Somo la 13: “Upendo wa Kidugu Udumu” 

Waebrania 13
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
1
Lesson Number: 
13

Somo la 13: “Upendo wa Kidugu Udumu” 

(Waebrania 13) 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza. 

Utangulizi: Chukulia kwamba unaelekea kufa na hivyo unaamua kuandika barua ya mwisho kabisa kwa watoto wako. Utaandika nini? Yumkini itajumuisha ushauri wa kuishi maisha yanayoakisi kile ulichojifunza katika kipindi cha uhai wako. Unataka watoto wako waishi vizuri, na kuepuka kudhuriwa na uamuzi mbaya. Waebrania 13, somo letu la juma hili, inaonekana kuwa kama barua ya mwisho. Hebu tuzame kwenye somo letu la Waebrania na tuone inatupatia ushauri gani wa maisha! 

I.   Upendo wa Kidugu 

A.   Soma Waebrania 13:1. “Upendano wa ndugu” ni upendo wa namna gani? (Nadhani tutagundua hilo katika vifungu vinavyofuata.) 

B.   Soma Waebrania 13:2. Katika zama za leo, wageni wanaweza kuwa watu wa hatari. Kitabu cha Waebrania kinatutaka tuwatendee nini wageni? (Kuwakirimu na kuwa wema kwao.) 

1.   Tunatakiwa kuwa wema kwa wanafamilia wenzetu na kwetu binafsi. Unalinganishaje jambo hili hili na kuwa wema kwa wageni wanaoweza kuwa watu wa hatari? (Tunatakiwa kutumia akili ya kawaida (mantiki) na kuutafuta uongozi wa Roho Mtakatifu.) 

a.   Je, hatupaswi kuwa waoga kwa kuwa Mungu ndiye mdhibiti wa mambo na kwamba tunayatenda mapenzi yake? (Nilikuwa na mjomba wangu aliyekuwa afisa katika Kanisa la Jeshi la Wokovu. Hakuwa mwoga kwa wageni, na alifariki kwa uzee badala ya kufariki mikononi mwa mgeni. Alipitia uzoefu wa hatari ya kweli kabisa.) 

2.   Unadhani inamaanisha nini inaporejelewa kuwahudumia malaika pasipo kujua? (Kuna uwezekano wa kuwepo kwa jambo la kufurahisha linalohusu kuwakirimu wageni. Unaweza kuwa na fursa ya kipekee ya kufanya kazi na viumbe wasio wa ulimwengu huu (supernatural beings).) 

C.   Soma Waebrania 13:3. Watu wengi wanadhani kuwa Paulo ndiye alikuwa mwandishi wa kitabu cha Waebrania. Paulo alifungwa jela mara nyingi. Je, unadhani hili linawarejelea wale waliofungwa jela kutokana na imani yao? 

1.   Tunaambiwa tujiweke kwenye nafasi ya wafungwa. Hiyo inaashiria nini kuhusiana na kufungwa kutokana na kuwa mwaminifu? (Tunatakiwa kuliangalia hili kana kwamba tunaweza kuadhibiwa kutokana na uaminifu wetu. Je, tungependa wengine watutendee nini? 

2.   Angalia rejea ya wale “wanaodhulumiwa” na “pia mlivyo katika mwili.” Hii inaashiria nini kuhusiana na asili ya wafungwa? (Inaashiria kwamba wapo gerezani isivyo haki (wamedhulumiwa) na kwamba hao ni washiriki wa kanisa (sehemu ya mwili).) 

a.   Je, hii inamaanisha kuwa tunapokwenda kuwatembelea watu tusiowajua waliopo gerezani, basi hatutumii njia sahihi ya huduma kwa magerezani? (Ni vizuri kupeleka injili kwa watu ambao kuna uwezekano wanatafakari upya maisha yao. Lakini, ushauri huu mahsusi katika kitabu cha Waebrania kuhusu upendo wa kidugu unaonekana kuwarejelea washiriki wa kanisa waliofungwa kutokana na imani yao.) 

