Somo la 12: Toka Kaskazini na Kusini Hadi Nchi Nzuri

(Danieli 11)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Hebu tufanye mapitio. Majuma matatu yaliyopita tulimwona Danieli akiomba na kufunga kwa ajili ya kufunuliwa uelewa wa maono ya kutisha aliyoyaandika katika Danieli 8. (Angalia Danieli 8:27.) Gabrieli alimwendea Danieli katika somo letu majuma mawili yaliyopita (Danieli 9) ili kutoa ufafanuzi wa yale maono. Juma lililopita, katika Danieli 10, Danieli anapokea ufunuo juu ya “vita vikubwa.” Kwa mara nyingine, anafanya maombi ili kupata uelewa. Gabrieli anakuja tena ili kutoa ufafanuzi. Juma hili pamoja na juma lijalo, tunajifunza hivi vita vikubwa. Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze zaidi!

 

 1.     Ufafanuzi wa Gabrieli

 

  1.     Soma Danieli 11:1. Nani anayezungumza? (Soma Danieli 10:20-21. Gabrieli anaendeleza anachokisema kwa Danieli katika sura ya 10 kuhusu pambano lisilo la kawaida dhidi ya viongozi wa Uajemi na Uyunani.)

 

   1.     Haya yanatokea katika kipindi gani? (Mwaka wa kwanza wa ufalme wa Umedi na Uajemi.)

 

  1.     Soma Danieli 11:2. Danieli alipatwa na maono kadhaa kuhusu Umedi, Uajemi na Uyunani. Je, hizi ni taarifa za kina zaidi kuhusu ufunuo ule ule? (Kwa kuwa Gabrieli anazungumza kabla Koreshi hajawa mfalme wa himaya ya Umedi na Uajemi, lazima tutakuwa tunawaangalia wafalme watatu waliomfuatia Koreshi wa Uajemi. Wanamaoni wanambainisha huyu mfalme wa nne kama Artashasta, ambaye, kwa mujibu wa Heredotus, alitumia miaka minne kuandaa safari (expedition) dhidi ya Uyunani.)

 

  1.     Soma Danieli 11:3-4. Je, Uajemi iliishinda Uyunani? Ikiwa sivyo, huyu “mfalme mwenye nguvu” ni nani? (Uajemi haikuishinda Uyunani. Kimsingi, Uyunani, chini ya uongozi wa Alexander Mkuu, baadaye iliivamia Uyunani na kuishinda. Alexander Mkuu alifariki katika umri mdogo sana. Matokeo yake, ufalme wake uligawanywa miongoni mwa majenerali wake wanne wakuu.)

 

  1.     Soma Danieli 11:5-8. Tunasoma habari za “Mfalme wa Kaskazini” na “Mfalme wa Kusini,” na tunaona taarifa nyingi kupita kiasi juu ya mshirika, usaliti, na hata kumhusu mwanamke anayejihusisha kwenye sakata la kushindania madaraka. Huyu “Mfalme wa Kusini” ni nani? (Kuna ukubaliano mkubwa miongoni mwa wanamaoni kuhusu historia hii. Lakini, tuna uthibitisho kamili kutoka kwenye Biblia. Kwa mahsusi Danieli 11:7-8 inabainisha vyombo kutoka kwenye “ngome” ya “Mfalme wa Kaskazini” vikipelekwa “Misri.” Hii inaendana na historia. Seluceucus, mmojawapo wa majenerali wa Uyunani, aliidhibiti Shamu (kwa upande wa kaskazini) na jenerali mwingine, Ptolemy, aliidhibiti Misri. Walikuwa na vita vingi kati yao.)

 

   1.     Tunapozungumzia kuhusu kaskazini na kusini, tunarejea jambo gani? (Yerusalemu. Hiki ndicho ambacho Danieli anakijali na kujihusisha nacho sana.)

 

  1.     Tutaruka Danieli 11:9-15 kwa sababu zinafafanua tu kwa kina zaidi mapambano kati ya Mfalme wa Kaskazini na Mfalme wa Kusini. Soma Danieli 11:16. Unadhani “Nchi Nzuri” ni ipi? (Soma Ezekieli 20:15. Hii ni Israeli. Sasa tunaona sababu ya taariza zote hizi za kina. Gabrieli anamwambia Danieli kwamba Israeli itavamiwa tena.)

