Uaminifu kwa Mungu

Swahili
(Luka 16, Matendo 5, Malaki 3)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.                           

 

Utangulizi: Miaka mingi iliyopita nilikutana na kikundi cha walimu wa shule ya serikali ambao walitaka kujifunza zaidi mambo gani yalihitajika katika kupata unafuu uliopo kwenye ajira za mashirika ya dini. Walikuwa na vipingamizi vya kidini kuhusu kutegemeza chama cha wafanyakazi. Jibu fupi walilokuwa nalo ni kwamba walihitaji kukiambia chama cha wafanyakazi juu ya imani zao za dini, na kuomba kwamba waruhusiwe kulipa michango ya chama kwenye shirika au chama cha kusaidia wenye shida ambacho wao na chama hicho cha wafanyakazi watakubaliana. Walimu hao walipokuja mahali pa kukutania, niligundua kuwa mmoja wao alikuwa na gari zuri jipya aina ya Cadillac. Baadaye, mmiliki wa gari hili aliuliza ikiwa nafuu hii ya shirika la kidini ilimaanisha kuwa anapaswa kujiuzulu kazi katika chama cha wafanyakazi. Nilishangaa, unawezaje kuwa na vipingamizi vya kidini kwa chama cha wafanyakazi na utake kusalia kuwa mwajiriwa wake? Fumbo hili lilifumbuliwa aliposema kuwa anahitaji kuwa mjumbe ili aweze kununua bima ya gari kwa bei ya chini! Imani yake ilikuwa na gharama, na gharama hiyo ilikuwa ni tofauti katika kiwango cha malipo ya bima. Angalia kama kutokuwa mwaminifu kunaweka gharama kwenye imani yako. Hebu tuchimbue namna mpya ambazo Biblia inaelezea maana ya kutokuwa na uaminifu.

 

 1.    Kufasili (kuelezea) Maana ya Kutokuwa na Uaminifu

 

  1.    Soma Luka 16:10-11. Utakumbuka kuwa hapo awali tulijadili kwa kina kisa kinachoelezea muktadha wa kauli hii. Hebu tusome tena kisa hicho ili kwamba sote tuwe na uelewa mmoja. Soma Luka 16:1-8. Ikiwa tukifasili kutokuwa na uaminifu kama suala rahisi la kutowadanganya watu, basi inaonekana tunahitaji fasili mpya, sawa? Yesu anaonekana kumsifia mwongo!

 

   1.    Kutokana na kisa cha meneja asiye mwaminifu, unafasili vipi hali ya kutokuwa na uaminifu? (Kushindwa kuwa mwerevu kwa fedha za Mungu. Kushindwa kutumia akili ya kawaida.)

 

   1.    Hebu tutafakari mambo kadhaa ambayo nimeyabainisha. Hospitali zenye uhusiano na kanisa langu zinawaajiri maafisa utawala ambao mara nyingine wanalipwa mara kumi zaidi ya anavyolipwa afisa tawala wa kanisa. Unadhani hiyo ni haki? Je, huo ni uaminifu?

 

    1.    Pia nimegundua kwamba kanisa linapokabidhiwa kuendesha biashara, biashara hiyo hufifia na hatimaye kufa. Kwa nini mshiriki wa kanisa anapokuwa anamiliki biashara, biashara hiyo inasitawi, na biashara inapokabidhiwa kwa kanisa, inafifia? (Binafsi ninaona kwamba kuwalipa wataalamu mishahara mikubwa ni kuwa na uhakika kwamba hospitali zinasitawi (tukichukulia kwamba kimsingi zinasitawi), ni kitendo cha werevu. Pia ninaona kwamba kuwakabidhi biashara watu wasio na utaalamu (na hawalipwi mishahara inayowastahili wataalamu), ambayo matokeo yake ni kufa kwa biashara hiyo ni kitendo cha kutokuwa na uaminifu – kwa mujibu wa fasili ya mfano wa Yesu kumhusu meneja asiye mwaminifu.)

