Somo la 12: Nabii Mwenye Wahaka

Yona 1-4, 2 Wafalme 14
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
3
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Nabii Mwenye Wahaka

(Yona 1-4, 2 Wafalme 14)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Unajisikiaje Mungu anapokuondoa kwenye jukumu unalolifurahia, na kukuweka kwenye jukumu usilolipenda? Kiukweli, jukumu jipya linakufanya uwe na wasiwasi sana. Nabii Yona ana ufahamu mkubwa kuhusu aina hii ya badiliko. Hebu tuzame kwenye somo letu kumhusu Yona na tujifunze zaidi!

 1.    Shujaa Wetu
  1.    Soma 2 Wafalme 14:23-25. Kutafakari jambo hili kunaweza kuyafanya macho yako yahamaki. Kwa ujumla tunao akina “Yeroboamu” wengi sana kwenye vifungu hivi. Je, kuna mtu anayeweza kuelezea jinsi ambavyo Yeroboamu hakugeuka na kuziacha dhambi za Yeroboamu? (Tunao akina “Yeroboamu” wawili tofauti. Yeroboamu wa I ni “Yeroboamu mwana wa Nebati” na Yeroboamu wa II ni “Yeroboamu mwana wa Yehoashi.”)
   1.    Tunajifunza nini kumhusu Yona? (Kwamba alimshauri huyu mfalme mwovu.)
   1.    Ni ushauri wa namna gani ambao Yona alimpa Yeroboamu wa II? (Ushauri kuhusu kurejesha mipaka ya Israeli.)
   1.    Kwa nini Mungu anamsaidia mfalme mwovu kama Yeroboamu wa II? (Ilikuwa ni muunganiko wa kujishughulisha kwa Mungu juu ya mateso ya watu na kutunza ahadi yake kwa watu wake. Mungu aliwapenda watu wake.)
   1.    Hii inatufundisha nini kuhusu utayari wa Mungu kufanya kazi na watu wasio wakamilifu? (Yu radhi. Hii ndio mada tutakayoona ikiibuka katika somo letu la Yona.)
  1.    Watu wa Israeli walimfikiriaje Yona? (Alikuwa mzalendo! Alikuwa shujaa wa taifa.)
 1.   Shujaa Wetu Atoweka
  1.    Soma Yona 1:1-2. Jiweke kwenye nafasi ya Yona. Wewe ni nabii na pia ni mzalendo. Ujumbe wako kutoka kwa Mungu umekuwa sehemu ya muhimu ya ushindi kwa adui. Ninawi imewaogofya watu wa Israeli kwa miaka mingi. Unalichukuliaje hili jukumu jipya?
   1.    Je, jukumu hili linafanana na jukumu lako la zamani? (Hapana. Sasa unakwenda kuwa nabii kwa adui.)
   1.    Kazi ya nabii ni kuwaendea watu wake mwenyewe, sawa? Kwa nini nabii mzalendo apelekwe katika nchi ya adui? (Mojawapo ya maoni yanabainisha kuwa Yona ndiye nabii pekee aliyetumwa kwenda kwenye taifa la kipagani. Ninashawishika kuamini kuwa Yona hakutaka kusikia amri hii kutoka kwa Bwana. Maoni mengine yanataarifu kuwa katika kipindi cha Yona Ninawi ulikuwa mji mkuu wa Ufalme wa Waashuri ambao hatimaye uliiangamiza Israeli.)
   1.    Hebu turejee nyuma kidogo. Wote walikubaliana (Mungu, Yona, na Waisraeli) kwamba watu wa Ninawi walikuwa waovu. Unadhani Yona angependelea suluhisho gani? (Waangamize tu. Huo ndio uliokuwa ujumbe wake kutoka kwa Mungu lilipokuja suala la maadui wa awali.)
  1.    Hebu turukie mbele kidogo. Soma Yona 3:4. Huu ndio ujumbe ambao hatimaye Yona aliwafikishia watu wa Ninawi. Kama kweli Yona alikuwa mzalendo, kwa nini hakutaka kuwatemea mate machoni Waashuri na kuwaambia kuwa mji wao utaangamizwa? (Tatizo la dhahiri ni kwamba hana jeshi la Israeli pamoja naye. Anakwenda Ninawi “peke yake.”)
