Somo la 10: Kumbuka, Usisahau

Mwanzo 9, Kumbukumbu la Torati 8, 15, & 24
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
4
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Kumbuka, Usisahau

(Mwanzo 9, Kumbukumbu la Torati 8, 15, & 24)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, unazeeka? Mimi ninazeeka. Unapokuwa mzee unakuwa na wasiwasi kuhusu kutokumbuka kwa sababu usahaulifu unaweza kuwa ni ishara ya tatizo kubwa. Kwa upande wangu, ninajiliwaza kutokana na ukweli kwamba mara zote suala la kumbukumbu limekuwa likinikabili. Nilipokuwa kijana barobaro (teenager), nakumbuka nikiwa ninaendesha gari kutoka nyumbani kuelekea chuo kikuu na sikuweza kukumbuka uelekeo wangu au kwa nini nilikuwa ninaelekea huko. Siku hizi mambo kama hayo kamwe hayanitokei, lakini kumbukumbu imekuwa suala la kisiasa nchini kwangu. Baadhi ya vijana wanataka kuharibu majengo ya kihistoria yanayokumbushia mambo ya kale. Wapinzani wao wanaamini kuwa kukumbuka mambo ya kale hutusaidia kuepuka kufanya makosa ya nyuma. Mungu anatuambia nini kuhusu umuhimu wa kukumbuka mambo fulani-fulani? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile inachosema!

