Roho Mtakatifu: Kazi Itendwayo Nyuma ya Pazia
Utangulizi: Kichwa cha somo letu kinatupatia changamoto ya uelewa wetu juu ya Roho Mtakatifu. Ninapolifikiria “jukwaa” ninakumbusha onyesho lenye matukio kadhaa. Je, umaarufu wa Roho Mtakatifu unategemeana na “matukio?” Je, matukio hayo yanategemea mahali onyesho linapofanyika? Nadhani inategemeana na mahali yanapofanyika. Fikiria juu ya uelewa wetu wa kawaida wa utendajikazi wa Mungu Baba. Yesu, kwa mujibu wa kitabu cha Waebrania, anatenda kazi kama Kuhani wetu Mkuu katika hekalu la mbinguni, akitoa kafara yake kwa ajili yetu [kwa niaba yetu]. Hapa duniani, Roho Mtakatifu anachukuliwa kama mbadala wa Yesu anayepatikana kila mahala. Roho anakaa ndani ya Wakristo ili kuuendeleza Ufalme wa Mbingu. Mungu Baba anauongoza ulimwengu. Ingawa tunaweza kubishana kuhusu kazi halisi ya kila mmoja, mawazoni mwangu Roho Mtakatifu anaonekana kuwa msitari wa mbele na mhimili maishani mwetu, kwenye “matukio”yetu ya kisasa. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tuone Biblia inachotuambia kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu kwenye “mazingira” mbalimbali katika historia ya ulimwengu!
1) Uumbaji
a) Soma Mwanzo 1:1-2. Unadhani kwa nini Mungu alianza ufunguzi wa Biblia kwa Mwanzo 1:1? Kati ya mambo yote ambayo Mungu angeweza kuyasema ili kujitambulisha kwetu, kwa nini achague kauli hii?
i) Je, Roho Mtakatifu ndiye mshirika wa kwanza katika Utatu Mtakatifu anayetambulishwa kwetu katika Biblia?
ii) Mojawapo ya ukosoaji wa Ukristo uliofanywa na dini mbili kuu zinazoamini juu ya uwepo wa Mungu mmoja ni kwamba kiuhalisia Ukristo hauamini juu ya uwepo wa Mungu mmoja kwa sababu Ukristo unaamini katika Mungu watatu. Wakosoaji hao wanasema kuwa Mungu hana baba wala mwana. Vifungu hivi vinasababisha tatizo gani kwenye hoja yao dhidi ya Utatu Mtakatifu? (Neno la Kiebrania lililotumika katika Mwanzo 1:1 kumaanisha Mungu ni “Elohim,” ambalo halimaanishi umoja bali uwingi. Hivyo, wale wanaopinga Utatu Mtakatifu wanapaswa, tangu mwanzo kabisa mwa ufunuo wa Mungu mwenyewe kwetu, kuelezea kwa nini neno la uwingi linatumika na kwa nini Roho Mtakatifu anarejewa yeye binafsi.)
b) Soma Mwanzo 1:3. Nani anayezungumza, Mungu Baba au Roho wa Mungu? Endapo ni Roho Mtakatifu, ni vigumu sana wajibu huu kuwa “nyuma ya pazia!”
i) Soma Yohana 1:1-3. Vifungu hivi vinasema kuwa nani aliyeumba ulimwengu? (Ukisoma hii sura yote, utaelewa kwamba “Neno” ni rejea ya Yesu. Hivyo, hii inasema kuwa Yesu aliumba ulimwengu.)
ii) Soma Wakolosai 1:15-16. Vifungu vinasema kuwa nani aliumba ulimwengu? (Yesu.)
iii) Soma Mwanzo 1:3, Mwanzo 2:7 na Ayubu 33:4. Vifungu vyote hivi vitatu vina jambo gani moja linalofanana? (Kutoa pumzi. Tunapozungumza tunatoa pumzi, tunapompumulia mtu pumzi mdomoni tunatoa pumzi. Ayubu anasema kuwa pumzi hii ni “Roho ya Mungu.”)
iv) Tunapaswa basi kuhitimisha nini kuhusu Uumbaji na wajibu wa Roho Mtakatifu? (Kwa mahsusi Biblia inabainisha kuwa “Mungu,” Yesu na Roho Mtakatifu walihusika katika Uumbaji. Nadhani ujumbe ni kwamba Washirika wote watatu katika Utatu Mtakatifu walihusika. Hata hivyo, Roho Mtakatifu katika kitendo cha kutamka na Uumbaji ukafanyika, na katika kupulizia pumzi ya uhai kwa wanadamu, kinachukua nafasi na wajibu wa muhimu sana.)
