Somo la 5: Ushuhudiaji Unaowezeshwa na Roho

(Matendo 1-2)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
3
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Ushuhudiaji Unaowezeshwa na Roho

 

(Matendo 1-2)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unajisikia kuwa na ukomo maishani? Kama ungekuwa mwerevu, mwenye mwonekano mzuri, mwenye karama ya kuzungumza, mzuri kwenye uhusiano, je, ungekuwa na ufanisi katika kazi yako? Juma lililopita tulijadili jinsi maombi yanavyotufikisha kwenye “uwezo wetu usio wa kawaida.” Juma hili tunajadili chanzo cha uwezo huo usio wa kawaida, Roho Mtakatifu. Ninaamini Roho Mtakatifu ananifanya kuwa bora zaidi ya jinsi nilivyo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu chanzo cha uwezo wetu usio wa kawaida!

 

 1.     Kutoka Upumbavuni

 

  1.     Soma Matendo 1:6. Yesu anapaa kwenda mbinguni na haya ni mazungumzo yake ya mwisho na wanafunzi wake. Utakumbuka kwamba tulijadili jambo hili majuma mawili yaliyopita. Je, inawezekana kwamba wanafunzi waliuliza swali lenye kukatisha tamaa zaidi?

 

  1.     Soma Matendo 1:3. Je, unadhani wanauelewa utume wao? Je, waliuelewa Ufalme wa Mungu? (Hiki ndicho kinachokatisha tamaa zaidi kwenye swali hili, inaonesha kwamba hawaelewi utume ulio mbele yao hata kama Yesu amekuwa akiuelezea (kwa mara nyingine) baada ya kufufuka kwake. Kibaya zaidi ni kwamba sasa Yesu anaondoka!)

 

   1.     Je, ni kweli kwamba wanafunzi ni wapumbavu? (Luka 24:25 inaelezea Yesu akitumia neno “mioyo mizito.” Tofauti na maneno yaliyopo kwenye kichwa cha habari, sidhani kama wanafunzi walikuwa na akili kidogo. Bali, walikuwa na mawazo yao kumhusu Masihi kiasi kwamba hawakutaka kuyaacha mawazo hayo.)

 

  1.     Soma Matendo 1:7-8. Je, ungetarajia kwamba wanafunzi wafahamu kila kitu?

 

   1.     Jambo gani lilikuwa la msingi kwao kufahamu? (Hawakuwa na haja ya kupata majibu yote, walichokihitaji ni Roho Mtakatifu.)

 

  1.     Soma Matendo 1:9. Je, Yesu alihitaji kupanda roketi? Au, je, alikuwa na usafiri wake binafsi?

 

   1.     Kama jibu lako ni “alikuwa na usafiri wake binafsi,” basi angeweza kuondoka muda wowote ambao angetaka, si ndivyo? Asingekuwa na haja ya ukomo wa muda, si ndivyo?

 

   1.     Kwa nini hakuchelewesha kidogo kuondoka kwake ili aweze kutoa fundisho la kufanya marekebisho kwa wanafunzi wake wenye mioyo mizito? (Alikuwa na uhakika wa uwezo wa Roho Mtakatifu kushughulikia hili tatizo kubwa.)

 

  1.     Soma Matendo 1:4-5. Kwa nini Yesu anamlinganisha Roho Mtakatifu na ubatizo?

 

   1.     Hii inatuambia nini kuhusu asili ya uhusiano wetu na Roho Mtakatifu? (Lengo ni kuzamishwa kikamilifu. Hatumwonji tu Roho Mtakatifu, tunatakiwa kuzama ndani ya Roho Mtakatifu.)

 

    1.     Unadhani inamaanisha nini kuzama katika Roho Mtakatifu?

 

  1.     Soma Matendo 1:14. Unadhani lengo la maombi yao ni lipi? (Lazima walikuwa wanaomba ili kwamba Yesu awapelekee kile alichokiahidi, Roho Mtakatifu. Ubashiri wangu ni kwamba waliomba ili wawe na uwezo wa kufanya naye kazi kikamilifu kama mashahidi.)

 

 1.   Ushuhudiaji Wenye Nguvu

 

  1.     Linganisha Matendo 1:13 na Matendo 2:1-2. Tunaambiwa kwamba walikuwa ndani ya nyumba Roho Mtakatifu alipowasili. Je, unadhani hii ni nyumba ile ile iliyozungumziwa katika Matendo 1:13? (Inaonekana kwamba ilikuwa nyumba ile ile ambamo walikuwa wanakaa na kuomba.)

 

   1.     Walikuwa wamekaa hapo kwa muda gani huku wakiomba? (Ukilinganisha Matendo 1:3 (siku 40) na Matendo 2:1 (Pentekoste ni siku 50 baada ya Pasaka), tunaona kwamba walikuwa wakisubiri kwa takriban siku kumi. Ungekuwa na hisia gani kama ungekuwepo pale? Je, ungechoshwa?

 

  1.     Soma Matendo 2:2-3. Kitu gani kilitokea kwa uchoshwaji wowote ambao ungeweza kuwa umetokea?

 

   1.     Unadhani kwa nini Roho Mtakatifu alikuja kwa njia hiyo yenye kuhitaji uzingativu?

 

  1.     Soma Matendo 2:4. Nani anayedhibiti mazungumzo ya wanafunzi? (Roho Mtakatifu.)

 

   1.     Hebu tupitie tena mjadala wetu kuhusu Matendo 1:6. Waliuliza swali la kipumbavu. Ni kwa jinsi gani karama hii kwa uhakika kabisa inalenga tatizo? (Sasa maongezi yao yanaongozwa na Roho Mtakatifu.)