 

  1.     Soma Danieli 11:19. Hii inatuambia nini kuhusu Mfalme wa Kaskazini? (Nguvu yake inakoma. “Hataonekana tena.”)

 

  1.     Soma Danieli 11:20-21 na Danieli 8:23. Utaona kwamba vifungu vyote viwili vinamrejelea mtu anayechukua mamlaka kwa kutumia njama. Unadhani hii inamwakilisha nani? (Umegundua kwamba Danieli 11 inaendana na Danieli 8 kwa namna nyingi? Ingawa wanamaoni wengi wanadhani hii inamrejelea Antiokasi Epifanesi, tulipojifunza Danieli 8 tuliona kwamba Rumi ya Upapa ndio inayoendana vizuri zaidi. Hiyo inamaanisha tuna kipindi cha mpito hapa, huenda kwa kuanzia kwenye Danieli 11:16, hadi kwenye upagani na Rumi ya Upapa. Hivyo, huu ni mwendelezo wa maono yaliyotangulia.)

 

  1.     Soma Danieli 11:22. Mkuu wa maagano ni nani? (Ninaamini kwamba huyu ni Yesu. Hiyo inaleta mantiki ikiwa Rumi ya kipagani ndio mamlaka yanayorejelewa hapa. Tatizo ni kwamba Danieli 11:22 haiwezi kurejelea Rumi ya Upapa na Danieli 11:22 kumrejelea Yesu.  Suluhisho la jambo hili ni kumbainisha mtu wa hila kama Tiberius, mfalme mwovu wa Rumi aliyetawala wakati Yesu aliposulubiwa.)

 

 1.   Mpito Kuelekea Siku Zijazo – Nadharia Mbili

 

  1.     Soma Danieli 11:27-28 na Danieli 11:40. Hebu subiri kidogo! Hapo awali tulisoma kwamba Mfalme wa Kaskazini “hakuonekana tena” (Danieli 11:9). Inawezekanaje tunamwona tena hapa?

 

   1.     Utaona kwamba Danieli 11:40 inarejelea “wakati wa mwisho.” Wafalme hao wawili (Kaskazini na Kusini) walikuwepo miaka mingi iliyopita. Tunawezaje kusoma kwamba walikuwa wanatenda jambo “wakati wa mwisho?” (Soma Danieli 12:2. Hii inaashiria kwamba wakati wa mwisho unafikia kipindi cha mwisho wa dunia ikiwa unaelewa kwamba wafalme wa Kaskazini na Kusini ni mamlaka zinazoshindana zilizoibuka baada ya kifo cha Alexander Mkuu, basi kipindi hiki hakileti mantiki kabisa kinapotumika kwao.)

 

    1.     Una namna yoyote ya kuona mantiki katika jambo hili? (Hebu turukie mbele hadi Danieli 11:40 na tuone kama tunaweza kuona mantiki yoyote ya jambo hili.)

 

  1.     Soma Danieli 11:40-41. Ikiwa hizi si mamlaka zile zile kama zile zilizoibuka kuanzia kipindi cha Alexander Mkuu, kwa nini kuwaita Mfalme wa Kaskazini na Mfalme wa Kusini? (Sehemu ya rejea, Israeli, haijabadilika. Hivyo, hii inarejea mamlaka ambayo kijiografia yapo katika pande zote mbili za Israeli.)

 

   1.     Hii inatuambia nini kuhusu umuhimu wa Israeli kwenye unabii? (Inaashiria kwamba kamwe Mungu habadili mtazamo wake kwa watu wake au mji wake.)

 

  1.     Ulipokuwa ukijifunza Danieli 11, je, kuna sehemu yoyote katika sura hiyo ambayo hadi kufikia hapa imeelezea matukio ya “kiroho?” (Kuna watu wengi wanaowafanya wafalme hawa wajao kuwa wa kiroho. Hata hivyo, hakuna kitu chochote katika Danieli 11 kinachoyafanya haya matukio ya kihistoria kuwa ya kiroho. Naam, hiyo ni mojawapo ya tabia tofauti ya Danieli 11, ni kauli sahihi kabisa ya matukio yajayo ya kihistoria. Wenye ufahamu zaidi kuhusu jambo hili kuliko mimi, kama vile William H. shea, wanajenga hoja kwamba vifungu hivi vinavyohusu mambo yajayo vinapaswa kufanywa kuwa vya kiroho. Kwa sababu hiyo, nitaweka nadharia ya kiroho kwanza, ikifuatiwa na nadharia ya “matukio halisi.”)