 1.    Kuikumbuka Gharika
  1.    Soma Mwanzo 9:8-11. Mungu anawahakikishia wanadamu kwamba kamwe hataiangamiza tena dunia kwa maji. Muktadha wa ahadi hii ni upi? (Ni punde tu wanadamu wameponea gharika lililoangamiza dunia nzima.)
   1.    Mungu anasema anawaahidi ndege, ng’ombe, na wanyama wengine. Kwa nini anatoa ahadi kwa viumbe wasioweza kutambua ujumbe ulionenwa kama huu? (Mungu aliwaangamiza wanadamu wote na wanyama ambao hawakuwemo safinani. Anatoa ahadi hadharani kwamba hatafanya hivyo tena. Nadhani ujumbe sio suala la kuwasiliana na wanyama, bali kuwapa thamani wanyama.)
  1.    Soma Mwanzo 9:12-16. Mungu alitupatia ishara ya ahadi gani? (“Upinde wangu winguni.”)
   1.    Je, Mungu anahitaji ishara? (Vifungu hivi vinatuambia kuwa ishara hii ni kwa ajili ya kumsaidia Mungu kukumbuka ahadi yake. Havizungumzii chochote kuhusu kutusaidia kukumbuka. Ni vigumu kuamini kuwa Mungu ana tatizo na kumbukumbu yake.)
    1.    Kwa hiyo basi Mungu anamaanisha nini hasa kwenye upinde wa mvua?
   1.    Siku hizi upinde wa mvua unatumiwa na wanaharakati wanaotetea haki za wasenge/mabasha. Kwa nini, kati ya ishara zote ambazo wangeweza kuzichagua, walichagua ishara hii? (Haileti mantiki yoyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Kama unataka ishara anuwai (diversity), basi ungechagua kitu chenye rangi nyingi tofauti-tofauti. Badala yake, ninadhani hii inaakisi kauli iliyotolewa katika Waefeso 6:12 (isome) kwamba Wakristo wanapaswa kutambua kuwa wapinzani wao halisi sio wanadamu wengine waliofariki, bali nguvu ovu za kilimwengu. Kwa muktadha huo, hii inaleta mantiki.)
 1.   Kukumbuka Mahitaji Yetu
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:7-9. Mungu anawapatia watu wake mahali pa namna gani? (Mahali pazuri!)
   1.    Kitu gani kinakuambia kuwa huu ulikuwa ni usasa wa hali ya juu? (Walitumia chuma na shaba.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:10-14. Mungu ana wasiwasi gani? (Kwamba watu wake watasahau kile alichowatendea.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:15-17. Je, Mungu ana wasiwasi kwamba watazeeka na kuwa wasahaulifu? Ikiwa sivyo, chanzo cha wasiwasi huo ni kipi? (Kwamba watadai kuhusika na kuwajibika kwa mali walio nayo.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:18. Kwa nini Mungu ndiye wanayepaswa kumshukuru? (Kwa sababu aliwapa “nguvu za kupata utajiri.”)
   1.    Hiyo inamaanisha nini? (Wanadamu wanawiwa na kuwajibika kila kitu kwa Mungu – ikiwemo uwezo wao wa kila siku kuendelea kuwa hai.)
   1.    Je, bado hili ni tatizo katika zama za leo? Je, wanadamu wanaelekea kudai kwamba wanawajibika kwa mafanikio yao maishani? (Nadhani hili ni tatizo sugu leo miongoni mwa wale wenye mafanikio.)
  1.    Hebu tuangalie mantiki ya mjadala wetu hadi kufikia hapa na tuone kama tunaweza kuwa na mada ya jumla. Je, kuna uhusiano kati ya watu wa Mungu kusahau kuwa Mungu ndiye chanzo cha mafanikio yao, na shughuli za kibasha/kisenge kuhusisha ishara ya ahadi ya Mungu ya kutokuwepo gharika? (Kiungo kati ya vitu hivi viwili ni kitabu cha Mwanzo. Kitabu cha Mwanzo kinatuambia kuwa Mungu aliwaumba wanadamu. Kitabu cha Mwanzo kinataarifu juu ya Gharika. Kama unakikataa kitabu cha Mwanzo na kuamini kuwa wanadamu waliibuka kutoka kwenye viumbe wenye seli nyepesi, basi unaikataa historia ya mwanadamu. Bila historia hiyo, kwanini usiamini kuwa unaweza kuifikiria jinsia yako? kwa nini usifikirie spishi (species) zako?)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:19-20. Mungu anatupatia onyo gani la dhati kuhusu kushindwa kukumbuka historia yetu? (Kwamba “hakika tutaangamia.”)
 1. Kukumbuka Mambo Yetu ya Zamani
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:18. Mungu anawaambia watu wake wakumbuke sehemu gani ya historia yao? (Kwamba walikuwa watumwa nchini Misri na kwamba Mungu aliwaweka huru dhidi ya utumwa.)
   1.    Je, una historia inayofanana na hiyo? Je, Mungu alikuokoa kutoka utumwani? (Sote tuna visa tofauti-tofauti vya jinsi Mungu alivyotusaidia, lakini ukweli wa jumla ni kwamba Mungu alituokoa kutoka kwenye mauti ya milele.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:19-21. Ni nani anayesaidiwa? (Mgeni, yatima, na mjane.)
   1.    Je, wao pekee ndiwo waliosaidiwa na kitendo hiki? (Hapana. Kifungu cha 19 kinamwahidi mkulima kwamba Mungu anaweza “akubariki katika kazi yote ya mikono yako.”)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:22. Kuna uhusiano gani wa kimantiki kati ya takwa hili na historia ya familia ya mkulima kama watumwa? (Mungu aliwasaidia pale ambapo hawakuweza kujisaidia. Mungu anasema kuwa kwa sababu hiyo unapaswa kuwasaidia wale walio na uwezo mdogo wa kujisaidia.)
  1.    Angalia tena katika Kumbukumbu la Torati 24:19-21. Kuna mafundisho mengine kadhaa ya kihistoria ambayo hatupaswi kutoyatilia maanani au kuyasahau. Tunayo madaraja mawili, mmiliki mali na wale wasiomiliki mali. Hii inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Mungu juu ya haki ya mmiliki mali? (Mungu anathibitisha tena haki ya mmiliki mali kuendelea kumiliki mali na kulima shamba. Mungu hatoi wito kwa mkulima kugawana shamba hili na wale wasiomiliki ahamba.)
   1.    Jambo gani linahitajika kwa wale walio na uwezo mdogo wa kujisaidia? (Wanatakiwa kufanya kazi ya kukusanya mganda, mizeituni, na zabibu. Mungu hawaruhusu wakae nyumbani na kusubiri kuletewa chakula.)
   1.    Kama mkulima, mgeni, yatima, na mjane wanatenda kile ambacho Mungu amewaelekeza, matokeo yake yatakuwa ni yepi kwa kuzingatia vitu walivyo navyo? (Ni mkulima pekee ambaye Mungu anaahidi kumbariki katika mazingira kama haya.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:11. Je, Mungu anaamini kuwa tatizo la watu maskini linaweza kutatuliwa? (Anasema kuwa siku zote watakuwepo maskini. Lakini, wale walio na mali wanapaswa kuwasaidia. Hebu tuangalie muktadha wa kifungu hiki katika sehemu inayofuata.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:1-3. Kuna mambo mengi yanayotokea katika mwaka wa Sabato (mwaka wa Saba), lakini hapa tutajikita kwenye suala la deni. Inamaanisha nini kusema kuwa mkopeshaji “akiachie alichomkopesha mwenziwe?” (Inamaanisha kuwa mkopeshaji hana tena mamlaka ya kisheria kuchukua sehemu yoyote ya deni ambalo bado halijalipwa.)
   1.    Je, kanuni hii pia inatumika kwa wageni? (Hapana.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:4. Lengo ni lipi? (Kutokuwepo kwa maskini miongoni mwa watu wa Mungu. Kwa ujumla tatizo la umaskini litaendelea kuwepo, lakini lengo la watu wa Mungu ni kuuondosha umaskini.)
  1.    Ongezea Kumbukumbu la Torati 15:5. Kama umesoma vifungu viwili vya mwisho kwa pamoja, Mungu ana mpango gani wa kuuondosha umaskini? (Kama watu watazitii sheria za Mungu, zikiwemo sheria za kuwanufaisha maskini, basi tatizo la maskini linapaswa kupotea.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:6-8. Je, Mungu anatarajia kwamba litakuwepo daraja la kudumu la watu maskini miongoni mwa wale wanaomtumikia Mungu? (Lengo ni kwamba watu wote wa Mungu wawe na mali ya kutosha. Kifungu cha 7 kinarejelea mtu kuwa maskini. Dhana iliyopo ni kwamba mazingira yasiyo rafiki yanaweza kukufanya uwe maskini. Katika hali kama hiyo, wenye mali wanatakiwa kusaidia.)
  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:9-10. Matajiri wanapaswa kuwa na mtazamo wa aina gani dhidi ya maskini? (Ni dhambi kutowapatia maskini kitu chochote kwa kuwa mwaka wa maachilio unakaribia. Badala yake, Mungu huwabariki wale walio na mtazamo wa ukarimu kwa maskini.)
  1.    Rafiki, Mungu anatutaka tukumbuke mambo ya zamani na kile alichokitenda na anachoendelea kututendea. Tukifanya hivyo, tutatambua na kukiri kwamba mali zetu zote zinatoka kwa Mungu. Fursa yetu ya kuupata uzima wa milele inatoka kwa Mungu. Hiyo inapaswa kutupatia mtazamo wa kuwahurumia maskini. Lakini matokeo ya mtazamo huo wa huruma sio kutufanya tuwe na vitu vichache, bali matokeo yake ni Mungu kutubariki zaidi. Je, utafanya uamuzi leo kukumbuka na kutii?
 1.   Juma lijalo: Kumbukumbu la Torati Katika Maandiko Yaliyofuata.