Paulo : Asili na Wito

(Matendo 9, Wagalatia 2)
Swahili
Year: 
2015
Quarter: 
3
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Majuma matatu yaliyopita tulishuhudia Yesu akipeleka injili kwa mwanamke wa Kisamaria pale kisimani. Majuma mawili yaliyopita, tulijifunza juu ya maono ya Petro yaliyomfanya apeleke injili kwa Korneli, akida wa Kirumi. Juma lililopita, tulijifunza matendo makuu aliyoyafanya Filipo katika kupeleka injili Ethiopia na Samaria. Paulo, mtu tutakayejifunza habari zake juma hili na lijalo, ni kiongozi wa kanisa la awali anayejulikana zaidi kwa kupeleka injili kwa Mataifa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu kisa chake cha kupendeza!

  1. Uongolewaji
    1. Soma Matendo 9:1-2. Biblia inaposema, “akizidi kutisha na kuwaza kuwaua,” je, “akizidi” inarejea jambo gani? (Haya ni mauaji ya Stefano kwa kupigwa mawe tuliyoyagusia tulipojifunza habari za Filipo. Sauli aliidhinisha kifo cha Stefano na ndiye alikuwa kiini cha mateso yaliyotokea katika kanisa la awali. Matendo 7:57-Matendo 8:3.)
      1. Je, inamaanisha nini kwamba Sauli anakwenda kwenye Masinagogi ya Dameski? (Alisababisha waumini wa mwanzo kukimbia kutoka Yerusalemu, sasa anawafuata Dameski!)
      2. Kwa nini Sauli anataka mamlaka ya Kipolisi kwa mtu yeyote anayeishi Dameski? (Hii inatupatia mtazamo wa pekee wa jinsi ambavyo waumini wa awali walichukuliwa. Lazima Baraza la Sanhedrin la Yerusalemu lilidai kuwa na mamlaka juu ya masinagogi yaliyokuwa nje ya Israeli, ingawa mamlaka ya Rumi ndio yaliyokuwa na nguvu kubwa. Hii inaashiria kuwa Wayahudi waliwachukuliwa Wakristo wapya kuwa kama aina fulani wa wafuasi wa dini ya Uyuda.)
    2. Soma Matendo 9:3-5. Je, endapo ungekuwa Sauli, ungefikiria nini?
    3. Soma Matendo 9:6-7. Mashuhuda wanathibitisha jambo gani? (Hii inaandikwa kwa namna ya kushangaza. Inaonekana watu walioambatana na Sauli waliiona nuru na kuisikia sauti ya Yesu. Hata hivyo, hawakumwona mtu yeyote.)
    4. Soma Matendo 9:8-9. Unadhani kitu gani kilimpofusha Sauli? (Nuru. Mwanga mkali unaweza kukupofusha angalao kwa kitambo fulani.)
      1. Kwa nini Sauli hakula wala kunywa? (Hebu jiweke kwenye nafasi yake: kwa dhahiri kabisa Yesu yu hai, na Mungu pia, na umekuwa ukiwashambulia wafuasi wake. Hiyo si hali nzuri.)
    5. Soma Matendo 9:10-14. Je, Anania anadhani kuwa Mungu hafuatilii habari zilizotokea hivi karibuni? Kwamba kwa namna fulani hakupata makala iliyoandikwa kwenye gazeti la Yerusalemu iliyomwelezea huyu mtu aitwaye Sauli? (Hii inaonekana kuwa fursa kubwa ya kupeleka injili hadi Anania anaposikia jina la mtu anayekwenda kumtembelea. Bahati nzuri ni kwamba Mungu anavumilia majibu ya ukimya (ki-ububu) kutoka kwetu.)
    6. Soma Matendo 9:15-16. Je, maelekezo haya yatamfanya Anania ajisikie vizuri? (Mungu anaonyesha kuwa anamfahamu Sauli. Ubashiri wangu ni kwamba rejea ya kuteseka kwa Sauli inadhamiria kumfanya Anania ajisikie vizuri kuhusu rekodi ya mateso ya Sauli.)
