Wanawake Katika Utume wa Yesu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Asubuhi moja katika juma hili nilisoma makala iliyokuwa ikisema kwamba wanawake wanatendewa kama wanyama maeneo mengi hapa duniani. Binafsi sifahamu kama jambo hilo ni kweli, lakini nina uhakika kwamba baadhi ya maeneo, na katika kipindi cha Yesu, wanawake hawakuwa na hadhi sawa na wanaume. Yesu alihusianaje na wanawake? Tunaweza kujifunza nini leo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Luka ili tujifunze zaidi!
- Ana
- Soma Luka 2:36-37. Tulipojifunza sura ya pili ya kitabu cha Luka, tulihitimisha kabla hatujafikia kwenye kisa cha Ana. Je, ungependa kuwa Ana? (Ana sikitiko kubwa maishani mwake, mumewe anafariki miaka saba baada ya kuoana. Anaamua kutoolewa tena, na kwa dhahiri hana mtoto yeyote.)
- Ungefanyaje endapo jambo hili lingekutokea?
- Ana anafanyaje? (Anayatoa maisha yake kutoa huduma kwa ajili ya Mungu.)
- Mungu anaitikiaje kujitoa kwa mwanamke huyu katikati ya sikitiko lake? (Alikuwa nabii mke, ikimaanisha kwamba Mungu alizungumza kupitia kwake.)
- Soma Luka 2:38. Nani ambaye ni “wao” katika fungu hili? (Muktadha uliopo ni wa Luka 2:25-34. “Wao” ni Mariamu, Yusufu, Simeoni na mtoto Yesu.)
- Mungu anampatiaje thawabu Ana kwa namna nyingine kutokana na uaminifu wake? (Anaonekana kutokuwa na watoto, lakini ni miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kutambulishwa kwa Mwana wa Mungu.)
- Niliposoma katika Luka 2:37 juu ya ratiba ya siku nzima ya Ana, sina hamu ya kubadilisha kazi. Luka 2:38 inapanuaje uelewa wetu wa shughuli zake (Ana) za kila siku? (Ibada yake, kufunga na kuomba kwake kulihusisha kuwaambia habari njema kumhusu Yesu wote “waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu.” Sasa fikiria kazi yake. Kwa wale wanaokuja hekaluni kutoa sadaka na kuabudu, anawafundisha kwamba utimilifu wa mfumo wa ibada wa hekalu umetimia!)
- Soma Kutoka 38:8. Hii inaashiria nini kuhusu asili ya kazi ya Ana? (Kwa dhahiri, alikuwa na wajibu wa utamaduni wa mwanamke “aliyetumika” mlangoni mwa hema ya kukutania.)
- Soma 1 Timotheo 2:12-13. Paulo anajenga msingi wa fundisho hili juu ya nini? (Uumbaji.)
- Soma 1 Wakorintho 14:33-35. Mafungu haya yanasema nini kuwahusu wanawake wawapo kanisani? (Yanasema kuwa wasizungumze.)
- Je, unalifahamu kanisa lolote lisiloruhusu kabisa wanawake kuzungumza?
- Kanuni mojawapo ya muhimu sana ya kuelewa mapenzi ya Mungu ni kwamba lazima tuone kile Biblia yote inachokisema juu ya mada fulani, na sio tu fungu moja au mafungu mawili. Angalia tena Luka 2:28. Je, Ana anaenenda kinyume na mipaka iliyobainishwa katika 1 Timotheo na 1 Wakorintho? (Ndiyo. “Kamwe hakuondoka katika hekalu” – kwa hiyo maneno yake yalitamkwa akiwa “kanisani.” Alipozungumza “habari za mtoto kwa watu wote … wakiutarajia ukombozi” alikuwa akiwafundisha wageni kwamba Yesu ni Masihi. Luka anapotuambia kwamba Ana alikuwa nabii mke, inamaanisha kwamba Mungu aliwasiliana na wanadamu kupitia kwake. Mungu anaidhinisha majukumu yake, kwa kuwa anampa thawabu kutokana na uaminifu wake.)
