Somo la 1: Upekee wa Biblia

(Kumbukumbu la Torati 32, 2 Timotheo 3, 2 Petro 1)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unafahamu jinsi Biblia unayoitumia kwenye somo hili ilivyopatikana? Baadhi ya watu wanadhani tafsiri ya Biblia ya KJV ndio ya asili (ya kwanza). Kimsingi, palikuwepo na tafsiri kadhaa za Kiingereza kabla ya tafsiri ya KJV. Na, kiukweli, Biblia ya kwanza haikuandikwa kwa Kiingereza. Biblia kamili haikuletwa na malaika kama jinsi ilivyo. Badala yake, ni mkusanyiko wa maandiko ya waandishi wengi, wote wakivuviwa na Roho Mtakatifu. Hakuna biblia yoyote ya asili (au hata vipandevipande) ambayo imewahi kupatikana hadi kufikia sasa. Kipande cha zamani kabisa, ambacho kilivumbuliwa hivi karibuni, kilipatikana takriban miaka 90 baada ya sisi kuamini kuwa kitabu cha Ufunuo kiliandikwa na Yohana. Ingawa hatuna Biblia za asili, Agano Jipya la Biblia ni kitabu bora kabisa kilichoshuhudiwa duniani! Ninamaanisha nini ninaposema “kushuhudiwa?” Tuna nakala nyingi zaidi za Agano Jipya kuliko andiko lolote la kale. Kwa maandiko ya kale kwa wastani tuna takriban nakala ishirini. Kwa upande mwingine, leo tuna nakala za kale takriban 24,000 za Biblia yote au sehemu ya Biblia. Huu mfululizo mpya wa masomo hauhusu jinsi tulivyoipata Biblia tunayoitumia leo, bali jinsi tunavyopaswa kutafsiri Biblia yetu. Hebu tuzame kwenye huu mfululizo mpya unaohusu Biblia!

 

 1.     Mtazamo wa Musa

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 32:48-50. Je, ungependa kufahamu lini hasa na jinsi utakavyokufa?

 

   1.     Ni nini itakayokuwa sababu ya muhimu kabisa ya kufahamu kabla? (Ili uweze kupangilia mambo yako vizuri.)

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 32:45. Musa anafanya nini hapa (na katika vifungu vilivyotangulia)? (Anatoa maneno yake ya mwisho ya ushauri kwa sababu anafahamu kuwa anakaribia kufa.)

 

  1.     Soma Kumbukumbu la Torati 32:46-47. “Maneno ya torati” ambayo Musa anayapendekeza ni yapi? (Kwa kiasi kikubwa sana Musa anafahamika kwa kuandika vitabu vitano vya kwanza vya Biblia. Hapa anazungumzia torati aliyoitoa (kwa njia ya Mungu) kwa watu wa Mungu.)

 

   1.     Kipaumbele chetu cha kwanza katika Biblia ni kipi? (Kuiweka “moyoni,” kuichukulia kwa dhati.)

 

   1.     Sababu ya kukifanya hiki kuwa kipaumbele chetu cha kwanza ni ipi? (Ili tuweze kuwafundisha watoto wetu kuyatii maelekezo yake.)

 

   1.     Kuna sababu gani ya kuichukulia Biblia kwa umakini mkubwa? (Biblia ndio “maisha” yetu.”)

 

    1.     Hii inamaanisha nini? Kwa nini maelekezo ya Biblia ndio maisha yetu? (Bila shaka hii hufungamanisha utii wetu na maisha ya baraka.)

 

    1.     Unahitaji nini kwa ajili ya watoto wako? Maisha ya baraka?

 

   1.     Soma Kumbukumbu la Torati 6:6-7. Unahimizaje umuhimu wa Biblia kwa watoto wako? (Mke wangu alikuwa mwalimu mkuu wa Biblia kwa watoto wetu kwa sababu alikuwa akiwafundisha nyumbani katika miaka yao ya awali. Mojawapo ya mambo ya muhimu niliyoyafanya ni kutenga muda wakati wa jioni ambapo tulisoma Biblia pamoja. Nilichagua tafsiri ya Biblia ambayo wangeweza kuisoma na kuielewa na kuwataka waisome. Kisha tulijadili kile tulichokisoma.)

 

  1.     Soma Ufunuo 12:17. Shetani anajisikiaje juu ya wale wanaomtangaza Yesu na kuzishika amri za Mungu?

 

   1.     Kwa sababu gani?

 

 1.   Yesu, Roho Mtakatifu na Biblia

 

  1.     Soma Yohana 1:14. Kwa nini Yesu anaitwa “Neno?” (Tunayo Biblia kwa ajili ya kutusaidia kuyaelewa mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Yesu ndiye kielelezo cha neno la Mungu. Anatusaidia kuyaelewa mapenzi ya Mungu.)

 

  1.     Soma Yohana 14:6. Yesu ni wa muhimu kiasi gani katika kuuelewa ukweli wa Mungu kwa ajili yetu? (Yeye ndiye njia pekee kwa sisi kumjongelea Mungu.)

 

  1.     Soma 2 Petro 1:21. Roho Mtakatifu ni wa muhimu kiasi gani kwa maneno ya Biblia? (Roho Mtakatifu “aliendana” na manabii.)

