Somo la 8: Uumbaji: Mwanzo Kama Msingi – Sehemu ya 1

Error message

Deprecated function: implode(): Passing glue string after array is deprecated. Swap the parameters in drupal_get_feeds() (line 394 of /home/krwester/gobibletranslations.org/includes/common.inc).
(Mwanzo 1 & 2, Yohana 1, Ufunuo 14)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tumekuwa tukiangalia kitabu cha Mwanzo katika masomo machache yaliyopita, lakini juma hili tutaingia kwa kina zaidi kwenye Uumbaji na ma-hitimisho yanayofuatia kutokana na Uumbaji huo. Kutafsiri kitabu cha Mwanzo kama historia, tofauti na analojia, au kibaya zaidi uzushi, ni muhimu kwa ajili ya tafsiri sahihi ya Biblia. Hebu tuchimbue mada hii kupitia kwenye somo letu la Biblia juma hili!

 

 1.     Mwanzo

 

  1.     Soma Mwanzo 1:1. Hapa unaona taarifa gani ya muhimu? (Kwamba mbingu na nchi zilikuwa na Mwanzo. Ziliumbwa kwa uwezo wa Mungu.)

 

  1.     Soma Yohana 1:1. Ni nani aliyekuwa na Mungu katika tukio hili? (Soma Yohana 1:14. Hii inaelezea kwamba Yesu ndiye “Neno” na kwamba Yesu alikuwa na Mungu na yeye ni Mungu. Kimsingi hii ni hoja yenye mashiko kwa ajili ya uelewa wetu wa Utatu Mtakatifu.)

 

  1.     Soma Yohana 1:2-3. Hii inatupatia ufafanuzi gani wa ziada kuhusu Uumbaji? (Kwamba Mungu (Yesu) “alifanya” “vitu vyote.”)

 

  1.     Soma Zaburi 19:1-2. Hii inasema nini kuhusu uthibitisho wa kile Biblia inachokisema? (Inatuambia kwamba “mbingu zauhubiri” na “anga laitangaza kazi ya mikono yake.”)

 

   1.     Je, hii ni kweli? Je, uelewa wa falaki na astrofizikia (sayansi ya hali ya nyota kikemikali na kimaumbile) vinathibitisha kile ambacho Mwanzo 1 na Yohana 1 zinakisimulia? (Ndiyo! Wanafalaki walibaini kuwa nyota ni “red shifted.” Sote tunaelewa kwamba mwendo wa vitu huathiri mawimbi ya sauti. Ukisimama karibu na reli sauti hubadilika kadri gari moshi (treni) linavyokaribia na kisha sauti hiyo hukuacha. Mawimbi ya sauti “yanasongana” kadri teni inavyokaribia na “yanajiendeleza” treni inapokwenda mbali. Vivyo hivyo kwa mawimbi ya mwanga. Kwa kuchunguza mawimbi ya mwanga wanasayansi waliweza kueleza kwamba ulimwengu ulikuwa unatanuka taratibu katika pande zote. Hiyo ilimaanisha kuwa ulimwengu ulikuwa na asili yake, mwanzo ambao unapaswa kuukokotoa.)

 

  1.     Ikiwa sayansi na Biblia vinatuambia kuwa mbingu na nchi zilikuwa na mwanzo, je, tunapaswa kuukubali ukweli huu?

 

 1.   Siku za Uumbaji

 

  1.     Soma Mwanzo 1:3-5. Siku hii ilikuwa na urefu gani kwa jinsi Musa (akivuviwa na Roho Mtakatifu) alivyoielezea? (Wanadamu wanaelewa “jioni na asubuhi” kuelezea kipindi cha saa 24.)

 

   1.     Je, maelezo haya yanaonekana kama analojia? (Maelezo haya yako mahsusi sana. Hitimisho lenye mantiki ni kwamba tunazungumzia siku halisi.)