 

    1.     Je, Roho Mtakatifu atayaongoza mazungumzo yako ili usiseme “mambo ya kipumbavu?”

 

  1.     Soma Matendo 2:5-6. Hii inajibuje swali nililoliuliza hapo awali kuhusu kuingia kwa roho Mtakatifu “kunakovuta uzingativu?” (Iliwafanya watu wasikilize. Iliwafanya watambue kwamba kuna jambo la pekee linaendelea.)

 

  1.     Hebu tujikite kwenye Matendo 2:6, sehemu ya mwisho. Lengo gani mahsusi linafikiwa na Roho Mtakatifu? (Kumfanya msikilizaji aelewe.)

 

   1.     Lengo lako la kwanza katika ushuhudiaji ni lipi? (Kueleweka. Ndio maana ninapinga matumizi ya tafsiri ya Biblia ambayo huwezi kuielewa.)

 

  1.     Soma Matendo 2:7-8. Ukomo gani wa wanafunzi unazungumziwa hapa? (Wanatarajiwa kuzungumza lugha moja pekee.)

 

   1.     Roho Mtakatifu amefanya nini kwenye kile walichokuwa wanakisema? (Matendo 2:4 inasema kuwa “walisema” kwa lugha nyingine. Matendo 2:6 inasema kuwa kila msikilizaji alisikia “kwa lugha yake aliyozaliwa nayo.”)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 14:20. Changamoto yetu katika ushuhudiaji ni ipi? (Kutumia akili ya kiutu uzima. Kutumia akili ya Mungu.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 14:21-22. Katika muktadha huu “unabii” unazungumzia jambo linaloweza kueleweka na “lugha” jambo lisiloeleweka na wengine. Tunaona fundisho gani la ziada kuhusu kushuhudia kwa njia ya wazi na inayoeleweka? (Tunatakiwa kueleweka vizuri tunaposhuhudia. Lakini, hata pale tunapoeleweka, baadhi hawatasikiliza.)

 

  1.     Hebu turejee kwenye Matendo 2. Soma Matendo 2:12-13. Je, madai ya kwamba wanafunzi wamelewa lina mantiki yoyote? (Huwi fasaha zaidi unapokuwa umelewa.)

 

  1.     Hebu turuke vifungu kadhaa. Soma Matendo 2:32-33. Petro anasema kuwa watu wanaona na kusikia nini? Je, ni ulevi? (Hapana. Ni ahadi ya Roho Mtakatifu ndio inayomwagwa.)

 

 1. Nguvu Katika Zama za Leo

 

  1.     Soma Matendo 2:15-17. Petro ananukuu vifungu vya mwisho vya Yoeli 2. Kauli ya Petro kwamba Yoeli 2 ilikuwa inatimizwa inatufundisha nini kuhusu ushuhudiaji leo? (Ikiwa matukio yaliyopo katika Matendo 2 yapo “katika siku za mwisho,” basi kwa dhahiri tunaishi katika siku za mwisho. Nguvu hii ipo kwetu.)

 

  1.     Hebu tusome tena Matendo 2:17 na Matendo 2:18. Je, Roho Mtakatifu anaweza kunena kupitia kwako? (Ndiyo! Kila mtu amejumuishwa. Wakiwemo wale wasio na hadhi ya kijamii (watumishi wa kiume na wa kike).)

 

  1.     Hebu turuke chini na tusome Matendo 2:37. Inawezekana baadhi ya watu waliwadhihaki wanafunzi, lakini wengine waliguswa na kuuliza wanachotakiwa kukifanya katika kujibu ujumbe wa Petro. Walitakiwa kufanya nini? (Soma Matendo 2:38-39. Walitakiwa kutubu, kubatizwa, na kupokea kipawa.)

 

   1.     Ni kipawa gani hicho? (Roho Mtakatifu.)

 

   1.     Matendo 2:39 inazungumzia ahadi. Ahadi gani inatolewa kwa Wakristo wote? (Bado hii inamrejelea Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ameahidiwa kwa wote wanaotubu na kubatizwa.)

 

  1.     Soma Matendo 2:41. Ni nini matokeo ya Roho Mtakatifu kutenda kazi kupitia kwa wanafunzi?

 

  1.     Soma Matendo 2:42-43. Wote walimpokea Roho Mtakatifu. Wote walistahili kutumia uwezo wake, kwa mujibu wa Yoeli 2. Kwa nini mitume pekee ndio waliotenda “maajabu na ishara?”

 

   1.     Je, kuna fundisho kwa ajili yetu leo katika jambo hili? (Roho Mtakatifu ni karama. Ameahidiwa kwetu. Lakini, jinsi Roho Mtakatifu anavyotenda kazi yeye mwenyewe ndiye anayejua. Tunatakiwa kujilinda dhidi ya mawazo dhahania na kiburi/majivuno kwenye suala hili juu ya nani anayeshughulikia utendaji wa karama hii.)

 

  1.     Rafiki, umepewa karama ya Roho Mtakatifu ikiwa umetubu na kubatizwa. Je, utaomba ili Roho Mtakatifu aongoze unenaji na ushuhudiaji wako? Je, utaomba ili atende kazi kupitia kwako ili uwalete wengi kwenye imani katika Yesu? Je, utamwomba akuponye uzungumzaji wako wenye “moyo mzito?” Kwa nini usimwombe sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Uwezekano Usio na Kikomo.