D.   Soma Waebrania 13:4. Kitabu cha Waebrania kinatuambia kuwa matokeo hasi ya kutoiheshimu ndoa ni hukumu ya Mungu. Kwa uzoefu wako, je, hilo ndilo tatizo pekee – kwamba hatimaye Mungu atahukumu? 

1.   Je, hii inahafifisha kuhesabiwa haki kwa imani pekee? (Kila mtu ambaye ameshaishi kupita umri wa wastani anatambua kuwa kutokuwepo kwa uaminifu kwenye ndoa huleta orodha ndefu ya matatizo. Unawatia uchungu wale unaowapenda. Dhambi za aina hii kwa dhahiri zinasameheka, tatizo linaibuka pale unapoamua kumgeuka Mungu na kuwa chini ya hukumu.) 

E.   Soma Waebrania 13:5. Je, kimsingi huu ni ushauri kwa masikini au kwa tajiri? (Huu unahusika kwa wote, lakini kwa uzoefu wangu masikini mara nyingi hawaridhiki. Baadhi ya matajiri wanaonekana kutoridhika na fedha, lakini mara nyingi ninaliona hili kwenye televisheni na sio miongoni mwa watu ninaowafahamu.) 

1.   Je, inaleta mantiki kwamba mara nyingi masikini hawaridhiki? (Kitabu cha Drive kinataarifu kuwa kuna kiwango cha kipato ambacho kuendelea kulipwa zaidi hakuleti motisha zaidi katika eneo la kazi. Kama uhaba wa fedha husababisha matatizo ya kujirudiarudia maishani, hilo (na uhaba wa kumtumaini Mungu) litasababisha kutoridhika.) 

2.   Jambo gani linazungumziwa hapa? (Mtegemee Mungu. Maisha yako yatavurugika kama unatafuta kujilimbikizia zaidi na zaidi. Kuutegemea upaji wa Mungu hukupatia amani na utulivu wa akili.) 

3.   Tiba ya kupenda fedha ni ipi? (Kumwamini Mungu pale anaposema, “Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”) 

F.   Soma Waebrania 13:6. Kifungu hiki kinaonekana kuwa nje kabisa ya mada. Vifungu vilivyotangulia vinatuambia kufanya jambo au kutokutenda jambo. Je, bado hili linazungumzia kuhusu kutopenda fedha? Au, je, linahusiana na vifungu vyote vilivyotangulia katika Waebrania 13? (Nadhani linarejelea vifungu vyote vilivyotangulia. Vifungu vilivyotangulia ni mifano hai ya kile inachomaanisha kuhusu kufuata amri ya Mungu kwamba tuwapende wengine kama tunavyojipenda wenyewe. Tukizifuata amri za Mungu zinazotukinga dhidi ya makosa yenye madhara, kwa muktadha huo, “Bwana ndiye anisaidiaye.”) 

1.   Je, kifungu hiki kinaahidi zaidi ya Mungu kukupatia ushauri wenye msaada tu? (Ndiyo. Kinatukumbusha kuwa Mungu ni mkuu kuliko adui yeyote wa kibinadamu. Mungu atatuokoa.) 

II.   Kuuzingatia Uongozi 

A.   Soma Waebrania 13:7. Je, hii inawarejelea viongozi wa kanisa? (Inawaelezea “viongozi” hawa kama wale “waliowaambia neno la Mungu.” Hii ni rejea ya watu kama mimi, wanaokukumbusha juu ya maneno ya Biblia.) 

1.   Jambo gani linamaanishwa kwa kusema “tena, kwa kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao?” (Fundisho sahihi linaakisiwa katika matokeo halisi. Unaweza kulijaribisha fundisho kwa kutumia maisha ya mwalimu.) 

a.   Je, hii ni njia ya busara ya kusema kuwa epuka mafundisho ya wale walio na matokeo mabaya? (Ninadhani hivyo.) 

