Somo la 5: Mgeni Katika Malango Yako

Kumbukumbu la Torati 10, Marko 12, Kumbukumbu la Torati 24
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
4
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Mgeni Katika Malango Yako

(Kumbukumbu la Torati 10, Marko 12, Kumbukumbu la Torati 24)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: “NIMBY” ni akronimi (acronym) inayoelezea uhaba/upungufu wa fikra, unafiki, na wakati mwingine kushindwa kwetu kuwatendea watu wengine kwa namna inayoendana na mafundisho ya Biblia. Kwa hiyo NIMBY ni kitu gani? NIMBY ni ufupisho wa “Not in my backyard” (Sio Katika Eneo Langu.) Mtu mwenye nadharia ya NIMBY atasema “Ninaunga mkono kabisa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya maskini, ninaunga mkono kabisa uzalishaji wa umeme kutokana na upepo, lakini ninapingana kabisa na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na mashine za kuzalisha umeme kwa kutumia upepo katika eneo linalonizunguka! Hebu tuzame kwenye Biblia zetu na tuone kile inachotufundisha kuhusu watu wadhaifu kabisa katika jamii, na kisha hebu tujaribu mioyo yetu na akili zetu na mantiki halisi ya fundisho hilo maishani!

  1.    Kuwa Tayari Kupokea Ushauri
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:12. Mungu ana matarajio gani kwetu? (Kumcha na kumpenda Mungu. Kuenenda katika njia zake. Kufanya hivyo kwa uhiyari.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:13. Tafsiri za Biblia za ESV, KJV, NIV, na Kiswahili zinahitimisha kifungu hiki kwa alama ya kuuliza. Tuchukulie kwamba watafsiri wamezingatia mantiki ya sentensi hii, kwa nini Mungu alifanye hili kuwa swali? (Mungu anatutaka tulitafakari jambo ili. Katika masomo yaliyotangulia tulijadili kwamba lengo la Amri Kumi ni kuyaboresha maisha yetu na kumpa Mungu utukufu. Mungu anatutaka tulitafakari hilo.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:14-16. Kifungu cha 16 ni taswira halisi! Unadhani Mungu anatutaka tufanye nini pale anapotuambia tuachane na usumbufu? (Anasisitiza badiliko la mtazamo. Kuwa wazi kwake. Usiendelee kutenda mambo kwa kuwa tu wewe au familia yako mara zote mmekuwa mkifanya hivyo.)
    1.    Soma Zaburi 51:10. Je, unaweza kubadili mtazamo wako? (Mtunga Zaburi anamwomba Mungu ambadili moyo wake na kumpa roho iliyotulia. Roho Mtakatifu anaweza kubadili mitazamo yetu ikiwa tutaomba kufanyiwa hivyo.)
  1.   Tenda Haki na Kuwa Mwenye Upendo?
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:17. Unapata hofu gani pale ambapo mtu mwenye mamlaka anaweza kuchukua uamuzi unaoathiri maisha yako? (Una wasiwasi kwamba mwenye mamlaka atakuwa na upendeleo (biased). Kama unaishi kwenye nchi iliyojaa rushwa, una wasiwasi kwamba uamuzi utatolewa kutokana na mbadilishano wa fedha.)
      1.    Mungu anafanyaje uamuzi? (Yeye ni muadilifu na hapokei rushwa.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:18 na Zaburi 146:9. Yatima, wajane, na wageni wana jambo gani linalofanana? (Hawana uwezo. Katika muundo wa jamii hawana ushawishi.)
      1.    Utaona kwamba yatima na mjane wanatendewa tofauti na mgeni. Wawili wa kwanza wanapata hukumu ya haki. Mgeni anapata upendo. Kwa nini utofauti huo?
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 10:19. Je, hii inaelezea tofauti hiyo? (Ndiyo. Inarudia amri ya kupenda na imejengwa juu ya watu wa Mungu kuwa “wageni katika nchi ya Misri.”)
      1.    Huu ni muktadha unaofurahisha. Watu wa Mungu walitendewaje Misri? (Walikuwa watumwa. Nadhani ujumbe uliopo ni kwamba tunapaswa kuzingatia jinsi ambavyo tungependa tutendewe.)
      1.    Neno la Kiebrania, msafiri, linamaanisha “mgeni.” Mtu anayepita. Nchini Marekani tunalo jambo la pekee la raia wengi wa nchi nyingine kuingia nchini kwetu isivyo halali – na hawaonekani kuwa wapitaji. Je, wana vigezo vya kuwa “wasafiri?”
      1.    Kama amri ilikuwa (kama ilivyo kwa wajane na yatima) ni kuwatendea “haki,” basi hawataruhusiwa kuingia kwa sababu wanafahamu kuwa wanakiuka sheria zetu. Haki inawahitaji wafuate sheria zilizopo kwa ajili ya kuingia nchini Marekani. Lakini, “upendo” (kwa maana ya chakula na mavazi) ndicho kinachotakiwa. Je, hilo linabadili mtazamo wako kuhusu jinsi ambavyo wale waliopo nchini isivyo halali wanapaswa kutendewa?
    1.    Angalia tena sehemu ya kwanza ya Kumbukumbu la Torati 10:18 inayotoa wito wa “hukumu ya haki” kwa watu dhaifu katika jamii. Nimeona taarifa nyingi za habari na video za watu wanaokuja nchini kupitia mpaka wa Kusini. Wote wamevaa nguo na sijasikia taarifa yoyote (kwa mshangao) kwamba wana tatizo la njaa. Wengi wanaonekana kuja kutafuta fedha zaidi. Je, hilo ndilo ulilolisikia? Je, hili liko sahihi?
