Somo la 5: Kukiuka Kusudio la Sheria

(Nehemia 5)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
4
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Umaskini husababishwa na nini? Nchini kwangu baadhi ya watu wanasema ni kwa sababu maskini walifanya chaguzi mbaya. Kama umehitimu shule ya sekondari ya juu (A-Level), ukapata kazi, usipate watoto hadi utakapooa au kuolewa, uwezekano wa wewe kuwa maskini ni mdogo sana. Watu wengine wanasema kuwa umaskini ni kosa la jamii. Unatokana na ubaguzi kwa misingi ya rangi au jinsia. Unatokana na mparanganyiko wa kiuchumi. Duniani kote, nadhani kwa kiasi kikubwa umaskini unasababishwa na sera ya serikali. Watu wengi ni maskini kutokana na athari za vita. Wengi ni maskini kwa sababu serikali inakataa kuruhusu uhuru wa kiuchumi. Wakati mwingine umaskini unakuwepo kutokana na matatizo ya hali ya hewa. Biblia inasemaje? Somo letu juma hili linahusu malalamiko juu ya umaskini. Hebu tuzame kwenye Biblia katika zama za Nehemia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu umaskini!

 

  1. Malalamiko

 

    1. Soma Nehemia 5:1-2. Mlengwa katika malalamiko haya kuhusu chakula ni nani? (Wayahudi wenzao.)

 

      1. Sababu ya umaskini iliyobainishwa ni ipi? (Wana familia kubwa.)

 

        1. Kuna kosa gani katika hilo? Kwa nini uwalaumu “Wayahudi wenzako” wakati wewe ndiye una watoto wengi?

 

      1. Hebu tujiulize swali la msingi. Nilidhani kwamba katika nyakati/zama za kilimo kuwa na watoto wengi ilimaanisha kwamba una chakula kingi, na si chakula kidogo. (Utaona kwamba kifungu cha pili kinasema “na tupate ngano.” Hiyo inaashiria kwamba hawalimi ngano yao wenyewe.)

 

    1. Soma Nehemia 5:3. Hapa sababu ya umaskini ni ipi? (Kukopa fedha.)

 

      1. Kwa nini kundi hili linakopa fedha? (Ili wapate ngano.)

 

      1. Sababu ya uhaba wa ngano ni ipi? (Njaa. Sasa hili linaanza kuleta mantiki. Kama kuna njaa, kuwa na matumbo mengi ya kuyalisha ni changamoto. Kama kuna njaa, bei ya chakula inapanda na unatafuta fedha za ziada kwa kukopa.)

 

    1. Soma Nehemia 5:4. Hapa chanzo cha umaskini ni kipi? (Sera ya serikali katika mfumo wa kodi kubwa.)

 

 

    1. Soma Nehemia 5:5. Unawezaje kulalamika kwamba umewafanya watoto wako mwenyewe kuwa watumwa? (Ingawa inaweza isiwe dhahiri, kifungu kinaelezea. Watu hawa maskini wameuza vitu vyao vingine, mashamba yao na mizabibu yao. Mali yao ya mwisho iliyosalia ni kuwauza watoto wao utumwani.)

 

  1. Jibu la Nehemia

 

    1. Soma Nehemia 5:6-7. Mwitiko wa kwanza wa Nenemia ni upi? (Amekasirika!)

 

      1. Kwa sababu gani? Je, amewakasirikia wale wanaolalamika au wale wanaolalamikiwa?

 

      1. Mwitiko wa pili wa Nehemia ni upi? (Anafanana na sisi. Anatafakari kilichosababisha huu umaskini.)

 

      1. Mwitiko wake wa tatu ni upi? (Kuwalaumu wale wanaoendesha nchi. Ameshafanya uamuzi kwamba wale wanaolalamika wako sahihi.)

 

    1. Angalia tena sehemu ya mwisho ya Nehemia 5:7. Nehemia anahitimisha kwamba chanzo cha umaskini ni kipi? (Sababu mojawapo ni kutoza riba.)

 

      1. Hebu subiri kidogo! Nina “deal” kwa ajili ya Nehemia. Akinipa $10,000 leo, nitamrejeshea miaka ishirini kutokea sasa. Je, hiyo ni haki? (Kuna kitu kinaitwa “thamani ya sasa.” Thamani ya kupata $10,000 miaka ishirini kutokea sasa ni ndogo zaidi kuliko thamani yake ya sasa. Riba inawakilisha tofauti iliyopo. Ukinipatia $10,000 sasa hivi bila kunitoza riba ninakuwa ninakuibia.)

 

    1. Soma Kutoka 22:25. Mikopo kwa maskini ilipaswa kushughulikiwaje? (Riba haikupaswa kutozwa. Hivyo, maskini walikuwa na malalamiko halali kuhusu kutozwa riba. Nehemia anasimama kidete dhidi ya utozaji riba kwa maskini.)

 

    1. Soma Kumbukumbu la Torati 23:19-20. Je, Mungu anakubaliana na dhana ya thamani ya sasa? (Ndiyo, kwa wageni. Utaona kwamba maelekezo haya kuhusu riba hayakomei kwa Waebrania maskini.)

 

    1. Soma Nehemia 5:8. Asili ya tatizo ni ipi? (Nehemia hazungumzii kwa umahsusi kuhusu kuwauza watoto kama watumwa, bali anazungumzia kuhusu kejeli ya kile kinachotokea. Wazazi wanawauza watoto wao kama watumwa kwa Mataifa, na kisha Nehemia na Waebrania wengine matajiri wanawanunua. Hili linaleta mantiki gani?

