Somo la 5: Kwa Maandiko Pekee – Sola Scriptura

(1 Wakorintho 4, Tito 1, Mathayo 19)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, umewahi kufikiria jinsi unavyoielewa Biblia? Nina mashaka kama kuna mtu ambaye katika hali ya kawaida ataitumia Biblia pekee ili kuielewa vizuri. Uelewa wangu juu ya kile ambacho Biblia inakifundisha kuhusu Mungu uliongezeka pale nilipokuwa mzazi. Mambo ya asili hunifundisha habari za Mungu. Katika masomo haya mara kwa mara huwa ninabainisha kwamba nimekuwa nikisoma maoni ya watu wengine ili kuelewa kifungu fulani cha Biblia vizuri zaidi. Dhana nzima ya kuwa na mwalimu inamaanisha kwamba uelewa au mtazamo wa mtu mwingine ni mwongozo wa kujifunza. Ni nini basi kinachomaanishwa tunaposema “Sola Scriptura,” yaani “Biblia pekee?” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.     Zaidi ya Kile Kilichoandikwa

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 4:1. Paulo anatoa ushauri kwenye jambo gani? (Jinsi ya kuwazingatia waalimu wa Biblia.)

 

   1.     Inamaanisha nini kusema kwamba Paulo (na wengine) wamekabidhiwa kuwa “mawakili wa siri za Mungu?” (Wana uelewa wa kina kuhusu Mungu.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 4:2. Nini kinatakiwa kwa wale waliokabidhiwa siri za Mungyu? (Wanatakiwa kuwa waaminifu.)

 

   1.     Nani anayebainisha uaminifu wao?

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 4:3-5. Paulo anasema kuwa nani anapaswa kutoa hiyo hukumu? (Anasema kuwa sote tutatoa hukumu, lakini hukumu ya Mungu ndio ya mwisho.)

 

   1.     Je, walimu wana agenda ya siri? (Miezi kadhaa iliyopita mmojawapo wa washauri wangu wa kuaminika kabisa alilalamika kwamba mitazamo yangu ya kisiasa ilikuwa inashawishi ufundishaji wangu. Mambo mengi yalitoa ushawishi katika ufundishaji wangu – uelewa wangu wa nyuma wa Biblia, uzoefu wangu, mafundisho yangu kwa watu wengine, mitazamo yangu ya kiuchumi na kisiasa. Bila shaka hii ni dhana ya kweli kwa walimu ulimwenguni kote. Paulo anashauri kwamba tuwe makini.)

 

   1.     Angalia tena 1 Wakorintho 4:4. Kama ilivyo kwa Paulo, ninapofundisha huwa ninapenda kuamini kwamba “dhamiri yangu haina wasiwasi.” Lengo langu ni kukufanya uelewe neno la Mungu vizuri. Paulo anamaanisha nini anapoandika, “hiyo hainifanyi nisiwe na hatia?” (Mwalimu mwaminifu anapaswa kutambua kwamba msingi wa makuzi na uelewa wetu na upendelevu wetu vinaongoza ufundishaji wetu.)

 

   1.     Angalia tena 1 Wakorintho 4:5. Paulo anapendekeza kwamba sote tutoe hukumu, lakini kisha anasema, “msihukumu neno kabla ya wakati wake.”

 

    1.     “Wakati wake” ni upi? (Ujio wa Yesu Mara ya Pili.”)

 

    1.     Je, hiyo inaleta mantiki yoyote? Kwa nini tusitoe hukumu kwenye usahihi, nia, na uaminifu wa mwalimu? (Nadhani anachokimaanisha Paulo ni kwamba Mungu pekee ndiye anayeweza kujua nia za mwalimu kwa usahihi kabisa. Katika 2 Petro 2:1 tunaonywa juu ya waalimu wa uongo. Akili ya kawaida inatuelekeza kuwaepuka.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 4:6. Kwa utangulizi huu, unadhani Paulo anatuambia nini anapoandika “mjifunze kutopita yale yaliyoandikwa?” (Anatuambia tusiamini hulka pendelevu ya waalimu na tuzingatie vifungu vya Biblia. Ukweli mkuu ndio wa muhimu, na si “hadithi za kutunga” za waalimu.)