    1.    Kama unakubaliana kwamba haki kwa watu wadhaifu katika jamii ni kanuni ya Kibiblia, tafakari jambo lifuatalo. Watu wanaoingia katika nchi isivyo halali hawatashindania nafasi za kazi na wale walio na uwezo katika jamii yetu. Badala yake, watashindana, na kushusha vipato, vya wale katika jamii yetu walio na uwezo mdogo kwa kuwa wana ujuzi mdogo wa kazi. Je, Wakristo wanapaswa kutafakari haki kwa raia wa sasa kama sehemu ya jinsi tunavyopaswa kushughulikia suala lililopo katika mpaka wetu wa Kusini?
    1.    Angalia tena Kumbukumbu la Torati 10:18. Mungu wetu wa upendo anaonyesha kiwango gani cha kujali kwa mgeni? (Anampatia chakula na mavazi.)
      1.    Taarifa ninayoisikia mara kwa mara ni kwamba watu wanaoingia nchini kwetu isivyo halali wanatafuta maisha mazuri – kuwa huru na kutafuta fedha zaidi. Je, hilo limo ndani ya viwango vya Kibiblia vya kujali? Au, linazidi viwango vya Kibiblia?
    1.    Soma Marko 12:29-31. Hebu tuulize maswali ya NIMBY. Je, uko tayari kumpeleka nyumbani kwako mtu yeyote aliye na chakula na mavazi, lakini anaingiza fedha kidogo kuliko wewe? Vipi kuhusu watu walio na nyumba ndogo?
      1.    Je, uko tayari kufanya hivi daima? Je, Marko 13:31 inaashiria kuwa hili linapaswa kutendeka?
    1.    Soma Kutoka 20:17. Ninamiliki mojawapo ya nyumba kubwa mtaani kwangu. Lakini, nimeona (hususani kwa msaada wa runinga na mtandao wa intaneti) nyumba nyingi zilizo kubwa kuliko nyumba yangu. Je, itakuwa sahihi kwangu kutaka kuishi kwenye nyumba kubwa, na ya kitajiri?
      1.    Je, mmiliki wa nyumba kubwa na ya kitajiri atashindwa katika wajibu wake wa upendo kwangu kama ataniambia kuwa hawezi kuishi na mimi? (Hapana. Na wala sitawaza kudai kwamba mtu aliye na mali nyingi kunizidi anigawie utajiri wake. Madai kama hayo, mawazoni mwangu, yanakiuka amri ya kutamani. Binafsi hicho ndicho kigezo ninachokitumia.)
  1. Kigezo cha Kujali
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:10-11. Ahadi ni ipi? (Ni dhamana ya mkopo.)
      1.    Hii inamtaka mkopeshaji awe na mtazamo gani? (Staha.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:12-13. Unadhani hapa dhamana ya mkopo ni ipi? (Koti la mtu au blanketi lake.)
      1.    Maelekezo haya yanatutaka tufanye nini, na yanazungumzia nini kuhusu maswali ya NIMBY niliyoyauliza? (Fikiria kumkopesha mtu ambaye kitu pekee alichonacho ni koti! Licha ya hayo, hili linaruhusiwa. Hii haimhitaji mkopeshaji kumpatia mtu fedha kwa kuwa tu yeye ni maskini. Hata hivyo, inamtaka mkopeshaji awe na huruma.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:14-15. Hapa kigezo cha kujali ni kipi? (Kumlipa mtumishi maskini siku anayomaliza kazi yake.)
      1.    Kwa sababu gani? (Kwa dhahiri haya ni makubaliano. Kifungu kinasema kuwa mtumishi “ameutamania.”)
      1.    Mgeni maskini anatendewaje kwenye suala la makubaliano ya kibiashara? (Anatendewa vile vile kama watumishi.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:17-18. Je, hiki ndicho anachokimaanisha Mungu anaposema kumpenda mgeni? Je, Mungu analinganisha upendo na haki? (Anataka haki kwa ajili ya mgeni. Lakini zingatia kwamba hii ni haki iliyopakwa rangi ya upendo. Tunaliona hili kwenye maelekezo ya kutochukua vazi la mjane kama dhamana ya mkopo.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 24:19-21. Je, mgeni, yatima, na mjane wanatakiwa kufanya kazi ili kujipatia chakula chao? (Naam. Mungu angeweza kusema kusanya chakula kilichosazwa na ukipeleke kwa maskini. Badala yake, Mungu alisema waache maskini wavune kilichosalia.)
      1.    Hii inazungumzia nini kuhusu mkulima “tajiri” anayetunza chakula kingi zaidi kwa ajili yake? (Kigezo cha kujali ni kupenda haki. Sio kumfanya kila mtu kuwa sawa. Kinamtaka maskini kufanya kazi na kinataka haki itendeke – kwamba utawala wa sheria uheshimiwe.)
      1.    Je, una uzoefu wowote unaoonyesha kuwa njia ya “haki ni upendo” ya Kumbukumbu la Torati ndio njia bora? (Nimegundua kwamba ninapompatia mtu kitu, huwa hashukuru vizuri. Kwa upande mwingine, pale anapokuwa amekifanyia kazi kitu hicho anakitunza vizuri sana.)
    1.    Rafiki, Mungu anatutaka tutafakari viwango vyake vya upendo kwa ajili ya wanadamu wenzetu. Viwango hivi vimejaa mantiki na kuheshimu hatimiliki. Vinasisitiza haki sawa kwa wote. Vinahitaji wema na kuzingatia jinsi ambavyo tungependa tutendewe. Je, utakuwa wakili wa Mungu katika kuwafikia watu wasio na uwezo katika jamii?
  1.   Juma lijalo: Tena Liko Taifa Gani Kubwa?