Somo la 1: Kuishi Katika Jamii ya Saa 24 Siku 7 za Juma

Mathayo 11, Yeremia 45, Mwanzo 2
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Kuishi Katika Jamii ya Saa 24 Siku 7 za Juma

 

(Mathayo 11, Yeremia 45, Mwanzo 2)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, maisha yamekubadilikia? Rejea nyuma miaka 25 iliyopita. Hicho ndicho kipindi ambacho kwa mara ya kwanza nilinunua simu ya mkononi na kuanza kutumia barua pepe. Habari njema ni kwamba sikuwa na haja ya kutafuta simu ya umma niliposafiri, na sikulazimika kuwa ofisini kwangu ili niweze kutuma barua. Habari mbaya kabisa ni kwamba sasa niliweza kufikiwa kimawasiliano wakati wowote katika siku na nilitarajiwa kutoa mrejesho ndani ya saa chache. Kabla ya hapo, ni nani ambaye kimsingi alifahamu kuwa tayari barua imeshafika ofisini kwangu? Mimi na mke wangu tulikuwa na mashine iliyojibu simu zetu zote nyumbani. Niliondokana na udhibiti wa ratiba yangu na kuingia kwenye jamii ya saa 24 siku 7 za juma. Je, uzoefu huu ni sawa na wako? Ikiwa ndivyo, basi somo hili ni kwa ajili yako! Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi.

