Somo la 3: Kuwaona Watu Kama Yesu Anavyowaona

(Marko 8 & 12, Matendo 1)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

Somo la 3: Kuwaona Watu Kama Yesu Anavyowaona

 

(Marko 8 & 12, Matendo 1)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Majuma mawili yaliyopita nilisoma sehemu ya maelezo ya Ellen white kuhusu kundi la watu lililoshinikiza mateso ya Yesu. Alisema kuwa malaika walioanguka walikuwa kwenye kundi lililohanikiza kifo cha Yesu. Je, hilo limebadilika? Je, pepo wamestaafu ili waishi maisha ya amani kule Scottsdale, Arizona? Kwa dhahiri pepo si watu. Je, kuna watu waovu? Juma lililopita tulijifunza (katika Marko 5) kisa cha mtu aliyekuwa na pepo. Yesu alimtumia mtu huyo kama shuhuda. Je, Yesu anawaendea watu wote kwa kutumia njia hiyo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

  1.     Kuona Miti

 

    1.     Soma Marko 8:22. Tunafahamu nini kuhusu imani ya huyu kipofu? (Hatufahamu habari zake kwa kina. Kwa dhahiri alikubali kwenda, lakini haionekani kama kipofu huyu ndiye aliyemwomba Yesu kwa ajili ya uponyaji.)

 

      1.     Kwa nini ni muhimu kumsihi Yesu amponye kipofu?

 

      1.     Kwa nini watu walitaka Yesu “amguse” kipofu? (Soma Mathayo 8:8. Akida wa Kirumi alitambua kwamba Yesu anaweza kuponya kwa mbali. Watu wanaomleta kipofu sio tu wanaamini kwamba lazima Yesu awe karibu, bali pia lazima amguse.)

 

      1.     Kama ungekuwa Yesu, je, ungejisikia kudhalilishwa kwa kitendo hiki? Unataka uombwe kutenda jambo jema, uwezo wako unachukuliwa kuwa na kikomo, na mtu anayetaka muujiza hauombi!

 

    1.     Soma Marko 8:23. Kwa nini Yesu alimchukua mtu yule na kumpeleka mbali na marafiki wake? Kwa nini amtoe nje ya kijiji? (Huu ni ushahidi zaidi kwenye nadharia ya kwamba mtu huyu hakuwa ameshawishika kwa Yesu, hivyo Yesu alitaka kuwa na muda wa faragha na mtu huyu.)

 

      1.     Utaona kwamba Yesu hamgusi tu mtu huyu, bali pia anamtemea mate ya macho na kumwekea mikono. Kwa nini? Hakuna tendo hata moja kati ya matendo haya mawili lililo muhimu kwa Yesu kuponya.

 

      1.     Soma 2 Wafalme 5:11. Naamani alidhani kuwa njia sahihi ya muujiza wa uponyaji ilipaswa kufanyikaje? (Alidhani kuwa matendo makubwa ya mguso yalipaswa kuendana na muujiza.)

 

      1.     Jibu la Naamani linatufundisha nini kuhusu matendo ya Yesu hapa? (Matendo ya Yesu yalikusudia kujenga imani ya mtu yule kwamba kuna jambo lilikuwa linatokea ili kuponya upofu wake.)

 

    1.     Soma Marko 8:24. Unafahamu kile ambacho mtu huyu anakizungumzia? (Ndiyo! Nilipokuwa chuoni uoni wangu ulikuwa hafifu. Kwa mbali niliweza kuwagundua marafiki wangu kwa namna walivyokuwa wakitembea. Walionekana kama “miti inayotembea.”)

 

      1.     Hii inamaanisha nini? (Muujiza wa Yesu ni sehemu tu ya mafanikio.)

 

        1.     Je, Yesu anajifunza jinsi ya kuponya? Je, uwezo wake umepungua? Je, mashaka ya Yesu kwamba angeweza kuponya kwa usahihi ndio sababu ya kumchukua na kumpeleka mtu huyu mbali na wengine – endapo ingetokea muujiza usiende vizuri? (Hakuna chochote kati ya haya kinachoendana na uwezo wa Mungu. Huu haukuwa mmojawapo wa miujiza ya awali ya Yesu.)

 

        1.     Hii inatuambia nini kuhusu historia ya kitabibu ya yule kipofu? Je, alikuwa kipofu tangu kuzaliwa? (Hapana. Alijua jinsi miti ilivyo. Alikuwa na uzoefu kama wangu – marafiki walionekana kama miti inayotembea wakati uoni wake ulipofifia.)

 

          1.   Je, Yesu na yule kipofu walikuwa peke yao bila uwepo wa mtu yeyote? (Hapana. Watu walikuwepo karibu yao.)

 

    1.     Soma Marko 8:25. Hatimaye Yesu anapatia! Je, hiyo ni kauli ya kweli? Je, Yesu anahitaji mazoezi ya vitendo?

 

      1.     Kama jibu lako ni “hapana” (ambalo ndilo jibu langu), kwa nini basi Yesu ana muujiza wenye “hatua mbili?” Kwa nini alihitaji majaribio mawili? (Kwa mchakato wa uondoshaji, ikiwa hili halihusiani na uwezo wa Yesu, basi inahusiana na imani ya yule kipofu. Sasa tunao mfululizo wa “viashiria” kwamba yule kipofu alihitaji kutiwa moyo. Alihitaji imani yake ikue.)

 

      1.     Kwa kuwa lengo la somo hili ni kutusaidia kuona kama Yesu aonavyo, tunajifunza nini kutokana na kisa hiki? (Kila mtu anahitaji njia binafsi ya kumfikia.)