 

  1.     Nadharia ya Kwanza: Soma tena Danieli 11:22. Mamlaka gani yalimuua Yesu? (Rumi. Tunaona mfanano wa Danieli 11 katika Danieli 2 na 8. Ikiwa hali ndio hiyo, basi Rumi (ya kipagani na Kipapa) itaufuatia Uyunani kuwa Mfalme wa Kaskazini. Hii pia inatenda kazi kijiografia.)

 

   1.     Je, Rumi bado ipo? (Ipo kwa maana ya kiuhalisia kama nchi na pia kiroho.)

 

   1.     Soma Danieli 11:40-42. Vipi kuhusu Mfalme wa Kusini? Kipengele gani cha kiroho kipo kwa Israeli leo? (Misri ilikuwa “mpinga Mungu,” yaani kinyume na Mungu wa kweli wa kwenye Biblia.)

 

    1.     Je, kuna vuguvugu lolote la “wapinga Mungu” leo? (Naam! Kwa kiasi kikubwa Ulaya hafuati misingi ya kidini (secular). Kuna ukuaji wa kasi wa ukanaji Mungu nchini Marekani. China inawashambulia Wakristo. Urusi ya zamani iliupinga Ukristo.)

 

    1.     Vifungu hivi vinatuambia kwamba Mfalme wa Kaskazini anazivamia nchi zote hizi, ikiwemo “Nchi Nzuri.” Je, inaleta mantiki kutarajia kwamba Ukatoliki unaivamia Israeli? Vipi kuhusu Ukristo kwa ujumla?

 

   1.     Soma Danieli 11:43-45. Unadhani hii inatabiri mustakabali wa Ukatoliki? Vipi kuhusu Ukristo? (Mojawapo ya matatizo ya kupanua wigo wa Ukatoliki kujumuisha Ukristo wote ni kwamba katika Agano la Kale lote, “Kaskazini” iliwakilisha maadui wa watu wa Mungu. Hivyo, aina pekee ya Ukristo inayoendana na tafsiri hapa, kama suala la kihistoria, ni aina fulani ya Ukristo wa uongo.)

 

  1.     Nadharia ya pili: Soma tena Danieli 11:40-42. Nchi gani iliyo kaskazini mwa Israeli inaendana na maelezo haya kwa kuzingatia matukio halisi? (Marekani imeivamia Mashariki ya Kati kwa “magari ya vita” (vifaru), “farasi” (ndege) na “merikebu nyingi.”

 

   1.     Je, kuna mataifa katika Mashariki ya Kati ambayo Marekani haijayapunguza nguvu?

 

   1.     Je, itakuwa sahihi kusema kuwa Marekani “imeivamia Nchi Nzuri?” (Kiuhalisia, Israeli inaitegemea Marekani. Endapo maadui wa Israeli wasingekuwa wanaiogopa Marekani, nadhani wangeishambulia Israeli kwa shari na ghadhabu.)

 

   1.     Danieli 11:40 inasema kuwa Mfalme wa Kusini atashindana na Mfalme wa Kaskazini kwenye pambano? Je, kuna yeyote aliyeshindana – kwa kuchukua hatua za kwanza katika pambano – dhidi ya Marekani? (Ikiwa Mfalme wa Kusini inaurejelea Uislamu na mataifa yanayomuunga mkono, basi jibu ni “ndiyo.” Marekani ilishambuliwa na Uislamu tarehe 11 Septemba, 2001.)

 

   1.     Soma Danieli 11:43-45. Unaweza kuona uwezekano wa jambo hili kuwa nchi ya Marekani katika siku zijazo?

 

  1.     Rafiki, hakuna mtu anayepaswa kulazimisha kiimani uelewa wa mustakabali wa Danieli 11. Watu wa Mungu walikosea kabisa uelewa wa jinsi ambavyo Yesu angekuja na kuwatumikia wanadamu mara ya kwanza. Nadhani unyenyekevu mkubwa unahitajika katika kutabiri matukio yanayouzunguka ujio wa mara ya pili kwa ajili yetu hii leo. Wakati huo huo, ninakutia moyo uwe makini ili uone jinsi Mungu anavyoenenda katika siku zijazo!

 

 1. Juma lijalo: Toka Mavumbini Hadi Kwenye Nyota.