Somo la 7: Lugha, Kifungu na Muktadha

Somo la 7: Lugha, Kifungu na Muktadha
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Chukulia kwamba una mtoto ambaye hujawahi kukutana naye. Unayo fursa ya kuwasiliana na mtoto huyo kwa njia ya barua. Utamwambia nini mtoto huyo? Utaamuaje kwamba kipi cha muhimu kabisa cha kukisema? Je, utatumia lugha ambayo ni rahisi kueleweka? Je, unaweza kuwa na wasiwasi kwamba mtoto wako anaweza asielewe muktadha wa maandishi yako? Haya ndio mambo ambayo Mungu alikabiliana nayo alipoivuvia Biblia. Huenda ili kuthibitisha kwamba barua pekee haitoshi, Mungu alimtuma Mwanaye ili kutusaidia kuielewa barua yake vizuri zaidi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuelewe vizuri zaidi fikra ya Mungu katika kutupatia Biblia!

 

 1.     Lengo

 

  1.     Soma 2 Timotheo 3:16. Unapotafakari maneno haya: “mafundisho, kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwaadibisha,” mambo gani ya kawaida yanakujia mawazoni mwako? (Ukuaji na mabadiliko.)

 

   1.     Hiyo inatufundisha nini kuhusu dhamira ya Mungu kwenye barua yake kwa wanadamu?

 

   1.     Hiyo inatoa dhana gani kuhusu wanadamu? (Mungu alidhamiria Biblia ilete mabadiliko kwa wanadamu. Tunapaswa kurekebisha uelekeo wetu na kujifunza zaidi juu ya lengo la Mungu maishani mwetu.)

 

  1.     Soma 2 Timotheo 3:17. Lengo la Mungu maishani mwetu ni lipi? (Kutenda matendo mema na kuyatenda kwa ukamilifu.)

 

   1.     Angalia maneno “kukamilishwa kikamilifu.” Unajisikiaje unapotengeneza kitu au kukipachika kitu hicho mahala fulani na huna zana sahihi?

 

    1.     Je, umetafakari kwamba Mungu anataka kukupatia zana bora kwa ajili ya kutenda jambo kwa uzuri? Uelewa mzuri wa Biblia unatufanya tuwe na ufanisi zaidi.

 

   1.     Hiyo inatuhabarishaje juu ya imani yetu katika haki kwa njia ya neema pekee? (Kwa dhahiri Mungu anatamani tutende matendo mema na tuyatende vizuri. Matendo yetu ni ya muhimu kwa Mungu.)

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 32:46. Tuliangalia kifungu hiki hivi karibuni. Ni lipi lililo mojawapo ya matendo ya muhimu kabisa kwetu? (Kuwafundisha watoto wetu mapenzi ya Mungu.)

 

   1.     Tunatendaje jambo hili? Mmojawapo wa wacha Mungu ninaowafahamu katika maisha yangu ana mtoto ambaye, nadhani ni sawa kusema hivyo, ni adui wa injili. Wajukuu wake wanaonekana kumwacha Mungu mbali zaidi kuliko hata mwanaye.

 

    1.     Baada ya kifo cha huyu mcha Mungu, niliamua “kutatua” jambo hili. Nilidhamiria kumwongoa kijana huyu. Nilishindwa vibaya sana! Kijana huyu alipiga hatua kutoka kutokuwa na upande wowote kunihusu mimi (neutral) hadi kunichukia. Nadhani nilipungukiwa zana sahihi. Una maoni gani?

 

   1.     Wazazi wangu walitumia fedha nyingi sana kuwapeleka watoto wao kwenye shule ya kanisa. Matokeo yake ni kwamba asilimia fulani ya watoto wao ni waasi dhidi ya kanisa. Jambo gani halikwenda sawa? Tunaweza kujifunza nini kutokana na jambo hili?

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 32:47. Kuna umuhimu gani wa kuwafundisha watoto wetu kanuni za Kibiblia? (Zinayaathiri maisha yao hapa duniani na ni muhimu sana kwa ajili ya maisha ya milele.)

 

   1.     Mojawapo ya malalamiko ya shule ya kanisa ni kwamba ilitekeleza kanuni nyingi zisizo na msingi na za kidikteta. Ikiwa lengo la kuwafundisha watoto wetu ni kuwasaidia kuwa na maisha bora, je, tunapaswa kujaribisha kanuni zetu kwa kuuliza endapo kanuni ni ya muhimu kwa ajili ya kuishi maisha sahihi? Je, hili ni eneo ambalo tunahitaji “zana” bora? Hebu tuangalie hilo katika sehemu inayofuata.

 

 1.   Mtazamo wa Kufundisha?

 

  1.     Soma 1 Wafalme 3:5-6. Sulemani anasema Mungu alikuwa na mtazamo wa namna gani dhidi ya Daudi? (Mungu alikuwa mwema.)

 

   1.     Ni muhimu kiasi gani kufundisha utu wema kwa watoto wetu?

 

    1.     Ikiwa wewe ni mzazi, unafanya jambo gani ili kufundisha utu wema kwa watoto wako?

 

   1.     Mungu alifundishaje jambo hili kwa Mfalme Daudi? (Tunapoyatafakari maisha ya Daudi, utu wema si jambo la kwanza linalotujia akilini.)

 

    1.     Unaelezeaje jambo hili – kwamba maisha ya Daudi hayaakisi wema wa Mungu? (Uwezekano wa majibu mawili unanijia akilini. Kwanza, kwamba wema wa Mungu ulivumilia baadhi ya tabia mbaya kwa upande wa Daudi. Pili, tunaweza tusiwe tunamwelewa Daudi kwa usahihi.)

