Somo la 1: Kwa Nini Ushuhudiaji?

(Yakobo 5, Waebrania 6, Yohana 7, 1 Timotheo 2)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Kwa Nini Ushuhudiaji?

 

(Yakobo 5, Waebrania 6, Yohana 7, 1 Timotheo 2)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Dhana ya kuhesabiwa haki kwa njia ya imani pekee ni pana kuliko suala la wokovu. Inaelezea uhusiano mpana walio nao wanadamu kwa Mungu. Kwa mfano, nilipojisikia hatia kwamba sikuwaongoa majirani wangu, ilitokea kwamba mimi si mzuri katika kuwaongoa watu wengine. Hiyo ni kazi ya Mungu. Nilipokuwa nikifyeka nyasi za jirani wangu, nikiwatembelea majirani hospitali, na kujaribu kufanya nao mazungumzo kwa lengo la kuwapelekea injili, nilidhani kwamba nilipungukiwa ujuzi wa “kumaliza kazi.” Upumbavu kiasi gani! Mfululizo wa masomo yetu katika robo hii unahusu jinsi tunavyoshirikiana na Mungu katika kazi yake ya kuuvuta ulimwengu kwake. Hebu tuchimbue somo letu la kwanza kuhusu ushuhudiaji na tuone kile Biblia inachokisema!

 

 1.     Kuwarejesha?

 

  1.     Soma Yakobo 5:19-20. Je, tunapaswa kujaribu kuwashuhudia wale walioliacha kanisa?

 

   1.     Roho ya nani inaokolewa dhidi ya kifo, mtu anayeshuhudia au anayeshuhudiwa? (Lazima imaanishe mtu anayerejeshwa. Biblia haifundishi kwamba tunaokolewa kwa kuwaongoa wengine. Hiyo itakuwa kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo.)

 

   1.     Ni nani ambaye wingi wa dhambi zake unafunikwa? Mtu anayeshuhudia au mtu anayeshuhudiwa? (Hili ni swali gumu zaidi. Mtu anayeongolewa upya anasamehewa. Ingawa ni dhahiri kwamba dhambi zetu hazisamehewi kutokana na matendo yetu, yumkini kuwaongoa wengine hufidia upungufu mwingine maishani mwetu.)

 

  1.     Soma Waebrania 6:4-6. Ngoja niulize tena, je, tunapaswa kujaribu kuwashuhudia wale walioliacha kanisa? (Kifungu hiki kinasema “haiwezekani kuwafanya upya tena.”)

 

  1.     Katika jambo hili ongezea Waebrania 10:26-27. Je, Yakobo anahusika kwenye ndoto za mchana? Linapokuja suala la washiriki wa zamani, je, “hakuna sababu ya maana” ndilo jibu la mada ya somo letu, “Kwa Nini Ushuhudiaji?”

 

  1.     Hebu tusome zaidi katika Waebrania ili tuone kama tunaweza kuelewa jambo hili. Soma Waebrania 6:7-8. Kwa nini Waebrania inalinganisha kauli yake isiyo na maana na ulimaji wa mazao? Unapata mazao mapya kila mwaka! Hiyo inaonekana kukinzana na kauli ya “mara unaporudi nyuma, mara zote unakuwa mpotevu.”

 

  1.     Soma Waebrania 6:9-10. Je, hii inaonekana kama wapokeaji wa barua hii wameanguka? Kwa nini aseme “tumesadiki mambo yaliyo mazuri zaidi?” Kwa nini aseme “Mungu si dhalimu hata ayasahau matendo yenu mema ya zamani?”

 

  1.     Hebu tupitie tena Waebrania 6:4-5. Je, unamfahamu mtu anayeendana na maelezo haya na kisha baadaye akaanguka?

 

   1.     Je, hili linaweza kueleweka kumaanisha kwamba ikiwa imani yangu itaanguka, basi haikuwa sawa tangu mwanzo? Je, hili linaweza kueleweka kumaanisha kwamba wale ambao kweli wanaenenda na kutembea na Mungu kwa ukaribu hawataanguka?

 

   1.     Ikiwa tutahitimisha kwamba Waebrania na Yakobo hazikinzani, hii inatufundisha nini kuhusu jinsi ya kuwashuhudia wale walioliacha kanisa? (Inatufundisha kwamba hapo kabla kuna jambo ambalo halikuwa sahihi katika uelewa wao wa Mungu. Tunatakiwa kuwasaidia wawe na uelewa sahihi wa Mungu.)

 

 1.   Vipi Kama Utaanguka?

 

  1.     Soma Warumi 1:18. Mungu ana mtazamo gani dhidi ya wale “waipingao kweli?” (Anajisikia “ghadhabu” dhidi yao.)

 

   1.     Kifungu hiki kinatuambia kuwa “vitendo visivyo vya haki” hukandamiza ukweli kumhusu Mungu. Je, umewahi kujisikia kwamba umeshindwa kushuhudia wakati ambapo ungeweza kufanya hivyo? Je, umewahi kuzingatia kwamba kushindwa kwako kuzungumzia jambo maana yake ni kwamba mtu fulani anapoteza fursa ya pekee ya kuisikiliza injili?