    7. Soma Matendo 9:17-19. Je, hiki ndicho alichokitarajia Sauli?
      1. Je, Sauli ametubu? Je, kuna sababu yoyote ya kutufanya tuamini kwamba Sauli amebadilika? (Soma Matendo 9:11-12. Sauli alikuwa akiomba na Mungu akamtumia ujumbe kuhusu Anania na yeye (Sauli) kuponywa.)
      2. Je, umewahi kujiingiza kwenye dhambi kubwa ya kutisha, na kisha ukatubu na kujisikia afueni baada ya kusamehewa? Je, hicho ndicho kimemtokea Sauli? (Kitendo hicho kinaonekana kumtokea Sauli. Anabatizwa, anakula na kupata nguvu tena baada ya majaribu haya.)
    8. Soma Matendo 9:20-22. Kwa nini Paulo hakutumia miaka kadhaa kujifunza Biblia, ajifunze mambo kadhaa kutoka kwa wanafunzi wa Yesu waliokuwepo, na kisha atoke na kwenda kuhubiri? (Soma Matendo 23:6 na Matendo 22:2-3. Akiwa kama Mfarisayo aliyefundishwa chini ya Gamalieli, Sauli alikuwa mwanafunzi wa kiwango cha juu kabisa wa Biblia. Alitumia maarifa aliyokuwa nayo, na akayaboresha ili yaendane na ufunuo wa kwamba Yesu ndiye Masihi aliyetabiriwa na kuahidiwa. Pia tunafahamu kutoka katika kitabu cha Wagalatia 1:15-18 kwamba baadaye Sauli aliondoka Dameski na akatumia muda wa miaka mitatu kujifunza.)
    9. Soma Matendo 9:23-25. Watu waliuitikiaje uongofu wa Sauli? (Walitaka kumwua.)
  2. Makao Makuu
    1. Soma Matendo 9:26. Je, Sauli alisafiri moja kwa moja kwenda Yerusalemu kutokea Dameski? (Hapana. Paulo hatuambii kipindi cha muda kamili, lakini alikaa Arabuni kwa muda wa miaka mitatu kabla hajarejea Yerusalemu. Wagalatia 1:18. Baada ya kujifunza kwa muda wa miaka mitatu (“Mungu … alipoona vyema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake,” (Wagalatia 1:15-16), alirejea katika makao makuu ya Yerusalemu.)
      1. Je, nawe ungekuwa unamwogopa Sauli? (Sauli anaanzisha mateso yanayohusisha kuwaua Wakristo, kisha anapotea kutoka kwenye ramani kwa miaka mitatu, halafu anarejea akiwa na jina jipya. Matendo 13:9. Ndio, nitakuwa na mashaka.)
    2. Soma Matendo 9:27-30. Je, kipindi Paulo alipokuwa makao makuu kilikuwa na manufaa yoyote? (Ndiyo. Barnaba ni mtu mwerevu na anamkubali Paulo. Kisha, Wakristo waliopo Makao Makuu wanamsaidia Paulo kuwaponyoka wale wanaotaka kumwua.)
  3. Jukumu
    1. Soma Wagalatia 2:1. Utakumbuka kwamba Paulo alitoroka kutoka Yerusalemu ili kuwakwepa wale waliokuwa wanataka kumwua. Kipindi hiki cha miaka 14 kinaonekana kuonesha kipindi ambacho Paulo alikuwa kwenye kazi yake ya utume kwa Mataifa katika eneo la “Asia Minor” (maeneo ya Uturuki).)
    2. Soma Wagalatia 2:2. Inawezekanaje Paulo awe anapiga mbio bure? (Viongozi wanaweza wasiwe wanaikubali kazi yake kwa Mataifa kama kazi halali.)
      1. Paulo anasema (“wale wanaoonekana kuwa viongozi.” Je, hawafahamu walio viongozi wa kanisa?
    3. Soma Wagalatia 2:3-5. Mtazamo wa Paulo ni upi kuhusu kama waongofu wapya wanatakiwa kutahiriwa kwa mujibu wa maelekezo ambayo Mungu alimpa Ibrahimu? (Mwanzo 17:9-11)?