 

  1.     Soma Mwanzo 1:14. Hapa ni baadaye katika Uumbaji. Ni nini lengo la “mianga katika anga la mbingu” (“Kuwa ishara ya nyakati takatifu.” Zimewekwa kama watunza muda.)

 

   1.     Hiyo inaashiria nini kuhusu ile “jioni na asubuhi” ya awali? (Inasababisha mashaka kidogo mawazoni mwangu. Kwa upande mmoja, utunzaji muda ulikuja baadaye. Kwa upande mwingine, maelezo ya awali yanaonekana kutazamia uumbaji wa watunza muda.)

 

  1.     Soma Mwanzo 2:4 katika tafsiri ya KJV au ESV. Kiebrania kinatumia neno “yom” ambalo tafsiri zote mbili za KJV na ESV zinalitafsiri kama “siku.” Tafsiri ya NIV inahafifisha neno hili kwa kulitafsiri kama “lini.” Hili ni neno lile lile la Kiebrania linalotumika vile vile katika sura mbili za kwanza za kitabu cha Mwanzo kumaanisha “siku.” Hapa “siku” (yom) ina urefu gani? (Hapa inamaanisha angalao siku sita. Kitabu cha Mwanzo sura ya 1 & 2 kina maelezo yote ya uumbaji. Ukiichukulia Biblia kiuhalisia, na ukaona kwamba “yom” “siku” inatumika kumaanisha kitu kingine zaidi ya saa 24 halisi, hiyo inaashiria nini kuhusu uelewa sahihi wa “yom?” (Inamaanisha inaweza isiwe na ukomo wa saa 24.)

 

   1.     Je, kuna sababu yoyote nzuri ya kuzichukulia “siku ndefu” katika Uumbaji? (Ikiwa sababu ni kujumuisha nadharia ya uibukaji, jibu ni “Hapana,” kwa sababu nadharia hiyo inakinzana moja kwa moja na maelezo ya Uumbaji. Lakini, kama sababu ni kufungamanisha ufunuo wa Mungu katika Biblia na ufunuo wa Mungu katika mambo ya asili, basi hii inaonekana kuwa sababu halali ya kutafakari dhana hii.)

 

  1.     Pitia kwa haraka haraka Mwanzo 1. Je, siku zote sita zimefafanuliwa kama “jioni na asubuhi?” (Ndiyo.)

 

   1.     Hii inaashiria nini kwetu? (Inaashiria kwamba hizo ni siku halisi zenye saa 24. Nadhani hoja bora zaidi ni kwamba siku za Uumbaji ni siku halisi zenye saa 24. Lakini, sina imani kali kuhusu jambo hili kwa sababu kuna hoja yenye mantiki iliyojengwa juu ya usomaji halisi wa Biblia kwamba “yom” inaweza kumaanisha zaidi ya saa 24.)

 

 1. Sabato

 

  1.     Hebu tujiulize swali ambalo inawezekana kweli linamhangaisha msomaji. Vipi kama siku zote za Uumbaji si siku halisi zenye saa 24, hii inaiathirije Sabato? (Angalia Mwanzo 2:1-3)? (Sidhani kama inahafifisha utunzaji wa Sabato kwa namna yoyote. Bado Sabato ni ukumbusho wa Uumbaji. Bado Kutoka 20 inaelekeza kwamba utunzaji huu uwe kwenye “siku ya saba” halisi.)

 

  1.     Soma Ufunuo 14:6-7. Maelezo ya Uumbaji ni ya muhimu kiasi gani kwenye injili? (Kifungu hiki kinaarifu kwamba malaika anahubiri “injili ya milele” kwa wanadamu. Mwanzo wa injili ni kumwabudu Mungu Muumbaji wetu.)

 

  1.     Soma Marko 2:27-28. Kama mtu alifanyika kwa ajili ya Sabato, kanuni za aina gani za utunzaji wa Sabato ni sahihi?

 

   1.     Kama Sabato ilifanyika kwa ajili ya wanadamu, ukichukulia maelezo ya kitabu cha Mwanzo, njia gani ya utunzaji wa Sabato ni sahihi?