  1.    Soma Yona 1:3. Mji wa Ninawi ulikuwa karibu na mji wa sasa wa Mosul nchini Iraq. Kuna yeyote anayefahamu ulipo mji wa Yafa. Vipi kuhusu Tarshishi? (Maoni ya “The Bible Knowledge Commentary” yanatuambia kuwa Yafa ni mji wa sasa wa Jaffa nchini Israeli. Yumkini Tarshishi ulikuwa ni mji wa Tartessus Kusini mwa Hispania – takribani maili 2,500 magharibi mwa Yafa.)
   1.    Je, Yona anaelekea kwenye uelekeo sahihi? (Hapana. Alikuwa anaelekea uelekeo tofauti na ule aliotakiwa kwenda.)
   1.    Unadhani Yona alikwenda bandarini na kupanda meli yoyote aliyoiona? (Mfuatano wa maelezo uliopo katika kifungu cha 3 unaashiria kuwa aliufikiria mji wa Tarshishi kabla hajafika bandarini. Yona alidhamiria kuwa umbali wa takribani maili 3,000 kati yake na kule alikotakiwa kwenda.)
  1.    Soma Yona 1:4-6. Mungu anajaribu kumfikia nani? (Yona, yule aliyekuwa amelala.)
   1.    Ikiwa Mungu anamtafuta Yona, kwa nini watu wengine wengi wasio na hatia wanahusika?
    1.    Kwa nini mmiliki wa merikebu apate hasara ya kuharibika kwa chombo, abiria wapoteze mizigo yao, na mabaharia wateseke kiakili?
   1.    Je, utapendekeza kuwa Mungu awe na lengo lililochakatwa madhubuti linapokuja suala la kushughulikia dhambi? (Hakuna mtu hata mmoja kati ya watu wengine aliyekamatika kwenye “mzozo” kati ya Mungu na Yona aliyefahamu habari za Mungu. Uzoefu huu uliwafundisha kuhusu Mungu wa kweli aliyekuwa wa thamani zaidi kuliko mzigo wowote au amani/utulivu walioupoteza kwenye mchakato huu. Yona 1:16 inaonekana kama ni matokeo ya mfulilizo wa masuala ya kiinjilisti!)
 1. Shujaa Wetu Amezwa
  1.    Soma Yona 1:12 na Yona 1:15-2:2. Hadi kufikia hapa kwenye kisa chetu, Mungu anadhibiti nini na hadhibiti nini? (Anadhibiti hali ya hewa na samaki. Hadhibiti utii wa watu.)
   1.    Unaichukuliaje imani ya Yona katika hatua hii? “Ndipo” katika Yona 2:1 inahitimisha kuwa ni baada ya Yona kuwa ndani ya tumbo la samaki kwa muda wa siku tatu ndipo aliomba. Sina uhakika kama Yona anapata sifa ya kuwa na imani kuu.)
  1.    Soma Yona 2:3-4. Mijadala ya kesi mahakamani imenionesha kuwa watu wawili waaminifu kabisa wanaweza kuelezea tukio moja kwa namna tofauti kabisa. Je, unaona kile kilichomtokea Yona kwa namna ile ile alivyokiona? Je, “aliongozwa” kutoka mbele za Mungu?
  1.    Soma Yona 2:10. Je, Yona anastahili jambo hili?
 1.   Ujumbe
  1.    Soma Yona 3:3-5. Unaichukuliaje toni (sauti) ya ujumbe wa Yona? Je, ni sauti ya kuvutia, yenye uchangamfu, na iliyobuniwa kwa ajili ya mtu wa kisasa?
