Somo la 5: “‘Njoni Kwangu... ’”

Mathayo 11
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
3
Lesson Number: 
5

Somo la 5: “‘Njoni Kwangu... ’”

 

(Mathayo 11)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.         

Utangulizi: Unajisikiaje kuhusu kufanya uchaguzi wa kuwa Mkristo? Kadiri mwisho wa dunia unavyozidi kukaribia hili litakuwa jambo ambalo watu wengi watalitafakari. Hakuna mtu anayependa kuwa kwenye matatizo. Hakuna mtu anayependa kutukanwa na kuonewa. Kwa miaka mingi vyombo vya habari vikubwa vimewakashifu Wakristo kwamba si watu werevu, wasio na elimu kubwa, na wenye kuongozwa kirahisi. Idadi ya watu wenye nafasi za mamlaka wanaouchukia Ukristo inaongezeka. Je, kuna sababu yoyote yenye mantiki katika jambo hili? Kwa nini watu wengi wanamkataa Yesu? Somo letu juma hili linapitia sababu za kwa nini tumwendee Yesu badala ya kumkataa. Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze zaidi kutoka kwenye Biblia!

  1.    Kuukataa Ukristo
    1.    Soma Mathayo 11:20-21. Ni jambo gani ambalo lingewashawishi wakaazi wa miji hii kutubu na kuwa Wakristo? (“Matendo makuu” ya Yesu.)
    1.    Soma Ezekieli 26:4-6. Kwa nini Sidoni inaangamizwa kabisa? (Wakaazi wake walikataa kumkiri Mungu.)
      1.    Utaona Yesu anasema kuwa matokeo ya Sidoni yangeweza kuwa tofauti endapo angekuwepo mahali pale “zamani zile” na kutenda matendo yake makuu. Unalielezeaje jambo hili? Kipindi hicho Mungu alikuwa Mungu. Je, kuna watu wanapotea kwa sababu ya bahati?
    1.    Soma Luka 12:47-48. Je, baadhi ya watu watapigwa zaidi katika ujio wa Mara ya Pili kutokana na bahati? Je, hiyo ni haki?
      1.    Zingatia kwenye sehemu ya mwisho ya Luka 12:48. Je, Yesu anazungumzia wokovu? Anazungumzia jambo gani? (Sidhani kama Yesu anazungumzia wokovu. Mada yake inahusu kujiandaa kwa ajili ya marejeo. Yesu anatuambia kuwa tunavyoendelea kujiandaa kwa ajili ya marejeo yake, kwa kadiri “unavyopewa” vingi, ndivyo vitakavyotakwa vingi kwako.)
      1.    Sasa tumia maelezo haya kwenye Mathayo 11:20-21. Je, Yesu anasema kuwa wokovu unapatikana kwa bahati? (Hapana. Anasema kuwa sote tunajua, watu wengine wana njia kubwa zaidi ya kuiendea injili. Wengine wanakuzwa katika imani na wazazi Wakristo wenye upendo. Watu hao wana mengi ya kujibu.)
    1.    Hebu tutumie jambo hili kwetu. Soma Yohana 20:29. Watu wengine wanafanana na Tomaso na wanaamini kuwa uzoefu wa kumwona Yesu kwa macho yao ndio unaotakiwa. Je, hiyo inamaanisha kuwa watu wa Korazini na Bethsaida (Mathayo 11:21) wana faida zaidi yetu kwenye kipengele cha kumpokea Yesu? (Ninadhani tunahafifisha manufaa yetu. Yesu alipotembea duniani, madai yake yalikuwa jambo jipya na yalibishiwa na viongozi wa dini waliokuwepo. Hivi leo, tunao mamilioni wanaomwamini Yesu. Maelfu ya miaka ya kumwamini Yesu yamefungua njia kwa ajili yetu leo.)
    1.    Soma Mathayo 11:23-24 na Yuda 1:7. Je, mabasha (wasenge) wa Sodoma wangeweza kuokolewa? Je, kuna ujumbe kwetu kwa ajili ya mabasha hivi leo? (Mathayo anasema kuwa kumwamini Yesu ndio suala la msingi kwa kila mmoja wetu. Yesu anaashiria kuwa Sodoma ingeweza kuokolewa.)
    1.    Kama ungetakiwa kuelezea kwa ufupi vifungu vya Mathayo 11 ambavyo tumevijadili hadi kufikia hapa, ungevielezeaje? (Ni jambo la kutisha kujua habari za Yesu na kisha kumkataa. Ukataaji una matokeo mabaya.)
  1.   Kuukubali Ukristo
    1.    Soma Mathayo 11:25. Inaonekana kwamba vyombo vikubwa vya habari vilikuwa sahihi! Je, hii inamaanisha kuwa wenye “hekima na akili” wanaukataa Ukristo?
      1.    Je, ungependa mtu akuambie kuwa kiwango chako cha uelewa kinaendana na kile wa “mtoto mchanga?”
    1.    Soma Mathayo 11:26. Hii inakuwa mbaya zaidi kwa muda mfupi tu! Je, ni kwa jinsi “impendezavyo Mungu” kwamba wapumbavu pekee wasioweza kuwa na uelewa kwa kuwa wanafikiri kama watoto wanaweza kuukubali Ukristo? Je, hiki ndicho kinachozungumziwa hapa?
      1.    Je, kuna mtu ambaye angependa kutoa ufafanuzi mzuri zaidi?
      1.    Mfikirie mtu ambaye ana “hekima na uelewa.” Mtu huyo atasema nini kuhusu namna ya kutimiza mambo makubwa maishani?
      1.    Jordan Peterson anapowapendekezea vijana wadogo kuwa hatua ya kwanza ya kuwa na kazi/taaluma nzuri ni kusafisha vyumba vyao, unadhani anamaanisha nini? (Peterson, kama ilivyo kwa kila mtu mwerevu mwenye kutumia akili ya kawaida, anajenga hoja kwamba tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuwajibika ikiwa tunataka kutimiza mambo makubwa.)