 

   1.     Unadhani inamaanisha nini kusema kwamba Roho Mtakatifu “aliendana” na manabii? Ni kazi gani inaelezewa hapa? (Roho Mtakatifu ni msukumo, njia ya wanadamu kuyaelezea mapenzi ya Mungu. Mojawapo ya maoni yalisema kwamba neno la Kiyunani ni lile lile lililotumika kuwasha injini ya boti. Upepo huendesha boti kama Roho Mtakatifu anavyomwendesha nabii.)

 

  1.     Soma Yohana 3:34. Hapa Roho Mtakatifu anafanya nini kwa kuyazingatia maneno ya Mungu? (Mantiki, kwa mara nyingine, ni kwamba Roho Mtakatifu ndio njia ambayo wanadamu wanachapisha neno la Mungu.)

 

  1.     Soma Yohana 16:13-14. Tunafahamu kwamba Roho Mtakatifu ni sehemu ya Utatu Mtakatifu, lakini pia anajitegemea. Hapa wajibu wake ni upi kwa kuzingatia maneno ya Mungu? (Hii inatuambia mambo mawili. Kwanza, kwamba Yesu anazungumza na Roho Mtakatifu ambaye anafanya tuyaelewe maneno hayo. Pili, Roho Mtakatifu atayaelekeza mawazo yetu kuuelewa ukweli wa Mungu. Yeye ni mjumbe na pia mfasiri.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 2:9-11. Haya ni maneno mazuri sana. Yanasema kwamba Roho Mtakatifu pekee ndiye anaeyaelewa mawazo ya Mungu. Tunapaswa kumgeukia nani kwa ajili ya msaada katika kuielewa Biblia kwa usahihi?

 

  1.     Soma 2 Wakorintho 3:6. Ni nini matokeao ya kuijua torati bila uwepo wa Roho Mtakatifu? (Kifo. Hii inatufundisha kwamba kujifunza Biblia bila msaada wa Roho Mtakatifu kuongoza uelewa wetu ni hatari.)

 

 1. Mianzo ya Biblia

 

  1.     Soma 2 Timotheo 3:14-17. Ingawa tuna watu wa aina zote kutoka maeneo mbalimbali maishani walioandika sehemu za Biblia, asili ya kweli ya Biblia ni ipi? (“Imevuviwa na Mungu.”)

 

   1.     Lengo moja la Biblia ni lipi? (Kutuelekeza kwenye wokovu. Kutufanya tuwe na hekima kwenya mada hiyo. Kuchechemua imani kwa Yesu.)

 

  1.     Soma Matendo 28:25. Nani aliye wakala hai katika “kuivuvia” Biblia kupitia kwa watu walioiandika? (Roho Mtakatifu. Utaona kwamba kifungu hiki kinasema kuwa Roho Mtakatifu “alinena” “kwa kinywa cha nabii Isaya.” Hii inathibitisha vifungu vya awali tulivyovisoma vinavyoelezea ukuu wa Roho Mtakatifu kwenye uwepo wa Biblia.)

 

  1.     Soma 2 Petro 1:16-17. Hapa tunaona vyanzo gani vingine vya Biblia? (Ushuhuda wa watu. Petro anatuambia kwamba ametuambia kile ambacho amekiona na kukisikia yeye mwenyewe.)

 

 1.   Unabii

 

  1.     Soma 2 Petro 1:19-21. Tunamtenganishaje mwanadamu na Mungu katika unabii? (Mapenzi ya mwanadamu na tafsiri ya mwanadamu si chanzo. Bali wanadamu waliandika kile kilichotoka kwa Mungu kwa njia ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. (Hapo awali tuliangalia kifungu cha 21.)

 

  1.     Tumetoka kujifunza kitabu cha Danieli. Kimejaa unabii. Tulijifunza “ujumbe gani mkuu” kutoka kwenye huu unabii mbalimbali wa Biblia? (Kwamba Mungu ndiye mdhibiti. Hata tulijifunza muda kamili ambao utume wa Yesu ulitabiriwa.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 15:3-5. Je, ni Danieli pekee aliyetabiri ujio wa Yesu? (Paulo anathibitisha kwamba vipengele vingine mahsusi vya maisha ya Yesu vilitabiriwa kwenye Biblia.)

 

 1.     Badiliko

 

  1.     Soma Waebrania 4:1-2. Je, tunaweza kuwa na imani isiyo na matokeo ya utii kwa Mungu? Ikiwa ndivyo, je, imani hiyo ina uzuri wowote kwetu? (Imani bila utii “haina maana.”)

 

  1.     Soma Waebrania 4:6, na Waebrania 4:9-11. Unalinganishaje hili na haki kwa imani pekee? (Matokeo ya imani ya kweli ni kuwa na uhusiano na Mungu. Hatima yake ni utii.)

 

  1.     Soma Waebrania 4:12-13. Biblia inatuongozaje kwenye huu uhusiano sahihi? (Kujifunza Biblia huleta mguso wa jinsi ambavyo Mungu angependa tuishi na jinsi tulivyoyaacha mapenzi yake. Hii ni muhimu kwa sababu kwa dhahiri Mungu anatuona jinsi tulivyo. Tunaweza kujipumbaza na kuwapumbaza wengine, lakini hatuwezi kumpumbaza Mungu.)

 

  1.     Rafiki, je, umeshawishika kwamba Biblia inaakisi mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yako? Roho Mtakatifu ni wa muhimu kwa ajili ya uelewa sahihi wa Biblia. Kujifunza Biblia ni muhimu kwa imani iletayo utiifu. Je, utajitoa kujifunza Biblia mara kwa mara? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie kupata uelewa? Kwa nini usifanye agano hilo sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Chanzo na Asili ya Biblia.