 

  1.     Soma Isaya 58:13-14. Tunawezaje kuiita Sabato kuwa ya “kupendeza” wakati hatuwezi kutenda kilicho cha furaha?

 

   1.     Je, Isaya anahitajika kufanya mkutano na Yesu ili kujadiliana naye na kufikia hitimisho moja juu ya kile inachomaanisha kwa Sabato kufanyika kwa ajili ya wanadamu? (Utaona kwamba Isaya anairejelea Sabato kama “siku takatifu.” Nadhani hilo linatusaidia kuelewa. Tunaweza kufurahia mambo yanayoendana na siku iliyotengwa kumsherehekea Mungu kama Muumbaji wetu.)

 

    1.     Je, jibu nililolipendekeza hivi punde linaendana na maoni ya Yesu kwamba Sabato ilifanyika kwa ajili ya wanadamu?

 

 1.   Ndoa

 

  1.     Soma Mwanzo 2:22-25. Unadhani inamaanisha nini kwa mwanamume na mwanamke kuwa “mwili mmoja?” (Soma Mathayo 19:4-6. Hii inazungumzia ndoa, na huenda kwa umahsusi zaidi, kuwa na watoto.)

 

  1.     Soma Mathayo 19:3. Tulijadili kisa hiki kwenye somo la nyuma kwenye mfululizo huu. Unadhani kwa nini Mafarisayo walitaka kufahamu kama jambo la pekee linaweza kutumika kwenye kanuni iliyopo katika kitabu cha Mwanzo?

 

   1.     Je, tunapaswa kuwa na mwitiko huo huo katika zama za leo kwa wale wanaotafuta sababu maalum kwa ajili ya ndoa kutokana na vigezo vilivyopo katika kitabu cha Mwanzo? (Yesu alikataa mapendekezo maalum yanayokinzana na kanuni.)

 

   1.     Leo tuna “Mafarisayo” wangapi wanaotafuta sababu maalum zinazokinzana na mfano wa kitabu cha Mwanzo kuhusu ndoa? (Mahakama Kuu ya Marekani imeshikilia msimammo kwamba ndoa kati ya watu wawili wa jinsia moja ni haki ya kikatiba. Watu wengi zaidi wanaishi pamoja bila kuwa na ndoa.)

 

 1.     Muhtasari

 

  1.     Angalia masuala muhimu katika kitabu cha Mwanzo ambayo tumekuwa tukiyajadili. Mangapi kati ya masuala haya yanashambuliwa na dunia ya kipagani katika zama za leo? (Yote yanashambuliwa vikali.)

 

   1.     Unadhani kwa nini hili ni kweli?

 

  1.     Soma tena Ufunuo 14:7. Kama tunayakataa maelezo ya Uumbaji, tuna uwezekano mkubwa kiasi gani kukataa dhana ya hukumu?

 

   1.     Ikiwa tunaamini kwamba uwepo wetu umetokana na bahati na matokeo ya asili, hiyo itaathirije utiifu wetu kwa Mungu? Hiyo itaathirije tamaa yetu ya kumpa utukufu?

 

   1.     Shambulizi hili la pamoja kwenye teolojia inayotokana na maelezo ya Uumbaji inaashiria nini kuhusu uwepo wa Shetani? (Inanifanya nitafakari kwamba mwanzilishi yuko vitani dhidi ya Mungu.)

 

  1.     Rafiki, je, utayaamini maelezo ya Uumbaji? Je, utakubali kile ambacho Mungu amekifunua kwetu kuhusu mianzo yetu na uhusiano wetu na Mungu? Ikiwa huna uhakika, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu afunue mawazo yako kupokea kweli ya Mungu?

 

 1.   Juma lijalo: Uumbaji: Mwanzo Kama Msingi – Sehemu ya 2.