- Je, majukumu ya Ana yanaweza kulinganishwa na mafundisho ya Paulo? (Mimi ni mwalimu ninayekiri kile asichokifahamu. Bado sijafanyia kazi jambo hili, lakini ninadhani kwamba ni muhimu kwamba katika 1 Timotheo 2:12 Paulo anasema kuwa huu ni uzoefu wake binafsi (“simpi mwanamke ruhusa”). Kamwe sijawahi kuwa kwenye kanisa ambalo wanawake hawarusiwi kabisa kuzungumza, kitendo kinachoashiria kwamba hakuna mwenye mamlaka katika mazingira yanayonizunguka anayekubali kwamba 1 Wakorintho 14:34 inaakisi mapenzi ya Mungu.)
- Soma Luka 2:36-37. Tulipojifunza sura ya pili ya kitabu cha Luka, tulihitimisha kabla hatujafikia kwenye kisa cha Ana. Je, ungependa kuwa Ana? (Ana sikitiko kubwa maishani mwake, mumewe anafariki miaka saba baada ya kuoana. Anaamua kutoolewa tena, na kwa dhahiri hana mtoto yeyote.)
- Mariamu na Martha
- Soma Luka 10:38. Martha ana shughuli gani? (Ni mmiliki wa nyumba. Lazima itakuwa ilikuwa nyumba yenye ukubwa wa kutosha kuweza kumhudumia Yesu na wanafunzi.)
- Soma Luka 10:39-40. Je, ombi la Martha ni la haki? (Kwa nini Yesu ndiye anayetakiwa kutoa uamuzi? Nadhani ni kwa sababu Mariamu anamsikiliza Yesu, na inaweza iwe vizuri kumwambia aache kumsikiliza Yesu.)
- Soma Luka 10:41-42. Je, wewe ni nani, Martha au Mariamu? (Ninasikitika kwamba nini ni Martha – najishughulisha ili mambo yaende vizuri.)
- Mariamu anafanya nini kilicho bora? (Anamsikiliza Yesu.)
- Martha aliyemo ndani yangu anasema, “Bado utakuwa na mtazamo wa Yesu wa “lakini kinatakiwa kitu kimoja tu” linapokuja suala la kula wakati hakuna chakula kilichoandaliwa?”
- Hebu tuangalie fundisho kwa upana hapa. Unadhani utamaduni uliashiria kwamba wajibu sahihi wa mwanamke ni upi? (Kutenda kile alichokuwa akikifanya Martha.)
- Yesu anasema kuwa wajibu “bora” wa mwanamke ni upi? (Mafunzo ya kiroho.)
- Je, hili ni suala tu lenye ukomo wa muda kiutendaji? Mariamu anaweza kuendelea na upishi na kufanya usafi baada ya Yesu kuondoka?
- Kisa hiki kinawafundisha nini wale wanaoenenda kama Martha? (Kuwa na wasiwasi na masikitiko sio jambo “linalohitajika” maishani mwetu.)
- Wanawake Wenye Huruma
- Soma Luka 8:1-3. Yesu amewatendea nini wanawake hawa? (Aliwaponya matatizo yote yaliyowakabili. Na kwa kuongezea, Yesu anawaruhusu kusafiri pamoja naye.)
- Soma tena Luka 8:3. Unadhani kwa nini Luka anabainisha kwamba wanawake walikuwa wakimtegemeza Yesu na wanafunzi kifedha? (Hii inaonesha upendo wao wa ndani kabisa kwa Yesu na kumjali. Waliweka fedha zao ilipo mioyo yao. Pia inaonesha jambo fulani kuhusu Yesu na wanafunzi wake wa kiume waliokuwa radhi kusaidiwa na wanawake.)
- Mariamu Kahaba
- Soma Luka 7:36. Kwa ujumla Yesu ana shida na Mafarisayo. Kwa nini Farisayo anamwalika Yesu chakulani?
- Soma Luka 7:37-38. Mwanamke huyu aliingiaje nyumbani kwa Farisayo? (Hii inaashiria kwamba ilikuwa ni nyumba kubwa wakiwemo watu wengi wakila.)