 

  1.     Angalia tena 1 Wafalme 3:6. Sulemani hamwiti baba yake “mwema,” bali anamwelezea Daudi kama “mwenye haki na unyofu wa moyo.” Je, unaliona jambo hilo kuwa ni sahihi?

 

   1.     Je, kuna tofauti kati ya matendo yetu na kilicho mioyoni mwetu? (Angalia Warumi 8:5.)

 

   1.     Je, tunapaswa kuwafundisha watoto wetu masomo ya mioyo? Ikiwa ndivyo, tunawafundishaje?

 

  1.     Soma Hesabu 6:22-23. Haruni na wanawe ni akina nani? (Makuhani. Wale waliokuwa waamuzi kati ya watu na Mungu.)

 

  1.     Soma Hesabu 6:24-26. Mungu anawaambia nini watu wake?

 

   1.     Ni mitazamo gani chanya inayopaswa kuwa matokeo ya baraka hii? (Kuwa na tumaini kwamba Mungu “atatulinda.” Tutatiwa moyo kwamba Mungu atatutabasamia (“atatuangazia nuru ya uso wake”) na kuwa mwema kwetu. Tutakuwa na ujasiri kwamba Mungu anatuangalia kiasi kwamba anajua kila kitu kinachotokea maishani mwetu.)

 

    1.     Je, hivi ndivyo unavyomtazama Mungu? Je, mitazamo hii inaakisiwa maishani mwako? Je, umewafundisha watoto wako kwamba huu ndio mtazamo wa Mungu kwao?

 

     1.   Utaona kwamba jambo la mwisho lililotajwa ni “amani.” Kama uliyaelewa mambo ya awali yaliyosemwa kuhusu mtazamo wa Mungu kwako, je, matokeo ya kawaida ni kwamba utakuwa na amani?

 

   1.     Je, mitazamo hii ni “zana” bora tunazozitumia kuwafundisha watoto wetu masomo ya mioyo?

 

   1.     Unadhani Mungu alikuwa na lengo gani kwa kuandika juu ya mitazamo hii?

 

  1.     Soma Hesabu 6:27. Inamaanisha nini kuliweka jina la Mungu juu ya wana wa Israeli? (Nadhani inamaanisha kuwa wataakisi tabia ya Mungu, ambao matokeo yake ni baraka juu yao.)

 

 1. Angalia Jambo Hili

 

  1.     Soma Mwanzo 1:26-27. Dhana gani inarudiwa mara tatu katika vifungu hivi? (Vitu viwili vinarudiwa. Kwanza, tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Pili, Mungu alitutengeneza, “alituumba.”)

 

   1.     Kwa nini maneno haya yanarudiwa? Je, Musa ni mwandishi ambaye hawezi kwenda kwenye ujumbe moja kwa moja? (Kurudiarudia ndio njia ambayo waandishi wa Biblia wanaitumia kusisitiza jambo.)

 

   1.     Mungu anatufundisha nini kwa msisitizo huu? (Mungu alitudhamiria tuwe kama yeye! Wanadamu ni wa pekee kwa sababu wana uwezo wa kutengeneza vitu kutokana na uwezo wao mkubwa wa kufikiri.)

 

    1.     Hiyo inaashiria nini kuhusu namna tunayopaswa kuishi?

 

  1.     Hebu turejee nyuma na tusome Mwanzo 1:25. Angalia vifungu vitatu hapa: Mwanzo 1:25-27. Je, kuna kitu katika namna ambayo hivi vifungu vitatu vimepangiliwa, jambo linalotufundisha zaidi kuliko jinsi vilivyoandikwa? (Muktadha unatuonesha uhusiano. Wanadamu wana sifa zinazofanana na Mungu zaidi kuliko wanyama, hivyo wana nafasi ya juu duniani. Mungu aliwaumba wanadamu “kwa sura na mfano wake,” hivyo tuna hadhi ya pekee, lakini hadhi hiyo ni ya chini kuliko ile ya Mungu.)

 

   1.     Unaweka umuhimu gani kwenye kauli ya kwamba Mungu aliwaumba “mwanamune na mwanamke?” Je, Mungu anafikisha ujumbe kuhusu uumbaji wake? Je, kuna cha kujifunza kutokana na muktadha huu? (Huu ni ubunifu mkuu wa Mungu.)

 

   1.     Nimekuwa mla mbogamboga (vegetarian) katika miaka yote ya utu uzima wangu. Ninaamini Biblia inatufundisha kuwa wema kwa wanyama. Angalia Kutoka 20:10. Kuna maoni miongoni mwa baadhi ya wala mbogamboga kwamba wanyama hawapaswi kuliwa au kutendewa tofauti na wanadamu. Je, hii inaendana na ubunifu mkuu wa Mungu? Tunapaswa kuwa na mtazamo gani kwa wanadamu wenzetu? (Wanadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanadamu hawakuumbwa hivyo. Tunatakiwa kuelewa mpangilio huu wa mambo kwa sababu bila mpangilio huo hatuwaheshimu wanadamu wenzetu inavyotakiwa.)

 

  1.     Rafiki, je, unauelewa vizuri ujumbe wa Mungu kwako? Je, unatamani kuwa na zana bora za kuutangaza Ufalme wa Mungu? Kwa nini usimkaribishe Roho Mtakatifu akusaidie ili uweze kusonga mbele katika kuakisi mitazamo ya Mungu?

 

 1.   Juma lijalo: Uumbaji: Mwanzo Kama Msingi – Sehemu ya Kwanza.