   1.    Je, ujumbe huu unavutia ubatili wa wananchi? Je, ujumbe huu unavutia udadisi wa wananchi?
   1.    Je, inawezekana kuwa ujumbe ulifanywa kimuhtasari kwetu kwa lengo la kufupishwa?
   1.    Wananchi wa Ninawi walikuwa na sababu gani za kumwamini Yona? (Kila kitu kwenye kisa hiki hadi kufikia hapa hakileti mantiki kinapotazamwa kwa vipimo vya kibinadamu. Mkono wa Mungu umekuwepo kwenye kila jambo. Imani yangu ni kwamba hakuna tofauti yoyote hapa. Sababu ya watu wa Ninawi kuamini ni kwamba Roho Mtakatifu anafanya kazi mioyoni na akilini mwao. Ujumbe wenyewe hauonekani kuwa na mvuto.)
  1.    Soma Yona 3:6-9. Kifungu cha 6 kinaanza kwa kusema, “Habari ikamfikia mfalme.” Hebu niambie, unadhani mfalme alisikia nini? (Alisikia kwamba jambo fulani la pekee lilikuwa linaendelea katika ufalme wake. Nabii wa kigeni alikuwa amekuja na ujumbe wa maangamizi na watu wote walimwamini.)
   1.    Je, mwitikio wa Mfalme wa Ashuru ndio kile ulichokitarajia? (Watu wangapi wa muhimu hawapendi kukubali wazo “linalotoka chini?” Ninadhani Mfalme alizoea kuliongoza taifa – na si kuwafuata watu.)
  1.    Soma Yona 3:10 na Yona 4:1-2. Fikiria kampeni ya kiinjilisti ya Billy Graham ambayo matokeo yake ni kuongoka kwa mji wote, kuanzia juu hadi chini. Kisha ingiza “Billy” kwenye kifungu chetu cha Biblia badala ya “Yona.” Unaweza kulifikiria hilo?
   1.    Yona ana shida gani? (Anajipenda yeye pamoja na hadhi yake zaidi kuliko anavyompenda Mungu au watu wengine.)
   1.    Unadhani Yona aliichukuliaje rehema ya Mungu kwake? Je, alifadhaika kuhusu Mungu kumrehemu kama alivyofedheheka kwa Mungu kuwarehemu watu wa Ninawi?
  1.    Soma Yona 4:3-4. Hii inatufundisha nini kumhusu Mungu? (Je, ulikuwa tayari kumwacha Yona afe baada ya kusikia kile alichokisema katika Yona 4:1-2? Hata hivyo, Mungu anadhihirisha rehema kwa kujaribu kusemezana jambo hili na Yona. Mungu anaonekana kama vile yuko kwenye nafasi ya mshauri.)
  1.    Soma Yona 4:5. Unadhani Yona alitumaini kuwa jambo gani litautokea mji? (Ninadhani alikuwa anasubiria moto ushuke kutoka mbinguni.)
   1.    Kwa kuzingatia Yona 4:3, Yona alikuwa na sababu gani kuamini kuwa Mungu atasusha moto? (Sababu pekee ninayoweza kuiona ni kwamba Yona alijitolea kufa alipotambua kuwa Mungu atadhihirisha rehema. Tuchukulie kwamba Yona ana kasoro kitabia anayoonekana kuwa nayo, mlolongo wa mantiki yake ni kwamba Mungu ananichukulia kuwa mimi ni mtu wa muhimu sana kiasi kwamba atauangamiza Ninawi sasa hivi kwa kuwa nimemwambia ni afadhali nife kuliko kuishi.)
   1.    Utaupatia alama gani utendaji kazi wa Yona?
  1.    Rafiki, usikose tumaini ling’aalo kutoka kwenye kitabu hiki. Watu wa Ninawi wenye vurugu na wanaotisha wanasamehewa na neema ya Mungu pale wanapomgeukia. Mungu anaendela kufanya kazi kwa upole na Yona aliyebadilika ili kutimiza malengo yake hapa duniani. Bila kujali kama umekuwa mwovu kwa nje, au Mkristo kwa nje mwenye moyo uliopindishwa na wenye ubinafsi, bado Mungu anataka kukuvuta karibu naye. Je, utaitikia leo?
 1.    Juma lijalo: Pumziko la Mwisho.