        1.    Je, hiyo ndio injili ya Yesu? Je, mtoto atapokea kwa moyo njia ya Peterson? (Hiki ndicho anachokimaanisha Yesu: njia ya kawaida ya kupata mafanikio sio njia ya wokovu. Sio ujumbe wa injili. Wokovu ni zawadi ya bure kutoka kwa Mungu na imani ya kawaida ya mtoto ndio njia bora ya kuipata zawadi.)
    1.    Soma Mathayo 11:27. Tulipokiangalia kifungu hiki hivi karibuni, nilikiita kuwa ni “fumbo.” Kinaonekana kusema kuwa Yesu pekee na Mungu Baba ndio wanaojuana. Kuna jambo gani la pekee kwenye kanuni hii? (Yesu anaweza kuchagua kumfunua Mungu Baba kwetu.)
    1.    Soma Mathayo 11:28. Sasa Yesu anabainisha kigezo anachokitumia kufunua “mambo yaliyofichwa” kuhusu Mungu. Kigezo hicho ni kipi? (Wale wanaokuja na ni wahitaji.)
      1.    Kigezo hicho ni kigumu kiasi gani? (Watu wenye mafanikio ya hali ya juu wana uwezekano mdogo sana kuamini kuwa ni wahitaji.)
      1.    Utaona kwamba Yesu anatoa ofa yake kwa “nyote msumbukao.” Je, hili si kundi la Jordan Peterson? Wale wanaofanya kazi ili kupata mafanikio? (Ndilo! Yesu anatuambia kuwa njia ya kuuendea Ukristo “imefichwa” na inapatikana kupitia kwake pekee. Njia hii ni kinyume na ile ya mafanikio ya kidunia. Mtoto yeyote anaweza kugundua jambo hili!)
    1.    Soma Mathayo 11:29-30. Je, Yesu anafanana na kiongozi yeyote wa kidunia au mungu wa kipagani? (Upole na unyenyekevu wa moyo ni kinyume tu cha kile ambacho ulimwengu unakitarajia.)
      1.    Tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii kiasi gani ili kuungana na vuguvugu la Yesu? (Tunalo pumziko! Kazi ni rahisi na mzigo ni mwepesi.)
      1.    Je, wanafunzi wangekubaliana na uchunguzi huu baada ya Yesu kuwaacha na kwenda mbinguni? (Hii inafanana sana na somo letu majuma mawili yaliyopita. Tunda la Roho linajumuisha amani, bali maadui wa injili husababisha mgawanyiko. Maadui wa injili ndio wanaosababisha ugumu na mizigo.)
      1.    Yesu anawapatia kazi gani maalumu wale watakaomfuata kama Wakristo? (Kujifunza habari zake.)
    1.    Hebu tutulie kidogo na tutafakari mjadala wetu hadi kufikia hapa. Je, unawapenda watu wavivu au unawapenda watu wenye hekima, waelewa na wenye bidii ya kazi? (Kwa hakika ninawapenda watu wanaofanya kazi kwa bidii. Biblia inazungumzia mambo mengi hasi kuhusu watu wavivu na inazungumzia mambo mengi mazuri kuhusu watu wenye juhudi. Hata Amri Kumi zinasema katika Kutoka 20:9 “siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote.”)
      1.    Utafikia hitimisho gani juu ya mjadala wetu hadi kufikia hapa unaoendana na fundisho la kawaida la Biblia? Unaoendana na Amri Kumi?
      1.    Wangapi kati yenu mnateleza kwenye skii ya majini na pia kuteleza katika theluji kwa kutumia relitheluji? Kama unaweza kufanya vyote viwili, hebu nieleze, zikoje? (Unalalia kwa nyuma unapoteleza kwenye maji ili kuweka kanieneo (pressure) kati ya reli ya kutelezea na maji. Unapoteleza kwenye theluji, kwa ujumla unalalia mbele ya relitheluji ili kuendelea kuwa na msawazo/usawa kamili.)
      1.    Kama uzoefu wako pekee ungekuwa ni wa kuteleza kwenye theluji, je, “uelewa wako wenye hekima” ungekunyima uwezo wa kuteleza kwenye maji?
        1.    Kwenye mazingira kama haya, je, ingekuwa bora kuteleza kwenye maji kama mtoto mdogo? Kwamba umtumaini tu mwalimu wako na kuachana na maarifa yako ya awali?
    1.    Soma Luka 18:24-25. Mjadala wetu hadi kufikia hapa unatufundisha nini juu ya maana ya kauli ya Yesu hapa? (Kama una mafanikio makubwa sana yaliyotokana na bidii ya kazi na hekima, itakuwa vigumu kuachana na mafundisho hayo. Katika ubao wa mjadala kwenye mada inayohusu mbinu za kuteleza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine nilisoma maandishi haya: “Ninaona kuwa, kutakuwepo na kuachana na tabia zilizotopea (zilizokolea).”)
    1.    Rafiki, ikiwa unafanya kazi kwa bidii na kufanikiwa katika dunia hii, injili inakupa wito wa kuachana na baadhi ya tabia zilizotopea (zilizojengeka). Si rahisi, na Roho Mtakatifu anahitajika. Lakini kumchagua Yesu ni bora zaidi kuliko kumkataa. Je, utafanya uamuzi leo, kwamba “Roho Mtakatifu, tafadhali nifundishe njia sahihi ya kuiendea injili?”
  1. Juma lijalo: Kupata Pumziko Katika Uhusiano wa Kifamilia.