 

    1.     Je, kutokuwa na haki kulimo ndani yako ndio kunakokusababishia kushindwa kushuhudia?

 

  1.     Soma Warumi 1:19-20. Hii inatuambia nini kuhusu fursa ya kila mtu kujifunza habari za Mungu? (Mambo ya asili humfundisha kila mtu habari za Mungu. Wote “hawana udhuru” wa kutoyachunguza “mambo ya Mungu.”)

 

   1.     Je, hii inafafanua kinachomaanishwa na vitendo visivyo vya haki kuukandamiza ukweli? (Haizungumzii kushindwa kwa waamini, inawazungumzia wale wanaojaribu kuficha ukweli wa dhahiri kuhusu Mungu unaofunuliwa kwenye mambo ya asili.)

 

   1.     Ngoja basi nikuulize tena, “Kwa nini ushuhudiaji?” Ikiwa kila mtu ana ushuhuda wa mambo ya asili, kwa nini wewe unahitajika?

 

  1.     Soma Warumi 1:21-23. Inamaanisha nini kusema “wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu?” (Kila mtu anayo fursa ya kuwa na uhusiano na Mungu wa kweli wa mbinguni. Hawa wapumbavu (angalia kifungu cha 22) walipendelea kuwa na uhusiano na “mfano wa sura ya binadamu [na wanyama].” Fursa iliyopotea kiasi gani!)

 

   1.     Wapumbavu hawa wana madai gani? (Kwamba wao ni werevu!)

 

    1.     Je, unayaona haya leo? Je, wapo wale waliomkataa Mungu, na kisha wakadai kwamba wao ni werevu kuliko wale wanaomkiri Mungu na kumshukuru?

 

   1.     Mungu anatamani tufanye nini? Je, tunaweza kumwamini Mungu wa mbinguni lakini bado tukawa wapumbavu tunaojidai kwamba ni werevu? (Kifungu cha 21 kinatuambia kuwa mzizi wa kushindwa si kumtii Mungu au kumshukuru.)

 

    1.     Yatafakari maisha yako. Je, unamshukuru Mungu? Je, unamtii badala ya kudai sifa kwa ajili yako?

 

   1.     Tunawezaje kumshuhudia mtu ambaye ana uhakika kwamba yeye ni mwerevu kuliko sisi?

 

  1.     Soma Warumi 1:24-25. Ikiwa Mungu “aliwaacha,” je, ni upumbavu kudhani kwamba tunaweza kuwashuhudia na kuwaongoa watu kama hivi?

 

  1.     Soma Warumi 1:26-28. Kwa mara nyingine, tunaona maneno “Mungu aliwaacha.” Je, Mungu anawaacha kwenye uangamivu wa milele? (Sidhani. Mungu anatupatia sote uhuru wa kuchagua. Hivyo, Mungu anawaacha kwenye uamuzi wao wa kiovu. Bado Mungu anataka waokolewe, na hivyo tuna fursa ya kushuhudia.)

 

 1. Maji Yaliyo Hai (Maji ya Uzima)

 

  1.     Soma Yohana 7:37-38. Unadhani inamaanisha nini kwa “mito ya maji yaliyo hai” kutiririka kutoka moyoni mwako?

 

  1.     Soma Ufunuo 22:1-2. Je, hii ni aina ile ile ya maji ya uzima?

 

  1.     Soma Yohana 7:39. Tunapata uelewa gani wa ziada wa “maji ya uzima” kutoka katika kifungu hiki? (Hii inamzungumzia Roho Mtakatifu!)

 

   1.     Hebu tuyaweke mambo yote haya pamoja. Tumekuwa tukijadili kile tunachoweza kukifanya na tusichoweza kukifanya kuhusu ushuhudiaji. Vifungu hivi katika Yohana 7 vinabadilije mwelekeo wa mazungumzo? (Si suala la kile tusichoweza kukifanya, bali ni suala la kile tusichoweza kujizuia bali kukifanya. Maji ya uzima hububujika kutoka kwa Mkristo katika mito! Ushuhudiaji wetu hutokea wenyewe.)

 

  1.     Soma 1 Timotheo 2:1-2. Nani anayepaswa kuwa kwenye orodha yako ya maombi?

 

   1.     Kwa nini tunapaswa kuwaombea watu walio kwenye nafasi za mamlaka? (Kwa kiasi fulani, ni ili tuweze kuishi “maisha ya utulivu na amani.”)

 

   1.     Je, maombi haya yana mantiki? Kuna uhusiano gani kati ya kuwaombea watu “wenye mamlaka” na kuishi maisha ya utulivu na amani? (Watawala wa mataifa mbalimbali huwekwa kwenye mamlaka ili kutiisha utaratibu na haki. Utaratibu huruhusu wananchi wote kuishi maisha ya utulivu na amani. Viongozi wanawajibika kuwaruhusu watu kumwabudu Mungu na kudumisha heshima na mali yao.)

 

  1.     Rafiki, Mungu ana mpango kwa ajili yako. Anataka Roho Mtakatifu amiminike kutoka kwetu katika kuwashuhudia wengine maishani. Anataka tuwaombee viongozi ili waushinde uovu na kutiisha utaratibu na amani. Je, utafanya hivyo leo?

 

 1.   Juma lijalo: Shuhuda wa Kuvutia: Nguvu ya Ushuhuda Binafsi.