      1. Kwa nini ndugu wawe wa “uongo“ endapo tu wanahoji kile Mungu alichomwambia Ibrahimu?
    4. Soma Wagalatia 2:6-7. Paulo anaonekana kuwa na staha kiasi gani kwa uongozi? (Baadhi ya ukosoaji wa uongozi wa kanisa unanifanya niwe mnyenyekevu. Lakini, hapa Paulo naonekani kutoonesha staha.)
    5. Soma Wagalatia 2:8. Paulo anasema kuwa rejea muhimu ya kuamua kama unatenda jambo sahihi ni ipi? (Mungu kuwa mtendaji katika kazi yako ya utume.)
      1. Tafakari jaribu hilo. Je, kuna mashirika ya kidini unayodhani kuwa hayautangazi Ufalme wa Mungu, lakini yanaonekana kusitawi?
        1. Ikiwa hivyo ndivyo, je, unaelezeaje hali hiyo? (Soma Marko 9:38-40. Kwa dhahiri, Mungu alikuwa pamoja na Paulo. Yesu anafundisha kuwa “hema” ni kubwa linapokuja suala la kuitangaza injili.)
    6. Soma Wagalatia 2:9-10. Je, “Yakobo, Petro na Yohana” ndio nguzo za kanisa la awali? (Ndiyo!)
      1. Je, hii inamaanisha kwamba Paulo haoneshi staha kwa viongozi wa kanisa wanaokubalika?
      2. Au, je, tuchukulie kwamba Paulo alikuwa nje ya mji kwa muda wa miaka 14? (Namna bora ya kuangalia jambo hili ni kwamba muda mrefu uliopita, Paulo alipokuwa mjini, alikutana na Petro na Yohana kwa muda mfupi tu. Wagalatia 1:18-19. Paulo si mtu anayefahamu kwa undani masuala ya Yerusalemu. Anasema kuwa kazi yake kwa Mataifa inategemezwa na watu aliodhani kuwa ni viongozi wa kanisa la awali.)
    7. Soma Wagalatia 2:11-13. Je, sasa mtazamo wako umebadilika? Je, sasa Paulo anawakosoa Petro na Yakobo, “nguzo zinazosifika na kuheshimika” za kanisa la awali? (Uzito wa ushahidi unaonesha kuwa Paulo haoneshi staha.)
      1. Kuna nini cha kujifunza kwa ajili ya kazi yetu ya utume? (Viongozi si wakamilifu mara zote. Si mara zote wanayaelewa mapenzi ya Mungu kwa ukamilifu. Petro anao ujumbe kutoka kwa Mungu moja kwa moja – hicho ndicho anachokizungumzia katika Wagalatia 1:15-17. Katika hali hii hatatofautiana na wanadamu.)
    8. Soma Wagalatia 2:14-16. Ujumbe wa Paulo una umuhimu gani? (Umuhimu wa injili! Umuhimu wa kuhesabiwa haki kwa imani. Sasa tunaona kwa nini Paulo hakuyumba katika ujumbe huu.)
      1. Soma tena Wagalatia 2:13. Barnaba ni mshirika wa kutumainiwa wa Paulo. Suala hili lina ugumu kiasi gani? (Inaonesha kuwa watu wenye imani njema wapo kwenye pande zote mbili katika suala la tohara. Lakini, Paulo anajenga hoja kwamba kuna upande mmoja pekee ulio sahihi, na ni upande unaoendana na kafara ya Kristo, lakini hauendani na maelekezo ya Mungu kwa Ibrahimu.)
      2. Je, tuna masuala kama hayo kanisani leo?
    9. Soma Wagalatia 2:20-21. Rafiki, je, umeiweka kando neema? Kama ndivyo, kwa nini usiamue sasa hivi kuungana na Paulo katika dhamira yake ya kuishi maisha ya kuhesabiwa haki kwa imani!
  4. Juma lijalo: Paulo: Utume na Ujumbe.