2) Tukio Letu Kivitendo
a) Soma Kutoka 25:8-9. Hekalu la Mungu duniani lilitakiwa kutengenezwaje? (Na wanadamu, kwa mujibu wa maelezo kamili ya Mungu.)
b) Soma Kutoka 31:1-5. Unaweza kuiitaje taaluma ya Bezaleli hii leo? (Yeye ni fundistadi katika sanaa na kazi za mkono. Yeye ni msanii. Anatengeneza vitu kwa kutumia rasilimali za aina mbalimbali. Anafanya kazi kwa mikono yake.)
i) Roho Mtakatifu anamtendea nini Bezaleli? (Anampatia hekima, maarifa na ujuzi katika kazi za mikono yake.)
ii) Hiyo inatufundisha nini juu ya Roho Mtakatifu na kazi zetu? Roho Mtakatifu anaweza kuchukua wajibu gani katika kazi zetu kila siku za maisha yetu? (Roho Mtakatifu sio tu chanzo cha uelewa wa mambo ya kiroho, bali pia anatupatia hekima, maarifa na ujuzi wa kufanya kazi zetu za kila siku – hata kama kazi hiyo ni ya ujenzi! Je, umemwomba Roho Mtakatifu akufanye uwe bora kazini kwako?)
iii) Hapa utagundua kwamba kazi ya “ujenzi” ilikuwa ni kazi ya kujenga hekalu. Unadhani hiyo inaleta utofauti? Je, bado Roho Mtakatifu angetoa usaidizi ikiwa Bezaleli angekuwa anafanya ubunifu na ujenzi wa jirani yake? (Ndiyo. Soma 1 Petro 4:10 na Warumi 12:6-8. Tunaweza kuwa na karama ya “kutoa huduma” au “kusaidia mahitaji ya watu wengine” na hii ni karama ambayo mtu anapewa na Mungu.)
3) Mazingira (mandhari) ya Mawazo Yetu
a) Soma Yohana 16:13-14. Tulijifunza vifungu hivi juma lililopita, lakini hebu tuone kama tunaweza kuona jambo jipya. Yesu anasema kuwa Roho Mtakatifu atatuongoza kwenye “kweli yote.” Kuufahamu ukweli kunamfanyia nini Yesu? (Kunampa utukufu.)
i) Je, ulimwengu unahoji kwamba sayansi inapingana na Biblia? Vifungu hivi vinatuambia nini? (Ukweli uko upande wa Yesu. Ukweli unaendana na Mungu wetu kiasi kwamba ukweli humpa Yeye utukufu.)
b) Soma Yohana 15:26. Maneno gani yanatumika kwa Roho Mtakatifu? (“Msaidizi [Mshauri]” na “Roho wa kweli.” Hii inatia msisitizo kwenye wazo la kwamba Roho Mtakatifu yupo hapa kwa ajili ya kutuongoza kwenye kweli na kutuletea hiyo kweli.)
i) Ni “ukweli” gani mahsusi unaotajwa kwenye hiki kifungu? (Roho Mtakatifu “atamshuhudia” Yesu. Ushuhuda huo ni kwamba Yesu ni Mungu. Kwamba Yesu alifanyika mwanadamu ili kutuokoa kutoka dhambini mwetu.)
c) Baadhi ya watu wanahoji kwamba kumzingatia sana Roho Mtakatifu unaweza kuondoa uzingativu kwa Yesu. Je, umeliona hilo?
i) Unadhani hilo linawezekana?