 

    1.    Je, mambo mengine si “jambo la uaminifu mdogo?” (Uaminifu ambao Yesu alikuwa anauzungumzia, kwa muktadha alioutoa, si jambo dogo. Ni suala la kutoa mali zote kwa ajili ya kuutangaza Ufalme wa Mungu, badala ya kuwa suala la wizi.)

 

 1.   Kutokuwa na Uaminifu wa Kiroho

 

  1.    Soma Matendo 5:1-2. Je, kuna jambo lolote lisilo la uaminifu hadi kufikia hapa? (Hapana.)

 

  1.    Soma Matendo 5:3-5. Jambo gani lisilo la uaminifu na jambo gani ni la uaminifu? (Kitendo cha uaminifu ni kuzuia sehemu ya fedha za ardhi unayoimiliki, na kutoa fedha zilizosalia kwa Mungu. Kitendo kisicho cha uaminifu ni kusema uongo kama umetoa hesabu kamili ya fedha za mauzo yote kwa Mungu.)

 

   1.    Kitu gani kiliwahamasisha Anania na Safira kujiingiza kwenye uongo huu? (Soma Matendo 4:32-35. Walitaka waonekane watakatifu na wenye kujitoa kikamilifu kama watu wengine. Kwa kuangalia mambo yote haya kwa pamoja, vifungu hivi vinaonesha kwamba hakuna aliyetakiwa kuuza kiwanja chake au nyumba yake, lakini baadhi yao walifanya hivyo.)

 

    1.    Je, utaiita dhambi hii kuwa ni ya majivuno? Au, uroho?

 

    1.    Je, hii ni aina ya kutokuwa na uaminifu?

 

    1.    Je, jaribio lolote unalolifanya ili uonekane mtakatifu zaidi au mwenye kujitoa zaidi kuliko jinsi ulivyo ni dhambi?

 

  1.    Soma Matendo 5:7-11. Hapa Petro anasema kuwa dhambi ni ipi? (“Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana?”)

 

   1.    Walimjaribuje Roho Mtakatifu? Roho Mtakatifu anaujua ukweli, hivyo hakudanganyika.

 

   1.    Utaona kwamba Matendo 5:4 pia inasema kuwa hapa dhambi ni kumdanganya Mungu. Unawezaje kumdanganya Mtu anayefahamu kila kitu?

 

  1.    Soma Yohana 12:4-6. Ikiwa kuchukua fedha za Mungu kuwasilisha vibaya utakatifu wako ni dhambi, kwa nini basi Yuda hakuuawa kwa kile kinachotaarifiwa kwenye vifungu hivi?

 

  1.    Hebu turuke vifungu vichache katika Matendo 5 ili tuone kama tunaweza kutambua vizuri zaidi dhambi iliyosababisha vifo vya Anania na Safira. Soma Matendo 5:12, 14-16. Kwa nini watu wanaponywa hata kama jambo linalohusika ni kivuli cha Petro kuwaangukia? (Ni uwezo wa Roho Mtakatifu. Ni kuamini katika uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

   1.    Je, Anania na Safira walimwamini Roho Mtakatifu? (Hapana. Hawakuamini katika uwezo wa Roho Mtakatifu, vinginevyo wangejua kwamba wasingeweza kumdanganya. Nadhani hicho ndicho kiini cha sababu ya wao kuhukumiwa mara moja. Walimfikiria Roho Mtakatifu kwa kiwango cha chini sana kiasi kwamba waliamini kuwa wangeweza kumdanganya yeye na mawakala wake, mitume, katika kipindi ambacho Roho Mtakatifu alikuwa anafanya kazi katika kiwango cha juu kabisa cha uwezo wake.)

 

 1. Uwezo wa Zaka

 

  1.    Soma Mambo ya Walawi 27:30-34. Kifungu cha mwisho kinasema kuwa maagizo haya yalitolewa kwa ajili ya wana wa Israeli. Je, maagizo hayo yanahusika kwetu leo?