 

      1. Huna furaha kwamba Nehemia hashutumu uuzaji wa watoto moja kwa moja? (Soma Kutoka 21:2. Hatuwezi kuwa na taswira kamili pasipo kuelewa kifungu hiki. Kwa ujumla, Waebrania hawakutakiwa kuwamiliki Waebrania wenzao kwa muda mrefu. Katika mwaka wa saba, mtumwa wa Kiebrania aliachwa huru. Bila shaka hii ilishusha thamani yao, hivyo wazazi wanawauza watoto wao kwa Mataifa. Endapo wangewauza kwa Wayahudi wenzao, ingekuwa ni sawa na kuwakopesha kwa ukomo wa muda fulani.)

 

 

      1. Chanzo cha tatizo hili ni nani? Angalia tena Nehemia 5:8. Nani anayenyamaza? (Lazima hawa ni wazazi. Kwa dhahiri si matajiri ambao wanawanunua tena Wayahudi.)

 

    1. Soma Nehemia 5:9. Nehemia anaibua hoja gani hapa? (Hadhi ya Mungu. Watu wake [Mungu] wanaonekanaje machoni mwa maadui wao? Watu wa Mugu wanashughulikaje na matatizo yao?

 

      1. Huwa unajiuliza swali hilo unapokabiliana na matatizo? Sululisho lako litaonekanaje huko duniani?

 

    1. Soma Nehemia 5:10. Nehemia anafanya nini ili kutatua tatizo? (Anawakumbusha maelekezo ya Mungu katika jambo hilo na anaongoza kwa mfano. Anakopesha fedha na ngano, lakini hatozi riba.)

 

      1. Je, unawaambia watu wafanye mambo ambayo hauko radhi kuyafanya?

 

    1. Soma Nehemia 5:11-12. Matokeo ni yapi? (Wale wanaotoza riba na kuchukua mashamba ya wadeni wao wanakubali kuacha na kuwarejeshea mashamba.)

 

      1. Vipi kuhusu watoto? (Hili linapaswa kutibu tatizo la kuuza watoto. Wale wanaoteseka na njaa kwanza wanakopa ngano na fedha. Lakini, rasilimali zao zinapokuwa zimekwisha, wanawauza watoto wao. Hii inarejesha rasilimali zao.)

 

      1. Umegundua kwamba kiwango cha riba inayotozwa kimewekwa wazi hapa? Wanatoza takriban asilimia 12 kwa mwaka.

 

    1. Soma Nehemia 5:13. Nehemia anafanya jambo gani jingine ili kuwa na uhakika kwamba tatizo limetatuliwa? (Analazimisha kwamba watu wale kiapo mbele ya makuhani ili watende kama walivyoahidi. Kwa dhahiri, katika kusanyiko hili wale ambao wamekuwa wakitoza riba wanajisikia kuwa chini ya shinikizo kubwa. Hataki waje wabadili mawazo yao hapo baadaye.)

 

    1. Soma Nehemia 5:14-16. Nehemia anafanya jambo gani jingine ili kutatua tatizo la umaskini? (Anashusha kodi. Hachukui mapato ambayo anastahili kama liwali.)

 

      1. Umewahi kumsikia kiongozi wa kisiasa kama Nehemia ambaye hakuchukua mshahara wowote?

 

      1. Umewahi kumsikia kiongozi wa kisiasa ambaye anaondoa kodi ili kuwasaidia maskini?

 

  1. Kanuni za Leo

 

    1. Soma tena Nehemia 5:9. Tuliliangalia hili hapo awali. Hili ni jambo muhimu kiasi gani? (Kwani kumpa Mungu utukufu si wajibu wetu wa msingi? Nehemia anajali sana kuhusu ambavyo njia wanayoitumia Waebrania kwenye umaskini inavyoathiri hadhi ya Mungu miongoni mwa wapagani.)

 

      1. Tunawezaje kutumia kanuni hiyo leo? (Baadhi ya kanuni hizi zinatumika miongoni mwa mwili wa waumini. Si kanuni ambazo lazima ziwe sera ambayo serikali ya kidunia inapaswa kuitumia.)

 

 

    1. Kitu gani kinachoonekana kuwa chanzo kikuu cha umaskini katika Nehemia 5? (Njaa. Linaonekana kama tatizo linalotokea mfululizo. Njaa huleta shinikizo kubwa la kifedha kwa watu. Yumkini wale wenye rasilimali chache waliumizwa zaidi.)

 

      1. Kitu gani kinaweza kufanywa kuhusu njaa? (Hakuna kinachoweza kufanywa, tukichukulia kwamba njaa hiyo haijasababishwa na mwanadamu, isipokuwa kama ni kuweka akiba ya rasilimali kwa ajili ya nyakati ngumu.)

 

    1. Chanzo cha umaskini kinachofuata ni kipi? (Vitendo vya ukopeshaji.)

 

    1. Je, hivi ndivyo matatizo yanavyoibuka maishani mwako? Jambo lililo nje ya udhibiti wako linaibuka. Hujajiandaa kwa ajili ya jambo hilo. Watu wengine wanaichukulia hali yako kuwa fursa kwao.

 

      1. Tunajifunza nini kutoka kwa Nehemia? (Kuyageukia majibu ya Mungu kwa matatizo yetu. Kuenenda kile tunachokihubiri. Kudai uwajibikaji.)

 

    1. Rafiki, utafanya suala la kumtukuza Mungu kuwa kipaumbele maishani mwako?

 

  1. Juma lijalo: Kusomwa kwa Neno.