- Kwa nini mwanamke huyu anafanya hivi? (Inaonekana Yesu amemtendea jambo fulani lililomgusa moyo wake. Analia anapofikiria kile ambacho Yesu amemtendea.)
- Soma Luka 7:39. Je, ungegundua jambo hili kama ungekuwa Yesu? (Naam!)
- Kwa wanaume, je, mnefanyaje endapo jambo hili lingewatokea? (Kama asingekuwa analia, ningechukulia mabusu haya na kuguswaguswa kuwa ni kiashiria cha mahusiano ya kingono.)
- Ungetafsirije mawazo ya Farisayo: “naye ni wa namna gani” na “ya kwamba ni mwenye dhambi?” (Baadhi ya watu wanasema kuwa mwanamke huyu si kahaba, kwa sababu hitimisho hilo halihitajiki na lugha hiyo. Kwa kuwa sisi sote ni wadhambi, ninashawishika kudhani kwamba haya sio maoni kuhusu hali ya jumla ya wanadaamu, badala yake ni kwamba alikuwa amefanya makosa ya uhusiano wa kingono katika siku za nyuma. Kimsingi, jambo hilo linaendana na wazo la kwamba huenda Farisayo aliona kitendo hiki kama ambavyo nionavyo – mazingira ya kukaribisha suala la ngono.
- Soma Mathayo 26:7. Hii inaongezea nini kwenye mjadala unaohusu asili ya njia aliyoitumia mwanamke huyu? (Asingetumia manukato ya “bei ghali” endapo manunuzi haya yangekuwa ya kibiashara.)
- Soma Luka 7:40-43. Je, ungejibu vivyo hivyo kama alivyojibu Simoni Farisayo?
- Soma Luka 7:44-47. Tumia kauli hii kanisani kwako. Je, watu ambao wamekuwa “wema” maishani mwao mwote wana hisia ndogo kuhusu injili na Mungu? (Nadhani jambo hili ni kweli.)
- Angalia kauli isiyo ya kawaida, Yesu anasema “amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi – kwa kuwa amependa sana.” Je, dhambi zinasamehewa kutegemeana na upendo wetu? Vipi kuhusu neema? (Yesu anauelezea mtazamo. Sidhani kama msamaha ni suala la maneno matupu, ni suala la mtazamo. Yesu anasema mwanamke huyu ana shukrani kubwa kutokana na kuokolewa kwake kutoka dhambini. Shukrani hiyo ndio inayokuwa upendo.)
- Unapotambua kwamba Mungu amesamehe dhambi yako kubwa, je, hiyo inaongeza upendo wako kwa Yesu?
- Angalia kauli isiyo ya kawaida, Yesu anasema “amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi – kwa kuwa amependa sana.” Je, dhambi zinasamehewa kutegemeana na upendo wetu? Vipi kuhusu neema? (Yesu anauelezea mtazamo. Sidhani kama msamaha ni suala la maneno matupu, ni suala la mtazamo. Yesu anasema mwanamke huyu ana shukrani kubwa kutokana na kuokolewa kwake kutoka dhambini. Shukrani hiyo ndio inayokuwa upendo.)
- Soma Luka 7:48-50. Niambie kuhusu tofauti iliyopo kati ya mwanamke huyu asiye na jina na Simoni Farisayo. Nani ambaye ni kiongozi wa dini halisi? Nani ambaye anamtumikia Mungu vizuri? Nani ambaye anafundishwa hapa?
- Rafiki, tunaweza kuona kutoka kwenye visa hivi kwamba Mungu anawathamini wanawake. Alimheshimu Ana kwa kumleta Yesu kwake. Mungu alimpa Ana ujumbe wake ili aufikishe kwa wageni hekaluni kwamba Yesu amekuja. Mungu aliichukulia elimu ya dini ya Mariamu kuwa ya muhimu zaidi kuliko kazi ya kawaida. Yesu alimtumia mwanamke mdhambi kufundisha fundisho la muhimu juu ya upendo kwa Farisayo. Mungu anawatumia wanawake kufundisha! Je, utajifunza zaidi kuhusu wajibu wa wanawake katika utume?
- Juma lijalo: Yesu, Roho Mtakatifu na Maombi.