 

   1.     Paulo ananukuu jambo. Majuma mawili yaliyopita tuliangalia chanzo cha kile ambacho Yesu alikinukuu alipokabiliana na majaribu na maswali. Je, hii inaakisi jambo kwenye Agano la Kale? (Hakuna mwanamaoni hata mmoja niliyemsoma aliyekuwa na chanzo cha dhahiri kwenye nukuu hii. Mwanamaoni mmoja alipendekeza kwamba maoni ya Paulo ni mwendelezo wa kauli zake za awali katika 1 Wakorintho 1:19, 1 Wakorintho 3:20 na 1 Wakorintho 1:31.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 4:7. Je, kuna mawazo yoyote halisi? Paulo anapendekeza nini linapokuja suala la waalimu? (Anasema kwamba waalimu wote wanajifunza kutoka kwa wengine. Hawapaswi kudai kwamba wana fundisho “jipya” na hivyo kuwa bora kuliko waalimu wengine.)

 

   1.     Je, hii ni kweli? Huna mawazo halisi? (Nina mawazo ya aina nyingi sana halisi. Lakini, kuhitimisha kwamba mimi ndio wa kwanza kuwaza jambo fulani ni upumbavu. Mtu anawezaje kujua walichokifikiria watu wengine wote katika kipindi chote cha historia?)

 

   1.     Bado ninahangaishwa na maelekezo ya “usihukumu chochote.” Je, sasa una uelewa mzuri zaidi wa jambo hili kwa kuzingatia kwamba tumezingatia vifungu vingine? (Kama msingi wetu ni Biblia, inaleta mantiki kupunguza ukosoaji kwa mwalimu.)

 

   1.     Endapo ungeweza kuandika juu ya vifungu hivi kwa ufupi, ungefanyaje? (Usiweke tumaini kubwa sana kwa waalimu. Wana upendelevu (upendeleo) na wao si chanzo halisi cha mawazo. Badala yake, tunapaswa kuweka tumaini letu kwenye Biblia ambayo inawakilisha mawazo ya Mungu.)

 

 1.   Shikilia kwa Umadhubuti

 

  1.     Soma Tito 1:7-8. Paulo anaandika kuhusu ofisi ya “askofu” kanisani. Askofu anatakiwa kuwa na vigezo gani?

 

  1.     Soma Tito 1:9. Je, Paulo anahamasisha mafundisho ya kimapokeo? Tunalinganishaje jambo hili na kupuuzia umuhimu wa waalimu na kuitegemea Biblia pekee?

 

   1.     Angalia maneno yasemayo “neno la imani.” Hiyo inatulizaje dhana ya kushikilia kwa umadhubuti mafundisho ya nyuma?

 

  1.     Soma Tito 1:10. Jiweke kwenye nafasi ya Paulo. Je, tohara ni ujumbe wa kimapokeo, uliotolewa na Mungu na kutekelezwa kivitendo na watu wa Mungu kihistoria? Nani aliye mwasi linapokuja suala la tohara? (Ningekuwa ninaunga mkono tohara, na nikamsikia Paulo akimwambia Tito jambo hili, ningeshtuka. Paulo alikuwa anajaribu kubadili jinsi hali ilivyo.)

 

   1.     Hii inatufundisha nini kuhusu “waasi” “wenye maneno yasiyo na maana na wadanganyaji?” Je, hii inamaanisha kwamba Paulo hajitambui? Au, kung’ang’ania “neno la imani” inaweza isiwe sawa na kun’ang’ania ujumbe wa kihistoria?

 

  1.     Soma Tito 1:11. Hapa inaonekana Paulo sio tu kwamba anawahukumu waalimu wengine, bali pia anawaelekeza waumini “kuwanyamazisha.” Unapatanishaje (unalinganishaje) maelekezo haya?