 

        1.     Je, Yesu alijali hadhi yake katika kutengeneza njia binafsi kwa ajili ya mtu huyu? (Hapana. Lakini, hii inaweza kuwa sababu ya Yesu kumchukua mtu huyu na kumpeleka mbali na watu – ili watu hawa wasifikie hitimisho lisilo sahihi kumhusu Yesu.)

 

        1.     Ikiwa mahitimisho ndio suala lililopo, kwa nini basi muujiza huu unaofuata hatua mbili katika Biblia? (Ili tuweze kuchimbua kwa ajili ya kupata ujumbe wa kweli.)

 

    1.     Soma Marko 8:26. Kwa nini? Vipi kuhusu marafiki waliomleta mtu huyu kwa Yesu? (Hii inaibua maelezo mbadala ya kwa nini Yesu alimtoa mtu huyu kutoka kwenye kundi la watu ili kutenda huu muujiza.)

 

      1.     Je, hii inaweza kuhusiana na kukua kwa imani ya mtu huyu katika Yesu? Je, inawezekana kwamba Yesu alitaka mtu huyu atumie muda mtulivu kutafakari yote yaliyomtokea?

 

  1.   Majibu Magumu

 

    1.     Soma Marko 12:18-19. Kisa kinachofuata ni kile cha ndugu saba kumwoa mwanamke mmoja. Unadhani kwa nini Masadukayo walimuuliza Yesu swali hili?

 

      1.     Kwa nini Biblia inatuambia mtazamo wa Masadukayo juu ya ufufuo? (Ujumbe uliopo ni kwamba kiukweli Masadukayo hawatafuti taarifa, wanatafuta kumtega Yesu.)

 

      1.     Tutaona kwamba Yesu anajibu swali hili.  Kwa nini alijibu, na kwa nini jibu hili limo kwenye Biblia? (Swali, jibu, na kumbukumbu iliyowekwa ni kwa ajili ya watu – ambao sasa wanakujumuisha wewe na mimi.)

 

    1.     Soma Marko 12:23-24. Unalichukuliaje jibu la Yesu? Je, ni gumu? Je, linafedhehesha? (Lina pande zote mbili, ni gumu na linafedhehesha, hususan pale unapotafakari kwamba lilielekezwa kwa viongozi wa dini waliodai kuijua Biblia.)

 

      1.     Hii inatufundisha nini kuhusu kuwaona watu kama Yesu anavyowaona? Je, Yesu anataka watu wauone upande wake mgumu? (Hii inaonesha kwamba Yesu anajibu majibu tofauti kwa watu tofauti. Jibu la Yesu kwa mtego huu ni tofauti sana na jibu lake kwa wale wanaoutafuta ukweli.)

 

    1.     Soma Marko 12:25. Je, taarifa hii imo ndani ya Agano la Kale? Je, ndoa mbinguni imejadiliwa? (Masadukayo waliamini katika vitabu vitano vya kwanza pekee vya Agano la Kale. Siamini kama jambo hili limejadiliwa mahali popote katika Agano la Kale.)

 

      1.     Je, Yesu hatendi haki kusema kwamba swali lao linaonesha kuwa hawayajui Maandiko?

 

    1.     Soma Marko 12:26-27 na Kutoka 3:6. Hebu elezea jibu la Yesu na kama anatenda haki kwa Masadukayo? (Suala si ndoa mbinguni, bali ni ufufuo. Yesu anawaambia kuwa kushindwa kwao kuelewa Kutoka 3:6 ndio sababu wamekosea kuhusu ufufuo.)

 

      1.     Je, hii inamaanisha kwamba Ibrahimu, Isaka na Yakobo wako hai leo? (Jibu zuri zaidi ni kwamba Mungu hawaachi watu wake katika mauti ya milele. Atawafufua katika uzima wa milele. Jambo ambalo, kimsingi, ndio kiini cha utume wa Yesu.)

 

  1. Macho ya Yesu Leo

 

    1.     Soma Matendo 1:8. Hili ni jambo la mwisho kabisa ambalo Yesu alilisema kabla hajachukuliwa mbinguni. Jambo gani ni la muhimu kwetu ili tuwe mashuhuda wanaostahili? (Uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

      1.     Tafakari njia mbili za kuiangalia mada yetu. Njia moja ni kujifunza (kama ambavyo tumekuwa tukifanya) jinsi Yesu alivyowajibu wengine ili tuweze kujifunza kuwaangalia wengine jinsi Yesu alivyowaangalia. Njia nyingine ni kumfanya Roho Mtakatifu ayavuvie mawazo yetu ili tuwaone wengine kama Yesu alivyowaona. Njia gani inaonekana kuwa na ufanisi zaidi? Je, njia hizo haziendani?

 

    1.     Hebu tuangalie kilichohamasisha jibu la Yesu. Soma Matendo 1:6. Ungejisikiaje kama ungekuwa Yesu na haya ndio mazungumzo yako ya mwisho? (Ningesikitika sana kwamba wanafunzi bado hawakuelewa utume wangu.)

 

    1.     Soma Matendo 1:7. Yesu anawapa jibu la namna gani? Hii inatufundisha nini kuhusu kuwashuhudia na kuwaangalia wengine kama Yesu alivyowaangalia? (Yesu hakuwapa jibu gumu. Hakuwauliza kwa nini hawakuwa wakisikiliza. Badala yake aliwaahidi nguvu ya Roho Mtakatifu.)

 

    1.     Angalia tena Matendo 1:8. Ni nini lengo la Yesu la ushuhudiaji kwa ajili yetu? (Anza sehemu mahalia na uende “hata mwisho wa nchi.”)

 

    1.     Rafiki, nguvu ya Roho Mtakatifu ni muhimu katika ushuhudiaji. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie uwaone wengine na utume kama Yesu anavyowaona?

 

  1.   Juma lijalo: Nguvu ya Maombi: Kuwaombea Wengine.