Somo la 2: Familia

(Kumbukumbu la Torati 6)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
4
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Familia

(Kumbukumbu la Torati 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV®inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kama wewe ni mzazi, hebu jiulize, je, kuna wakati ambapo watoto wako waliamini kila ulichowaambia? Je, pia kuna wakati waliamini takribani kila ambacho hukukisema? Hii inaweza kutia chumvi ukweli mbalimbali kwa wengi wetu, lakini ninadhani wote mnakubaliana kuwa kuna kipindi maalumu ambacho watoto wetu wako tayari kufundishika. Katika siku za nyuma, umma uliungana na Wakristo kuwafundisha watoto wetu ujumbe chanya. Akilini mwangu hii inanikumbusha kipindi cha televisheni cha “Andy Griffin Show.” Je, vipindi kama hivyo bado vipo katika zama za leo kwenye televisheni za kidunia? Sidhani. Wakati siku hizi watoto wetu wanaangalia mtandao katika umri mdogo sana, wanafundishwa nini na mtandao huo? Somo letu la leo linahusu kile ambacho Biblia inawafundisha wazazi kuhusu kuwaelimisha watoto wetu. Hebu tuzame kwenye Biblia na tujifunze zaidi!

Elimu Kubwa Kuliko Zote

Soma Kumbukumbu la Torati 6:1. Ni nani aliye chanzo cha maelekezo tunayokwenda kuyasoma? (Mungu! Mungu anamwambia Musa, naye Musa anawaambia watu.)

Je, umewahi kujiuliza kama jambo fulani linastahili kufundishwa? Jadi ya fundisho hili ni ipi? (Inatoka kwenye chanzo cha juu kabisa na bora.)

Utaona kuwa kifungu hiki kinazungumzia ufundishaji wa siku zijazo. Kama hadi kufikia hapa hujawafundisha watoto wako kwa usahihi, je, umechelewa?

Soma Kumbukumbu la Torati 6:2. Unadhani Biblia inamaanisha nini inaposema “kumcha” linapokuja suala la kufundisha habari za Mungu? (Siyo hofu, bali heshima. Mtazamo huu unathibitishwa utakaposoma sura nzima. Mungu hawatishii watu kwa namna itakayosababisha hofu.)

Kutakuwa na athari gani kubwa kwa kuwaelimisha watoto wako kwa usahihi? (Utaweza kuacha athari kwenye vizazi vingi.)

Utakuwa na athari gani maishani mwako? (Utii kwa Mungu hurefusha maisha.)

Soma Kumbukumbu la Torati 6:3. Manufaa gani mengine yanatokana na elimu ya kimungu? (Maisha yako yatakuwa mazuri. “Upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana.” Utaona kuwa maneno haya yanaelekezwa kwa watu wa Mungu kwa ujumla, na si kwa watoto pekee.)

Soma Kumbukumbu la Torati 6:4-5. Tulichokuwa tukikisoma hadi kufikia hapa ni “tangazo” la kuzingatia mpango wa elimu ya Mungu. Kanuni ya kwanza ya elimu ya kimungu ni ipi? (Tunamzingatia Mungu wetu kipekee na kumpenda kikamilifu.)

Kumbukumbu la Torati 6:4 inaitwa “Shema” katika tamaduni za Kiyahudi. Kiuhalisia inamaanisha “sikiliza na utii.”)

Kwenye mfululizo wa masomo yetu yaliyopita kuhusu ushuhudiaji, nilisisitiza umuhimu wa Utatu Mtakatifu na nilipokea maoni hasi kwenye dhana hii. Je, dhana ya “Bwana Mungu wetu, Bwana ni mmoja” inatuzuia tusiamini katika Utatu Mtakatifu? (Angalao mtu mmoja anayenishinikiza kwenye hoja hii alikubali kwa nguvu zote kuwa Yesu ni wa “kiungu” – ikimaanisha kuwa yeye ni Mungu. Kama huamini kuwa Yesu ni Mungu, basi wewe si Mkristo kutokana na uelewa wangu wa Biblia. Kama unakubali kuwa Yesu ni Mungu, hiyo inamaanisha huna Mungu mmoja bali Mungu wawili.)

Unapoangalia Kumbukumbu la Torati 6:4-5 na kutafakari maana na muktadha wake, je, unadhani inamuacha Mungu Yesu au Utatu Mtakatifu? (Muktadha ni kwamba watu wa Mungu, wakati wakiwa Misri, waliingizwa kwenye miungu mingi. Wataendelea kukabiliwa na miungu mingine. Nadhani anachokimaanisha Mungu wa kweli ni kwamba hii inayojidai kuwa “miungu” mingine si mungu hata kidogo. Mungu wetu ni Mungu pekee, na ni wa pekee. Yeye ndiye Mungu.)

Unaielewaje dhana ya kumpenda Mungu “kwa moyo wako wote ... kwa roho yako yote ... na kwa nguvu zako zote?”

Kama utafundisha jambo hili, unatakiwa kulielewa, sawa?

Soma Kumbukumbu la Torati 6:6. Amri hii “kuwa katika moyo wako” inamaanisha nini? (Sio tu kwamba unatakiwa kuuamini wewe mwenyewe, bali pia unatakiwa kuwa sehemu ya msingi ya mtazamo wako.)

Soma Kumbukumbu la Torati 6:7. Mara kwa mara nimesikia kuwa “muda utumikao kwenye kazi” ni kipengele cha muhimu sana katika kujifunza. Kwa mfano, mwaka mzima wa masomo humsaidia mtoto kushika kile alichofundishwa. Mungu anasema nini kuhusu “muda utumikao kwenye kazi” na kanuni zake? (Anauidhinisha.)