 

   1.     Ni njia ipi nzuri ya kuaminika ya kuhukumu nia? (Endapo mwalimu ananufaika kutokana na fundisho lake kwa njia isiyo ya uaminifu.)

 

  1.     Soma Tito 1:12-14. Hili ndilo neno lako jipya kwa juma hili: “walafi” – “wavivu.” Haya ndio maneno anayoyatumia Albert Barnes kuelezea “walafi wavivu.” Sasa unayaelewaje maelekezo ya Paulo kuhusu kutowahukumu walafi? (Kuangalia namna ya kuzichukulia kauli zote za Paulo kama ni za kweli, lazima itakuwa alimaanisha kwamba tunatakiwa kusubiria ujio wa Yesu Mara ya Pili kwa ajili ya hukumu ya kweli kwa waalimu.)

 

   1.     Je, viwango vya leo vya usahihi wa kisiasa vinaweza kuhimili njia ya Paulo hapa?

 

 1. Mwanzo

 

  1.     Soma Mathayo 19:3. Ni nini asili ya jaribu la Mafarisayo?

 

  1.     Soma Mathayo 19:4-5. Yesu anageukia chanzo gani chenye mamlaka katika kujibu jaribu hili? (Maelezo ya kitabu cha Mwanzo.)

 

   1.     Hii inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Yesu juu ya nadharia ya uibukaji wa mianzo? (Anathibitisha kwamba si kweli. Wanaume na wanawake hawakuibuka. Waliumbwa kama watu wazima.)

 

   1.     Hii inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Yesu juu ya ndoa? (Ndoa ni kati ya mwanaume na mwanamke kwa sababu wameumbwa ili wazaliane.)

 

  1.     Soma Mathayo 19:6. Yesu anatumia maelezo ya uumbaji kutatua mgogoro wa kimaandiko. Je, jambo hilo linatosha kwetu leo katika kutatua migogoro ya kimaandiko?

 

  1.     Soma Mathayo 19:7. Sasa tunaingia kwenye mgongano. Musa ana fundisho tofauti la kimapokeo. Hapa mwasi ni nani? Nani anayejaribu kubadili hali kama jinsi ilivyo?

 

   1.     Unapotafakari maswali haya, rejea nyuma kwenye swali langu la msingi kwenye sehemu hii: Ni nini asili ya jaribu la Mafarisayo? ikiwa amri ya Musa ni ya dhahiri, ni kwa namna gani hili ni jaribu? (Lazima palikuwepo na mgogoro kwenye jambo hili. Vinginevyo, lisingekuwa jaribu.)

 

  1.     Soma Mathayo 19:8-9. Je, Yesu anasema kwamba uzinzi “uliruhusiwa” na Musa kwa kuwa watu walikuwa na mioyo migumu?

 

   1.     Musa si aina fulani hivi ya mtu wa kishetani. Bali alikuwa kiongozi maalum wa Mungu. Hii inatufundisha nini kuhusu mapokeo yanayochipukia kutoka kwa viongozi wazuri? Hii inazungumzia nini kuhusu neema ya Mungu?

 

   1.     Tunajifunza nini kuhusu ufasiri wa Maandiko kutokana na anachokisema Yesu hapa? (Kwa jibu sahihi tunatakiwa kurejea nyuma kwenye Biblia na kuifanya kuwa juu ya mafundisho/mapokeo hata kama ni ya wafuasi wakubwa wa Mungu. Sola Scriptura!)

 

  1.     Rafiki, je, utaifanya Biblia kuwa chanzo chako kikuu cha kumwelewa Mungu? Nadhani si vibaya kufuatilia ushauri wa kimapokeo, wasomi wa kale, na waalimu wa leo. Hata hivyo, hatimaye wote hao wanatakiwa kujaribiwa kwa viwango vya Biblia. Je, utakubali kutumia njia hiyo leo?

 

 1.   Juma lijalo: Kwa Nini Ufasiri Unahitajika?