 1.    Pumziko la Yesu
  1.    Soma Mathayo 11:27. Je, hili ni fumbo? Inaonekana kama Yesu anasema kuwa Mungu Baba pekee na Mungu Mwana ndio wanaojuana. Je, kuna upekee wowote? (Ndiyo! Yesu anaweza kuchagua kumfunua Mungu kwetu.)
  1.    Soma Mathayo 11:28-29. Unadhani kuna uhusiano gani kati ya kumjua Mungu na pumziko? (Lazima liwe jambo la “kujua” kwa kuwa Yesu anatuambia kuwa anaweza kutusaidia kumjua Mungu, na kwamba ikiwa “tutajifunza kutoka kwa [Yesu]” tutaielewa nira nyepesi na rahisi.)
   1.    Je, ukweli kwamba Yesu ana “moyo mpole na mnyenyekevu” unahusianaje na mzigo wetu? (Kwa kawaida, miungu ilikuwa na madai makubwa kwa wanadamu. Yesu anatuambia kuwa yeye hayuko hivyo. Hatushurutishi.)
   1.    Yesu anaifanyaje mizigo yetu kuwa myepesi? Anatupatiaje pumziko? Je, matumizi yake ya neno “nira” yanahusiana kivyovyote vile na jibu hili? (Neno la Kiyunani linamaanisha kuunganisha au kuhusisha. Dhana iliyopo ni kwamba Yesu anashiriki mzigo wetu.)
   1.    Hebu ngoja nirejee nyuma kidogo katika jambo hili. Je, Yesu anasema kuwa atajibu lundo la barua pepe zangu na kupunguza idadi ya simu ninazopigiwa kwenye simu yangu ya mkononi?
    1.    Ikiwa umesema, “hapana,” Yesu anaashiria nini? (Utagundua kwamba pumziko lililoahidiwa ni kwa ajili ya “nafsi” zetu. Strong anatuambia kuwa hii si rejea ya fikra ya kimantiki, bali ni dhahania zaidi ya moyo wako. Ninakuja na dhana ya kwamba Mungu anatupatia mtazamo unaorahisisha mzigo wetu.)
     1.   Je, umewahi kupitia uzoefu nilioupendekeza hivi punde?
    1.    Kiwango gani cha shinikizo maishani mwako kinasababishwa na mambo yasiyoleta tofauti yoyote halisi katika kipindi cha muda mrefu?
    1.    Kwa nini kumjua Mungu vizuri zaidi husaidia kupambanua kilicho cha muhimu na kile ambacho ni shinikizo tu la muda mfupi? (Tunatakiwa kuangalia mizigo maishani mwetu kwa kuzingatia umilele. Kitu gani hasa kinacholeta tofauti? Huo ndio mtazamo tunaouhitaji.)
  1.    Soma Marko 6:7 na Marko 6:12-13. Kwa kuzingatia kipimo cha umuhimu wa umilele, utazipa nafasi gani shughuli za thenashara (wanafunzi)?
  1.    Soma Marko 6:30-32. Je, utaweza kuchukua pumziko na kuacha kuhubiri injili, kutoa pepo, na kuwaponya wagonjwa?
   1.    Kwa nini Yesu anawaambia wachukue pumziko? (Anafundisha kanuni ya pumziko hata pale ambapo kimantiki ungeweza kuhitimisha kuwa hakuna kilicho cha muhimu zaidi.)
   1.    Mtu anaweza kusema, “Inaonekana kuwa huduma ya utume ya wanafunzi imekwisha, hivyo ilikuwa ni muda wa kawaida kwa ajili ya pumziko.” Kwa kuwa walikuwa wamejifunza kutenda mambo haya, je, kutenda mambo haya yote ya muhimu bado ni matumizi mbadala ya muda wao?
  1.    Je, pumziko lako ni la muhimu zaidi kuliko kupeleka injili kwa mtu au kumponya mtu?
   1.    Soma 2 Samweli 7:12. Hii inaashiria kuwa jibu mojawapo ni lipi? (Hii ni sehemu ya kile kinachomaanishwa kwenye kushiriki mizigo na Mungu. Atawainua wengine kutenda kazi ambayo hatuifanyi. Je, kweli unadhani kuwa mtu yeyote atapotea kwa sababu umechukua pumziko?
  1.    Soma Marko 6:33-34. Je, dunia itashirikiana nawe katika kutafuta kwako pumziko?
 1.   Mtazamo wa Baruku
  1.    Soma Yeremia 45:1. Baruku, mwana wa Neria ni nani? (Yeye ni mwandishi wa nabii maarufu wa Biblia, Yeremia.)
  1.    Soma Yeremia 45:2. Ni jambo gani lisilo la kawaida kuhusu hali hii? (Mungu ana ujumbe kwa ajili ya Baruku. Kwa kawaida, Mungu ananena na Yeremia ambaye anamwambia Baruku nini cha kuandika kwa manufaa ya wengine. Huu ni ujumbe binafsi kwa Baruku.)
  1.    Soma Yeremia 45:3. Niambie kuhusu mtazamo wa Baruku? Amejikita kwa nani? (Amejizingatia mwenyewe. Anaendelea kujirejelea na matatizo yake.)
   1.    Baruku anabainisha tatizo gani linalohusiana na somo hili? (“Hapati pumziko.”)
  1.    Soma Yeremia 45:4. Mustakabali gani ulio mbele ya Baruku? (Mambo yanayomzunguka hayatamwendea vizuri.)
   1.    Kwa nini Mungu anamwambia hivi Baruku? Ikiwa Baruku anajikita kwenye maumivu yake na kutokuwa kwake na pumziko, Mungu anampa ujumbe gani? (Mungu anaashiria badiliko la mtazamo. Usijizingatie kupita kiasi na umuhimu wako.)
   1.    Miaka mingi iliyopita nilikuwa ninasikiliza kitabu kinachohusu vita vya Marekani vya wenyewe kwa wenyewe, hususani pambano la Gettysburg. Mwandishi alisema kuwa mpambano wa kurushiana risasi ulikuwa mkali sana kiasi kwamba majani yote, magugu na vichaka vilikatwa na kuwa vifupi sana. Wanadamu hawakuweza kustahimili hili, na watu 50,000 walifariki kwenye vita hiyo. Niliposoma hili, nikatafakari “Kwa nini ninadhani kuwa mimi ni wa muhimu sana?”
  1.    Soma Yeremia 45:5. Lengo la Baruku kwa ajili yake ni lipi? (Mambo makuu!)
   1.    Mungu anasema nini kuhusu lengo hilo? (Usiyatafute.)
   1.    Badala yake Mungu anamwahidi nini Baruku? (Miongoni mwa mabaya ambayo yanakuja katika nchi, ataishi.)
   1.    Maelekezo ya Mungu kwa Baruku yanahusianaje na kauli ya Baruku kwamba hawezi kupumzika?
   1.    Kiwango gani cha kukosa kwako pumziko ni matokeo ya msukumo wako wa kutaka mambo makuu?
  1.    Tumetoka kusherehekea Siku ya Baba nchini Marekani, na miongoni mwa baraka nyingi ambazo baba yangu alinipatia ni msukumo wa kuwa mtu bora. Aliumba roho ya ushindani ndani yangu. Wengi hawatakubaliana kwamba hili ni jambo jema, lakini ninalichukulia kuwa miongoni mwa baraka kubwa za Mungu kwangu. Je, ujumbe kwa Baruku unaniambia kuwa siko sahihi?
   1.    Ni kawaida kiasi gani kukutana na watu wasio na malengo?
  1.    Soma Danieli 6:3. Unaielewaje “roho bora” ya Danieli iliyompa msukumo wa ukuu?
  1.    Soma Mithali 22:29. Je, unadhani mtendakazi “mjuzi” ni mtendakazi “bora?”
  1.    Tunapaswa kuhitimisha nini baada ya kusoma neno la Mungu kwa Baruku, kwa kuzingatia roho ambayo Mungu aliiweka ndani ya Danieli, na kwa kuzingatia kile ambacho Mithali inakipendekeza kwetu kama watendakazi? (Kazi yetu inapaswa kuwa bora. Lakini kujizingatia kunakotafuta ukuu binafsi ni adui wa pumziko. Usiwe mvivu, usiwe hobelahobela, lakini usijinyime pumziko kwa kuwa unaendeshwa. Tafuta ubora na uulinganishe na pumziko.)
 1. Kupumzika kwa Wakati
  1.    Pitia kwa harakaharaka Mwanzo 1 kisha usome Mwanzo 2:1-3. Vitu vilivyoumbwa kila siku katika siku za Uumbaji vina umuhimu gani?
   1.    Mpangilio huu unaashiria kuwa umuhimu wa pumziko la Sabato ni upi? (Mpangilio huupatia angalao hadhi sawa na mambo yote yaliyo ya msingi maishani.)
  1.    Soma tena Mwanzo 2:3. Sabato “inabarikiwa” na “kutakaswa.” Je, hiyo inapaisha umuhimu wake juu ya kile kilichotimizwa katika siku zilizotangulia?
   1.    Unahitimisha nini kutokana na ukweli kwamba Mungu aliifanya Sabato kuwa sehemu ya namna alivyopangilia muda – na ukweli kwamba mzunguko huu wa kila juma unaendelea hadi leo?
  1.    Rafiki, je, utachukua mzunguko wa kazi na pumziko kwa makini zaidi? Je, utaupa kipaumbele ambacho Muumba wako anaupatia?
 1.   Juma lijalo: Wahaka (Kukosa Utulivu) na Uasi.