Hapa maelekezo ya Mungu yamebainishwa kwa kina. Je, una mapendekezo ya kutekeleza hili? Ninafahamu kwamba ninapokaa na mjukuu wangu, wakati mwingine ninapata changamoto jinsi ninavyopaswa kuanza kujadili habari za Mungu.

Au, je, kifungu kinamaanisha kuwa hatupaswi kuuwekea ukomo wa muda mjadala wa Mungu kwenye nyakati fulani za siku?

Soma Kumbukumbu la Torati 6:8-9. Unadhani kuwa Mungu alimaanisha jambo hili lichukuliwe hivyo kiuhalisia? (Hata leo, baadhi ya Wayahudi wanalichukulia jambo hili kiuhalisia. Huenda utendaji wa kawaida kabisa ni kuweka “mezuzah” juu la mlango wa mbele ya nyumba. Hiki ni kikasha kidogo chenye maandiko machache ndani yake.

Soma Kumbukumbu la Torati 11:20. Kifungu hiki kingine (na kuna vifungu kadhaa vinavyofanana na hicho) kinafanya ionekane kuwa Mungu anadhamiria jambo hili lieleweke kiuhalisia.)

Soma Matendo 15:28-29. Ukisoma sura yote, utaona kuwa mgongano uliopo ulihusu tohara – kama ishara ya uhusiano na Mungu. Ikiwa tohara haihitajiki tena kwa Mataifa, hii inaashiria nini kuhusu matakwa ya Kumbukumbu la Torati 6:8-9?

Soma Wakolosai 2:11. Tunaona kwamba tohara haijasahaulika, bali inachukua mfumo mpya. Utaendeleaje kutimiza Kumbukumbu la Torati 6:8-9 kwa namna mpya?

Je, “njia yako mpya” inaweza kuwa na ufanisi zaidi? Kuvaa kitu kichwani mwako inaweza kufanana na kuvaa miwani – mapema tu utaizoea sana kiasi kwamba unasahau kama umeivaa.

Soma 1 Samweli 7:12. Muktadha ni shambulio la kushtukiza lililoelezewa katika 1 Samweli 7:10-11. Jiwe hili la Eben-ezeri linatuambia nini kuhusu kuwafundisha watoto wetu na kukumbuka kile alichokifanya Mungu? (Linatuonesha njia za ubunifu ili kutusaidia kukumbuka kile ambacho Mungu ametutendea.)

Mimi na mke wangu tuna kitabu ambacho tunakiita jiwe letu la Eben-ezeri. Katika kitabu hicho tunaweka kumbukumbu ya matukio muhimu ambayo Mungu ametubariki na kutusaidia.

Soma Kumbukumbu la Torati 6:10-11. Ungesema nini kama Mungu angekutendea hayo? Je, kuna uwezekano wowote kwamba ungesahau hii zawadi kubwa?

Soma Kumbukumbu la Torati 6:12. Hapa tunaona onyo gani kuhusu elimu? (Kwamba tutasahau hadi baraka kubwa kabisa. Sidhani kama suala ni “kusahau” kwa kadiri jambo linavyozidi kuzoeleweka kwenye baraka na kudhani kuwa kwa namna fulani hivi tunastahili vitu hivyo.)

Soma Kumbukumbu la Torati 6:13. Unakumbuka tulijadili juu ya kinachomaanishwa kwenye “kumcha” Mungu? Unapopitia kile tulichojifunza kwenye sura hii, muktadha huo unakufundisha nini juu ya kile kinachomaanishwa kwenye kumcha Mungu? (Sura hii inaelezea mambo ambayo Mungu aliwatendea watu wake au atakayoyatenda kama watamtii. “Kumcha” si hofu, bali ni kumtii Mungu kwa upendo na ulinzi wake. Ni utii kwenye kanuni ya kwamba kuzingatia amri zake hufanya maisha yetu yawe mazuri.)

Miungu Mingine

Soma Kumbukumbu la Torati 6:14. Hii inaonekana kuwa lengo la msingi la elimu ya Mungu. Mwabudu yeye [Mungu] na si miungu mingine. Katika dunia yangu hakuna mtu ninayemfahamu anainama kuabudu mungu aliyemtengeneza. Je, unamfahamu mtu yeyote anayefanya hivi?

Je, hii inamaanisha kuwa fundisho kubwa kabisa la kielimu sasa halina umuhimu tena?

Ninawasikia watu wakisema kuwa gari la mtu au nyumba ya mtu ndio mungu wao. Uwezekano mkubwa ni kwamba huo ni upuuzi, nani anayeabudu gari lake au nyumba yake?

Katika kuzingatia zaidi kilichomaanishwa, ni nini lililokuwa lengo la kuabudu miungu ya uongo? (Watu walidhani wangenufaika kutokana na kuiabudu. Mafanikio yatamtegemea mungu wa uongo.)

Je, suala hili lipo katika zama za leo – bila kutumia sanamu ya kuchonga? (Miongoni mwa vitu vingine, tunazitegemea akili zetu, fedha zetu, uzuri wetu, na kazi zetu.)

Je, miungu hii inaendana na mjadala wetu wa Kumbukumbu la Torati 6?

Kama umejibu, “ndiyo,” je, unafanya nini kuwaelimisha watoto wako kuhusu hiyo miungu ya uongo?

Rafiki, je, mara zote akilini mwako utazingatia elimu ya watoto wako? Je, utaifanya kuwa sehemu ya mambo yote unayoyafanya nao? Kwa nini usianze leo?

Juma lijalo: Sheria Kama Mwalimu.