d) Soma Matendo 2:1-4. Jiweke kwenye nafasi hii kisha uniambie uzoefu unaoupitia? (Sauti ya uvumi wa upepo, kushuhudia ndimi za moto zikiwakalia watu, na sauti za lugha za kigeni.)
i) Ikiwa nitakuuliza kama Roho Mtakatifu alijizingatia yeye mwenyewe au alimzingatia Yesu kwenye haya matukio, utasemaje?
e) Soma Matendo 2:14 na Matendo 2:22. Unasemaje sasa kuhusu zingatio la kazi ya Roho Mtakatifu kwenye haya matukio? (Mwanzoni inaweza kuonekana Roho Mtakatifu alikuwa anajizingatia kwa sababu ya hizi sauti na mionekano isiyo ya kawaida. Lakini, tunaona kuwa hii ilikuwa tu njia iliyotumiwa na Roho Mtakatifu ili kupata usikivu wa watu ili kwamba ukweli kumhusu Yesu uweze kuwasilishwa. Kutokana na jambo hili tunajifunza kwamba matukio yasiyo ya kawaida yaliyoanzishwa na Roho Mtakatifu ni ya muhimu katika kuzingatia wokovu kupitia kwa Yesu.)
4) Roho Mtakatifu Akitenda Kazi Pamoja na Yesu
a) Soma Luka 1:30-33. Ungeielewaje ahadi hii endapo ungekuwa Mariamu?
b) Soma Luka 1:34. Swali la muhimu kabisa mawazoni mwa Mariamu ni lipi? (Yeye ni bikira. Sio tu kwamba atakuwa na wakati mgumu sana kimaumbile wakati wa kujifungua, bali pia ujauzito utamfanya aonekane mbaya.)
i) Kutokana na ahadi kwamba Mariamu atakuwa mama wa “Mwana wa Aliye Juu,” unaelezeaje kwamba hili ndilo swali “kati ya mambo yote” analoamua kuliuliza?
c) Soma Luka 1:35 na 1 Petro 3:18. Hii inazungumzia nini juu ya uwezo wa Roho Mtakatifu? (Hii inatukumbusha kwamba Mwanzo 2:7 inatuambia uwezo wa kuanzisha uhai umo ndani ya Roho Mtakatifu.)
i) Vifungu hivyo vinasema nini juu ya wajibu ambao Roho Mtakatifu anaweza kuutimiza maishani mwako? (Ikiwa wewe, kama ilivyo kwa Mariamu, uko radhi kutumiwa na Roho Mtakatifu, anaweza kuyajaza maisha yako kwa uwezo usio wa kawaida! Anaweza kukuhuisha!)
d) Soma Luka 1:38. Hii inatuambia nini kuhusu Mariamu? (Bila kujali matatizo yanayoakisiwa kwenye swali lake la “Litakuwaje neno hili,” hii ni kauli ya imani ya kustaajabisha sana.)
e) Soma Luka 3:21-22 na Luka 4:1-2. Hii inatuambia kuwa Yesu alibatizwa katika Roho Mtakatifu na kwamba “alijawa” Roho Mtakatifu. Kwa nini hilo ni la muhimu wakati Yesu ni Mungu? (Ingawa tuna uwezo mdogo wa kuelewa, jambo hili lina mantiki sana. Utatu Mtakatifu “umejawa” na Roho Mtakatifu.)
i) Soma Mwanzo 1:26-27. Hii inaashiria nini kuhusu wewe na mimi na Roho Mtakatifu? (Kwamba kama kweli unataka kufanana na Mungu, unatakiwa kujawa na Roho Mtakatifu pia!)
f) Soma Wagalatia 5:22-26. Je, wazo la kuwa na Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu ni dhana ya kufikirika? (Hapana. Vifungu hivi vinatuonesha kuwa Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu hutupatia mabadiliko ya kivitendo na ya muhimu maishani mwetu. “Tunaishi kwa Roho.”)
g) Rafiki, je, utamwomba Roho Mtakatifu akae ndani yako ili alete tofauti maishani mwako kivitendo? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?
Juma lijalo: Uungu wa Roho Mtakatifu.