamba hatupaswi kulazimisha haki zetu? Ikiwa ndivyo, unaielezeaje Yohana 18:22-23? (Nadhani kusoma kifungu hiki kwa haki kabisa ni kwamba Yesu alipinga kupigwa kofi. Hata hivyo, katika muktadha mpana, Yesu alikuwa “hapingi” kwa sababu angeweza kuziita mbingu zishuke ili kuwaangamiza maadui wake wakati ule ule. Lakini, hii inaashiria kwamba Yesu anatoa “namna bora” ya maoni juu ya kupinga na bila kubainisha kwamba ni dhambi kuupinga uovu.)

 

  1.     Soma Mathayo 22:40. “Torati yote na manabii” ni kitu gani? (Agano la Kale!)

 

   1.     Tafakari kidogo jibu lote la Yesu (Mathayo 22:36-40). Jibu lake linasisitiza nini? (Upendo.)

 

    1.     Je, kwa upande wako utasema kwamba “upendo” ndio mada kuu ya Agano la Kale?

 

   1.     Fikiria swali ambalo Yesu analijibu, “Ni amri ipi iliyo kuu?” Je, hiyo inamaanisha kwamba kila kilichosemwa na kutekelezwa kwa maelekezo ya Mungu katika Agano la Kale ni kitendo cha upendo? Angalia, kwa mfano, Mambo ya Walawi 24:16 na Mambo ya Walawi 20:27. (Hamasa iliyo nyuma ya Agano la Kale ni upendo kwa Mungu na upendo miongoni mwetu. Hiyo haizuii utawala wa sheria au adhabu. Mambo hayo ni sehemu ya muhimu ya upendo.)

 

 1. Chanzo cha Yesu kwa Maswali ya Sabato

 

  1.     Soma Mathayo 12:1-2. Sehemu gani ya matendo ya wanafunzi si halali? Kula masuke ya mtu mwingine (yasiyo yako)? Kuvunja na kula masuke siku ya Sabato? (Kwa dhahania shtaka sio la wizi, kwa sababu hilo litakuwa kosa likitendeka siku yoyote ile. Lazima shtaka litakuwa ni kuvunja masuke siku ya Sabato.)

 

   1.     Unadhani wanafunzi waliyachukulia matendo yao kuwa ni makosa? Au, walikuwa tu na njaa na hawakujali chochote?

 

  1.     Soma Mathayo 12:3-4. Una maoni gani juu ya jibu la Yesu kwamba Daudi pia alitenda jambo lisilo halali alipokuwa na njaa? Vipi endapo wanafunzi wangekuwa wanafanya uzinzi, je, rejea ya Daudi lingekuwa jibu sahihi?

 

   1.     Utaona kwamba Yesu anasema kuwa kula mikate “haikuwa halali.” Je, Yesu anaitumia Biblia kama mamlaka yake? (Hebu tuendelee kusoma.)

 

  1.     Soma Mathayo 12:6-8 na Hosea 6:6. Hosea sura ya 6 inawahusu watu wa Mungu baada ya kuadhibiwa vikali kwa kugeuka na kumwacha Mungu. Yesu anatoa maana gani kwenye maneno haya katika Hosea? (Kama Mafarisayo walimkiri Yesu kama Masihi, na hawakumgeuka, wangeyatambua mamlaka yake aliposema juu ya kilicho sahihi siku ya Sabato. Yesu ni Bwana wa Sabato na anaamua kipi kilicho sahihi.)

 

  1.     Nimeruka Mathayo 12:5. Isome. Je, kimsingi makuhani “wanainajisi” Sabato? (Yesu anasema kwamba “hawana hatia.”)

 

   1.     Yesu anatufundisha nini kuhusu Sabato? (Rehema, kutenda mambo ya msingi ili kuutangaza ufalme wa Mungu, ndio thamani kuu.)

 

  1.     Soma Marko 2:27-28 kwa ajili ya maoni ya ziada yaliyotolewa na Yesu. “Thamani kuu” ni ipi katika kisa hiki cha wanafunzi kuvunja masuke siku ya Sabato? (Kuwaweka wanadamu kuwa wa thamani kuliko Sabato. Lengo la Sabato ni kuwa baraka kwa ajili yetu. Hivyo, kuwaonesha rehema wanafunzi wenye njaa siku ya Sabato ndio njia sahihi ya kuitazamia Sabato.)

 

  1.     Rafiki, unaona jinsi Yesu alivyoitumia Biblia kujibu majaribu na changamoto? Aliichukulia Biblia kama kitabu chenye mamlaka, nasi pia tunapaswa kuichukulia vivyo hivyo. Je, utaichukulia na kuikiri Biblia kama mamlaka maishani mwako?

 

 1.   Juma lijalo: Biblia – Chanzo Chenye Mamlaka cha Teolojia Yetu.