 

  1.    Soma Waebrania 7:5. Nani anayestahili zaka? (Wana wa Lawi.)

 

   1.    Je, tunao uzao huo hapa leo?

 

  1.    Soma Waebrania 7:1-2 na Waebrania 7:6-10. Utoaji zaka wa Ibrahimu una uhusiano gani na mfumo wa kafara, Walawi, au maagizo ya Sinai? (Hauna uhusiano, isipokuwa tu kusema kwamba Ibrahimu alitoka katika ukoo wa Lawi, na Ibrahimu alitoa zaka kwa Melkizedeki.)

 

   1.    Hiyo inaashiria nini kwetu leo? (Kwamba ni jambo jema kutoa zaka, kwamba tunao mfano wa utoaji zaka usio na uhusiano na mfumo wa huduma ya kafara.)

 

  1.    Soma Malaki 3:8-11. Je, unaamini anachokisema Mungu kuhusu baraka zitokanazo na utoaji zaka?

 

   1.    Ikiwa huamini, je, uko sawa na Anania na Safira?

 

  1.    Hebu tujikite kwenye Malaki 3:10-11 kama tukio la uwekezaji. Tuchukulie kwamba dalali wa bidhaa anakujia na kukwambia kwamba ikiwa utawekeza asilimia 10 ya fedha zako kwenye huu mfuko mmoja, utapata faida zisizo na kikomo. Utasemaje? Utasemaje ikiwa dalali amekuwa katika kazi hiyo miaka yote, na alikuwa na hadhi na sifa kubwa katika fani yake? (Ningesema kuwa hebu tuwekeze! Hili ni jambo zuri sana la kibiashara!)

 

   1.    Sasa tuchukulie kwamba watoto wa mtu tajiri sana wanakujia na kulalamika kwamba baba yao anawatakas wawekeze kwenye mpango huu. Je, ungeshauri waangalie namna ya kuepuka huu uwekezaji? Au watafute namna ya kutafsiri upya maelekezo ya baba yao? (Mtu yeyote mwenye kutumia akili ya kawaida, mtu yeyote mwerevu, angesema, “Unanitania? Unapinga kupata utajiri?” Nadhani jambo la muhimu zaidi halizungumzii suala la zaka kuhitajika leo, kinachomaanishwa ni kwamba ni nani hatachukulia fursa hii kwa umakini? Hususani, pale ambapo upande wa chini unaweza kuwa unamwibia Mungu?)

 

   1.    Juma hili kuna mtu ametaarifu kwamba kutoa zaka kamwe hakujaonekana kumnufaisha. Utamjibuje? (Katika Malaki 3:10 Mungu anatukaribisha “tumjaribu.” Hiyo inanipa mashaka juu ya usahihi wa taarifa ya “hakuna manufaa.” Maishani mwangu, nimepitia uzoefu wa kupata faida kubwa!)

 

  1.    Soma Malaki 3:13-16. Ikiwa unatilia shaka kwamba Mungu anakupa tuzo kwa kuwa mwaminifu, kwa nini usitengeneze “hati ya ukumbusho” kukukumbusha baraka zake? Ifanye iwe hai kila mara!

 

  1.    Soma Malaki 3:12. Je, unajisikia furaha kuwapatia zawadi watu wengine?

 

   1.    Endapo mngekuwa na taifa la watoa zawadi, je, mngeliita “taifa lenye furaha?” (Tatizo ni mtazamo tunaouleta kwenye utoaji zaka. Ukiuchukulia kama ni mzigo na punguzo la kipato chako, basi umeshindwa kabisa kuelewa anachokimaanisha Mungu. Ukarimu sio tu kwamba unaiinua nafsi yako na kukupatia furaha, bali pia unakutajirisha.)

 

  1.    Rafiki, je, unaanza kuona kwamba “uaminifu kwa Mungu” sio tu kuepuka kusema uongo? Ni suala la umahiri katika kushughulika na mambo yake. Ni kuamini katika uwezo na mamlaka ya Roho Mtakatifu. Ni mtazamo wa ukarimu unaoakisi baraka maishani mwako. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, aubadilishe moyo wako ili ukumbatie baraka za ukarimu?

 

 1.   Juma lijalo: Matokeo ya Utoaji wa Zaka.