2.   Tunapoambiwa “kuiiga imani yao” je, hii inamaanisha kuiga maisha ya walimu ambao imani yao ina matokeo mazuri? 

B.   Soma Waebrania 13:8-9. Madhehebu yangu yana kile ninachoweza kukiita mtazamo wa “kimabadiliko” wa watu wa Mungu. Mafundisho ya kanisa letu ni uelewa ulio na uhalisia sana wa Biblia – ulio juu ya imani za wale waliotutangulia. Vifungu hivi vinaashiria tahadhari gani kwa mtazamo huu? 

1.   Kejeli iliyopo ni kwamba baadhi ya watu katika madhehebu yangu pia wanasema, isivyowiana, kwamba “mabadiliko” yanapaswa kukomea kwenye mafundisho yetu halisi. “Nguzo” zetu zinapaswa kuzingatiwa. Je, haya ni majisifu au uelewa wa Biblia uliostaarabika?   

2.   Ujumbe gani unatolewa pale kifungu cha 8 kinaposema kuwa Yesu habadiliki? 

3.   “Mafundisho ya namna nyingine nyingine” yanaonekana kuwa na muktadha mahsusi. Ni muktadha gani huo? (Mafundisho yanayoihafifisha neema na kuendeleza vitendo fulani vya ulaji. Je, unaona mambo kama hayo kanisani kwako?) 

C.   Soma Waebrania 13:10. Ni akina nani hao “waihudumiao ile hema?” (Hii ni rejea ya Walawi na mfumo wa kafara.) 

1.   Kwa nini hawana “ruhusa kula” vitu vya hemani? (Hema letu ndilo imani yetu katika dhabihu ya Yesu aliyekufa badala yetu. Kama humkiri Yesu, basi huna haki ya kula katika hilo hema.) 

2.   Utaona kwamba kitabu cha Waebrania kinajadili jambo hili kwa kuzingatia chakula. Je, hiyo inatupatia utambuzi zaidi wa Waebrania 13:9 na maoni yake juu ya rehema dhidi ya vyakula? (Ninadhani inatupatia. Ingawa mjadala wetu wa awali ni uelewa mmoja, hii inaashiria kuwa utatuzi halisi ni kati ya neema na njia ya kupata chakula ambayo inafungamanishwa kwa ukaribu kabisa na mfumo wa hekalu. 

D.   Soma Waebrania 13:11-14. Kwa nini tunapaswa kuwa “nje ya kambi?” Je, hii si kauli ya ajabu? (Dhana iliyopo ni kwamba sisi sio miongoni mwa watu maarufu, bali tuko miongoni mwa wale wanaoteseka kwa kupata lawama kama wafuasi wa Yesu. Nje ya kambi ni mahali pazuri kuwepo kwa sababu lengo letu la kweli ni kuishi ndani ya Yerusalemu Mpya.) 

E.   Soma Waebrania 13:15-16. Shukurani ni ya muhimu kiasi gani? Tunapaswa kutenda jambo gani? (Kumtukuza Mungu na kuwasaidia wengine huakisi shukurani yetu.) 

F.   Soma Waebrania 13:17. Je, kimsingi ujumbe huu ni wetu, au wa viongozi? (Ujumbe ni kwa viongozi. Ujumbe unawaambia kuwa watapaswa “kutoa hesabu” ya uongozi wao, na kwamba wanapaswa kuwa na mtazamo sahihi.) 

1.   Je, hii inahitaji utii usio na vigezo? (Rejea ya kuwajibishwa na rejea ya kutoa manufaa kwa washiriki inatuambia kuwa viongozi wanaweza kufanya makosa ambayo hatupaswi kuyaidhinisha.) 

G.   Rafiki, je, utauchukulia kwa dhati ushauri wa mwisho uliotolewa katika kitabu cha Waebrania? Utakupatia maisha ya amani. 

III.   Juma lijalo tunaanza mfululizo mpya katika kitabu cha Mwanzo.